Ukraine na Urusi zakubaliana kubadilishana wafungwa wa kivita
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov amewaambia waandishi wa habari wa Ukraine kuwa "Tumejadili suala la kusitisha mapigano. Na suala la kubadilishana [wafungwa]. Alikuwa akizungumza baada ya mazungumzo na Urusi kumalizika.
Muhtasari
- Takriban watu 100 waliuawa katika shambulizi la Israel kaskazini mwa Gaza - waokoaji
- Ukraine na Urusi zakubaliana kubadilishana wafungwa wa kivita
- Rais wa Gabon aliyeondolewa madarakani aachiwa huru baada ya miaka miwili
- Maafisa wa Ukraine na Urusi wakutana kwa mara ya kwanza mazungumzo ya ana kwa ana baada ya miaka mitatu
- 'Seneti haina mamlaka ya 'kumvua Kabila kinga - afisa wa chama
- Mifupa ya kale ya India yapata nyumba ya makumbusho miaka sita baada ya kufukuliwa
- Idadi ya mabilionea yapungua Uingereza huku Mfalme akiongezeka katika Orodha ya Matajiri- Sunday Times
- Bunge la Uganda laidhinisha matumizi ya serikali ya 2025/26 yaliyopendekezwa
- DRC: Tume yaundwa kujadili kinga ya aliyekuwa Rais Joseph Kabila
- Marekani 'yasononeshwa' na hali ya kibinadamu Gaza
- Mkurugenzi wa zamani wa FBI anachunguzwa kwa kinachodaiwa kuwa tishio kwa Trump
- Mahakama ya Juu Marekani yagawanyika katika kesi ya uraia wa kuzaliwa
- Chris Brown ashitakiwa kwa kumshambulia mtu kwenye klabu ya Usiku
- Amani ya Ukraine iko kwa Trump na Putin yasema Marekani
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Dinah Gahamanyi
Takriban watu 100 waliuawa katika shambulizi la Israel kaskazini mwa Gaza - waokoaji

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Muombolezaji wakati wa mazishi ya Wapalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel katika hospitali ya Indonesia huko Beit Lahia Takriban watu 100 wakiwemo watoto wameuawa katika mashambulizi makubwa ya ardhini, anga na baharini yaliyofanywa mapema Ijumaa huko Gaza kaskazini mwa Gaza, jeshi la ulinzi la raia linaloongozwa na Hamas na wakaazi wamesema.
Upande wa utetezi wa kiraia ulisema takriban nyumba tisa na mahema ya makazi ya raia zilishambuliwa kwa bomu usiku mmoja na ulipokea simu nyingi kutoka kwa watu waliokwama.
Mashahidi pia waliripoti mabomu ya moshi, na mizinga huko Beit Lahia.
Jeshi la Israel lilisema "linaendesha operesheni ya kutafuta na kubomoa maeneo ya miundombinu ya magaidi" kaskazini mwa Gaza na "limewaangamiza magaidi kadhaa" katika siku iliyopita.
Hili ni shambulio kubwa zaidi la ardhini kaskazini mwa Gaza tangu Israel ianze tena mashambulio yake mwezi Machi.
Maelezo zaidi:
Ukraine na Urusi zakubaliana kubadilishana wafungwa wa kivita
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov amekuwa akitoa maelezo kwa wanahabari wa Ukraine baada ya mazungumzo na Urusi kumalizika.
Umerov anasema Ukraine na Urusi zimekubali kubadilishana wafungwa 1,000 wa vita.
"Tumejadili suala la kusitisha mapigano. Na suala la kubadilishana [wafungwa]. Matokeo yake ni kubadilishana watu 1,000 kwa 1,000.
Hayo ni matokeo ya mkutano wetu." Tarehe ya kutekeleza mpango huo imewekwa, lakini haijawekwa wazi, anasema.
Umerov pia anasema uwezekano wa kufanyika kwa mkutano kati ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin ulijadiliwa na kwamba tangazo kuhusu duru mpya ya mazungumzo litatangazwa hivi karibuni.
"Njia zote" za kusitisha mapigano pia zilijadiliwa, Umerov alisema.
Soma pia:
Polisi kuchunguza kisa cha kutoweka kwa sanamu ya shaba ya Melania Trump

Chanzo cha picha, JURE MAKOVEC/AFP/Getty Images
Sanamu ya shaba ya Melania trump karibu na mji alikozaliwa nchini Slovenia imetoweka, miaka mitano baada ya kuwekwa mahali ilipokuwa sanamu ya mbao iliyoharibiwa na kuchomwa moto
Polisi wa Slovenia wamesema kwamba walikuwa wamearifiwa kuhusu wizi katika kijiji cha Rozno, ambapo sanamu hiyo ilikuwa, siku ya Jumanne.
Maafisa "walifanya ukaguzi wa eneo la uhalifu na kukusanya taarifa," msemaji wa polisi Alenka Drenik Rangus alisema katika taarifa Ijumaa. "Jaji mchunguzi na mwendesha mashtaka wa wilaya waliarifiwa kuhusu wizi huo."
Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa na mamlaka.
Picha zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya Kislovenia zinaonyesha sehemu kubwa ya sanamu hiyo ikiwa imekatwa kwa msumeno, na kuacha tu miguu na vifundo vyake vikiwa vimeunganishwa kwenye shina la mti ambalo ilisimikwa.
Sanamu hiyo ilikuwa kando ya mto karibu na Sevnica, mji mdogo wa kupendeza ulio umbali wa kilomita 90 (maili 56) mashariki mwa mji mkuu wa Slovenia Ljubljana.
Kabla ya sanamu hii ya shaba kuibiwa, sanamu yake asili ya mbao ilichomwa moto mnamo Julai 2020 na waharibifu. Ilichomwa vibaya, kisha ikaondolewa kutoka kwenye kilele chake kabla ya kuonyeshwa kwenye jumba la sanaa katika mji wa Slovenia wa Koper baadaye mwaka huo na kwenye maonyesho huko Croatia mnamo 2023.
Pia unaweza kusoma:
Rais wa Gabon aliyeondolewa madarakani aachiwa huru baada ya miaka miwili

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa zamani wa Gabon, Ali Bongo, ambaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya 2023, ameondoka nchini na sasa yuko Angola, mamlaka nchini humo imetangaza.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii mamlaka nchini Angola iliongeza kuwa familia ya Bongo pia imeachiliwa huru na imeungana naye mjini Luanda.
Mke wa Bongo na mwanawe, Sylvia na Noureddin, walikabiliwa na mashtaka ya ulaji rushwa na walikuwa wamefungwa gerezani mwaka wa 2023.
Mashtaka hayo hayajawahi kuangaziwa hadharani lakini wakili wa Bi Bongo anasema mteja wake hakustahili kushikiliwa na kuongeza kwamba hatua hiyo ilikuwa kinyume cha sheria.
Kuachiliwa kwa familia hiyo kumekuja baada ya Rais wa Angola João Lourenço, ambaye kwa sasa anaongoza Umoja wa Afrika, kuzuru Libreville na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Gabon Brice Oligui Nguema - jenerali wa zamani aliyeongoza mapinduzi dhidi ya Bongo kabla ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa rais mwezi uliopita.
Mwendesha mashtaka wa Gabon Eddy Minang anasema Bi Bongo na mwanawe wameachiliwa kwa muda tu, na ni hatua ambayo ilifikiwa kwa misingi ya kiafya akiongeza kwamba kesi dhidi ya wawili hao zitaendelea.
Katika picha zilizotolewa na ofisi ya rais wa Angola, Bongo anaonekana akilakiwa alipowasili uwanja wa ndege, na nyuma yake kuna mwanamke anayesadikiwa kuwa mke wake.
Ali Bongo, ambaye baba yake Omar Bongo alitawala Gabon kwa zaidi ya miongo minne, aliongoza nchi hiyo kwa miaka 14 alipoondolewa madarakani katika mapinduzi ya 2023.
Maelezo zaidi:
Maafisa wa Ukraine na Urusi wafanya mazungumzo ya ana kwa ana baada ya miaka mitatu

Chanzo cha picha, EPA
Mazungumzo ya amani nchini Uturuki leo kati ya Urusi na Ukraine yanaendelea. Ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu kwa wajumbe kutoka nchi hizo mbili kuwa katika chumba kimoja.
Lakini , inaonekana kuna nafasi kubwa baina yao ndani ya chumba cha mazungumzo pande mbili zinaonekana kuwa mbali sana.
Zelensky anasema jukumu la timu yake linalenga kusitisha mapigano mara moja, huku Warusi wakisema hapo jana kuwa lengo lao ni amani ya muda mrefu na kuondoa "sababu kuu za mzozo huu".
Ikitafsiriwa kutoka Kremlin-speak - hii ina maana kwamba hawana nia kabisa ya kusitisha mapigano, wana nia ya kushughulikia kile kilichoanzisha vita hivi kutoka kwa mtazamo wa Kremlin - kuwepo kwa Ukraine kama taifa huru.
Jambo la kushangaza mkuu wa ujumbe wa Urusi alisema jana kwamba Urusi iko tayari kujadili maelewano - lakini haiko wazi alimaanisha nini nini.

Chanzo cha picha, Dmytro Vlasov/BBC
Maelezo ya picha, Ujumbe wa Ukraine, akiwemo mkuu wa ulinzi wa nchi hiyo, uko kwenye mazungumzo ya ana kwa ana 
Chanzo cha picha, Dmytro Vlasov/BBC
Maelezo ya picha, Ujumbe wa Urusi umeketi mkabala na Waukraine Tunatumai ni hatua mbele na ishara ya kubadilika kidogo kwa upande wa Urusi. Lakini, yeye ndiye mtu pekee kutoka katika ujumbe wa Urusi ambaye ametaja maelewano.
Wengine katika ujumbe huo wanashikilia bado matakwa yao ya awali, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na uanachama wa Nato kwa Ukraine na udhibiti wa Urusi wa angalau mikoa mitano ya Ukraine.
Matakwa yote ya Urusi hayakubaliki kabisa kwa Zelensky.
Soma pia:
'Seneti haina mamlaka ya 'kumvua Kabila kinga - afisa wa chama

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Joseph Kabila, ambaye aliitawala DRC kuanzia 2001 hadi Januari (1) 2019, anakanusha kufanya kazi na M23 Afisa mkuu katika chama cha Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila ameiambia BBC kwamba Bunge la Seneti la nchi hiyo "halina mamlaka ya kisheria", siku moja baada ya kuanzisha hatua ya kumvua kinga yake.
Francine Muyumba, kutoka chama cha upinzani cha PPRD ambacho chama tawala cha Congo kilimtimua tarehe 4 Aprili mwaka huu , ni Seneta na wakili wa zamani. Yeye sawa na Joseph Kabila, anaishi nje ya nchi.
Siku ya Alhamisi, Bunge la Seneti nchini DRC ilianza kujadili hoja ya kumfungulia mashtaka Kabila. Iwapo yataidhinishwa, Kabila atapoteza wadhifa wake kama "seneta wa maisha", kumaanisha kuwa atapoteza kinga yake na kufunguliwa mashtaka ya kisheria.
Ombi hilo lilitolewa na Inspekta Jenerali wa Jeshi la DRC (FARDC).
Katika mahojiano na BBC Africa Daily, Muyumba alisema: "Seneti haina mamlaka ya kisheria hata kidogo," ya kumvua Kabila kinga yake ya urais.
Afisa huyo mwenye umri wa miaka 38 aliongeza kuwa ingawa hakuna aliye juu ya sheria, Mahakama ya Katiba inapaswa kuamua juu ya ombi hili "kama wana ushahidi wa kutosha" dhidi ya Kabila.
Unaweza pia kusoma:
Mifupa ya kale ya India yapata nyumba ya makumbusho miaka sita baada ya kufukuliwa

Chanzo cha picha, Kushal Batunge/BBC
Mkono wa kulia wa kiunzi umekaa kwenye mapaja yake na mkono wake wa kushoto ukiwa umening'inia hewani, kana kwamba umeegemea kwenye fimbo.
Mifupa ya binadamu mwenye umri wa miaka 1,000 ambaye alizikwa akiwa ameketi nchini India imehamishwa hadi kwenye jumba la makumbusho miaka sita baada ya kuchimbwa.
BBC ilikuwa imeripoti mapema mwezi huu kwamba mifupa hiyo ilikuwa imeachwa ndani ya makazi yasiyokuwa na ulinzi ya turubai karibu na eneo la uchimbaji katika jimbo la Gujarat magharibi tangu 2019 kwasababu ya mabishano ya ukiritimba.
Siku ya Alhamisi, mifupa ilihamishiwa kwenye jumba la makumbusho la eneo hilo, maili chache tu kutoka mahali ilipochimbuliwa.
Mamlaka zinasema kuwa itaonyeshwa kwa umma baada ya taratibu za kiutawala kukamilika.
Unaweza pia kusoma:
Idadi ya mabilionea yapungua Uingereza huku Mfalme akiongezeka katika Orodha ya Matajiri- Sunday Times

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mfalme huyo sasa anakadiriwa kuwa na thamani ya £270m zaidi ya marehemu mama yake Malkia Idadi ya mabilionea wa Uingereza imepungua huku utajiri wa kibinafsi wa Mfalme Charles ukipanda na kufikia sawa na wa waziri mkuu wa zamani Rishi Sunak na mkewe Akshata Murty, kulingana na Orodha ya hivi punde ya Sunday Times.
Orodha ya kila mwaka ya watu 350 tajiri zaidi nchini Uingereza ilifichua kupungua kwa mabilionea katika historia ya jarida hilo.
Wakati huo huo katika mwaka uliopita, utajiri wa Mfalme umeongezeka kwa £30m hadi £640m, na kuongeza nafasi 20 hadi 258 akiwa na Sunak na Murty.
Wanaoongoza orodha hiyo kwa mwaka wa nne mfululizo ni familia ya Hinduja nyuma ya shirika la India la Hinduja Group, ambalo, licha ya kupungua kwa utajiri, limerekodiwa kuwa na thamani ya zaidi ya bilioni 35.
Idadi ya mabilionea ilipungua hadi 156 mwaka huu kutoka 165 mwaka 2024, idadi hiyo ikiongesha kupungua kwa kasi zaidi katika historia ya miaka 37 ya Orodha ya Matajiri ya Sunday Times.
Unaweza pia kusoma:
Chama cha Tigray kinasema marufuku dhidi yake inatishia makubaliano ya amani ya Ethiopia

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Kujivuta kwa juhudi za utekelezaji wa makubaliano ya amani kumeibua hofu ya kuzuka tena kwa ghasi huko Tigray Chama kikuu cha upinzani nchini Ethiopia kimetoa wito kwa Umoja wa Afrika kuingilia kati juhudi za upatanishi kati yake na serikali baada ya bodi ya uchaguzi kubatilisha hadhi yake ya kisheria kama chama.
Chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) kinasema hatua ya kukipiga marufuku kufanya shughuli zozote za kisiasa ni "hatari" na ni "tishio kubwa" kwa makubaliano ya 2022 ambayo yalimaliza miaka miwili ya mzozo katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.
Chama hicho kinachotawala Tigray na kutawala nchi nzima kwa miaka mingi, kilipigwa marufuku Jumatano kwa kushindwa kufanya mkutano mkuu.
Uamuzi huo unafuatia miezi kadhaa ya mvutano wa kisiasa huko Tigray na unakuja kabla ya uchaguzi wa nchi nzima ambao unatarajiwa kufanyika Juni mwaka ujao.
Chama hicho kiliongoza muungano ambao ulifanya mapinduzi ya 1991 na kutawala Ethiopia hadi 2018 wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipoingia madarakani.
Ilipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili dhidi ya serikali vilivyomalizika kwa makubaliano yaliyotiwa saini Novemba 2022 baada ya maelfu ya watu kuuawa na mamilioni kufurushwa makwao kaskazini mwa Ethiopia.
Pia unaweza kusoma:
Bunge la Uganda laidhinisha matumizi ya serikali ya 2025/26 yaliyopendekezwa

Chanzo cha picha, Reuters
Wabunge wa Uganda wameidhinisha bajeti inayopendekezwa na serikali kwa mwaka wa fedha unaoanza Julai.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki itatumia shilingi trilioni 72.4 za Uganda (dola bilioni 20) katika mwaka wa fedha wa 2025/26 (Julai-Juni), ikiwa ni mabadiliko kidogo kutoka kwa matumizi ya mwaka unaoishia mwezi ujao ambayo yanafikia shilingi trilioni 72.1, bunge lilisema kwenye ujumbe wa mtandao wa kijamii wa X hapo jana Alhamisi.
"Bunge limezingatia na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka ya fedha 2025/2026," ilisema.
Bunge halikusema ni sekta zipi zitapokea fedha nyingi lakini serikali iliwahi kusema siku za nyuma, vipaumbele vya matumizi katika mwaka ujao wa fedha vitakuwa katika sekta ya kilimo, utalii na madini yakiwemo mafuta ya petroli.
Waziri wa Fedha Matia Kasaija anatazamiwa kuwasilisha bajeti hiyo bungeni rasmi Juni 12 na kutoa maelezo zaidi kuhusu mahali pesa hizo zitatumika.
Uganda inatekeleza miradi ya miundombinu ili kuanza uzalishaji wa kibiashara wa mafuta ghafi mwaka ujao.
Miundombinu hiyo inajumuisha bomba la mafuta ghafi lenye thamani ya dola bilioni 5 kusaidia nchi hiyo isiyo na bandari kusafirisha mafuta yake kwenye masoko ya kimataifa kupitia Tanzania.
DRC: Tume yaundwa kujadili kinga ya aliyekuwa Rais Joseph Kabila

Chanzo cha picha, Reuters
Tume Maalum umeundwa katika bunge la Jamhuri ya Kidemkrasi ya Congo, kuanza kujadili suala la kuondolewa kwa kinga ya kutokamatwa kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila.
Tume hiyo ina masaa 72 kuwasilisha ripoti yake kwa bunge la Seneta.
Mjadala huo uliofanyika wakati wa kipindi cha kikao maalum jana, Alhamisi.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa na mgawanyiko bungeni wengine wakiunga mkono hoja hiyo ilihali wengine wakirejelea kifungu cha 224 cha sheria za utaratibu wa Seneti, wakiamini kwamba utaratibu huu unapaswa kuwasilishwa kwa kupigiwa kura bungeni.
Ikiwa hoja ya kutaka aondolewe kinga itaungwa mkono, atapoteza hadhi yake ya kuwa seneta wa kudumu na hivyo basi kuweza kushtakiwa.
Kabila anashukiwa kuwa na uhusiano na Congo River Alliance, muungano wa makundi ya waasi.
Anashtakiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu, na kushiriki katika harakati za uchochezi.
Vitendo hivyo vinadaiwa kutokea baada ya muda wake wa urais.
Soma zaidi:
Marekani 'yasononeshwa' na hali ya kibinadamu Gaza

Chanzo cha picha, Reuters
Maoni yake yalikuja wakati Wapalestina wasiopungua 114 waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel siku ya Alhamisi, maafisa wa afya walisema.
Alipoulizwa na BBC ikiwa utawala wa Trump ulisalia nyuma ya vitendo vya kijeshi vya Israel kutokana na ukubwa wa mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel na mashambulizi yake dhidi ya hospitali, kwa mara nyingine tena alitoa wito kwa Hamas kujisalimisha na kuwaachilia mateka na kusema hakuwezi kuwa na amani maadamu kundi hilo lipo.
Gaza imekuwa ikizuiwa na Israeli kupata chakula na vifaa vingine vya kibinadamu kwa wiki 10 huku vikosi vya Israel vikizidisha mashambulizi kwa kile wanachosema ni wapiganaji wa Hamas na miundombinu kabla ya upanuzi uliopangwa wa mashambulizi yao ya ardhini huko Gaza.
Soma zaidi:
Mkurugenzi wa zamani wa FBI anachunguzwa kwa kinachodaiwa kuwa tishio kwa Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkurugenzi wa zamani wa FBI James Comey anachunguzwa na Huduma Maalum ya Usalama baada ya kushirikisha kisha kufuta ujumbe kwenye mtandao wa kijamii, ambao Warepublican walidai kuwa ulichochea ghasia dhidi ya Rais Donald Trump.
Comey alichapisha kwenye Instagram picha ya kombe la baharini lililoandika nambari "8647", ambayo aliandika: "Kombe la baharini kwenye matembezi yangu ya ufukweni."
Nambari 86 ni istilahi ya misimu ambayo fasiri zake ni pamoja na 'kukataa' au 'kuondoa', kulingana na kamusi ya Merriam-Webster, ambayo pia hivi karibuni imetumika kama neno linalomaanisha 'kuua'.
Trump ni rais wa 47 wa Marekani. Waziri wa Usalama wa Ndani Kristi Noem alidai kuwa ujumbe huo ulikuwa wito wa kuuawa kwa Trump, lakini Comey alisema anapinga ghasia.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, msemaji wa Huduma Maalum ya Usalama Anthony Guglielmi alisema: "Tunachunguza chochote ambacho kinaweza kuchukuliwa kama tishio dhidi ya walinzi wetu.
"Tunafahamu kuhusu ujumbe kwenye mitandao ya kijamii wa Mkurugenzi wa zamani wa FBI na tunachukulia matamshi kama haya kwa uzito mkubwa sana. Zaidi ya hayo, hatutoi maoni yoyote kuhusu masuala ya kijasusi ya ulinzi."
Comey alifuta ujumbe wa Instagram, akisema katika ufuatiliaji kwamba "alidhani [makombe ya baharini] yalikuwa ujumbe wa kisiasa".
"Sikugundua baadhi ya watu wanahusisha nambari hizo na ghasia," aliongeza. "Haijawahi kunitokea lakini napinga vurugu za aina yoyote kwa hivyo nilifuta ujumbe huo."
Soma zaidi:
Mahakama ya Juu Marekani yagawanyika katika kesi ya uraia wa kuzaliwa

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump amewasilisha kesi ya kusitisha uraia wa kuzaliwa katika Mahakama ya Juu Marekani siku ya Alhamisi, kwenye kesi ambayo inaweza kusaidia zaidi ajenda yake kuhusu uhamiaji na masuala mengine.
Kesi hiyo inauliza ikiwa majaji wa mahakama ya chini wanapaswa kuwa na uwezo wa kuzuia amri za rais kwa nchi nzima - kama walivyofanya katika kesi hii. Majaji hawakuonekana kufikia muafaka kwani walijadili pande zote mbili.
Mwanasheria mkuu wa Marekani alisema kuwa mahakama za chini zilivuka mamlaka yao, akiongeza kuwa mamlaka hii inapaswa kupunguzwa.
Wakati huo huo, wakili mkuu wa New Jersey – akitoa hoja zake kwa niaba ya kundi moja - alisema kumuunga mkono Trump kutaunda mfumo wa uraia wenye dosari.
Hii itazua "machafuko", alisema wakili, Jeremy Feigenbaum.
Haijabainika ni lini mahakama itatoa uamuzi wake. Iwapo itakubaliana na Trump, basi anaweza kuendelea na matumizi yake mapana ya maagizo ya rais kutekeleza ahadi za kampeni bila kusubiri idhini ya bunge – huku mahakama ikiwa na fursa ndogo sana ya kufanya ukaguzi.
Chris Brown ashitakiwa kwa kumshambulia mtu kwenye klabu ya Usiku

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Chris Brown akifanya onyesho katika Tamasha la Muziki la Tycoon huko Detroit, Michigan mwezi uliopita. Mwimbaji wa Marekani Chris Brown amefunguliwa mashtaka kwa madai ya kumdhuru mtu kwa kukusudia, kulingana na polisi wa Metropolitan.
Polisi inasema shtaka hilo linahusiana na madai ya kumshambulia mtu, ambayo inasemekana yalifanyika katika klabu ya burudani usiku katikati mwa London mnamo tarehe 19 Februari 2023.
Mwanamuziki huyo, 36, alikamatwa katika hoteli moja mjini Manchester asubuhi ya Alhamisi.
Bado anazuiliwa na atafikishwa katika mahakamani ya Manchester siku ya Ijumaa.
"Tumeidhinisha Polisi wa Metropolitan kumshtaki Chris Brown kwa kosa moja la kumdhuru mtu, kinyume na kifungu cha 18 cha Sheria ya Makosa dhidi ya Mtu 1861", Adele Kelly, naibu mwendesha mashtaka mkuu wa CPS London North.
Aliongeza kuwa "mashtaka ya uhalifu dhidi ya mshtakiwa huyu yapo hai" na "ana haki ya kusikilizwa kuwezesha mchakato kuendeshwa bila upendeleo".
Gazeti la The Sun lilisema mwimbaji huyo wa R&B alikuwa amewasili uwanja wa ndege wa Manchester kwa ndege ya kibinafsi Jumatano alasiri.
Kwa sasa yuko kwenye ziara na ameratibiwa kufanya maonyesho kadhaa kote Uingereza mnamo mwezi Juni na Julai.
Amani ya Ukraine iko kwa Trump na Putin yasema Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Marco Rubio amesema hana matarajio makubwa katika mazungumzo ya amani ya Ukraine na Urusi yanayotarajiwa kufanyika Uturuki - na kwamba Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin wanahitaji kukutana ili hatua iweze kupigwa.
"Sidhani tutapiga hatua hadi Rais Trump na Putin wazungumze moja kwa moja juu ya suala hii," alisema baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Nato kusini mwa Uturuki.
Volodymyr Zelensky alithibitisha kuwa Ukraine itatuma wajumbe kwa ajili ya mazungumzo hayo mjini Istanbul, lakini alikosoa ujumbe wa "ngazi ya chini" unaotumwa na Moscow.
Hata hivyo, msaidizi wa rais wa Urusi Vladimir Medinsky, alisisitiza kuwa timu ya Kremlin ina "uwezo wote muhimu".
Mapema siku hiyo, Trump - ambaye anazuru Mashariki ya Kati - pia alisema ilikuwa vigumu kupiga hatua kubwa katika mazungumzo ya amani hadi yeye na Putin wakutane ana kwa ana.
Mazungumzo ya Istanbul yanaashiria mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja kati ya Urusi na Ukraine tangu mwaka 2022.
Urusi imedokeza kuwa inataka kuendelea kuanzia pale walipoishia.
Yaliyokuwa yakijadiliwa yalijumuisha Ukraine kuwa nchi isiyoegemea upande wowote, kupunguza ukubwa wa jeshi lake na kuachana na matarajio ya uanachama wa Nato - masharti ambayo Ukraine imekataa mara kwa mara.
Mapigano nchini Ukraine yanaendelea, huku Urusi ikisema kuwa vikosi vyake vimeteka vijiji viwili zaidi katika eneo la mashariki la Dontesk siku ya Alhamisi.
Moscow sasa inadhibiti takriban 20% ya eneo la Ukraine, pamoja na rasi ya kusini ya Crimea ambayo ilitwaa kwa njia isiyo halali mnamo mwaka 2014.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 16/05/2025.
