Mgogoro kati ya Kenya na Somalia: Uhusiano unaoundwa kati ya Kenya na Somaliland una maana gani?

Chanzo cha picha, Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni Kenya/twitter
- Author, Mohammed AbdulRahman
- Nafasi, Mchambuzi
Kenya na Somalia zimeingia katika mvutano wa kibalozi kutokana na kile Somalia inachodai ni kuingiliwa katika mambo yake ya ndani, kutokana na uhusiano wa Kenya na jimbo la Jubaland. Madai ambayo Kenya na Jubaland zimeyakanusha. Katikati ya mwezi huu, Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmaajo akatangaza kuuvunja uhusiano na jirani yake Kenya.
Mvutano huu ulipamba moto zaidi kufuatia ziara ya siku mjini Nairobi ya Rais Musa Bihi Abdi wa eneo lililojitenga miongo mitatu sasa na kujiita Jamhuri ya Somaliland na kuanzishwa uhusiano mpya kati ya pande hizo mbili ikiwa ni pamoja na Kenya kutangaza itafungua ofisi ya ubalozi mdogo mjini Hargeisa .
Historia inajirudia
Itakumbukwa mara baada ya uhuru 1963 Kenya ilipigana vita na kundi la waasi wa Kisomali lililojulikana kama "Shifta", lililokuwa likidai eneo la Kaskazini Mashariki ya Kenya lenye wakazi wengi wenye asili ya Kisomali, ili liunganishwe na Somalia.
Sambamba na hayo, utawala wa mwanajeshi Mohamed Siad Barre, ulipalilia hisia za kuwepo kwa Somalia iliokubwa. Ncha tano kwenye nyota ziliomo katika bendera yake zimekuwa zikitajwa kuwakilisha maeneo yanayokaliwa na wenye asili ya Kisomali.

Chanzo cha picha, Getty Images
Maeneo hayo ni Djibouti, Mkoa wa Kaskazini Mashariki ya Kenya na kusini mwa Somalia. Vita vya Shifta vilimalizika 1967 kwa kusainiwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Serikali kuu mjini Mogadishu imedai kwamba Kenya inajiingiza kwenye masuala yake ya ndani. Hoja inayotoa ni kwamba imekuwa na ushawishi mkubwa kwa Rais wa Jubaland Ahmed Mohamed Islam ikiwa na lengo la kuendeleza masilahi yake ya kisiasa na kiuchumi ndani ya Somalia.
Madai hayo yamekanushwa na pande zote mbili, Kenya na serikali ya mkoa huo. Mvutano kati ya Jubaland na serikali ya Shirikisho ulipamba moto baada ya Farmajo kulikataa ombi la Islam kumtaka awaondowe wanajeshi wa Somalia katika jimbo hilo.
Kwanini uhusiano na Somaliland?
Kenya inaiangalia Somaliland kuwa mshirika muhimu katika Pembe ya Afrika katika vita dhidi ya magaidi wa Al Shabab. Pia usalama uliopo Somaliland ambayo tokea ilipotangaza kujitenga na Somalia 1991 baada ya kuangushwa utawala wa Mohamed Siad Barre ni muhimu katika kukuza biashara na vitega uchumi.

Chanzo cha picha, Wizara ya masuala ya nchi za kigeni Kenya
Umuhimu huo umejitokeza zaidi tangu miaka miwili iliopita kufuatia hali mpya ya maelewano baina ya Ethiopia na Eritrea ,Eritrea na Djibuti na pia Somalia. Mabadiliko yaliojiri kutokana na juhudi za Waziri mkuu wa Ethiopia Dr Abiy Ahmed tangu alipoingia madarakani 2018.
Kenya ni mshirika wa kutegemewa katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Mashariki na Pembe ya Afrika ( IGAD), ambapo nchi zote hizo pamoja na Uganda na Sudan Kusini ni wanachama .
Ziara ya hivi karibuni mjini Nairobi ya Rais Musa Abdi Bihi wa Somaliland na mazungumzo yake na Rais Uhuru Kenyatta, imesababisha hasira zaidi upande wa Somalia. Jumuiya ya kimataifa na Somalia zinaitambua Somaliland kuwa sehemu ya Shirikisho la Somalia.
Lakini bila shaka Bihi atakuwa akiyaangalia matukio ya ziara yake mjini Nairobi kuwa ni mafanikio ya kidiplomasia kwa Somaliland ambayo kwa muda mrefu inapigania itambuliwe kama nchi huru. Kubwa katika mafanikio hayo ni matamshi ya mjumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Afrika anayehusika na miundombinu, Raila Odinga.
Mwanasiasa huyo mkongwe Waziri mkuu wa zamani wa Kenya, ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa akitaka iharakishe mchakato wa kuitambua Somaliland kama nchi huru. Somaliland imeweza kuunda taasisi za kiutawala licha ya mivutano baina ya vyama vya kisiasa kuhusu uchaguzi wa bunge.
Uchaguzi umeahirishwa mara kadhaa tokeo ulipofanyika ule wa mwisho 2005. Kimsingi kuna makubaliano ya chaguzi za bunge na serikali za mitaa zifanyike 2021.
Jumuiya ya Kimataifa na dola huru ya Somaliland
Licha ya kutokuwa na uhusiano rasmi wa kibalozi na nchi za nje na Jumuiya ya Kimataifa, ina mahusiano katika ngazi isiyo rasmi na baadhi ya nchi zikiwemo Ethiopia na Misri pamoja na taasisi za kimataifa zisizokuwa za kiserikali.

Chanzo cha picha, Ikulu ya rais Kenya
Baadhi ya duru za kisiasa zinaashiria wakati umewadia kuitambua Somaliland zikiamini ni hatua itakayosaidia kupatikana suluhisho la kisiasa lililo imara na la kudumu Somalia.
Swali linaloulizwa ni kwasababu gani Jumuiya ya kimataifa inasita kuitambua Somaliland wakati ilishinikiza Sudan Kusini ipewe haki ya kujiamulia mustakbali wake yenyewe?

Chanzo cha picha, Ikulu ya rais Kenya
Kufuatia uamuzi wake katika kura ya maoni kujitenga na jirani yake wa kaskazini, lilizaliwa taifa changa huru na kuwa mwanachama wa 54 Umoja wa Afrika. Ni wazi Shinikizo lilitokana na masilahi ya kiuchumi, utajiri wa mafuta .
Wadadisi wanaamini kuitambua Somaliland kutasaidia kuimarisha usalama na maendeleo katika Pembe ya Afrika na pia kuwapa haki wakaazi wa eneo hilo la Somalia kujiamulia mustakbali wao.
Mwaka ujao 2021, Kenya inajiandaa kukalia kiti chake cha mjumbe asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka miwili, na huenda Somaliland ikatarajia uungaji mkono mkubwa wa Kenya katika kampeni yake ya kutambuliwa kimataifa kama dola huru.
Katika wakati huu ambapo uhusiano wa Kenya na Somalia ni tete, Farmaajo binafsi anakabiliwa na changamoto nyumbani kuelekea uchaguzi wa bunge. Anashutumiwa kwamba anajaribu kuchelewesha uchaguzi wa bunge, ili mkakati wake umsaidie aweze kuchaguliwe tena 2021.
Tayari mvutano kuhusu muundo wa Tume ya Uchaguzi umesababisha kushindwa kufanyika uchaguzi uliopangwa mwezi huu. Farmaajo anaweza kuutumia uamuzi wa kuyarundika majeshi yake katika mpaka na Kenya kama kisingizio kimoja wapo cha kuahirisha uchaguzi ili abakie madarakani.
Tangu 1991 baada ya kuanguka kwa utawala wa Siad Barre, taifa hilo liliingia kwenye vurugu huku wapiganaji wa koo mbali mbali nchini Somalia, wababe wa kivita, wanamgambo waliowania kujitenga na makundi ya kidini, wakipigana baina yao.
Ikitambua kwamba usalama wa Somalia ni muhimu kwa usalama wake binafsi Kenya imekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuleta suluhisho. Ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa wawakilishi wa makundi hayo waliopiga kambi mjini Nairobi kwa kipindi kirefu kutafuta suluhisho.

Chanzo cha picha, Ikulu ya rais Kenyatta/twitter
Mazungumzo yao yaliyodhaminiwa na Umoja wa Afrika , Jumuiya ya nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa .
Baada ya vuta nikuvute hatimaye mwaka 2004 makundi hayo yalikubaliana kuunda serikali ya mpito ingawa hadi leo yameshindwa kuwa na serikali imara.
Uwepo wa wanajeshi wa Kenya nchini Somalia
Kinachosubiri ni nini kitafuata baada ya Farmaajo kuamua kuvunja uhusiano na Kenya na hasa kuendelea kuwepo kwa wanajeshi wa Kenya nchini Somalia ?
Kenya ni sehemu ya kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM), ikiwa na wanajeshi zaidi ya 3,600 ,wengi wao wako katika mkoa wa Jubaland ambao mji wake mkuu ni Kismayo.
Hilo ni eneo ambalo ni kitovu cha harakati za wapiganaji wa kundi la kigaidi la Waislamu wa itikadi kali la Al Shabab wenye mafungamano na mtandao wa Al Qaeda.
Mgogoro huu wa Somalia na Kenya unaashiria umuhimu haja ya Kenya kuendelea na harakati zake za kijeshi Somalia, kwani hali yoyote ya usalama katika mipaka yake ndiyo kipaumbele.












