Mzozo wa Tigray: Msaada mkubwa wa kibinadamu unahitajika

Wahudumu wa shirika la msalaba mwekundu wakitoa msaada kwa waathirika

Chanzo cha picha, Reuters

Mahitaji ya watu walioathirika na mapigano ya jimboni Tigray nchini Ethiopia ni ''makubwa mno'', Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu limetahadharisha.

''Watu wa Tigray... wamepoteza msimu wa mavuno,'' Mkurugenzi wa operesheni wa ICRC, Dominik Stillhart, ameiambia BBC wakati wa ziara yake Ethiopia.

Alisema kuwa kulikuwa na '' masuala muhimu yanayohusu huduma za afya'' kuwafikia wahitaji.

Serikali ya Ethiopia awali ilisema kuwa watu milioni 1.5 walifikiwa.

Maelfu ya watu wanaripotiwa kuuawa na karibu milioni mbili wameyakimbia makazi yao.

Karibu wakimbizi 100,000 wa Eritrea waliokuwa wakiishi katika makambi ya wakimbizi ya UN katika jimbo Tigray wamekwama katika mzozo huo.

Mzozo huo uliibuka mwezi Novemba baada ya chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) kudhibiti kambi kadhaa za kijeshi Tigray baada ya kuvunjika kwa mahusiano na serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed mjini Addis Ababa.

Serikali kuu- ambayo imejitangazia ushindi- ilizuia kuingia Tigray hasa vyombo vya habari na mashirika ya misaada.

Sababu ya mzozo

TPLF ilikuwa chama tawala huko Tigray, na takriban wapiganaji 250,000 chini ya uongozi wake, kwa karibu miaka 30.

Iliondolewa mamlakani tarehe 28 mwezi Novemba baada ya wanajeshi wa serikali ya Ethiopia kuteka mji wa Mekelle.

Bwana Abiy aliishutumu TPLF kwa vitisho dhidi ya mamlaka ya Ethiopia, na kujaribu kupindua serikali yake kwa kuteka vituo vya jeshi mapema mwezi huo