Je, Kukatizwa kwa uhusiano wa kiplomasia kati ya Kenya na Somalia kuna maana gani?

- Author, Hezron Mogambi
- Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi
Tangazo la kukatizwa kwa uhusiano wa kiplomasia kati ya Kenya na Somalia kulikotokea juma hili kumesababishwa na mambo kadhaa ambayo yana athari nyingi katika eneo zima.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa waziri wa habari wa Somalia, nchi yake iliamua kusitisha uhusiano wa kiplomasia kati ya nchi hizi mbili kwa sababu "Kenya ilikuwa imeingilia uhuru wa taifa la Somalia."
Waziri Osman Dubbe alieleza kuwa Somalia ingewaita wawakilishi wake wote kutoka Kenya na kuwapa wawakilishi wa Kenya nchini Somalia siku saba kuondoka.
"Jamhuri ya muungano ya Somalia imefikia uamuzi huu kwa nia ya kuijibu Kenya kwasababu ilienda kinyume na makubaliano na kuingilia masuala ya ndani ya nchi ya Somalia," Bw. Dubbe alieleza.
"Serikali ya Kenya sasa inafanya juhudi za kugawa nchi ya Somalia kuwa nchi mbili ilhali tuna uhusiano mkubwa kati yetu."
Athari za kukatiza uhusiano
Hatua hii ya kukatiza uhusiano kati ya nchi hizi mbili jirani na zenye umuhimu katika ukanda huu huenda ikaongeza tishio la ukosefu wa usalama ikikumbukwa kwamba Marekani ilitangaza kuondoa wanajeshi wake ambao wamekuwa nchini Somalia kwa miaka mingi -hatua ambayo wadadisi wengi wa usalama kwenye eneo hili wanasema huenda ikahamasisha kundi la kigaidi la Al-Shaabab kuongeza juhudi zake za kutatiza usalama zaidi.
Kilicho bayana ni kuwa hatua hii haijatokea ghafla bin vuu.
Uhusiano kati ya nchi hizi mbili jirani umekuwa ukidorora katika miaka ya hivi karibuni nayo hatua hii ikichukuliwa na Somalia siku moja tu baada ya Kenya kuwa mwenyeji wa rais wa Somaliland, eneo la kaskazini magharibi ambalo lilijitangazia uhuru kutoka kwa Somalia mwaka wa 1991.

Pia ikumbukwe kwamba hii si mara ya kwanza ambapo kumekuwa na uhasama kati ya Mogadishu na Nairobi.
Itakumbukwa kwamba mwaka 2019 Kenya ilimrejesha balozi wake baada ya Mogadishu kuamua kunadi maeneo ya gesi na mafuta katika mzozo wa kimaeneo.
Nchi hizi mbili zilirejesha uhusiano miezi michache baadaye.
Huku eneo hili likiwa halijatambuliwa kimataifa, eneo la Somaliland limekuwa na amani ikilinganishwa na maeneo mengine ya Somalia huku eneo hili likiwa limejiundia jeshi lake, usimamizi wake, na mfumo wa kifedha.

Akiwa Kenya, kiongozi wa Somaliland, Muse Bihi na Rais Kenyatta walikubaliana kwamba nchi ya Kenya itafungua ubalozi mdogo katika mji mkuu wa Somaliland, Hargeisa kufikia Machi huku shirika la ndege la Kenya Airways na mashirika mengine ya ndege ya Kenya yakianzisha safari za moja kwa moja kati ya Nairobi na Hargeisa.
Eneo la Jubaland
Pia, kuna uhasama kati ya serikali kuu ya Somalia na eneo la Jubaland, ambayo inapakana na Kenya, ambapo wasimamizi wa eneo hili wanaishutumu serikali ya Mogadishu kwa kupanga njama ya kumwondoa Rais Ahmed Madobe na kumweka mtu mwingine wanayemtaka ili kuendelea uongozi wao katika sehemu hii inayojisimamia.
Rais Madobe ni mshirika wa Kenya, ambayo inaliona eneo la Jubaland kama sehemu inayosaidia kuzuia mashambulizi ya kigaidi ya kundi la Al-Shabaab ambao wamekuwa wakifanya mashambulizi nchini Kenya.
Kenya pia imejipata ikishutumiwa na Somalia kwa kudaiwa kumficha mtoro muhimu ambaye alikuwa waziri kule Jubaland ambaye alikuwa ameshikwa na Mogadishu kwa "makosa mabaya ya jinai" lakini akatoroka kutoka jela January mwaka huu.
Pia, Somalia imeishutumu Kenya kwa kuingilia kampeini za kisiasa zinazoendelea nchini humo huku uchaguzi ukiwa umepangiwa kufanyika mwishini mwa mwezi huu kama njia ya kujizatiti kama nchi kustawisha mfumo wake wa kidemokrasia na kuondoka katika madaraka.
Kujibu madai haya, serikali ya Kenya ilisema kwamba itaunda kamati ili kuyashughulikia madai haya ya Somalia na kusaidia kutatua tofauti zilizopo kati ya nchi hizi mbili.
Changamoto za nchi ya Somalia

Nchi ya Somalia tayari inakumbwa na changamoto nyingi— mafuriko, viwavi na janga la Covid-19 — na Jumanne tu, makundi ya upinzani na waungaji mkono wao walipigana na polisi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu wakianzisha maandamano yenye nia ya kuisukuma serikali kuhakikisha kwamba kura itakapopigwa itakuwa kwenye misingi ya haki.
Waandamanaji mjini Mogadishu walimshutumu Rais Mohamed Abdullahi Mohamed - anayejulikana kwa jina la utani "Farmaajo" - kuhusiana na kucheleweshwa kwa uchaguzi uliocheleweshwa wa maeneo bunge.
Uchaguzi huo ulipaswa kufanyika mwanzani mwa mwezi huu lakini kukatokea matatizo kuhusiana na watakaosimamia bodi ya uchaguzi.

Matatizo katika uhusiano kati ya Kenya na Somalia hayajaanza siku za hivi karibuni bali yamekuwepo hata tangu enzi za kikoloni. Matatizo haya yamejumuisha uhusiano mbaya na vita kati ya koo mpakani, mashambulizi ya kigaidi, mauaji ya jumuia kama ilivyofanyika katika mauaji ya Wagalla mwaka 1984 na mauaji katia chuo kikuu cha Garrissa ya mwaka wa 2015.
Itakumbukwa kwamba mwaka wa 2011, Operation Linda Nchi ilianzishwa kati ya majeshi ya Kenya na majeshi ya Somalia dhidi ya kundi la Al-Shabaab.
Baadhi ya Wakenya wamejiunga na kundi haramu la Al-Shabaab kwa sababu ya hali ya umaskini na sababu nyinginezo katika maeneo ya Mombasa na kaskazini mwa Kenya.
Hali hii imekuwa ikiisumbua nchi ya Kenya kwa muda kwa sababu ya mashambulizi ya kundi la Al-Shaabab na hasara na vifo vitokanavyo.
Pia, kuna mzozano ambapo kesi iko mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki(International Court of Justice) kuhusiana na mpaka kati ya nchi hizi mbili ambapo Kenya inadai kwamba sehemu fulani ya bahari Hindi ni yake ilhali Somalia inadai ni sehemu ya nchi hiyo ambako kunasemekana kuwa na mafuta na gesi yenye dhamana kubwa.

Chanzo cha picha, International Court of Justice)
Ukweli kwamba Kenya inachangia vikosi vya kijeshi nchini Somalia kama sehemu ya kikosi cha kudumisha amani kinachoongozwa na Umoja wa Mataifa ambacho, pamoja na serikali ya Somalia, kinapigana na kundi la wanamgambo waliojihami la al-Shabaab linalohusishwa na al-Qaeda unaweza kutatiza mambo mengi iwapo uhusiano huu utakatizwa kwa muda mrefu.
Pia, ikumbukwe kwamba majeshi ya Marekani yanapondoka kama ambayo serikali ya nchi hiyo imeitisha, basi mwanya itapatikana kwa makundi ya kigaidi ambayo yatatatiza usalama katika ukanda mzima na kuleta hasara kubwa.
Isisahaulike kwamba nchi ya Kenya ilichaguliwa kuchukua kiti kinacholiwakilisha bara la Afrika katika Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa Juni na kwa sadfa au mpango, mwakilishi mpya wa Kenya kwenye umoja huo ni balozi Martin Kimani.
Kabla ya kuteuliwa kwake Bw. Kimani amekuwa akifanya kazi kama balozi maalum kushughulikia masuala ya ugaidi na alikuwa mkurugenzi wa kituo cha Kenya kuhusiana na mapambano dhidi ya ugaidi tangu mwaka wa 2015.








