Ni miungano gani ya kijeshi yenye nguvu kati ya mataifa yanayovutana Mashariki ya Kati?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Katika siasa za kimataifa, ukoo wa Al Thani wa Qatar unafuata mkakati wa wazi wa kujiimarisha kama msuluhishi muhimu katika migogoro ya kikanda.
    • Author, Jose Carlos Cueto
    • Nafasi, BBC

Vita kati ya Israel na Hamas vinaashiria mwanzo wa moja ya vipindi vya misukosuko katika historia ya hivi karibuni ya Mashariki ya Kati.

Vurugu hizi zinachochea hofu ya kuongezeka kwa vita katika Mashariki ya Kati. Mbali na mzozo huo, eneo hilo limetikiswa na mapigano kati ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon.

Mashambulizi kati ya majeshi ya Magharibi na waasi wa Houthi nchini Yemen; Operesheni za Iran nchini Iraq, Syria na Pakistan; na mashambulizi ya wanamgambo wengine wanaoiunga mkono Iran dhidi ya Marekani, Israel na washirika wao.

Kuna ushindani kati ya Taifa la Israel na ulimwengu wa Kiarabu. Lakini pia kuna mgawanyiko wa kidini kati ya Washia - ambao kwa jadi wanawakilishwa na Iran - na Sunni - ambao nguvu zao kuu ni Saudi Arabia.

Iran na makundi yenye silaha

 c

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Iran na Saudi Arabia ndizo mataifa mawili makubwa katika ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa.

"Mhimili wa upinzani" unaundwa na vikundi vyenye silaha vinavyoungwa mkono na Iran, kama vile Hezbollah huko Lebanon; Wanamgambo wa Kishia nchini Iraq, Afghanistan na Pakistan; Hamas na makundi mengine ya wapiganaji katika maeneo ya Palestina na waasi wa Houthi nchini Yemen.

Wana itikadi za chuki dhidi ya Marekani na Israel. Wote kwa kiwango kikubwa au kidogo, wameshambulia maeneo ya Israel au washirika wake tangu vita vya Gaza kuanza Oktoba.

"Mhimili wa upinzani ni makundi ambayo ni zao la mapinduzi ya Irani ya 1979 na yanfanya kazi kama njia ya kueneza malengo yake ya kisiasa," anaelezea Lina Khatib, mkurugenzi wa Idara ya masomo ya Mashariki ya Kati ya Chuo Kikuu SOAS, London.

Wataalamu wanasema makundi haya yalizaliwa kutokana na kutoridhika na hali halisi ya kisiasa katika nchi zao - na Iran inachukua fursa ya hisia hii kupanua ushawishi wake wa kikanda.

Katika makala iliyochapishwa mwaka 2020 na mwandishi wa BBC, Kayvan Hosseini, anasema, "makundi yote haya yalipata msaada wa vifaa, kiuchumi na kiitikadi kutoka Iran."

Michael Kugelman, mkurugenzi wa Asia Kusini wa Kituo cha utafiti cha Wilson, anasema mchango wa dini hauwezi kupuuzwa kwa sababu ya ukaribu wa Iran na makundi ya Kishia na ukaribu wa Wasaudi na Sunni."

Lakini, anasisitiza kwamba mivutano hiyo inahusiana zaidi na kupigania mamlaka kuliko tofauti za kidini. Mano, uungaji mkono wa Iran kwa Hamas dhidi ya Israel, licha ya kundi hili la kijeshi ni la Sunni.

Au pia Hamas na Hezbollah wameunga mkono pande tofauti katika vita vya Syria, lakini wote wameungana katika lengo lao la kuimaliza Israel.

Kambi ya nchi za Kiarabu

C

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Mabadiliko ya Saudi Arabia yaliharakishwa na matarajio ya Mohammed bin Salman
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Saudi Arabia imechukua hatua nyingi katika miaka ya hivi karibuni kujiimarisha kama kiongozi katika ulimwengu wa Kiarabu.

Miongo michache iliyopita, kitovu cha ulimwengu wa Kiarabu kilikuwa Misri, nchi ambayo ilikuwa na ushawishi mkubwa kisiasa, kitamaduni na wingi wa watu katika eneo hilo.

Lakini uhawishi umehama. Baadhi ya nchi ndogo - kama Falme za Kiarabu na Qatar - zilijitokeza. Hasa kutokana na kushika hatamu Mwanamfalme Mohammed bin Salman mwaka 2017, "Saudi Arabia imebadilika sana ndani na kimataifa."

"Kuongezeka ushawishi wa Saudi Arabia kumechangiwa na kukuwa kwa uchumi wake na uungwaji mkono uliotolewa na Marekani wakati wa urais wa Donald Trump kama hatua ya shinikizo dhidi ya Iran," anaelezea mtaalamu wa Mashariki ya Kati, Haizam Amirah-Fernández.

Wataalamu wanakubali kwamba Saudi Arabia ndiye kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Kiarabu, shirika la kikanda la nchi 22.

"Kwa ujumla, ingawa kila nchi ina malengo yake, hata Misri na Jordan zinafuata miongozo iliyowekwa na Saudia," anaelezea Khatib.

Kwa takriban miaka arobaini, Saudi Arabia na Iran zimekuwa katika ushindani wa wazi ambao baadhi ya wataalamu wanasema ni "Vita Baridi mpya Mashariki ya Kati."

Katika miaka ya hivi karibuni, mvutano huo umezidi kukuwa kutokana na vita katika eneo hilo.

Nchini Yemen, Saudi Arabia inaunga mkono vikosi vya serikali katika vita vyao dhidi ya waasi wa Houthi tangu 2015.

Iran, inashutumiwa na wapinzani wake kuunga mkono Houthi, lakini imekanusha kutuma silaha kwa kundi hilo, lililohusika na mashambulizi ya droni dhidi ya miji na miundombinu ya Saudia.

Saudi Arabia pia inaitumu Iran kuingia Lebanon na Iraq, ambapo wanamgambo wa Kishia wamejilimbikizia ushawishi mkubwa wa kisiasa na kijeshi.

Machi 2023, uhusiano wa Saudia na Iran uliingia katika enzi mpya kwa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na makubaliano ya usalama, biashara, uchumi na uwekezaji chini ya mazungumzo yaliyosimamiwa na China.

Qatar kama mpatanishi

C

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdoulahian alikutana na kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh nchini Qatar mwishoni mwa Disemba.

Qatar ni sehemu ya kambi inayoongozwa na Saudi Arabia, ingawa pia ina jukumu la kuwa mpatanishi. Na kuifanya kuwa nchi ya kipekee katika kanda hiyo.

Hivi sasa, Qatar ina jukumu la kipekee kama wapatanishi kati ya Israel na Hamas. Kwa miaka mingi, nchi hii tajiri imekuwa ikihusika katika kuzileta pamoja nchi au makundi pinzani.

Lakini kuna nyakati za changamoto kwa nchi hiyo.

"Mwaka 2017, Qatar ilikabiliwa na vikwazo kutoka Saudi Arabia, Bahrain, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Yemen na Libya, ilianza kuonekana kama tishio kutokana na malengo yake ya kisiasa," anasema Khatib.

Qatar ni nchi tajiri sana lakini ndogo, udogo huo katika mazingira magumu - kama mwanasayansi wa siasa Mehran Kamrava anavyoeleza katika kitabu chake Qatar: Small State, Big Politics – ‘hutafuta ushirikiano wa aina mbalimbali ili kulinda usalama wake na kuboresha hadhi na nafasi yake ya kidiplomasia.”

Vikwazo kwa Qatar viliondolewa 2021 na uhusiano na majirani zake, hasa Saudi Arabia, unaonekana kuwa katika hali nzuri.

"Qatar bado inataka kujiimarisha kama nchi ya upatanishi na maridhiano kama sehemu ya mkakati wake wa kijiografia na kisiasa," anasema Khatib.

Vipi kuhusu Israel?

CX

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Vita vya Israel huko Gaza vimeongeza kukataliwa kwa taifa la Kiyahudi kati ya nchi za Kiarabu

Amirah-Fernández anafafanua kesi ya Israeli kama mfano usio wa kawaida katika eneo hilo. Khatib anasema Israel "inajiendesha kwa uhuru, bila ya kuwa katika muungano na nchi yoyote."

Israel imekuwa ikiendesha vita vya muda mrefu, ambavyo havijatangazwa dhidi ya Iran na wanamgambo wengine. Kuna uhasama wa kiwango lakini haufikii hatua ya migogoro kamili na wa wazi.

Israel pia ina uhusiano mgumu na majirani zake wa ki-arabu.

Israel - pamoja na Uturuki na Iran - ni nchi zisizo za Kiarabu katika Mashariki ya Kati, na Israel haitambuliwi kama taifa na nchi nyingi katika eneo hilo.

Kati ya nchi zote za Kiarabu, ni Misri pekee tangu 1979, Jordan tangu 1994 na Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Morocco na Sudan tangu 2020 ndizo zinazolitambua taifa la Israel.

Amirah-Fernández, anasema kutotambuliwa huko na idadi kubwa ya nchi ni kutokana na ukweli kwamba "Israel inaendelea kuonekana kama mvamizi dhidi ya Waarabu-Waislamu kutokana na migogoro yake na Wapalestina."

Kabla ya kuanza vita dhidi ya Hamas Oktoba 7, 2023, Israel ilikuwa katika mazungumzo ya kurekebisha uhusiano na Saudi Arabia, ambayo ingekuwa hatua kubwa ya maendeleo kwa nchi hiyo.

Hata hivyo, siku chache baada ya shambulio hilo, iliripotiwa kuwa mamlaka ya Saudi iliitaka Marekani kusitisha mazungumzo hayo.

Wataalamu wanaamini Israel itaendelea kukosa mashirikiano na mahusiano Mashariki ya Kati, ikiwa hakuna suluhu la wazi la mzozo wake na Wapalestina.