Nchi gani ni watengenezaji na watumiaji wakuu wa droni Mashariki ya Kati?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Ndege ndogo zisizo na gharama zinaruka angani bila kizuizi. Hupaa na kutua katika mji, msitu, au kwenye meli za vita baharini. Hupeleleza, kufuatilia, kulenga na hata kubadilisha mkondo wa mapigano. Silaha mpya haihitaji jeshi kubwa, mtu anayeiongoza hukaa ardhini.
Katika mazingira ya eneo la Mashariki ya Kati yaliyojaa migogoro ya silaha, iwe kati ya majeshi au makundi, droni ni silaha inayozua hofu. Kila mtu anamiliki ndege zisizo na rubani kwa namna moja au nyingine kutokana na udogo wao na gharama ndogo.
Taasisi ya Mafunzo ya Sera ya Kimataifa (ISPI) inakadiria kuwa nchi za Mashariki ya Kati (bila kujumuisha Israel) yametumia angalau dola bilioni 1.5 kununua ndege zisizo na rubani za kijeshi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Ushindani wa silaha ulianza lini?
Baadhi wanaamini mwanzo wa mbio za silaha za ndege zisizo na rubani zilianza na kile kinachojulikana kama Arab Spring, lakini mbio hizo zilianza mapema kuliko hapo kwa maoni ya Dkt. James Patton Rogers, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sera na Teknolojia katika Chuo Kikuu cha Cornell.
Anasema mbio hizo zilianza mwishoni mwa miaka ya 1970 au mapema miaka ya 1980. Israel na Iran zimekuwa zikitengeneza ndege zisizo na rubani tangu wakati huo, na nchi zote mbili zinazingatia mifumo ya silaha za klushambulia mbali kama sehemu muhimu ya ulinzi wa taifa.
Lakini mabadiliko makubwa ya kutumia ndege hizi kama njia ya wazi ya kushambulia yalianza wakati Uturuki ilipotumia ndege hizo kuzuia jeshi la Syria kuharibu vikosi vya upinzani mnamo 2020. Ndege zisizo na rubani za Uturuki za Bayraktar zilizuia zaidi ya magari 100 ya kivita ambayo yalikuwa mbele ya vikundi vya upinzani. .
Baada ya hapo, droni zilianza kutumika kwa wingi Mashariki ya Kati na kuzalishwa kwa idadi.
Muhammad Suleiman, mkurugenzi wa Mpango wa Teknolojia ya Kimkakati na Usalama wa Mtandao katika Wakfu wa Mashariki ya Kati, anasema kuna wahusika wakuu watatu wanaotengeneza ndege zisizo na rubani Mashariki ya Kati.
Israel

Chanzo cha picha, REUTERS
Israel ni nchi ya kwanza, kwa mujibu wa Suleiman, kwa sababu ni "nchi ya kwanza kutumia ndege zisizo na rubani katika Vita vya Lebanon mwaka 2006, na bila shaka ni kutokana na msaada kutoka kwa Marekani.
Israel inachukuliwa kuwa moja ya wazalishaji na wauzaji wakubwa wa ndege zisizo na rubani, kwani ndege zisizo na rubani zinawakilisha asilimia 25 ya jumla ya mauzo ya silaha za Israeli mwaka 2022, kulingana na taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Israel.
Moja ya ndege zisizo na rubani za Israel ni "Eitan," ambayo inaweza kubaki angani kwa masaa 36 mfululizo na kubeba kilo 1,000 za makombora.
Israel pia ilianzisha mashambulizi na operesheni kwa kutumia ndege zisizo na rubani za Hermes 450 na Hermes 900, na kuzitumia katika vita vyake huko Gaza, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.
Uturuki
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uturuki inashika nafasi ya pili, ambayo, kwa maoni ya Suleiman, ilianza kutengeneza ndege zisizo na rubani kwa kutegemea miundo na leseni za Magharibi, hasa kutoka Marekani, na uzalishaji ulitokana na malighafi ya ndani ya Uturuki.
Ndege isiyo na rubani ya Bayraktar TB2, ambayo inaweza kubaki angani kwa saa 24 kwenye mwinuko wa hadi futi 25,000, inahesabiwa kuwa ni ndege ya kwanza iliyozalishwa na Uturuki.
Suleiman anaongeza kuwa droni ilikuwa silaha mashuhuri zaidi ya Uturuki nchini Syria kuanzia mwaka 2016, na pia nchini Libya mwaka 2019, wakati Uturuki ilipotuma ndege zisizo na rubani za Bayraktar ili kumzuia Jenerali Khalifa Haftar, ambaye alikuwa kwenye lango la Tripoli akielekea kulishika jiji hilo.
Kulingana na data rasmi ya Uturuki, mwaka 2022, Baykar, kampuni inayotengeneza ndege zisizo na rubani, ilisaini mikataba ya usafirishaji wa ndege hizo kwa nchi 27, na mapato ya jumla ya dola za kimarekani bilioni 1.18, na wanunuzi mashuhuri ni Ukraine, Poland, Azerbaijan, Morocco, Kuwait, Emirates, Ethiopia, Turkmenistan, Kyrgyzstan, Romania na Albania.
Iran

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Nchi ya tatu ni Iran, ambayo ilitegemea droni za bei nafuu kwa sababu iko chini ya vikwazo vya kiuchumi. Iran ilianza kutengeneza programu za ndege zisizo na rubani tangu miaka ya 1980, wakati wa vita dhidi ya Iraq (1980-1988).
Mpango wa Tehran wa kuzalisha ndege zisizo na rubani na kusafirisha baadhi ya ndege hizo kwenda Urusi umeibua hasira kwa Marekani, ambayo iliweka vikwazo kwa mtandao wa mashirika kumi na watu wanne walioko Iran, Malaysia, China na Indonesia.
Vikwazo hivyo ni kwa sababu ya kuwezesha kuiuzia Iran vifaa vya kielektroniki vya asili ya Marekani kwa shirika lenye uhusiano na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema.
Marekani pia iliishutumu Iran kwa kuhusika katika kuwapa Wahouthi ndege zisizo na rubani ambazo zinashambulia meli katika Bahari ya Shamu.
Mwezi Oktoba mwaka jana, Wizara ya Ulinzi ya Iran ilizindua ndege isiyo na rubani ya "Mohajer 10" na kusema ina uwezo wa kuruka kwa saa 24 katika urefu wa hadi mita 7,000 kwa kasi ya kilomita 210, na ina uwezo pia ya kufanya shughuli katika umbali wa hadi kilomita elfu mbili.
Mataifa mengine

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
UAE na Israel zinafanya kazi kwa pamoja ili kuendeleza droni. Kampuni ya Emirati Edge na Kampuni ya Israel Aerospace Industries Company wanatengeneza mfumo wa kupambana na ndege zisizo na rubani, kulingana na Reuters, kwa lengo la kurudisha nyuma. mashambulizi yoyote ya droni.
Agosti 21, 2021, tovuti ya Habari ya Ulinzi ilisema kampuni mbili za Saudia zilitia saini makubaliano ya kushiriki katika utengenezaji na uundaji wa ndege isiyo na rubani ya "Sky Guard."
Ufalme huo pia umenunua ndege kutoka Uturuki, na pia ilitia saini mkataba Septemba 2023 na kampuni ya Uturuki baada ya miaka mingi ya mvutano wa kijiografia kati ya nchi hizo mbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Teknolojia ya Kimkakati na Usalama wa Mtandao katika Wakfu wa Mashariki ya Kati, Mohamed Soliman, anasema kwamba ushirikiano ambao Misri iliingia na nchi kubwa katika nyanja ya utengenezaji wa silaha kwa ujumla na kupata miundo ya kisasa na leseni za utengenezaji ziliweka mazingira mazuri ya utengenezaji wa droni.
Misri inazalisha ndege isiyo na rubani, yenye kasi ya kilomita 260 kwa saa, na inaweza kuruka kwa saa 30 mfululizo kwa hadi kilomita 240.
Katika maonesho ya IDEX 2023, jeshi la Misri lilionesha ndege ya Taba 1 na ile ya Taba 2. Ndege ya kwanza ina uwezo wa kutambua, kufuatilia na kuharibu shabaha na ina kasi ya kilomita 500 kwa saa, na inaweza kukaa angani kwa dakika 50 katika mwinuko wa kilomita 6.
Aina nyingine ambayo Misri inayo ni Ahmose, ni droni ya upelelezi, yenye kusafiri hadi kilomita 240, na inaweza kufanya kazi hadi urefu wa mita 7,000.
Anga yenye utata
Muhammad Suleiman, anasema, "hadi sasa, hakuna mifumo ya moja kwa moja ya kupambana na droni, na nyingi ya mifumo hii iko katika hatua ya majaribio."
Kampuni kadhaa zimetengeneza vifaa vya kushikiliwa kwa mkono au vilivyowekwa kwenye mabega ambavyo vinaweza kutumika kurusha wavu kwenye ndege zisizo na rubani, na kuzuia propela zake kuzunguka, na kusababisha kuanguka.
Dk. James Patton Rogers anasema, “sasa tumefikia kiwango cha kuenea bila kudhibitiwa kwa ndege zisizo na rubani Mashariki ya Kati. Leo kundi au serikali inaweza kutumia teknolojia ya droni.''











