Kwa nini Israeli inapenda kuchagua makomandoo na majenerali kuongoza nchi?

Chanzo cha picha, Reuters
Wiki hii imeanza kwa Israeli kushuhudia mabadiliko katika ofisi ya Waziri Mkuu, akitoka Benjamin Netanyahu na kuingia Naftali Benett.
Pamoja na tofauti zao nyingi za kisiasa, kitu kimoja kinawaunganisha, nacho ni wote ni makomando waliotumikia kikosi maarufu cha jeshi la Israeli cha Seyeret Matkal.
Wawili hao si wanajeshi pekee ambao wamefikia ngazi za juu za kisisasa nchini Israeli. Kiuhalisia, wanajeshi wastaafu wanaushawishi mkubwa katika siasa za taifa hilo, na wamekuwa wakishika nyadhifa za juu za kisiasa toka kuasisiwa kwa nchi hiyo miongo saba iliyopita.
Kuna sababu kubwa mbili zinazofanana ambazo wachambuzi wanazitaja kuwa ndiyo zinazowabeba wanajeshi katika siasa za Israeli. Jambo la kwanza ni sera ya usalama kuwa kipaumbele katika taifa hilo ambalo limegubikwa na vita na ghasia na majirani zake toka walipoitwaa kimabavu ardhi ya Palestina na kutekeleza sera za kizayuni.
Kutokana na migogoro ya kijeshi na vita vya mara kwa mara, jeshi la nchi hiyo limetoa maafisa na makamanda ambao wamekuwa wakipendwa na wananchi kwa mchango wao wa kuwalinda, hivyo wanapoingia kwenye siasa, rekodi zao katika uwanja wa vita huwa ni mtaji wa ufuasi na upendo kutoka kwa wapiga kura.
Waziri mkuu mpya, Bw Bennet alihudumu katika jeshi kutoka mwaka 1990 mpaka 1996, akiwa afisa katika kikosi maalumu cha makomando cha Seyeret Matkal. Katika kipindi hicho alishiriki katika mapambano dhidi ya wapiganaji wa kipalestina pamoja na mapambano dhini ya wapiganaji wa Lebanon.
Lakini, umaarufu wake na rekodi zake kama mwanajeshi kwa hakika si mkubwa kama ilivyo kwa baadhi ya watangulizi wake.
Benjamin Netanyahu - kukomboa ndege iliyotekwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Netanyahu, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina lake la utani la Bibi, ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa miaka mingi zaid madarakani.
Bibi pia ni komando kutoka kikosi cha Seyeret Mitkal ambaye ameshiriki vita na mapambano kadhaa. Kutoka mwaka 1967 alipojiunga na jeshi alishiriki katika vita ya chini kwa chini ambapo vikosi vya Israeli vilikabiliana na Misri, Jordan na wapiganaji wa kundi la PLO la Palestina. Mapambano hayo yaliendelea mpka mwaka 1970 ambapo makubaliano ya kusitisha mapigano yalipitishwa.
Mwaka 1972, Bibi alikuwa sehemu ya kikosi cha makomando 16 kilichofanikiwa kuikomboa ndege Sabena 571 iliyokuwa ikitoka Vienna, Austria kuelekea TelAviv, Israel. Ndege hiyo ilitekwa dakika 20 baada ya kupaa na wanachama wanne kundi la Black September ambao walikuwa wakishinikiza kuachiwa huru kwa wafungwa 315 wa kipalestina katika jela za Israeli.
Jumla ya abiria 90 walishikiliwa mateka, kabla ya makomando hao kuivamia ndege hiyo punde baada ya kutua wakijifanya ni mafundi waliotaka kuifanyia matengenezo ndege hiyo. Ndani ya dakika mbili tu, makomaando hao waliwaua watekaji wawili wa kiume na kuwakamata washirika wao wawili wa kike.
Abiria mmoja tu alipoteza maisha katika operesheni hiyo. Komando mmoja tu alijeruhiwa kwa kupigwa risasi ya bega, naye ni Netanyahu.
Ehud Barak - mwanajeshi mwenye rekodi kubwa ya ufanisi

Chanzo cha picha, AFP
Kikosi cha makomando 16 walioikomboa ndege ya Sabena 571 kiliongozwa na Ehud Barak.
Barak ni moja kati ya wanajeshi watatu ambao wanaamika kuwa ni bora zaidi kuwahi kutokea nchini Israeli. Alitumikia jeshi hilo kwa miaka 35 na kufikia cheo cha juu zaidi cha Luteni Jenerali na kuwa mkuu wa majeshi.
Barak na Netanyahu walikuwa kikosi kimoja cha makomando jeshini, lakini mwaka 1999 wawili hao waligombea uwaziri mkuu kupitia vyama pinzani.
Netanyahu ambaye alikuwa anahudumu katika awamu yake ya kwanza ya uwaziri mkuu aliangushwa na Barak.
Ariel Sharon - 'Muuaji wa Beirut'

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 2001, Barak aliitisha uchaguzi mkuu maalumu, aliangushwa na mwanajeshi mwengine maarufu, Jenerali Ariel Sharon akachukua hatamu za uwaziri mkuu.
Kwa wananchi wengi wa Israeli, Jenerali Sharon ni shujaa wa vita, lakini kwa Wapalestina na Walebanoni ni 'muuaji na mhalifu wa kivita'.
Sharon alikuwa miongoni mwa makamanda wa kwanza wa jeshi mwaka 1948 baada ya makundi ya wapiganaji wa kiyahudi yalipojiunga na kuunda jeshi baada kujitangazia uhuru na kuundwa kwa taifa la Israeli. Toka hapo aliendelea kuongoza vikosi kadhaa kwenye vita zote muhimu na za awali katika historia ya taifa hilo.
Waziri mkuu wa zamani wa taifa hilo, Yitzhak Rabin alimtaja Sharon kuwa "kamanda stadi zaidi wa majeshi ya ardhini katika historia yetu."
Katika vita vya Yom Kippur mwaka 1973, vikosi vya Sharon vilipenya mpaka ndani ya Misri, na wakati vita hivyo vilipokwisha, walikuwa katika mji wa Suez, kilomita 101 tu nje ya mji mkuu wa Misri, Cairo.

Chanzo cha picha, Reuters
Lakini Sharon pia alifahamika kwa jina 'muuaji wa Beirut' ama kwa Kingereza 'butcher of Beirut'. Jina hilo alipewa wakati akiwa Waziri wa Ulinzi wa Israel kutokana na mauaji ya raia baina ya 500 mpaka 3,500 wengi wao wakimbizi wa kipalestina. Kundi lililotekeleza mauji hayo lilikuwa mshirika wa jeshi la Israeli na jeshi hilo chini ya uongozi wa Sharon lingeweza kuzuia maafa hayo lakini hawakuingilia kati.
Sharon alihudumu kama waziri mkuu kutoka 2001 mpaka 2006. Alifariki Januari 2014 baada ya kuwa mgonjwa mahututi kwa miaka nane.












