Mwanamuziki Maarufu wa Tanzania aacha muziki kutokana na msongo wa mawazo

Venessa Mdee

Chanzo cha picha, Vanessa/Facebook

Vanessa mdee ni miongoni mwa wanamuziki maarufu wa kike nchini Tanzania na barani Afrika.

Siku kadhaa zilizopita Mdee alitangaza kuacha shughuli zote za muziki na burudani kupitia Podcast yake inayoitwa 'Deep dive with Vanessa Mdee'

Katika maelezo yake anasema amekua akikabiliana na msongo wa mawazo kwa muda mrefu kutokana na shughuli za muziki.

''Nimekua nikiishi kwa nje najificha lakini ndani nakufa, nilikuwa siwezi kulala hadi ninywe pombe''

''Sina hamu tena ya kufanya muziki, sina hamu tena ya kuhudhuria shughuli yoyote ya kupokea tuzo, kuanzia sasa sitajihusisha tena, hapana, ni msongo wa mawazo, ni shinikizi kubwa'' anasema Vanessa.

Aidha katika mambo ambayoo amesema yamesababisha kuwa na msongo wa mawazo kwenye tansia ya muziki, ni jinsi ambavyo anatakiwa kuishi Maisha Fulani kila siku ambayo si ya kweli kwake yeye binafsi na matakwa yake.

Vanessa ameongeza pia gharama za kuendesha shughuli ya muziki zilikua kubwa kuliko faida yake.

''Nafanya show kwa dola 1000 , hapo unatakiwa kutoa gharama ya kila kitu, kuwalipa watu, mimi mwenyewe, sehemu ya kuishi, gharama za kusafiri, hapo hapo ule, ujenge, usaidie familia''.

Vanessa mdee

Chanzo cha picha, Venessa/Facebook

Vanessa Amefikia uamuzi huu baada ya kuwa katika tasnia ya muziki kwa zaidi ya miaka 10.

Anasema kila mwaka amekua akirudia mfumo wa Maisha huo huo, amekua akiridhisha wengine lakini hakua na furaha yeye binafsi.

''Nimekua nikiridhisha watu wengine kila siku kwa miaka 13, nimekua kwenye muziki kwa miaka saba, lakini nimeanza kujihusiha zaidi ya miaka 13, na kila siku hali ni ile ile''.

Baada ya kutoa maamuzi yake Vanessa anasema amepata ujumbe wa wasanii mbalimbali wakimwambia amefanya uamuazi mzuri, na baadhi wanapitia hali kama yake lakini hawajapata ujasiri wa kuweka wazi.

''Baada ya kuongea kwenye podcast yangu, nilipokea ujumbe kutoka kwa watu, wengine wanamuziki, wananiambia asante sana, mimi napitia asilimia 100 hali kama yako, maamuzi yangu hayakua mepesi na ni ngumu kwa mtu ambaye hayupo kwenye tasnia sio rahisi kuelewa''.

Umaarufu

Vanessa amejizolea umaarufu mkubwa wakati anashiriki katika vipindi vya kituo cha televesheni cha MTV nchini Afrika kusini, na baadae akaingia katika soko la muziki na kushinda tuzo kadhaa za muziki barani Afrika na nchini Tanzania.

Wamamuziki wakubwa duniani waliopitia msongo wa mawazo.

Wanamuziki wengi ulimwenguni kwa wakati tofauti wamejitokeza na kuweka wazi kuwa wamewahi kuapata msongo mawazo na kusumbuliwa na afya ya akili.

Nick Minaj aliweka wazi juu ya kusumbuliwa na afya ya akili pamoja na msongo wa mawazo mwaka 2011, akizungumza na jarida la Cosmo Minaj alisema amekua kuwa na mawazo ya kuondoa uhai wake.

''Nilihisi mambo yalikua hayaendi kabisa, nikajiuliza hivi nikilala na nisimake kwani itakuaje?'' Minaj aliliambia jarida la Cosmo.

Mwanamuziki AKA kutoka afrika kusini, amewahi kuweka wazi juu ya msongo wa mawazo unatokana na aina ya Maisha ambayo anatakiwa kuishi kama mtu maarufu.

''Ukiwa mwanamuziki inabidi uishi kwa uwazi, kila kitu unatakiwa uweke wazi hadi jinsi ganin unaishi Maisha yako, jambo ambalo huleta msongo wa mawazo''.

Vanessa mdee

Chanzo cha picha, Venessa/Facebook

Mariah Carey nae aliweka wazi juu ya kuwa na matatizo ya akili lakini alikua akificha na kudhani kuwa ni kukosa usingizi tuu.

''Hadi sasa nilikua nikikataa kuwa na tatizo lolote, niliishi kwa uoga na kujificha na wasiwasi kuwa mtu anaweza kutoa siri yangu.

''Nilikubali hali yangu, nikawa karibu na watu wanaonitakia mema pamoja na kuanza kufanya muziki kitu ninachokipenda sana''. Mariah Carey aliliambia jarida la people.

Hivi karibuni nae Selena Gomez alitangaza kuwa anashinda ya akili ama Bipolar.

''Nilienda katika moja ya kituo kikubwa cha afya na baada ya miaka mingi sana nikagundulika kuwa na bipolar, alisema Gomez katika mtandao wa Instagram alipokua ameshiriki Instagram live kwenye ukurasa wa msanii Miley Cyrus.

Kwanini wanamuziki wengi wanapitia msongo wa mawazo?

Nicky Lidbetter kiongozi wa shirika ya Anxiety Uk linajihusisha na masuala ya afya ya akili anasema kuwa wanamuziki wapo katika hatari ya kupata mshutuko wa akili ama 'Panic attack' kutokana na kutaka kuridhisha mashabiki wao hasa katika matamasha.

''Mara nyingi wapo katika haraka, lakini pia wanajaribu kuwaridhisha mashabiki ambao mara nyingi wana hasira kwanini amechelewa kupanda jukwaani. Lidbetter aliiambia BBC katika kipindi cha 5 live.

Lidbetter Anasema kuwa kupona ama kumaliza msongo wa mawazo kwa wanamuziki ni ngumu sana, lakini inawezekana kama wakibadili mfumo na kufanya mambo kwa hatua.

''Unaweza kupona lakini ni ngumu sana kwasababu upo kwenye macho ya jamii, na una msukumo bado wa kutumbuiza kwenye halaiki ya watu, huwa tunawashauri wafanye mambo taratibu'' anasema Lidbetter.