Je, kurudi DR Congo kwa Joseph Kabila kuna maana gani wakati huu wa vita?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa zamani wa DR Congo, Joseph Kabila ameahidi kurejea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo baada ya kutokuwepo kwa miaka miwili.
Kurejea kwa Bw Kabila kutakuwa na maana gani katika eneo hilo lililokumbwa na vita, ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameteka eneo la Mashariki ya nchi, lenye utajiri wa madini na kuwalazimisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao?
Kabila alikua rais mwaka 2001 na kukaa madarakani karibu miaka 20. Muhula wake wa pili na wa mwisho wa kikatiba ulimalizika Desemba 2016, lakini alikataa kuondoka, na kusababisha maandamano mabaya.
Alifanikiwa kusalia madarakani kwa miaka miwili zaidi na hatimaye akakubali kuondoka madarakani mwaka 2018 kufuatia uchaguzi wa mwezi Desemba.
Januari 2019, alikabidhi madaraka kwa mrithi wake Félix Tshisekedi. Mwaka 2023, aliondoka DRC. Msemaji wake, Barbara Nzimbi, amerudia kusema aliondoka kwa sababu za kitaaluma.
Hata hivyo, Joseph Hammond, kutoka taasisi ya kupambana na misimamo mikali ya iDove, anasema maisha ya kisiasa ya Kabila hayakuwa imara kama angesalia DRC, hivyo kuondoka kwake kulikuwa kwa kimkakati.
"Akiiga mfano wa baba yake Laurent Kabila, alikwenda nje ya Congo. Nadhani aliondoka DRC katika juhudi za kuendeleza maisha yake ya kisiasa kwa njia nyingine," aliambia BBC.
Kabila anasema alikuwa akijishughulisha na programu za masomo katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Januari 2024, tasnifu yake ya udaktari kuhusu uhusiano wa siasa za Afrika na Marekani, China na Urusi iliidhinishwa katika Chuo Kikuu cha Johannesburg.
Wakati akiwa nje ya DRC, Kabila pia alitembelea nchi nyingine kadhaa za Afrika, ikiwa ni pamoja na Ethiopia, ambako alikutana na viongozi wa upinzani Moïse Katumbi na Claudel Lubaya mjini Addis Ababa; na Namibia, ambako alihudhuria mazishi ya Rais wa kwanza wa Namibia, Sam Nujoma.
Kuibuka kwa M23

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwishoni mwa 2021, M23 ilianza kuibuka tena na iliendelea kusonga mbele kimkakati na kupata kasi zaidi mwaka 2023 na 2024.
Mapema mwaka huu, waasi wa M23 walisonga mbele na kuchukua udhibiti wa miji miwili muhimu - Goma na Bukavu. Takriban watu 8,500 wameuawa tangu mapigano yalipoongezeka mwezi Januari, kulingana na serikali ya Congo.
Kulingana na UN, Wakongo milioni 5.6 ni wakimbizi wa ndani DRC, na zaidi ya milioni 4 wanatoka katika majimbo ya mashariki ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri.
Desemba mwaka jana, mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Angola yalivunjika baada ya Rwanda kuitaka serikali ya DRC kuzungumza moja kwa moja na M23. Licha ya shinikizo la kimataifa kuongezeka, viongozi mjini Kinshasa walikataa kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na waasi.
Katika mahojiano na BBC, Waziri Mkuu wa DRC Judith Suminwa Tuluka alisema serikali yake inataka kufanya mazungumzo na nchi jirani ya Rwanda, ambayo inaituhumu kuunga mkono M23.
Mwezi Machi, Rais wa DRC Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame walitoa wito wa "kusitishwa mara moja kwa mapigano" mashariki mwa DR Congo, baada ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja nchini Qatar.
Kwa nini Kabila anarudi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika taarifa yake, Joseph Kabila alisema kurejea kwake kumechochewa na nia ya kusaidia kutatua mzozo unaozidi kuwa mbaya wa kitaasisi na kiusalama nchini DRC.
Pia aliliambia jarida la lugha ya Kifaransa la Jeune Afrique anataka "kuchukua jukumu la kutafuta suluhu baada ya miaka sita ya kuwa nje na mwaka mmoja uhamishoni."
Lakini kuna uvumi kwamba ana nia nyingine.
Tshisekedi amemshutumu Kabila hadharani kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na Alliance Fleuve Congo – muungano wa waasi ambao M23 ni sehemu yake.
Kabila amekanusha tuhuma hili.
Ben Radley, mwanauchumi na mhadhiri wa maendeleo ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Bath ameiambia BBC, Kabila ana uhusiano na waasi.
"Baadhi ya wachambuzi wanasema kiongozi wa AFC, Corneille Nangaa, aliyekuwa mkuu wa zamani wa tume ya uchaguzi chini ya Kabila na mshirika wa karibu wa Kabila, hilo huenda linamaanisha Kabila anahusika na uasi," anasema.
Kurejea kwa Kabila hakika kuna utata na viongozi wa Kinshasa hawaoni kwamba hilo ni jambo zuri.
Waziri wa mambo ya nje Thérèse Kayikwamba Wagner, alisema serikali ya Congo haihitaji kuhusika kwa Kabila katika kutatua mzozo wa usalama katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Kulingana Joseph Hammond, kurejea kwa Kabila kuna uwezekano wa kuleta amani mashariki mwa DRC ikizingatiwa kwamba bado ni maarufu katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo - lakini pia kunaweza kuzidisha mzozo wa kisiasa nchini humo.
"Naamini ana uwezo wa kuleta makubaliano ya amani na M23 ikiwa atataka kufanya hivyo, ingawa nadhani analiona suala la M23 kama fursa kwake kujiimarisha ndani ya siasa za DRC kwa kiwango cha juu," anasema.
Radley anakubali kwamba Kabila ana uzito wa kutosha wa kisiasa na uwezo wa kusaidia kuleta mazungumzo kati ya serikali na waasi.
"Kabila amekuwa mkosoaji mkubwa wa Tshisekedi tangu alipoondoka madarakani, hivyo haijulikani ni jinsi gani Tshisekedi atakuwa tayari kuhudhuria mazungumzo yoyote yanayopatanishwa na Kabila," anasema.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi












