Makaburi ya kushangaza ya zama za kale yagunduliwa

Chanzo cha picha, BBC/KEVIN CHURCH
Makaburi ya ajabu ya zama za kati (miaka 1100-1500) yamepatikana huko Wales, na kuacha maswali kwa wanaakiolojia. Inaaminika ni ya karne ya 6 au 7 BK, makaburi 18 kati ya 70 yamechimbwa hadi sasa.
Baadhi ya mifupa iliyohifadhiwa vizuri huzikwa kwa njia zisizo za kawaida, na mabaki ya vitu pia yanaibuka kutoka katika eneo la makaburi.
Ingawa habari zaidi kuhusu jamii ya zamani imeanza kufichuliwa sasa, lakini kuna changamoto imejitokeza. Makaburi hayo yapo katika uwanja wa Fonman Palace, karibu na njia ya kurukia ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Cardiff.
Timu inaondoa kwa uangalifu safu ya udongo ili kufichua makaburi ambayo yako kwenye mawe kwa muda mrefu.

Chanzo cha picha, BBC/KEVIN CHURCH
Summer Courtes, mwanaakiolojia wa mifupa kutoka Chuo Kikuu cha Reading, anasema mifupa iko katika hali nzuri licha ya kuwa na umri wa miaka 1,500 hivi.
"Baadhi ya meno yake yamechakaa sana, inaweza kuashiria walitumia meno kama zana. Yawezekana walikuwa na kazi ya kusuka, kusafisha ngozi au kutengeneza vikapu. Na walikuwa wanavuta vitu kwa meno yao ya mbele."
Lakini baadhi ya mifupa yanazusha maswali - waliozikwa wamelala kwa namna tofauti. Baadhi wamelala mgongo mgongo, (mazishi ya kawaida), baadhi wamelazwa ubavu na wengine wamelazwa magoti yao yakigusana na vifua.
Wanaakiolojia hawajui hilo lina maana gani. Je, makaburi yalitumika kipindi ambacho taratibu za kuzika zilikuwa zikibadilika? Au, wengine walionekana ni tofauti na wakazikwa tofauti?

Chanzo cha picha, BBC/KEVIN CHURCH
Vitu vilivyopatikana karibu na makaburi pia vimeshangaza wataalamu. Vipande vya sahani na vikombe na mifupa ya wanyama ambao walichinjwa na kuchomwa.
Dkt. Andy Seaman, mtaalamu wa mambo ya kale katika Chuo Kikuu cha Cardiff, ambaye anaongoza timu ya uchimbaji, anasema sio kama makaburi ya kisasa, hapa hapakuwa sehemu tu ya kuzika watu, watu waliishi pia.
"Tunapofikiria makaburi, tunayafikiria kama maeneo yaliyotengwa ambayo hayawezi kufikiwa, lakini makaburi haya yanaonekana yalikuwa muhimu kwa maisha ya hao watu," anaeleza.
"Siyo tu mahali ambapo watu huzikwa, ni mahali ambapo jamii hukusanyika. Wanazika watu wao, lakini pia wanafanya shughuli za aina nyingine za kijamii kama kula, kunywa, nk."
Wakati wa kuchimba, sauti ilisikika: "Nimepata kipande cha glasi."

Chanzo cha picha, BBC/KEVIN CHURCH
Andy Seaman, anaamini glasi hiyo imetoka Bordeaux, Ufaransa. Sio kitu pekee kutoka nje. Timu ya watafiti pia imepata mabaki ya vyombo vya udongo ambavyo vinaaminika kuwa vya Afrika Kaskazini.
Tudor Davies wa Chuo Kikuu cha Cardiff anasema, "Tuna ushahidi watu hawa walikuwa na vitu vilivyoagizwa kutoka nje ambavyo vingeweza kupatikana tu kupitia biashara au kuletwa hapa na watu matajiri."

Chanzo cha picha, BBC/KEVIN CHURCH
Watu waliozikwa hapa ni akina nani?
Utafiti zaidi unahitajika ili kujua tarehe sahihi na habari zaidi kuhusu watu waliozikwa hapa zitaelezwa kupitia uchambuzi wa vinasaba DNA.
Makaburi haya yatatoa picha juu ya enzi ambayo bado hatuifahamu sana. Hata hivyo, itachukua muda mrefu kujibu maswali kuhusu watu ambao waliishi na kufa hapa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












