Hatua ya Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudia kuitetea Iran dhidi ya Israel ina maana gani?

Mohammed bin Salman ndiye mrithi wa kiti cha ufalme nchini Saudi Arabia, lakini kutokana na uzee wa babake, amechukua uongozi wa mambo mengi muhimu ya nchi yake.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Sio kitambo sana, utetezi wa Muhammad bin Salman kwa "uhuru wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran" dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya Israel ulionekana kutowezekana.

Saudi Arabia haikuwa tu inajaribu kusimama mbele ya Iran, bali pia ilikuwa katika mchakato wa kuitambua Israel na kuunda muungano wenye nguvu dhidi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati.

Lakini sasa ukurasa umegeuka kabisa. Mwanamfalme kijana wa Saudia, kama mtawala asiye rasmi katika nchi yake, siku ya Jumatatu, akitoa hotuba muhimu kwa wakuu wa nchi za Kiislamu, aliiomba "jumuiya ya kimataifa" kutoiruhusu Israel kuishambulia Iran.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Saudi Arabia (WAS), Mohammed bin Salman alisema: "Saudi Arabia inaitaka jumuiya ya kimataifa kutekeleza majukumu yake ya kudumisha usalama na amani kwa mataifa na kukomesha uchokozi wa utawala wa Israel dhidi ya mataifa ya Palestina na Lebanon na kuuwajibisha utawala huo wa kimabavu kutoa wito wa kuheshimu mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na sio kushambulia ardhi yake.

Maandishi ya Kiarabu hayataji "utawala unaokalia kwa mabavu", lakini wakati huo huo, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alirejelea "udhibiti wa Israel ulio kinyume cha utaratibu" na kuishutumu nchi hiyo kwa kufanya mauaji ya halaiki. Kwa ujumla, sauti ya hotuba ya Bin Salman inapingana sana na Israeli, na ndani yake anawatetea waziwazi Wapalestina na Walebanon.

Taarifa fupi ya Mwanamfalme wa Saudia kwa Iran imegonga vichwa vya habari licha ya Rais wa Iran Masoud Pezeshkian kutokuwepo katika mkutano huu wa dharura.

Uamuzi unaotajwa kuwa wa ajabu kufanywa na Iran, ambao sababu za wazi bado hazijatajwa.

Wakati muhimu kwa mashariki ya kati

Katika muongo mmoja uliopita, Kuimarika kwa nguvu za Mohammed bin Salman katika muundo wa madaraka wa Saudi Arabia, uhusiano kati ya Riyadh na Tehran umebadilika kabisa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa kuegemea Washington na uhusiano wa kihistoria wa nchi yake na Marekani, mwana mfalme wa Saudia alikua mmoja wa wahusika muhimu katika eneo hilo, ambaye alitoa moyo na roho yake kuidhibiti Iran.

Ingawa Iran na Saudi Arabia chini ya miaka miwili iliyopita, kwa upatanishi wa China, walipunguza sheria kali na kujiondoa katika baadhi ya maeneo kwa lengo la kupunguza mvutano na kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia.

Hakukuwa na mikakati sawia katika sera ya kigeni ya Tehran na Riyadh.

Saudi Arabia tangu jadi imekuwa moja ya washirika wakubwa wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, na katika sera ya kigeni, inafanya juhudi kubwa kutotilia shaka maslahi na matakwa ya Washington.

Wakati huo huo, historia ya ushindani wa kieneo kati ya Saudi Arabia na Iran ni ndefu zaidi kuliko umri hasa wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Wakati huo huo, harakati mpya za kidiplomasia na undugu zinazoibuka baada ya Oktoba 7 huko Mashariki ya Kati zimekuwa jambo la kila siku.

Wakati huu, Iran ilifanya jitihada kubwa za kujisogeza karibu na Jordan na Israel na kufanikiwa kuitenga nchi hii wakati wa mapigano yake ya kijeshi na Israel.

Na sasa ni kana kwamba ni zamu ya Saudi Arabia kupambanua upya nafasi yake katika mizani ya madaraka katika eneo la Mashariki ya Kati katika zamu hizi muhimu.

Mashambulizi makubwa ya Israel na mauaji ya Wapalestina yanaendelea pamoja na mashambulizi ya mabomu na uingiliaji wa kijeshi katika nchi hii ya Lebanon.

Licha ya ripoti za mara kwa mara za mashirika ya kimataifa zinazopinga maandamano na wito kutoka katika taasisi kama vile Umoja wa Mataifa au Mahakama ya Hague, bado hakuna matumaini ya wazi ya kusitishwa kwa mapigano na kukomeshwa kwa mgogoro huu.

Sambamba na mashambulizi ya Israel, mgombea ambaye anajulikana kwa kuiunga mkono Israel alishinda uchaguzi nchini Marekani na ameahidi kuwa na mkataba mgumu zaidi na Iran.

Baadhi ya wadadisi wachache wanaamini kwamba hatari ya mapigano ya kijeshi katika Mashariki ya Kati itaongezeka kuanzia siku Donald Trump atakapoingia katika Ikulu ya White House (Desemba 30).

Ikiwa matazamio hayo yatakuwa kweli,mataifa mengi katika Eneo hilo hususan yale yenye ukaribu na uhusiano mzuri na Marekani kama Saudi Arabia yatakabiliwa na swali la msingi wataendelea kuiunga mkono Iran au watabaki na msimamo wa wastani katika uingiliaji wa kijeshi?

Gaza imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa kibinadamu kwa zaidi ya mwaka

Chanzo cha picha, getty

Ni katika wakati ambapo kiwango cha hasira ya umma dhidi ya Israel miongoni mwa jamii za Kiislamu duniani kimefikia juu zaidi, "kutopendelea upande wowote" kwa viongozi wa nchi kama vile Saudi Arabia, Misri, Jordan na Umoja wa Falme za Kiarabu katika mzozo huu unaozikabili nchi hizo mbili,Iran na Israel zinaweza kugharamika Zaidi na kuathiri uhalali na umaarufu wao.

Katika hotuba yake siku ya Jumatatu, Mwanamfalme Mohammed bin Salman alionyesha kwamba hataki kujulikana kama mfalme kibaraka wa Marekani na Israel.

Msimamo huu hauwezi tu kuwa na matokeo chanya kwa nafasi yake katika Eneo hilo lakini pia ni muhimu kwa nafasi na jukumu la Saudi Arabia katika uhusiano wa kiuongozi katika Eneo hilo.

Badala ya kukaa kimya "kwa kumuogopa Agha Balaser" na kupuuza mvutano kati ya Iran na Israel, nchi hii imeingia kwenye mchezo wa wazi dhidi ya Israel na kuipendelea Iran.

Kwa kuchagua mbinu ya mawasiliano ya kimkakati, alitoa hotuba yake kwa "jumuiya ya kimataifa" huku kwa kuzingatia msingi wa mpangilio wa hotuba hiyo kwa ulimwengu, alichagua kuulenga ulimwengu wa Magharibi kama hadhira halisi ya hotuba yake.

Hatua hii kwa hakika ni mwendelezo wa kampeni yake ya kina ya kuimarisha upya taswira ya Saudi Arabia na kufafanua upya nafasi ya nchi hii katika ngazi ya kimataifa, ambayo imeanzishwa kwa miaka kadhaa.

Kwa mtazamo huu, hotuba ya Mohammed bin Salman siku ya Jumatatu kwa hakika ni msisitizo usioandikwa kuhusu msimamo wa uongozi wa Saudia, ambao, umechukua mkondo wa watu wenye weledi katika kushughulikia mzozo huo, kana kwamba wahafidhina wa pande zote wamedhibiti hali hiyo.

Sasa, hatafuti tena ukaribu na Israel au Marekani ili kuweka mizani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Badala yake, wakati huu ana wasiwasi kuhusu Israeli kupata mamlaka zaidi; Mchakato ambao bado unaendelea na ikiwa hakuna mabadiliko makubwa ndani yake, unaweza kuongeza udhibiti wa Israeli katika eneo hilo.

Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Seif Abdalla