Korea Kaskazini: Binti wa Kim Jong Un anayetajwa kama 'mrithi wake ajaye' ni nani?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Luis Barrucho
- Nafasi, BBC World Service
Binti mdogo wa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ndiye mwenye "uwezekano zaidi" wa kumrithi , kwa mujibu wa shirika la ujasusi la Korea Kusini, National Intelligence Service (NIS). Lakini je tunajua nini kuhusu Kim Ju Ae, na ni kwa kiasi gani anaweza kuchukua nafasi ya baba yake siku moja?
Kim Jong Un ni msiri sana kuhusu familia yake na ni machache machache sana yanayojulikana kuhusu familia yake.
Alimtunza kwa siri mkewe, Ri Sol Ju, kwa muda baada ya harusi yao - hakuonekana hadharani kwa mara ya kwanza hadi ilipofika mwaka 2012.
Vyombo vya habari vya Korea Kusini viliripoti kuwa walifunga ndoa mwaka 2009 na kupata mtoto mwaka 2010. Pia anafikiriwa kuwa ndiye mama wa Kim Ju Ae, ambaye alizaliwa miaka michache baadaye.
Mara ya kwanza kwa Kim Ju Ae kutajwa hadharani ilikuwa mwaka 2013, baada ya nyota wa mpira wa kikapu wa Marekani Dennis Rodman kufanya ziara ya utata nchini Korea Kaskazini.
Rodman alisema kuwa alitumia muda na familia ya Kim, akipumzika kando ya bahari na "kumpakata mtoto wao", ambaye alimuita Ju Ae.

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Hata vyombo vya habari vya Korea Kaskazini "vinamtambua kama binti wa Kim Jong Un, bila kutaja jina au umri wake", anasema Fyodor Tertitskiy, ambaye anatafiti siasa za Korea Kaskazini katika Chuo Kikuu cha Kookmin mjini Seoul. "Hakuna kitu kingine kinachojulikana, angalau kwa umma," anaongeza. Anakadiria kuwa yuko kati ya umri wa miaka 10 na miaka 13.
Katika mkutano wa faragha mwaka jana, NIS iliwaambia wanasiasa wa Korea Kusini kwamba Kim Ju Ae hakuwahi kuandikishwa katika kituo rasmi cha elimu na alikuwa akisomea nyumbani mjini Pyongyang. Iliongeza kuwa alifurahia burudani kama vile farasi, kuogelea na kuteleza kwenye barafu.
Mmoja wa watu waliohudhuria mkutano huo baadaye aliwaambia waandishi wa habari kwamba Kim Jong Un anafurahia hasa ujuzi wake wa kuendesha farasi.
NIS ilisema alikuwa na kaka mkubwa na ndugu mdogo ambaye jinsia yake haijathibitishwa. Hawajawahi kuonekana hadharani.
Kuonakana hadharani

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kim Ju Ae alijitokeza hadharani mnamo Novemba 2022 alipohudhuria jaribio la kombora na baba yake na tangu wakati huo ameonekana akiwa kando yake mara kadhaa, katika matukio ya kijeshi na yasiyo ya kijeshi.
Hivi karibuni, katika sherehe ya mkesha wa mwaka mpya katika uwanja wa Pyongyang Mei 1, yeye na baba yake walibusiana kwenye shavu.
Mwezi Disemba, walihudhuria uzinduzi wa kombora la masafa marefu la Hwasong-18 la Korea Kaskazini (ICBM), ambalo ni kombora la masafa marefu zaidi katika silaha za nchi hiyo. Pia alikuwa pamoja naye kwa uzinduzi wa satelaiti ya upelelezi ya Malligyong-1 mnamo Novemba. Pyongyang ilidai kuwa itampa Kim Jong Un mtazamo wa ikulu ya White House.
Mnamo Februari 2023 Radio Free Asia iliripoti kuwa serikali ya Korea Kaskazini ilikuwa ikiamuru mtu mwingine yeyote aitwaye Kim Jun Ae kubadilisha jina lake, ambalo lilisemekana ni la kawaida linapokuja suala la utawala wa kiimla.
Waangalizi wa Korea Kaskazini pia wanabaini kuwa Kim Ju Ae sasa anatajwa kama binti "anayeheshimika", badala ya "mpendwa". Kivumishi "kuheshimiwa" kimehifadhiwa kwa ajili ya heshima zaidi ya Korea Kaskazini.
Katika kesi ya Kim Jong Un, kwa mfano, alitajwa kama "mshirika aliyeheshimiwa" tu baada ya hadhi yake kama kiongozi ajaye kuimarishwa.

Chanzo cha picha, Reuters
Kuna uwezekano akawa mrithi ?
Korea Kaskazini imejitenga sana na haijulikani kwa ulimwengu wa na wengi wanajiuliza kwanini kuonekana kwa Kim Ju Ae karibu na baba yake imekuwa mara kwa mara.
Raia wa Korea Kaskazini wanaambiwa kuwa Kims anatoka kwenye damu takatifu, ikimaanisha tu hao ndio watu wanaweza kuongoza nchi na baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa kumtambulisha kwa umma katika umri mdogo kama huo inaweza kuwa njia ya kiongozi wa Korea Kaskazini ya kuhakikisha kuwa binti yake anajiimarisha muda mrefu kabla ya kuchukua madaraka.
Hakuna pendekezo kwamba huenda kurithishwa kwake mamlaka kukatokea wakati wowote hivi karibuni, na uvumi wa zamani kwamba Kim Jong Un alikuwa katika hali mbaya ya afya umetupiliwa mbali.

Chanzo cha picha, KCNA/EPA-EFE/REX/Shutterstock
Wengine wanasema inaweza pia kuwa njia ya Kim Jong Un kuashiria kwamba yeye ni baba anayejali familia katika jamii iliyotawaliwa na mfumo dume.
"Pamoja na viongozi wa zamani Kim Jong Il na Kim Il Sung, kulikuwa na propaganda nyingi zinazolenga jukumu la kiongozi wa Korea Kaskazini kama mtu wa mama na baba," anasema Edward Howell, mhadhiri wa siasa katika Chuo Kikuu cha Oxford na mtaalam wa rasi ya Korea. "Kwa hiyo nadhani ishara hii pia imeendelea kwa kumuonyesha na baba yake hadharani."
Tangu kuanzishwa kwa Korea Kaskazini mwaka 1948, imekuwa ikitawaliwa na wanaume wa familia ya Kim na iwapo Kim Ju Ae atamrithi baba yake, atakuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza nchi hiyo.
Lakini "kuwa na mwanafamilia wa damu ya Kim ni muhimu sana kwa uongozi wa Korea Kaskazini iwapo ni mwanamke, ni bora kuliko kuwa na mtu ambaye sio kutoka wa familia ya Kim," Howell anasema.

Chanzo cha picha, Reuters
Anaamini pia kuna mgombea mwingine anayeweza kumrithi Kim Jon Un - dada wa kiongozi huyo, Kim Yo Jong, ambaye alitajwa kwa mara ya kwanza katika vyombo vya habari vya serikali mwezi Machi 2014.
Anashikilia nafasi ya juu katika chama tawala cha Wafanyakazi wa Korea.
"Yeye ana umri mkubwa zaidi kuliko Kim Ju Ae na ni wazi ana uzoefu zaidi katika siasa za Korea Kaskazini," anasema. "Kwa hivyo iwe ni binti au dada, wanaweza kuwa wote ni wanawake, lakini kuwa na Kim ni jambo muhimu zaidi."
NIS ya Korea Kusini pia ilisema bado inafikiria "uwezekano wote" kwani kuna "mambo mengi" yanayoendelea nchini humo.

Chanzo cha picha, Reuters
Fyodor Tertitskiy anaamini kuwa Kim Jong Un amekuwa "akiujaribu umma na maoni ya wasomi kuhusu uwezekano wa kurithi" kwa kumuonyesha Kim Ju Ae hadharani - jambo ambalo anasema halifanyiki hadi pale mrithi atakapothibitishwa.
Anakiri kwamba ni mapema kuzungumzia mrithi wa Kim Jong Un.
"Kama atasema, atakufa akiwa na umri sawa na baba yake, akiwa na umri wa miaka 70, hiyo itakuwa mwaka 2054. Hata kama tunadhani kwamba taifa la Korea Kaskazini litaishi hadi wakati huo katika hali yake ya sasa, jamii huenda isiwe sawa na ilivyo sasa," anasema.
"Pia, mtu anapaswa kutambua kwamba kuna tofauti kati ya kukubali usawa wa jinsia kwa ujumla na kumkubali mtawala wa kike," anaongeza.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












