Mohamed Salah, au "Mfalme wa Misri": Ni vipi mvulana mdogo akawa "nembo ya taifa"?

.
Maelezo ya picha, Mohamed Salah
    • Author, John Bennett
    • Nafasi, BBC News kutoka Cairo
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

"Kila ninapoingia hapa, siwezi kujizuia kumkumbuka namna alivyotembea, alivyotawala mpira. Lilikuwa jambo la kipekee kabisa; tofauti na lolote nililowahi kuona."

Hayo ni maneno ya mmoja wa makocha wa kwanza waliogundua kipaji cha mchezaji Mmisri, Mohamed Salah, akiwasimulia waandishi huku akisimama mbele ya lango jipya la kijani kibichi la Kituo cha Vijana cha Kijiji cha Nagrig.

Katika kijiji hiki cha Nagrig, kilichoko takribani saa tatu kufika kaskazini mwa mji mkuu wa Cairo, ndipo historia ya mmoja wa washambuliaji mahiri zaidi duniani ilipoanzia.

Salah ndiye aliyewezesha klabu ya Liverpool kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) mwezi Mei 2025.

Mitaani mwa Nagrig, Salah alianza kucheza soka akiwa na umri wa miaka saba, akiigiza mashujaa wake wa utotoni: mshambuliaji wa Kibrazili Ronaldo, kiungo fundi wa Kifaransa Zinedine Zidane, na gwiji wa Kiitaliano Francesco Totti.

"Mohamed alikuwa mdogo kimwili ikilinganishwa na wachezaji wenzake, lakini aliweza kufanya mambo ambayo hata wavulana wakubwa hawakuweza kufanya," anasema kocha wa kwanza wa Salah, Ghamry Abdel Hamid El-Saadani, akionyesha uwanja wa nyasi bandia uliopewa jina kwa heshima yake.

Pia unaweza kusoma:

"Mohamed alikuwa mdogo kimwili ikilinganishwa na wachezaji wenzake, lakini aliweza kufanya mambo ambayo hata wavulana wakubwa hawakuweza kufanya," anasema kocha wa kwanza wa Salah, Ghamry Abdel Hamid El-Saadani, akionyesha uwanja wa nyasi bandia uliopewa jina kwa heshima yake.

Salah, mwenye umri wa miaka 33, anakaribia kuanza msimu wake wa tisa akiwa na Liverpool kama winga na amefunga mabao 245 katika mechi 402 za ligi na vikombe tangu ajiunge na klabu hiyo mwaka 2017.

Mashabiki wa timu ya taifa ya Misri wameshikilia picha za "Mfalme wa Misri" Mohamed Salah kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika 2019.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nyota wa kwanza wa Misri kung'ara katika soka la kimataifa, Mohamed Salah, ametwaa mataji yote ya ndani akiwa na klabu ya Liverpool, pamoja na ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (Champions League).

Hata hivyo, bado hajafanikiwa kutwaa taji akiwa na timu ya taifa ya Misri.

Kwa kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) linatarajiwa kufanyika Desemba 2025, na Kombe la Dunia mwaka 2026, BBC Sport ilizuru Misri kuchunguza maana halisi ya Salah kwa taifa hili lenye watu milioni 115 wanaopenda soka kwa moyo wote na jinsi kijana kutoka familia ya kawaida alivyoibuka kuwa almasi ya taifa.

"Nakumbuka furaha ya baba yangu kila tulipomtazama Salah," anasema Lamis El-Sadig, akiwa katika Dentist Café, eneo la mashariki mwa Cairo.

"Baada ya Salah kujiunga na Liverpool, baba yangu na mimi tulikuwa hatukosi mechi yoyote kwenye runinga."

Kahawa hiyo maarufu, iliyopewa jina kutokana na taaluma ya awali ya mmiliki wake daktari wa meno imekuwa kitovu cha mashabiki wa Liverpool wanaokusanyika kutazama mechi kwenye skrini kubwa.

Lamis, akiwa amevaa jezi ya Liverpool yenye jina la baba yake mgongoni, anasema kwa hisia:

"Kwa masikitiko, alifariki miaka miwili iliyopita."

Anakumbuka:

"Kila wiki, tulikuwa na saa mbili za furaha zaidi nyumbani wakati wa mechi za Liverpool. Na hata nilipokuwa shule au kazini, baba alikuwa akinitumia ujumbe kunieleza kinachoendelea."

Lamis anaeleza kuwa Salah hakukulia katika familia yenye uwezo mkubwa:

"Lakini alijituma mno na kujinyima sana hadi kufikia mafanikio haya. Wengi wetu tunajitambua kupitia yeye''.

"Watoto wote wanataka kuwa kama Salah"

GG

Chanzo cha picha, BBC Sport

Nagrig ni kijiji kidogo cha kilimo kaskazini mwa Misri, kilichojaa mashamba ya jasmini na tikiti maji.

Barabarani, magari, pikipiki, mikokoteni na wanyama hutumia njia moja.

Hapa ndipo Mohamed Salah, anayejulikana kama "Mfalme wa Misri," alikulia.

"Familia ya Salah ndiyo msingi na siri ya mafanikio yake," anasema El-Saadani, kocha wake wa kwanza, aliyemlea tangu akiwa na umri wa miaka minane.

"Wanaishi hapa kwa unyenyekevu na heshima, watu wanawapenda sana."

Kituo cha Vijana cha Nagrig kimekarabatiwa kwa heshima ya Salah, na sasa uwanja wake unafanana na wa mazoezi ya wachezaji wa kulipwa.

"Familia ya Salah ilijitolea sana kwa ajili yake hasa baba na mjomba wake," anasema El-Saadani, akiwa karibu na bango la Salah na Kombe la Ligi ya Mabingwa.

Mitaani, watoto wamevalia jezi za Liverpool na Misri zenye jina lake.

Nje ya shule yake ya zamani kuna picha ya ukutani, na tuk-tuk hupita kwa kasi huku likiwa na bango la uso wake.

Kijijini humo bado kuna kinyozi aliyekuwa akikata nywele za Salah alipokuwa kijana.

"Mimi ndiye niliyempa nywele za msokoto na ndevu," anasema Ahmed Al-Masry.

"Marafiki walimshauri asinyoe kijijini, lakini aliendelea kuja kwangu. Kesho yake, walimuuliza: 'Kinyozi wako ni nani?'"hii ni kutokana na utanashati aliokuwa nao.

Kinyozi wa kijiji anakumbuka ustadi wa Salah katika soka, alipokuwa akicheza katika Kituo cha Vijana na mitaani mwa Nagrig.

GG

Chanzo cha picha, BBC Sport

Anaongeza:

"Kumbukumbu yangu kuu ni tulipokuwa tukicheza PlayStation. Salah kila mara alichagua Liverpool. Wengine walichagua Manchester United au Barcelona, lakini kwake ilikuwa Liverpool tu. Sasa hivi, watoto wote wadogo wa kijijini wanataka kuwa kama yeye."

Salah alipata mafunzo rasmi ya soka kwa miaka sita katika klabu ya El Mokawloon El Arab, yenye makao yake mjini Cairo, maarufu pia kama El Mokawloon.

Aliijiunga na klabu hiyo akiwa na umri wa miaka 14, na safari yake ya kucheza kandanda huku akiendelea na masomo iligeuka kuwa hadithi ya kipekee, si tu nchini Misri bali hata kimataifa.

Safari ngumu ni siri ya nguvu zake

GG

Chanzo cha picha, BBC Sport

Katika gari dogo la abiria aina ya Suzuki lijulikanalo kama "tonaya" lililosimama pembezoni mwa kijiji cha Nagrig, abiria wanangoja kwa wasiwasi.

Safari haiwezi kuanza hadi gari lijazwe.

Hapa ndipo safari ya kila siku ya Mohamed Salah kuelekea mazoezini ilipoanzia akiwa kijana.

"Ilikuwa safari ngumu na ya gharama kubwa," asema El-Saadany, kocha wake wa kwanza.

"Alisafiri peke yake mara nyingi. Fikiria mtoto anaondoka saa 4 asubuhi na kurudi saa 6 usiku. Safari hii ilihitaji mtu mwenye nguvu na malengo ya kweli," aliongeza.

Safari ya Salah ilikuwa kupitia Basyoun, kisha Tanta, hadi Kituo cha Ramses jijini Cairo, ambako alibadilisha tena usafiri kufika klabuni kwa mazoezi.

Baada ya mazoezi jioni, alianza safari ndefu ya kurudi kijijini kupitia njia ile ile.

GG

Chanzo cha picha, BBC Sport

Safari yetu fupi hadi Basyoun ilikuwa ngumu kutokana na joto kali na hali mbaya ndani ya basi, hivyo unaweza kufikiria jinsi Salah alivyovumilia safari ndefu kama hizi mara kwa mara alipokuwa kijana.

Hany Ramzy, aliyewahi kucheza katika timu ya taifa ya Misri na ligi ya Ujerumani, anaamini kuwa hali hizi ngumu zilimjenga Salah kuwa na akili ya ushindani na mafanikio.

"Kuanza soka nchini Misri ni vigumu sana," anasema Ramzy, ambaye alimpa Salah nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa mwaka 2011, na pia alimfundisha kwenye Olimpiki za London 2012.

"Nami nilitembea kilomita kadhaa kwenda mazoezini, na baba hakuweza kuninunulia viatu vya mpira," anakumbuka Ramzy.

"Ufanisi wa Salah unatokana na maisha haya magumu hali hizi humjenga mchezaji kuwa imara."

GG

Chanzo cha picha, BBC Sport

"Usiwe Beki!"

Kapteni Diaa, aliyemfundisha Salah katika timu ya taifa ya vijana ya Misri kwenye Kombe la Dunia la U-20 mwaka 2011 huko Colombia, anakumbuka changamoto walizopitia:

"Wakati huo kulikuwa na mapinduzi nchini, maandalizi yalikuwa magumu sana," anasema.

Anamkumbuka Salah kama kijana mwenye kasi na umakini wa hali ya juu:

"Alikuwa msikivu, hakujibizana, alisikiliza na kufanya kazi. Anastahili kila alichofikia."

Diaa alimtaka Salah asishuke hadi katika safu ya ulinzi, bali aelekeze nguvu kwenye mashambulizi.

Anakumbuka kwa kucheka:

"Katika mechi dhidi ya Argentina, alisababisha penalti kwa kurudi kutetea. Nilimwambia: 'Huwezi kuwa beki! Kaa mbele!'"

Baadaye, Salah alisema kocha wa Liverpool, Arne Slot, alimwambia asirudi katika eneo la safu ya ulinzi"Lakini mimi ndiye niliyemwambia hivyo kwanza!" asema Kapteni Diaa kwa tabasamu.

Mohamed Salah akiwa na jezi ya timu ya taifa ya Misri

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Mohamed Salah akiwa na jezi ya timu ya taifa ya Misri

Balozi mkuu wa Misri

Katika kijiji cha Nagrig, mama mzee anayeitwa Rashida anasimulia jinsi Mohamed Salah alivyoibadilisha jamii yao kupitia misaada na miradi ya maendeleo.

"Yeye ni kama kaka kwetu, mkarimu na mwenye heshima," anasema Rashida, mmoja wa wanufaika wa Taasisi ya Misaada ya Mohamed Salah.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa taasisi hiyo, Hassan Bakr, taasisi hutoa msaada wa kila mwezi, milo, na pakiti za chakula kwa mayatima, wajane, maskini, na wagonjwa.

Mbali na misaada hiyo, Salah pia amechangia ujenzi wa posta, kituo cha ambulansi, taasisi ya kidini, na ardhi ya mradi wa maji taka.

Anapokuwa kijijini, Salah hubaki mnyenyekevu, huvaa mavazi ya kawaida na hujichanganya na watu bila majivuno.

Wakati Liverpool ilipotwaa taji lake la 20 la EPL mwaka 2025, kijiji kilisherehekea mafanikio ya mwana wao.

Hata hivyo, licha ya mafanikio makubwa akiwa na Liverpool, Salah bado hajashinda taji na timu ya taifa ya Misri.

Misri ilifika fainali za AFCON mara mbili akiwa ndani ya kikosi, lakini walifungwa na Cameroon (2017) na Senegal (2021).

Huku AFCON 2025 ikitarajiwa kuanza Desemba 21, na Kombe la Dunia 2026 kufuata miezi sita baadaye, baadhi wanauliza kama Salah anahitaji kuthibitisha ubora wake kimataifa.

Lakini kwa Mido, nyota wa zamani wa Misri:

"Salah tayari ni gwiji wa Liverpool na Misri. Hana haja ya kujithibitisha kwa yeyote."

Mada zinazohusiana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid