Rais Samia: "Yaliyotokea yametutia doa"

Chanzo cha picha, Ikulu
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema matukio yaliyojitokeza nchini humo katika wiki za hivi karibuni yanaweza kuathiri kwa kiasi fulani taswira ya nchi kimataifa, hasa katika masuala ya kifedha na uwezo wa serikali kupata mikopo kutoka kwa taasisi za kimataifa.
Ametoa kauli hiyo Leo Novemba 18,2025 huko Dodoma wakati wa kuapisha baraza jipya la mawaziri katika Ikulu ya Chamwino.
Akizungumza mbele ya mawaziri wapya na viongozi waandamizi wa serikali, Rais Samia alisema kuwa uchumi wa Tanzania bado unategemea kwa kiwango kikubwa mikopo ya nje, na kwamba sintofahamu ya kisiasa iliyojitokeza inaweza kupunguza imani ya taasisi hizo.
"Rasilimali zetu ni chache, mara nyingi tunategema kupata kutoka nje, mikopo kutoka kwa taasisi mbalimbali, za kimataifa , mabenki ya kimataifa, lakini yaliyotokea nchini kwetu, yametutia doa kidogo, kwa hiyo huend ayakatupunguzia sifa ya kupata hiyo mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza wa awamu hii (ya sita)", alisema.
Rais Samia alieleza kuwa serikali imejipanga kurekebisha hali hiyo na kusisitiza kwa sasa miradi ya maendeleo katika muhula wa pili wa serikali ya awamu ya sita itaanza kutekelezwa kwanza kwa nguvu za ndani za kiuchumi.
"Tuna kazi ya kutafuta fedha humu ndani, kutumia rasilimali zetu alizotupa Mungu, tutaangalia njia gani tutazitumia tupate fedha ili tukatekeleze miradi ile ambayo tunakwenda kutekeleza", alisema na kuongeza "Muhula wa pili, wa awamu ya sita tutaanza kufanya miradi wenyewe halafu mashirika yatatukuta njiani tutakwenda nayo, hatutakaa kusubiri"
Mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais Samia yamekuja katika kipindi ambacho serikali inakabiliwa na changamoto za kurejesha hali ya utulivu na kuimarisha uchumi baada ya kipindi cha misukosuko ya kisiasa. Wachambuzi wanasema kwamba uzito wa kauli ya Rais umeonyesha namna matukio ya hivi karibuni yalivyoathiri misingi ya uaminifu wa kimataifa kwa Tanzania.
Nchi hiyo ilikumbwa na ghasia za maandamano ya siku tatu kuanzia Oktoba 29, 2025, siku ya uchaguzi, yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Maandamano hayo ya kutaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki, yameelezwa kuwa miongoni mwa machafuko makubwa zaidi nchini katika miongo ya karibuni.
Zaidi ya vijana 600 wwalikamatwa na kufunguliwa makosa yakiwemo ya uhaini. Hata hivyo wakati wa kulifungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wiki iliyopita Rais Samia alitangaza msamaha kwa vijana hao akisema kuwa vijana hao wengine walifuata mkumbo hivyo waachiwe kwa utaratibu na kurejeshwa kwa familia zao.
Maandamano ya mwaka huu Tanzania yanaelezwa ni makubwa kuliko yale ya Zanzibar ya Januari 2001, ambapo watu kadhaa waliuawa wakati wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) walipopinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 moja ya nyakati zilizotikisa historia ya kisiasa ya Tanzania.















