Vita vya awali vinafichua nini kuhusu hatari ya shambulio la ardhini Gaza?

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israel wakiwa kwenye kifaru karibu na mpaka wa Gaza, siku mbili baada ya shambulio la Hamas dhidi ya Israel.

Israel inakusanya makumi kwa maelfu ya wanajeshi karibu na mpaka na Gaza, wakionekana kujiandaa kwa mashambulizi ya ardhini. Ikiwa vikosi hivyo vitasonga, wanajeshi wa Israel watakabiliana na wapiganaji wa Hamas ndani ya eneo la mijini lenye watu wengi.

Firas Kilani, mwandishi wa BBC wa Kiarabu, ambaye ameangazia vita vingi katika Mashariki ya Kati na kadhaa kutoka ndani ya Gaza, anaelezea athari za zinazoweza kutokea iwapo kutakuwa na vita vya ardhini ndani ya Gaza.

Miaka mitano iliyopita, nilipokuwa nikitembelea kambi ya wakimbizi ya Pwani kaskazini mwa Gaza, niliona ajali tulipokuwa tukiendesha gari. Ilionekana kana kwamba tulikuwa tukitembea juu ya daraja badala juu ardhi ya lami.

Mpiga picha aliyekuwa nami alieleza kuwa sababu ya hii ni kutokana na shughuli za uchimbaji chini ya ardhi, ili kuunda mtandao mkubwa wa mahandaki. Mahandaki yaliyochimbwa na Hamas yenye urefu wa mamia ya kilomita, na mahandaki haya huliwezesha kundi hilo lenye silaha kusafirisha kwa siri vifaa kutoka chini ya mitaa myembamba na yenye watu wengi ya Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliapa "kuiponda na kuiangamiza" Hamas baada ya kuishambulia Israel tarehe 7 Oktoba na kuua zaidi ya watu 1,400.

Vikosi vya Israel tayari vimeshafanya mashambulizi ya anga huko Gaza, na inatarajiwa kuwa hatua yao inayofuata itakuwa ni shambulio la ardhini. Hili likitokea, mahandaki haya yatakuwa sehemu muhimu ya mkakati wa mapambano wa Hamas.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mtandao wa mahandaki ya chini ya radhi uliojengwa na Hamas huko Gaza unaruhusu wapiganaji kuzunguka bila kizuizi na wanaweza kusafirisha vifaa kwa siri.

Hamas walitarajia shambulio la ardhini na hivyo kuweka akiba ya chakula, maji na silaha.

Mahandaki haya, ambayo baadhi yake yanaaminika kuenea hadi Israel, huenda yakawaruhusu wapiganaji wa vuguvugu hilo kusonga mbele bila kuzuiwa na kuvizia wanajeshi wa Israel kutoka nyuma, wanapopitia kaskazini mwa Gaza.

Israel inaamini kuwa Hamas ina wanajeshi wasiopungua elfu ishirini, waliofunzwa matumizi ya bunduki za kujiendesha, maguruneti ya kurushwa kwa roketi, na makombora ya kukinga vifaru.

Makundi mengine, kama vile vuguvugu la Palestina la Islamic Jihad na vikundi vidogo vya Kiislamu, vinaweza kuongeza idadi ya wanajeshi hao.

Historia ya hivi majuzi imeonyesha jinsi mapigano yanavyoweza kuwa hatari katika maeneo ya mijini, na nimejionea mwenyewe kile kinachoweza kutokea wakati kikosi cha kijeshi kilichofunzwa vyema kinapojaribu kuzunguka na kumkandamiza adui aliyedhamiria katika hali kama hizo.

f

Vita vya mitaani

Mnamo 2016, nilikuwa na Kikosi Maalum cha Iraqi, wakati walipokuwa wakijiandaa kushambulia mji wa Mosul.

Mamlaka ndipo iliamua kuwazingira wanamgambo hao wa Kiislamu na kuhakikisha kuwa hakuna njia ya kuwaondoa. Sera hii iliufanya mji wa Mosul kukabiliwa na hali ya kikatili na mauti.

Siku hiyo tulipoingia katika wilaya ya kwanza ya Mosul, upinzani ulioonyeshwa na wanamgambo ulikuwa wa ajabu. Walirusha kila kitu kwa msafara wetu wa Humvees za kijeshi, kutia ndani bunduki, maguruneti na roketi zilizorushwa kwa bega.

Mitego ya kulipuka iliwekwa ndani au juu ya kila kitu unachoweza kufikiria - friji na televisheni katika nyumba za watu, pamoja na stash ya dhahabu na bunduki zilizoachwa chini.

Kuchukua au kukanyaga kitu kwa makosa inamaanisha kifo.

Wanajeshi wa Israel wanaweza kukabiliwa na hatari kama hizo iwapo watahamia Ukanda wa Gaza.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mapigano kati ya jeshi la Iraq na wapiganaji wa ISIS katika mji wa Mosul yaliendelea kwa zaidi ya miezi tisa mwaka wa 2016-2017
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati wa hatua za mwisho za Vita vya Mosul, niliona kwamba wanachama wengi wa vikosi vya Iraq walianza kupoteza mwelekeo. Mapigano yalikuwa makali sana na ya hatari, wangeweza kufikiria tu juu ya kunusurika, wala hawakuweza kuhatarisha kujaribu kuwalinda raia.

Kulikuwa na aina nyingine ya hatari, wadukuzi wakiwa wamejificha ndani ya majengo na kati ya vifusi, katika jiji lote. Vikosi vya Iraq mara nyingi viliamua kutumia nguvu za anga kulipua maeneo yote ili kuwazuia kufyatua risasi.

Vikosi vya Israel vinaweza kujikuta vinakabiliwa na chaguzi mbili: ama kuchukua hatari kubwa ya kupambana na wadunguaji waliofunzwa vyema wa Hamas, au kupiga mabomu na kusawazisha majengo yote chini ili kuwazuia wavamizi wa Hamas.

Kuhusu msafara wa vikosi tulioongozana nao mjini Mosul, ulikumbwa na milipuko kadhaa ya mabomu yaliyotegwa kwenye gari, na askari watano waliokuwa pamoja nasi walikufa kutokana na mlipuko mkubwa uliofuatia mashambulizi hayo.

Mshtuko uliokuwa juu ya nyuso za wale walionusurika walipoona mabaki ya wenzao ulionekana waziwazi.

Haijulikani kuwa Hamas hutumia mabomu ya magari, lakini hapo awali ilituma washambuliaji wa kujitoa mhanga kufanya mashambulizi, na aina hii ya shambulio inaweza kuwa na athari kubwa kwa vikosi vya usalama.

Haijabainika ni muda gani mashambulizi ya ardhini huko Gaza yatadumu, lakini upinzani mkali ulioonyeshwa na ISIS huko Mosul ulilazimisha vikosi vya Iraq kupigana kwa miezi tisa kabla ya kuweza kuudhibiti mji huo.

w
Maelezo ya picha, Msafara ambao Firas alisafiri hadi Mosul ulikumbwa na milipuko kadhaa ya magari

Njia salama.

Katika mji wa Raqqa nchini Syria mwaka 2017, hali ilikuwa tofauti, kwani kundi kubwa la wapiganaji lilizingirwa katika eneo lenye watu wengi.

Lakini wakati huu, muungano unaoongozwa na vikosi vya Marekani na Wakurdi uliamua kuwapa wapiganaji hao chaguo la kuondoka.

Nimeangazia mapambano ya Wakurdi dhidi ya ISIS kwa miaka mingi, na mmoja wa viongozi wao alinipeleka kwenye mkutano wa siri na kamanda wa Marekani huko Syria.

Aliidhinisha ombi kutoka kwa viongozi wa eneo la Kiarabu la kuruhusu wapiganaji wa ISIS na familia zao kuondoka Raqqa.

Makubaliano haya yalizuia uharibifu wa mji mzima, na kusitishwa kwa mapigano na kuondoka kwa wapiganaji kulifanya idadi ya majeruhi kati ya wanajeshi na raia kuwa chini sana kuliko ilivyokuwa huko Mosul.

Siku moja baada ya wapiganaji hao kuondoka, raia waliosalia mjini walitoka katika nyumba zao wakihisi faraja kwamba wamenusurika. Waliogopa kwamba wangekufa katika shambulio kubwa katika jiji hilo.

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na muungano wa Wakurdi wa Marekani, yalizuia kuendelea kwa mapigano katika mji wa Raqqa kwa muda mrefu.

Lakini jiografia ya Ukanda wa Gaza ni tofauti, ambayo ina maana ni vigumu kuona aina hii ya makubaliano kama chaguo kati ya Israel na Hamas. Raqqa ni mji wa mbali nchini Syria, na wapiganaji wanaoruhusiwa kuondoka wanaweza kuelekea katika mashamba Jirani.

Ukanda wa Gaza ni mdogo na mwembamba ukilinganisha na Raqqa, na hakuna maeneo ya jirani ambapo wapiganaji wa Hamas wanaweza kwenda.

Uhamisho

Hapo awali, mikataba ilifanywa ambayo ilisababisha watu kuhamishwa hadi mikoa ya mbali. Mnamo 1982, Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina ilikubali kuondoka mji mkuu wa Lebanon, Beirut - baada ya kuzingirwa na vikosi vya Israeli kwa miezi mitatu - na kuhamia nchi kadhaa tofauti.

Uongozi wa PLO ulikwenda Tunisia, na wanachama wengine walipata hifadhi Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Ingawa kufikia makubaliano kama haya inaweza kuwa njia ya kuepusha mapigano zaidi na vifo vya raia huko Gaza, ni ngumu kuliona hili kuwa linawezekana kisiasa. Serikali ya Israel iliahidi kuiangamiza Hamas baada ya shambulio lake la Oktoba 7, na kuruhusu uongozi wa Hamas kutorokea nchi ya kigeni kungesababisha upinzani wa umma.

Ikiwa hakuna chaguo lingine, eneo la kaskazini la Gaza linaweza kugeuka kuwa uwanja wa vita vya umwagaji damu na vita vya mitaani kati ya Hamas na vikosi vya Israeli, na makumi ya maelfu ya raia wanaweza kukamatwa katikati ya vita hivi.