"Tunakimbia kifo tunaangukia mauti " - Mwandishi wa BBC

ds

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Njiwa akiruka juu ya vifusi vya nyumba huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza
    • Author, Adnan Albrash
    • Nafasi, BBC

Mwandishi wa BBC, Adnan al-Barash na familia yake walilazimika kuhama tena licha ya kufuata agizo la Israel kwa wakazi zaidi ya milioni moja wa kaskazini mwa Gaza kuondoka.

Familia yangu na mimi tuliondoka Jabaliya kaskazini mwa Gaza siku ya Ijumaa, Oktoba 13, baada ya Israeli kuamuru wakaazi kuhama. Israel ilitangaza eneo la kusini kuwa eneo salama, na kwa sababu hiyo, mke wangu, binti zangu wanne na mwanangu waliondoka kuelekea jiji la Khan Yunis.

Kwa sasa tuko kusini lakini nimeona moshi mwingi na kusikia milipuko. Vyanzo rasmi na walioshuhudia wananiambia nyumba zao zimeshambuliwa kwa mabomu katika mashambulizi ya anga na familia zao zimeuawa.

Pamoja na kaka yangu na familia yake, tulifanikiwa kupata nyumba ambayo tulifikiri tulikuwa salama. Watu 12 tunaishi katika vyumba viwili na choo kimoja. Hakuna maji, umeme au mahitaji mengine.

Tuliambiwa kwamba jeshi la Israel liliwasiliana na mmiliki wa jengo hilo na kumwambia watalishambulia. Inasemekana mmiliki wa jengo hilo anasakwa kwa ushirikiano wake na vuguvugu la Hamas.

Wakati wa mchana nikiwa nikirekodi ripoti ya BBC, mke wangu, familia yangu na familia ya kaka yangu walihamishwa haraka. Hawakuweza kuchukua chochote kati ya vitu tulivyokuja navyo kutoka Gaza na wakakimbia haraka bila kujua wanaelekea upande gani.

Wakati wa kutoroka kwao, jengo karibu nao na lilipigwa na kombora, lakini kwa bahati nzuri hawakujeruhiwa.

Mimi na familia yangu hatuna makao. Hatukujua pa kwenda. Nilijawa na hofu. Mtu mmoja alipendekeza twende kwenye jengo la Msalaba Mwekundu lililoko Khan Yunis kwa sababu linaweza kuwa salama, lakini lilikuwa na watu wengi sana - koridoo na vyumba vilijaa watu.

Sikujua la kufanya. Niliendelea kujiuliza ikiwa turudi nyumbani kwetu kaskazini mwa Gaza, ambako ni hatari, au tukae kusini, ambako pia si salama.

Hakuna pa kujificha

WD

Chanzo cha picha, Adnan Albrash

Maelezo ya picha, Adnan Albrash, mwandishi wa BBC
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ni kana kwamba tunakimbia kutoka kifo kimoja hadi kingine. Hakuna hata sentimita moja salama huko Gaza.

Hatukuwa na nyumba ya kulala, kwa hiyo tulilala katika uwanja wa michezo karibu na jengo la Msalaba Mwekundu. Hali ilikuwa ngumu sana.

Mke wangu, watoto wangu, watoto wa kaka yangu na mke wake walikuwa wamelala chini. Lilikuwa tukio la kutisha ambapo hatukuwa na mahali pa kujificha wala pa kujikinga.

Tuliweka vipande vya boksi kwenye sakafu na kulala. Hali ya hewa ilikuwa ya baridi sana usiku huo, watoto walipigwa na baridi kali. Tuliazima mablanketi kwa watu waliokuwa karibu ili kuwafunika watoto na sisi wenyewe tulikesha usiku kucha bila kulala.

Asubuhi iliyofuata niliamua kuchukua familia yangu na Kwenda kwa rafiki yangu ambaye yuko katika kambi ya Nusirat katikati ya Ukanda wa Gaza.

Kabla hatujafika huko, makombora kadhaa yalipiga duka la mikate karibu na kambi hiyo. Mtu aliyeshuhudia aliniambia Jeshi la Anga la Israeli lilirusha roketi hizi. Inasemekana kwamba mamia ya watu walikuwa wamepanga foleni kununua mikate kwa sababu ya ukosefu wa chakula. Watu waliuawa na eneo hilo lilikuwa la kutisha.

Vifo na Majeruhi

Wizara ya Afya ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina inasema watu 3,500 wameuawa na 12,500 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano ili kupunguza "mateso makubwa kwa binadamu".

Mashambulizi ya Israel ni jibu kwa mashambulizi ya wapiganaji wa Hamas dhidi ya Israel, ambayo yaliua watu 1,300 Oktoba 7 na kuchukua mateka 199.

Jeshi la Israel lilisema Jumanne asubuhi - limepiga vituo vya kamandi, miundombinu ya kijeshi na wapiganaji, na maficho ya Hamas huko Khan Yunis na Rafah kusini, pamoja na maeneo mawili ya kaskazini.

Lakini mimi na kwa familia yangu, sauti za ndege za kivita ni kubwa sana na inatisha. Familia yangu iko katika kambi ya Nasirat na mimi niko Khan Yunis. Sijui nitakaa wapi usiku. Kwa kweli sijui niende wapi.