Mhalifu wa ngono Epstein amtaja Trump katika barua pepe mpya

Hayati Jeffrey Epstein alikuwa tajiri wa Marekani aliyepatikana na hatia ya uhalifu wa ngono dhidi ya watoto. Alikutwa amefariki kwenye chumba cha gereza 2019 akisubiri kesi nyingine kuhusu biashara ya ngono.

Muhtasari

Moja kwa moja

Asha Juma & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

    Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, hadi kesho.

  2. Mhalifu wa ngono Epstein amtaja Trump katika barua pepe mpya

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump, Melania Trump, Jeffrey Epstein na Ghislaine Maxwell katika picha ya pamoja February 12, 2000.

    Wabunge wa chama cha Democratic nchini Marekani wameweka hadharani barua pepe mpya za Jeffrey Epstein ambazo zinamtaja Rais wa Marekani Donald Trump.

    Barua pepe moja ni kati ya Jeffrey Epstein na mshirika wake Ghislaine Maxwell.

    Katika taarifa yao, chama cha Democrat kinaeleza katika barua pepe walizotoa leo kwamba moja inaonyesha mawasiliano binafsi kati ya Ghislaine Maxwell, na Jeffrey Epstein mwaka 2011, ambapo Epstein anasema Trump "alikaa saa nyingi nyumbani kwangu" na mwathirika wa biashara ya ngono, na kisha kumtaja Trump kama "mbwa ambaye hajabweka."

    Katika barua pepe nyingine kati ya Epstein na mwandishi Michael Wolff mwaka 2019, chama hicho kinasema Epstein anasema Trump "alijua kuhusu wasichana hao kwani alimtaka Ghislaine kuachana na mambo hayo."

    Hayati Jeffrey Epstein alikuwa tajiri wa Marekani aliyepatikana na hatia ya uhalifu wa ngono dhidi ya watoto. Alikutwa amekufa kwenye chumba cha gereza 2019 akisubiri kesi nyingine kuhusu biashara ya ngono.

    Alikuwa na ukaribu na watu mashuhuri, wakiwemo wanasiasa, wasomi, na wafanyabiashara, na alitumia utajiri na ushawishi wake kuwanyanyasa kingono na kuwasafirisha wasichana wengi wa umri mdogo kwa msaada wa mshirika wake wa muda mrefu, Ghislaine Maxwell.

    Democratic wanasema kuwa bado wanakagua hati 23,000 katika mafaili ya kesi ya Epstein.

    Trump alikuwa rafiki wa Epstein katika miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, na hajawahi kushtakiwa kwa makosa kuhusiana na ukaribu wake na Epstein.

    Trump amekuwa akikana makosa yoyote kuhusiana na Epstein, akisema tuhuma dhidi yake ni "uongo" ulioratibiwa na chama cha Democratic.

  3. Sita wafariki katika mkanyagano wakati wa usaili wa ajira za jeshi

    f
    Maelezo ya picha, Maelfu walijitokeza

    Takriban watu sita wamefariki dunia kufuatia mkanyagano wakati wa zoezi la kuwasaili vijana kwa ajili ya ajira za jeshi katika uwanja wa El-Wak katika mji mkuu wa Ghana, Accra. Wengine kadhaa wamejeruhiwa na kwa sasa wanapokea matibabu katika Hospitali ya Jeshi.

    Kulingana na Jeshi la Ghana, mkanyagano huo ulitokea kabla ya kuanza kwa zoezi la kusajili watu Jumatano asubuhi.

    Msemaji wa jeshi Kapteni Veronica Adzo Arhin katika taarifa yake Jumatano alisema mkanyagano huo ulichochewa na idadi kubwa ambayo haikutarajiwa ya waombaji ambao walikiuka itifaki za usalama na kukimbilia katika milango kabla ya uchunguzi wa kuwaruhusu kupita.

    Maelfu ya watu wanaotarajiwa kuajiriwa walikusanyika katika uwanja wa El-Wak ili kuandikishwa katika Jeshi la Ghana. Ghana ina kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana cha takriban 13%, na mazoezi kama haya ya kuajiri yana sifa ya kuwa na umati mkubwa wa watu na mara nyingi husababisha matukio ya fujo.

    Jeshi la Ghana lililazimika kuongeza muda wa kuajiri kwa wiki moja ili kushughulikia waombaji zaidi, kwani wengine walikuwa na shida katika mchakato wa kutuma maombi.

    Utulivu umerejeshwa, na zoezi la kuwasajili waajiriwa wa jeshi linaendelea.

  4. Bunge la Marekani lapanga kupiga kura kumaliza kufungwa kwa shughuli za serikali

    sx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bajeti ambayo itamaliza kufungwa kwa muda mrefu zaidi kwa shughuli za serikali nchini Marekani inaelekea kupigwa kwenye Baraza la Wawakilishi siku ya Jumatano.

    Siku ya 42 ya mzozo huo, wawakilishi wanarudi Washington kuamua kama wataidhinisha mpango wa Seneti wa fedha ambazo zitafadhili mashirika ya shirikisho kwa miezi miwili.

    Uongozi wa Republican ulionyesha imani kuwa mpango huo wa matumizi utapita katika baraza la chini la Congress, licha ya wingi wao finyu. Lakini viongozi wakuu wa chama cha Democratic wameapa kupinga mpango huo.

    Rais Donald Trump amedokeza kuwa atatia saini mpango huo kuwa sheria, Jumanne katika hafla ya Siku ya Veterani huko Arlington, Virginia.

    Ufungaji wa shughuli za serikali ulioanza tarehe 1 Oktoba, umewaacha wafanyakazi wa shirikisho milioni bila malipo, kukosa ufadhili wa chakula kwa Wamarekani wa kipato cha chini, na kuchelewesha safari za ndege.

  5. Walowezi wa Israel wachoma moto ghala la bidhaa huko Palestina

    cx

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Ghala la Beit Lid lilishambuliwa, na lori kuchomwa moto

    Makumi ya walowezi wa Israel wamefanya mashambulizi ya kuteketeza ghala la bidhaa huko Palestina, katika Kijiji cha cha Bedouin, na mashamba kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu siku ya Jumanne.

    Wapalestina kadhaa walijeruhiwa. Matukio hayo yalikuwa ya hivi punde zaidi katika msururu wa ghasia za walowezi.

    Haya yanajiri baada ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu kusema idadi ya mashambulizi ya kikatili yaliyofanywa na walowezi mwezi uliopita ni ya juu zaidi tangu ilipoanza kukusanya takwimu takriban miaka 20 iliyopita.

    Israel imejenga takriban makazi 160 ya Wayahudi wapatao 700,000 tangu ilipoukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki wakati wa vita vya Mashariki ya Kati vya 1967. – ni ardhi ambayo Wapalestina wanataka, pamoja na Gaza, kuwa taifa lao la baadaye. Takriban Wapalestina milioni 3.3 wanaishi kando yao.

    Makazi hayo ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa.

    Video za Jumanne zinaonyesha makumi ya wanaume waliofunika nyuso zao kwenye mlima mashariki mwa Tulkarm, na kisha ghala la Wapalestina huko Beit Lid lilishambuliwa, na lori kuchomwa moto.

    Mahema yanaweza kuonekana yakiwaka moto katika kijiji cha Bedouin cha Deir Sharaf, na sauti ya wanawake wakipiga kelele.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema kuwa wanajeshi walikwenda kwenye eneo la tukio "kutawanya ghasia na kuwakamata raia kadhaa wa Israel." Iliongeza kuwa askari walishambuliwa na walowezi waliokuwa wamekusanyika karibu na gari lao kuharibiwa.

    Polisi wa Israel walisema kuwa washukiwa wanne walikamatwa.

    Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) inasema kuwa Oktoba ilishuhudia zaidi ya mashambulizi 260 ya walowezi wa Israel na kusababisha hasara, uharibifu wa mali au vyote viwili - wastani wa matukio manane kwa siku.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Ukungu wavisaidia vikosi vya Urusi kusonga mbele katika mji wa Ukraine wa Pokrovsk

    dc

    Chanzo cha picha, Telegram

    Maelezo ya picha, Picha hii ya wanajeshi wa Urusi huko Pokrovsk kwenye ukungu ilionekana kwenye mitandao ya kijamii Jumatatu

    Ukungu mnene umewawezesha wanajeshi wa Urusi kusonga mbele zaidi katika mji muhimu wa kimkakati wa Pokrovsk mashariki mwa Ukraine.

    Kikosi cha Ukraine kinasema hali ya hewa, haswa ukungu mnene, imeifanya Moscow kuzidisha azma yake ya kuongeza idadi ya wanajeshi katika jiji hilo lililoharibiwa na kuvizingira vikosi vya Ukraine.

    Vikosi vya Urusi vimetumia zaidi ya mwaka mmoja kujaribu kuuteka mji huo. Jeshi la Ukraine linasema huenda sasa kuna wanajeshi 300-500 wa Urusi huko na Rais Voloydymyr Zelensky anasema hali bado ni ngumu.

    Wakati huo huo, mkuu wa jeshi Oleksandr Syrskyi anasema hali katika mstari wa mbele wa mapigano katika eneo la kusini mashariki mwa Zaporizhzhia "imezidi kuwa mbaya."

    Video imesambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha wanajeshi wa Urusi kwenye barabara wakiwa kwenye magari na pikipiki za kiraia.

    BBC imethibitisha mahali ambapo video hiyo ilirekodiwa ni kusini mwa mji huo kwenye barabara kuu ya Selidove-Pokrovsk.

    Kwa siku kadhaa ukungu umezuia ndege kuona, anasema rubani wa droni.

    Wiki moja iliyopita, Zelensky alikadiria kuwa kuna wanajeshi 300 wa Urusi wakipigana huko Pokrovsk. Video hiyo inaonyesha kwamba idadi hiyo huenda imeongezeka.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Ndugu wawili washtakiwa kwa mauaji ya mwanamuziki wa Afrika Kusini AKA

    sx

    Chanzo cha picha, Gallo via Getty Images

    Maelezo ya picha, Rapa Kiernan Forbes aliuawa akiwa njiani kwenda kutumbuiza kwenye klabu ya usiku

    Ndugu wawili wameshtakiwa kwa mauaji ya rapa wa Afrika Kusini, Kiernan Forbes, maarufu "AKA," baada ya kurejeshwa kutoka nchi jirani ya Eswatini.

    Siyabonga na Malusi Ndimande walirudishwa baada ya kushindikana kwa jaribio la muda mrefu la kisheria la kuzuia kurejeshwa Afrika Kusini.

    Forbes, msanii wa muziki wa kufoka foka, aliuawa nje ya mkahawa katika jiji la pwani la Durban mwaka 2023 pamoja na rafiki yake wa karibu, mpishi maarufu Tebello "Tibz" Motsoane.

    Afrika Kusini ina moja ya viwango vya juu vya mauaji duniani.

    Ndugu hao pia wameshtakiwa kwa mauaji ya Motsoane na watafikishwa mahakamani pamoja na washtakiwa wengine watano ambao tayari wako rumande kesi itakapoanza. Pia wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua na kumiliki bunduki kinyume cha sheria.

    Waliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Durban siku ya Jumanne chini ya ulinzi mkali wa polisi, huku mikono na miguu yao vikiwa vimefungwa pingu.

    Wakati wa mauaji yake, Forbes alikuwa Durban kutumbuiza wakati wa sherehe ya siku yake ya kuzaliwa.

    Polisi walitaja shambulio hilo dhidi ya watu hao wawili kuwa ni shambulio lililoratibiwa. Ingawa inaaminika Forbes ndiye aliyekusudiwa, huku bado haijafahamika ya kufanya mauaji hayo.

    Ndimande watarejea tena mahakamani Novemba 25 kwa ajili ya kusikilizwa kwa dhamana.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Israel imeharibu zaidi ya majengo 1,500 Gaza tangu kusitishwa mapigano

    D

    Chanzo cha picha, UNRWA

    Israel imeharibu zaidi ya majengo 1,500 katika maeneo ya Gaza ambayo yako chini ya udhibiti wa jeshi lake tangu kusitishwa kwa mapigano na Hamas kuanza tarehe 10 Oktoba, picha za satelaiti zilizokaguliwa na BBC zinathibitisha.

    Picha mpya - za hivi punde zaidi zilipigwa tarehe 8 Novemba - zinaonyesha majengo yote katika vitongoji vinavyodhibitiwa na Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) yamedondoshwa ndani ya mwezi mmoja, kwa njia ya ubomoaji.

    Idadi halisi ya majengo yaliyoharibiwa inaweza kuwa kubwa zaidi, kwani BBC imeshindwa kupata baadhi ya picha za setilaiti katika baadhi ya maeneo kwa ajili ya tathimini.

    Baadhi ya wataalam wanasema ubomoaji huo unaweza kukiuka masharti ya usitishaji mapigano yanayosimamiwa na Marekani, Misri, Qatar na Uturuki. Lakini msemaji wa IDF aliiambia BBC, ilikuwa ikitenda "ndani ya makubaliano ya kusitisha mapigano."

    Mpango wa amani wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa Gaza – unasema "operesheni zote za kijeshi, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya angani na mizinga, zitasitishwa.”

    Uchunguzi wa picha za satelaiti wa BBC umegundua kuwa uharibifu wa majengo huko Gaza unaofanywa na jeshi la Israel umekuwa ukiendelea kwa kiwango kikubwa.

    BBC ilitumia picha zilizopigwa kabla na baada ya kusitishwa kwa mapigano ili kuangazia mabadiliko, ambayo yanaweza kuonyesha uharibifu, kisha tukahesabu majengo yaliyoharibiwa.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Trump asema ana haki ya kuishtaki BBC

    x

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema ana "haki ya" kuishtaki BBC kuhusu jinsi hotuba yake ilivyohaririwa katika makala ya Panorama.

    Akizungumza na Fox News, amesema hotuba yake ya Januari 6, 2021 "ilikatwa" na jinsi ilivyowasilishwa "iliwapotosha" watazamaji.

    Ni mara ya kwanza kwa Trump kuzungumza hadharani kuhusu suala hilo tangu mawakili wake waiandikie BBC na kusema kwamba ataishitaki BBC kwa fidia ya dola bilioni 1 (£759m), ama shirika hilo liondoe makala hiyo, liombe msamaha na kumfidia.

    Msemaji wa BBC amesema: "Tunapitia barua hiyo na tutajibu moja kwa moja kwa wakati unaofaa."

    Mwenyekiti wa BBC Samir Shah hapo awali aliomba msamaha kwa "kosa katika uhariri."

    Trump amesema: "Kwa kweli walibadilisha hotuba yangu ya Januari 6, ambayo ilikuwa hotuba nzuri, ilikuwa hotuba iliyopoa, na waliifanya isikike kama hotuba kali.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Waandamanaji waingia katika ukumbi wa COP30 nchini Brazil

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waandamanaji waliokuwa wamebeba mabango yanayosema "misitu yetu haiuzwi" walivuka vizuizi vya usalama wakati mazungumzo ya hali ya hewa ya COP30 yakiendelea Jumanne usiku huko Belém, Brazili.

    Waandishi wa habari wa BBC waliwaona wafanyakazi wa usalama wa Umoja wa Mataifa wakikimbia nyuma ya safu ya wanajeshi wa Brazil wakipaza sauti kwa wajumbe kuwataka kuondoka mara moja kwenye ukumbi huo.

    Umoja wa Mataifa uliambia BBC kwamba tukio hilo lilisababisha majeraha madogo kwa wafanyakazi wawili wa usalama, pamoja na uharibifu mdogo katika ukumbi huo.

    Video katika mitandao ya kijamii zilionyesha waandamanaji ambao walionekana kutoka katika makundi ya kiasili na wengine wakipeperusha bendera zenye nembo ya vuguvugu la vijana wa mrengo wa kushoto wa Brazil liitwalo Juntos.

  11. Programu mbili maarufu za wapenzi wa jinsia moja zaondolewa kwenye Apple China

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Apple imethibitisha kuwa imeondoa programu mbili maarufu za uchumba za wapenzi wa jinsia moja nchini China - Blued na Finka - kutoka eneo la kupakua programu nchini humo kufuatia agizo kutoka kwa mamlaka.

    "Tunafuata sheria za nchi ambazo tunafanya kazi. Kulingana na agizo kutoka kwa Utawala wa Mtandao wa China, tumeondoa programu hizi mbili kutoka eneo la kununua huduma za mtandao la China pekee," msemaji wa Apple alisema.

    Hatua hiyo imeibua wasiwasi miongoni mwa jumuiya ya LGBT nchini humo.

    BBC imewasiliana na ubalozi wa China mjini Washington na makampuni yaliyo nyuma ya programu zote mbili kwa maoni.

    Blued ni mojawapo ya programu zinazotumiwa sana na wapenzi wa jinsia moja nchini China, ikiwa na makumi ya mamilioni ya wanaopakua programu hiyo.

    Soma zaidi:

  12. Aliyekuwa mke wa rais Gabon na mwanawe wahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela

    .

    Mke wa rais wa kwanza wa Gabon, Sylvia Bongo, na kijana wake wa kiume, Noureddin Bongo Valentin, wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kufuatia kesi ya ufisadi ya siku mbili huko Libreville.

    Wawili hao walihukumiwa licha ya kutokuwepo mahakamani siku ya Jumanne usiku, kifungo cha miaka 20 na faini ya milioni 100 za CFA francs, ambayo ni takriban pauni 135,000.

    Kama fidia ya uharibifu wa fedha katika taifa la Gabon, ambayo ilikuwa chama cha kiraia katika kesi hiyo, mahakama pia iliamuru Noureddin Bongo kulipa zaidi ya CFA Francs trilioni 1.201, sawa na karibu dola bilioni 1.6.

    Kesi hiyo katika mahakama ya Rufaa iliendelea katika mji mkuu bila ya wawili hao kuwepo, ambao waliruhusiwa kuondoka Gabon kwenda London kwa dhamana ya masharti Mei 2025 kwa misingi ya matibabu.

    Licha ya hukumu ya wawili hao kutolewa, kesi ya watuhumiwa wengine itaendelea hadi Ijumaa, waandishi wa eneo wameiambia BBC.

  13. Ronaldo asema Kombe la Dunia la 2026 litakuwa la mwisho kwake

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mshambulizi wa Ureno Cristiano Ronaldo amethibitisha kuwa Kombe la Dunia la 2026 litakuwa la mwisho kwake.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40, ambaye amefunga mabao 953 kwa klabu na nchi, pia alisema atastaafu soka katika "mwaka mmoja au miwili".

    Michuano ya Kombe la Dunia mwakani itakayofanyika nchini Canada, Mexico na Marekani, itakuwa ya sita kwa Ronaldo.

    Katika mahojiano kwenye Mkutano wa Tourise mjini Riyadh, alipoulizwa kama 2026 itakuwa Kombe lake la mwisho la Dunia, Ronaldo alisema: "Hakika, ndiyo. Nitakuwa na umri wa miaka 41 na nadhani [huu] utakuwa wakati wa mashindano makubwa."

    Ronaldo, ambaye anachezea klabu yake ya soka nchini Saudi Arabia akiwa na Al-Nassr, ndiye mfungaji bora wa muda wote wa kimataifa akiwa na mabao 143 - huku akiendelea kufikisha mabao 1,000 katika maisha yake ya soka.

    Soma zaidi:

  14. Rais wa Colombia aamuru kusitishwa kwa ushirikiano wa kijasusi na Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Colombia Gustavo Petro ameamuru kusitishwa kwa ushirikiano wa kijasusi na Marekani kama njia ya kupinga kampeni ya Marekani ya kufanya mashambulizi dhidi ya watu wanaodaiwa kuwa walanguzi wa dawa za kulevya katika visiwa vya Caribbean na mashariki mwa Pasifiki.

    "Mapigano dhidi ya dawa za kulevya lazima yaendane na haki za binadamu za watu wa Caribbean," Petrol alisema katika chapisho la X, akirejelea historia ya nchi hizo mbili za kushirikiana dhidi ya biashara ya dawa za kulevya.

    Petro, mpiganaji wa zamani wa mrengo wa kushoto wa vita vya guerilla, aliongeza kuwa hatua hiyo itaendelea kutekelezwa hadi pale Marekani itakapositisha mashambulizi dhidi ya meli katika visiwa vya Caribbean.

    Marekani imetuma vikosi vyake, katika eneo hilo tangu mwishoni mwa mwezi Agosti kama sehemu ya operesheni ambayo imewauwa watu wasiopungua 76 wanaodaiwa kuwa walanguzi wa dawa za kulevya katika takriban mashambulizi 19 eneo la Caribbean na mashariki mwa Pasifiki.

    Pia imetuma meli nyingine nne za kivita, ikiwa ni pamoja na USS Gerald R Ford inayosemekana kuwa kubwa zaidi ya kijeshi ulimwenguni.

    Rais wa Venezuela Nicolás Maduro amedai kuwa kutumwa kwa wanajeshi wa Marekani ni kisingizio cha kumuondoa madarakani.

    Soma zaidi:

  15. Taliban yaamuru wanawake kuvaa burka ili kuingia kwenye vituo vya afya, shirika la MSF linasema

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka ya Taliban nchini Afghanistan imewaamuru wagonjwa wa kike, walezi na wafanyakazi kuvaa burka - vazi kamili la Kiislamu - ili kuingia katika vituo vya afya vya umma katika mji wa magharibi wa Herat, shirika la matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) linasema.

    MSF ilisema vikwazo hivyo vilianza kutekelezwa kuanzia tarehe 5 Novemba.

    "Vikwazo hivi vinatatiza zaidi maisha ya wanawake na kuwazuia kupata huduma za afya," Sarah Chateau, meneja wa programu wa shirika hilo nchini Afghanistan, aliiambia BBC. Alisema hata wale "wanaohitaji huduma ya haraka ya matibabu" wameathirika.

    Msemaji wa serikali ya Taliban amekanusha madai ya MSF. Ripoti zinasema vizuizi vimelegezwa kwa kiasi tangu kuanza kuangaziwa kwa suala hilo.

    Soma zaidi:

  16. Jeshi la Venezuela lajiandaa kujibu iwapo Marekani itaishambulia

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Venezuela inapeleka silaha, ikiwa ni pamoja na vifaa vya miaka mingi vilivyotengenezwa na Urusi, na inajipanga kwa vita vya kuvizia au kusababisha machafuko ikiwa Marekani itaishambulia kwenye anga au ardhini, kulingana na vyanzo vyenye ufahamu wa juhudi zinazoendelea na nyaraka za upangaji zilizoonekana na Reuters.

    Mbinu hiyo inatumika kutokana na ukosefu wa wafanyakazi na vifaa katika nchi hiyo ya Amerika Kusini.

    Rais wa Marekani Donald Trump amependekeza uwezekano wa operesheni za ardhini nchini Venezuela, akisema "ndio itakayofuata" kufuatia mashambulizi kadhaa dhidi ya meli zinazodaiwa kusafirisha dawa za kulevya katika visiwa vya Caribbean na kuwasili kwa jeshi kubwa la Marekani katika eneo hilo.

    Baadaye alikanusha kwamba alikuwa anafikiria kutekeleza mashambulizi ndani ya Venezuela.

    Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, aliye madarakani tangu 2013, anasema Trump anataka kumuondoa madarakani na kwamba raia wa Venezuela na wanajeshi watapinga jaribio lolote kama hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Wanajeshi wa Marekani wawasili Caribbean

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kikosi cha wanamaji cha Marekani kilichojikita katika meli kubwa zaidi ya kivita duniani, USS Gerald R Ford, kimewasili katika visiwa vya Caribbean, Jeshi la Wanamaji la Marekani limethibitisha.

    Kuwasili kwa wanajeshi hao ambako ni agizo la Rais Donald Trump mwezi uliopita, kunafanyika huku mashambulizi yikiendelea dhidi ya meli za dawa za kulevya na mvutano wa nchi hiyo na Venezuela ukiendelea kutokota.

    Marekani hadi kufikia sasa imetekeleza takriban mashambulizi 19 dhidi ya boti katika visiwa vya Caribbean na mashariki mwa Pasifiki, na kusababisha vifo vya takriban watu 76.

    Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na maafisa wengine wa Venezuela wameishutumu Marekani kwa "kujitengenezea" mgogoro na kutaka kuiangusha serikali ya mrengo wa kushoto ya kisoshalisti.

    Hatua za kuwasili kwa meli ya kivita pia kunawadia huku kukiwa na mvutano kati ya utawala wa Trump na serikali ya Colombia ya Rais Gustavo Petro, ambaye Trump amemtaja kama "jambazi na mtu mbaya".

    Petro siku ya Jumanne aliamuru vikosi vya usalama vya umma vya nchi yake kusimamisha ushirikiano wa kijasusi na mashirika ya Marekani hadi mashambulio ya meli katika visiwa vya Caribbean yatakapokoma.

    Aliandika kwenye mtandao wa X kwamba mapambano dhidi ya madawa ya kulevya "lazima yawe chini ya haki za binadamu za watu wa Caribbean".

    Mapema mwezi wa Novemba, Trump alipuuza uvumi kwamba alikuwa akipanga kupindua serikali ya Venezuela au kuanzisha vita.

    Katika mahojiano na CBS - mshirika wa BBC wa habari wa Marekani - Trump alisema kwamba "kila meli moja unayoona imelipuliwa inaua watu 25,000 kwa madawa ya kulevya na kuharibu familia kote nchini."

    Pia unaweza kusoma:

  18. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 12/11/2025.