Machafuko yaliyoshuhudiwa Tanzania yalichochewa kutoka nje- Waziri Mkuu

Chanzo cha picha, Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri mkuu wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba amesema kuwa machafuko yaliyoshuhudiwa nchini humo wakati wa uchaguzi mkuu, yalichochewa kutoka nje.
Akiongea jijini Dar es Salaam, Nchemba alisema kuwa waliopanga machafuko hayo wanadhamira ya kupora rasilimali zake.
Serikali ya Tanzania, imedai kuwa maandamano yaliyosababisha maafa mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya taifa hilo, yalipangwa na kudhaminiwa na watu wenye nia mbaya na maslahi ya taifa hilo.
Akiongea wakati alipofanya ziara jijini Dar es Salaam kukagua uharibifu uliosababishwa na maandamano ya tarehe 29 mwezi uliopita Nchemba amedai kuwa wale waliofadhili ghasia na machafuko hayo wana njama ya kuvuruga amani na usalama wa taifa hilo ili wapore madini yake.
Nchemba alisema kuwa maandamano hayo yalikuwa na athari kubwa sio tu kwa miundombinu bali hata kwa maisha ya watu ambao walikufa au kujeruhiwa.
Alisema kuwa Tume iliyoundwa na rais Samia Hassan, itasaidia kubainisha chanzo cha maandamano hayo ili suluhu la kudumu lipatikane.
Tanzania haijatoa takwimu kuhusu idadi ya watu waliouawa au kujeruhiwa. Wakati huohuo serikali ya Tanzania imetangaza kuwa hakutakuwa na sherehe yoyote tarehe 9 mwezi ujao, na badala yake fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya sherehe hizo zitatumika katika kurekebisha miundombinu iliyoharaibiwa wakati wa maandamano hayo.
Wafuasi wa upinzani walikuwa wamedai kuwa watafanya maandamano makubwa zaidi tarehe 9 mwezi ujao, kuendeleza shinikizo dhidi ya utawala wa sasa, licha ya idara ya polisi kuonya kuwa maandamano yoyote hayataruhusiwa.
Unaweza kusoma;
















