Kenya yajiondoa katika kusikilizwa kwa mzozo wake wa majini na Somalia

Garsoorayaasha maxkamada ICJ

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Majaji wa mahakama ya ICJ

Kenya imejiondoa katika kikao cha kusikilizwa kwa kesi ya mzozo wa mpaka wa majini kati yake na Somalia katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), vyanzo vya serikali vimezungumza na BBC.

Kenya inaishutumu Mahakama ya Kimataifa ya ICJ, kwa kuwa na upendeleo kuhusu suala la umiliki wa eneo lenye ukumbwa wa kilomita za mraba 160,000 katika bahari Hindi.

Inasemekana kuwa eneo hilo lina utajiri wa mafuta na gesi.

Suala hilo ndio kitovu cha mzozo wa kidiplomasia ambao umeghubika nchi hizo jirani.

Kenya imetaka kesi hiyo icheleweshwe kusikilizwa wakati inazungumza na timu yake ya wanasheria na pia imeangazia janga la corona lakini mahakama ya ICJ imesema kuwa kesi hiyo inaanza kusikilizwa Jumatatu kwa njia ya mtandao.

Kenya pia inasema kwamba katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuna jaji raia wa Somali ikidai kwamba kwanza jaji huyo ajiondoe.

Somalia iliwasilisha kesi hiyo mwaka 2014, ikisema mpaka wa majini unastahili kufuata mpaka ya ardhini huku Kenya ikidai kuwa tangu mwanzo imekuwa ikichukua mkondo wa mstari wa usawa, umbo la pembe tatu kutoka wakati ambapo nchi hizo mbili zilikutana eneo la pwani.

Timu ya wanasheria wa Kenya pia inataka kuwasiliana na mahakama ya ICJ kwa dakika 30 Jumatatu kabla ya kuanza kusikilizwa rasmi kwa kesi hiyo.

Somalia pia nayo imeishutumu Kenya kwa kuingilia masuala yake ya ndani kwa kuunga mkono utawala wa eneo la Jubbaland dhidi ya serikali.

Hata hivyo nchi hizo mbili ni washirika katika vita dhidi ya kundi la wanamgambo wa Al-Shabab, ambalo linadhibiti maeneo ya vijijini ya Somalia na limetekeleza mashambulizi kadhaa nchini Kenya.

Kwanini Kenya imejiondoa ghafla katika kikao cha kusikilizwa kwa kesi hiyo?

Man looking towards the sea on March 4, 2011 in Lamu, Kenya.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Eneo linalozozaniwa na Kenya na Somalia linasemekana kuwa na utajiri wa mafuta na gesi

Kenya imejiondoa katika kusikilizwa kwa mzozo kati yake na Somalia, ofisi ya mwendesha mashtaka imezungumza na BBC.

Kulingana na vyombo vya habari, serikali inafikiria kuwasilisha malalamishi yake kwamba mahakama hiyo haitendei Kenya haki na pia imekataa kusikiliza maombi ya Kenya ya kuahirisha kusikilizwa kwa kesi hiyo kwasababu ya janga la virusi vya corona.

Mwanasheria Mkuu Kenya, Kariuki Kihara aliwasilisha matakwa yao wiki iliyopita katika Mahakama hiyo siku chache kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Hata hivyo kesi hiyo ya mzozo wa mpaka wa majini kati ya Kenya na Somalia imepangwa kuanza kusikilizwa Jumatatu.

Uamuzi huo pia unawadia wakati ambapo uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili umezorota.

Mengine ambayo Kenya inalalamikia

Kenya Somalia border

Serikali ya Kenya pia imeonesha kuwa inatilia shaka uaminifu na uwezo wa mahakama hiyo kutopendelea upande wowote hasa kwa kuwepo kwa jaji Abdulqawi Ahmed Yusuf, raia wa Somali wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Bwana Kariuki aliongeza kuwa kesi ya Kenya inahusisha mawakili wake kutoa hoja zao na haiwezi kusikilizwa kupitia njia ya sauti au video ikidai kuwa njia hizo "sio stahiki" katika kesi yenye uzito mkubwa na muhimu kama hiyo.

Mwanasheria wa Kenya pia amesema katika taarifa kwa mahakama hiyo kuwa Kenya imetafuta mawakili wapya ambao hawajakutana kujifahamisha suala hilo kwa undani, kwasababu ya ugonjwa wa virusi vya corona na kwamba Kenya haikuwa imejitayarisha vilivyo katika kesi hiyo.

Serikali ya Kenya iliwapiga kalamu mawakili walioiwakilisha nchi yake katika kesi hiyo mwaka 2019 na kuwakosoa kwa namna walivyoiwakilisha.

Mara nyingi mahakama hiyo hutegemea Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhakikisha maamuzi yake yana heshimiwa na sasa hivi Kenya ni mwanachama asiyewakudumu wa Baraza hilo.