Kwanini Ethiopia na Eritrea zinakaribia kuingia vitani?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Maadui wa muda mrefu, Ethiopia na Eritrea, wanaweza kuwa wanakaribia kuingia vitani, maafisa katika eneo lenye machafuko la Ethiopia ambalo liko katikati ya mzozo huo wameonya.
Hilo likitokea huenda likasababisha janga jingine la kibinadamu katika Pembe ya Afrika.
Mapigano ya moja kwa moja kati ya majeshi mawili makubwa zaidi barani Afrika yataashiria kikomo cha maridhiano ya kihistoria ambayo yalimpa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019, na yanaweza kuvutia mataifa mengine ya kikanda, wachambuzi wamesema.
Vita hivyo pia vinaweza kuzua mgogoro mwingine katika eneo ambalo kupunguzwa kwa misaada kumeathiri juhudi za kusaidia mamilioni ya watu waliokumbwa na migogoro ya ndani nchini Sudan, Somalia, na Ethiopia.
Kwanini wasiwasi wa vita umeibuka?

Chanzo cha picha, EDUARDO SOTERAS
Wasiwasi wa vita kuzuka upya unatokana na kutokuwa na utulivu mpya katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia, ambapo vita vya kiraia vya kati ya 2020 na 2022 vilisababisha vifo vya maelfu ya watu.
Siku ya Ijumaa tarehe 14 mwezi Machi 2025 kundi la waasi la chama cha kisiasa kikuu cha kaskazini mwa Ethiopia ya Tigray kimeteka ofisi za meya na chombo cha habari cha redio cha mkoa huo, Mekelle, kukizidisha hofu ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mkaazi mmoja wa Mekelle ameiambia BBC kuwa watu wameharakisha kutoa pesa walizokuwa wamehifadhi kwa benki wakihofia hali ya usalama kuzorota zaidi.
Wakati wa vita, vikosi vya Eritrea vilivuka mpaka na kuingia Tigray, vikiongoza mapigano kwa niaba ya jeshi la shirikisho la Ethiopia dhidi ya waasi waliokuwa wakiongozwa na chama tawala cha eneo hilo, Tigray People's Liberation Front (TPLF).
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, mkataba wa amani ulioafikiwa Mwezi Novemba 2022 ulileta mgawanyiko mkubwa kati ya Ethiopia na Eritrea, ambayo haikushirikishwa katika mazungumzo ya amani.
TPLF, ambayo ilikuwa ikiongoza utawala wa mpito wa Tigray kwa msaada wa serikali kuu, iligawanyika baada ya makubaliano hayo.
Kikundi cha upinzani kiliteka mji wa Adigrat wiki hii, kikiwashutumu walioko madarakani kwa kutetea maslahi ya Tigray, huku utawala wa mpito ukilaumu waasi hao kwa kushirikiana na Eritrea.
Kila upande unakanusha tuhuma za mwingine.
Linalozua hofu pia ni kauli ya afisa wa Tigray aliyeitoa hivi majuzi.
Wakati wowote vita kati ya Ethiopia na Eritrea vinaweza kuanza," Jenerali Tsadkan Gebretensae, makamu wa rais katika serikali ya mpito ya Tigray, aliandika katika jarida, The Africa Report, siku ya Jumatatu.
Wataalamu wanasema kuwa mgogoro huu unaweza kupelekea Ethiopia na Eritrea kuunga mkono makundi pinzani katika Tigray na hatimaye kuingia katika mizozo ya moja kwa moja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyanzo vya kidiplomasia na maafisa wa Tigray, Eritrea iliagiza kuhamasisha jeshi nchi nzima mwezi Februari, na Ethiopia ikatuma majeshi yake kuelekea mpaka wa Eritrea.
Hata hivyo, wawakilishi wa serikali za Eritrea na Ethiopia hawajazungumzia lolote kuhusu hilo.
Historia ya Uhusiano wa Ethiopia na Eritrea

Eritrea, ambayo ilikuwa koloni la Italia, ilitekwa na Ethiopia mwaka 1962.
Baada ya mapigano ya miongo mitatu yaliyofanywa na waasi wa Eritrea chini ya uongozi wa Isaias Afwerki, Eritrea ilipata uhuru wake mwaka 1993.
Hali ya uhusiano kati ya Eritrea na Ethiopia ilikuwa ya kirafiki mwanzoni, kwani waasi wa Tigray waliounga mkono serikali ya Ethiopia walimuondoa mtawala wa kijeshi wa Ethiopia, Mengistu Haile Mariam, mwaka 1991 kwa msaada wa waasi wa Isaias.
Hata hivyo, mvutano ulianza mwaka 1998 kati ya nchi hizi mbili kuhusu umiliki wa mji wa Badme, hali iliyosababisha vita vya miaka miwili na kusababisha vifo vya watu takriban 80,000.
Nchi hizo mbili zilikuwa katika hali ya vita rasmi hadi mwaka 2018, wakati Rais Isaias wa Eritrea na Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia, Abiy Ahmed, walikubaliana kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kurejesha uhusiano wa kiuchumi.
Makubaliano hayo yalileta upatanishi, kurudisha familia zilizokuwa zimegawanyika kwa miongo miwili, na kuruhusu safari za moja kwa moja kati ya miji mikuu ya Addis Ababa na Asmara.
Aidha, ahadi zilitolewa za kushirikiana katika kukuza bandari za Eritrea.
Kwa nini uhusiano kati ya Ethiopia na Eritrea umeharibika?
Uhusiano wa nchi hizi ulianza kudorora mwishoni mwa vita vya Tigray, wakati Ethiopia iliposaini Mkataba wa Pretoria na TPLF kumaliza mapigano.
Wasomi wanasema kuwa Eritrea ilikasirishwa kwa kutojumuishwa katika makubaliano hayo, ambayo yaliwaruhusu waasi wa TPLF, ambao Eritrea ina uadui nao mkubwa, kutawala Tigray.
Baadhi ya vikosi vya Eritrea vimeendelea kubaki katika ardhi ya Ethiopia, licha ya mkataba kuagiza kuondolewa kwa vikosi vyote vya kigeni.
Hata hivyo, Asmara haijajibu moja kwa moja tuhuma hizi.
Maafisa wa Eritrea pia wameonyesha kutoridhika na kauli za mara kwa mara za Waziri Mkuu Abiy tangu 2023, akisema kuwa Ethiopia, ingawa haina pwani, ina haki ya kupata ufikivu wa baharini.
Kauli hii imeonekana kama tishio la kijeshi kwa Eritrea, ambayo iko kwenye pwani ya Bahari ya Shamu.
Mnamo Septemba mwaka jana, Ethiopian Airlines ilisitisha safari za ndege kuelekea Eritrea, hali ambayo ilionyesha mporomoko wa uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Taarifa zinaonyesha kuwa akaunti ya benki ya kampuni hiyo ilifungiwa nchini Eritrea.
Aidha, mwezi mmoja baadaye, Eritrea ilisaini mkataba wa usalama na Misri na Somalia, mkataba ambao uliona kama hatua ya kukabiliana na mwelekeo wa Ethiopia wa kutaka kupanua mipaka yake.
Kuna uhasama wa wazi kati ya Ethiopia na Eritrea," Getachew aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu wiki iliyopita.
"Kinachonitia wasiwasi ni kwamba watu wa Tigray wanaweza tena kuwa waathirika wa vita nyingine".
Nchi zingine zimejibu vipi kuhusu wasiwasi wa vita
Nchi kadhaa zikiwemo Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya zimeonya kuhusu mvutano huo unaozidi kuongezeka, zikisema lazima "Vita visizuke tena".
Siku ya Alhamisi, Ufaransa ilitoa wito kwa raia wake huko Tigray "kuhifadhi vifaa vya dharura na kuchukua tahadhari kubwa". Katika taarifa, Umoja wa Afrika ulisema unafuatilia matukio ya Tigray kwa "wasiwasi mkubwa".















