Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: William Ruto ashinda uchaguzi licha ya mvutano

William Ruto

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili

Mgombea wa Urais kupitia Chama cha UDA nchini Kenya William Ruto ndiye Rais mteule nchini humo.

Ruto ameibuka mshindi baada ya kumshinda mpinzani wake wa karibu Raila Amollo Odinga wa Muungano wa Azimio baada ya kupata kura 7,176,141 dhidi ya mpinzani wake mkuu aliyepata 6,942930.

Akitangaza matokeo hayo katika ukumbi wa Bomas , mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati amesema kwamba Ruto amejipatia asilimia 50.49 ya kura naye Raila akaijipatia asilimia 48.85.

Vilevile mgombea wa chama cha Roots Party George Wajackoyah alipata 69969 huku mwenzake wa chama cha Agano Waihiga Mwaure akijipatia 31987.

Ruto ametangazwa mshindi huku kukiwa na mgawanyiko baada ya mgombea wa Muungano wa Azimio Raila odinga kususia sherehe ya kumtangaza mshindi.

Makamishna wanne kati ya saba wa tume hiyo ya uchaguzi walikataa kuridhia matokeo hayo ya Urais ambayo 'hayakuwa wazi'.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akimkabidhi William Ruto cheti chake cha kushinda Uchaguzi

Akizungumnza katika hotuba yake punde baada ya kutangazwa mshindi , Bwana Ruto alisema kwamba angependa kumshukuru Mungu kwa kumfikisha katika hatua hii.

''Najua kwamba baadhi ya watu walibashiri kwamba hatutafika hapa lakini kwasababu kuna Mungu Mbinguni tumefika. Shukran zangu ziwaendee Wakenya wote''.

Awali akimtangaza mshindi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi IEBC Wafula Chebukati alisema: Tumetembea safari ya kuhakikisha kwamba Wakenya wanashiriki katika uchaguzi ulio huru na wa haki.

''Haijakuwa safari rahisi, tunapozungumza makamishna wangu wawili na Afisa mkuu mtendaji wa IEBC wamejeruhiwa'',alisema.

Ruto aipongeza tume ya uchaguzi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC Wafua Chebukati

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Urais , rais Mteule William Ruto amepongeza shughuli nzima ya uchaguzi , licha ya kwamba baadhi ya makamishna hawakuweza kushiriki katika matangazo rasmi.

Ruto amesema kwamba anataka kuwa rais wa wote ili taifa liendelee kuangazia siku zijazo.

Kwa wale waliotukosea , nataka kuwaambia hakuna cha kuogopa, hatutalipiza kisasi, hatuna muda wa kuangalia nyuma, aliongezea.

Hii ni mara ya kwanza kwa bwana Ruto , 55, kuwania kiti cha Urais.

Alihudumu kama makamu wa raia kwa kipindi cha miaka kumi , lakini hatahivyo walitofautiana na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alimuunga mkono bwana Raila Odinga kumrithi.

Raila Odinga ambaye ni waziri mkuu wa zamani , 77, alikuwa akiwania kiti cha Urais kwa mara ya tano.

.

Pia unawezakusoma:

.