Ali Bongo ni nani: Huu hapa ni wasifu wa Rais wa Gabon

Rais wa Gabon, Ali Bongo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maafisa wa jeshi wameonekana kwenye televisheni ya taifa nchini Gabon wakisema wamechukua mamlaka.

Walisema wanafuta matokeo ya uchaguzi wa Jumamosi, ambapo Rais Ali Bongo alitangazwa mshindi.

Tume ya uchaguzi ilisema Bw Bongo alishinda chini ya thuluthi mbili tu ya kura katika uchaguzi ambao upinzani ulidai kuwa ulikuwa wa udanganyifu.

Kupinduliwa kwake kutakomesha familia yake iliyodumu kwa miaka 53 madarakani nchini Gabon.

Wanajeshi 12 walionekana kwenye televisheni wakitangaza kuwa wanafuta matokeo ya uchaguzi na kuvunja "taasisi zote za jamhuri".

Mmoja wa wanajeshi hao alisema kwenye chaneli ya televisheni ya Gabon 24: "Tumeamua kulinda amani kwa kukomesha utawala uliopo." Hii, aliongeza, ilikuwa chini ya "utawala usiowajibika, usiotabirika na kusababisha kuzorota kwa uwiano wa kijamii ambao unahatarisha nchi katika machafuko".

Lakini je Ali Bongo ni nani?

Ali Bongo Ondimba alizaliwa Februari 9 mwaka 1959 mjini Brazzaville na alifahamika kama mwana wa Alain Bernard Bongo (ambaye baadaye alifahamika kama Omar Bongo Ondimba) na Josephin Kama (baadaye Patience Dabany).

Kumekuwa na mjadala ikiwa Ali Bongo ni mwana wa Omar Bongo ikizingatiwa kuwa mama yake alikuwa mja mzito miezi 18 kabla ya kuolewa madai ambayo Ali Bongo amekuwa akipinga. Aidha, wakati wa kuzaliwa kwake mamake alikuwa na miaka 15.

Baada ya kusomea uwanasheria Ali Bongo alijitosa katika siasa za Gabon ambapo alijiunga na chama PDG mwaka 1981 na muda mfupi baadae aliteuliwa katika kamati kuu ya chama mwezi Machi mwaka 1983.

Baadae aliteuliwa kumwakilisha baba yake katika chama hicho nafasi ambayo ilimwezesha kujiunga na asasi kuu ya uongozi wa chama katika uamuzi ambao ulifikiwa katika kongamano maalum ya PDG mwaka 1986.

Ali Bongo ni mwana wa kiume wa rais Omar Bongo, ambaye aliongoza Gabon kiimla kutoka mwaka 1967 hadi alipofariki dunia mwaka 2009.

Mke wa Ali Bongo, Sylvia Bongo Ondimba, na watoto

Chanzo cha picha, Sylvia Bongo Ondimba/ Instagram

Maelezo ya picha, Ali Bongo amemuoa mzaliwa wa Ufaransa Sylvia, ambaye hapa anaonekaa akiwa na watoto wao wanne

Wakati wa utawala wa baba yake Ali Bongo aliwahi kuhudumu kama waziri wa mambo ya nje wa wa Gabon kati ya mwaka 1989 na 1991.

Pia aliwahi kuhudumu kama naibu kiongozi wa bunge la kitaifa kuanzia mwaka 1991 hadi 1999.

Wakati wa uchaguzi wa uraisi wa mwaka 2005 alifanya kazi kama mshirikishi wa vijana katika kampaini ya baba yake.

Baada ya uchaguzi huo alipandishwa cheo na kuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Gabon kuanzia Januari 21 mwaka 2006 huku akiendelea kushikilia wadhifa wa waziri wa ulinzi.

Rais Ali Bongo wa Gabon
Maelezo ya picha, Rais Ali Bongo wa Gabon

Alishikilia wadhifa huo hadi mwaka 2009.

Ali Bongo alitarajiwa kuwa mrithi wa baba yake Omar Bongo ikizingatiwa kuwa alimteua katika nyadhifa muhimu katika utawala wake.

Hata hivyo uungwaji mkono wa Ali Bongo ndani ya uongozi wa chama cha PDG ulihojiwa na vyombo vya habari na kulikuwa na maoni kwamba raia wengi wa Gabon walimchukulia kama ''mtoto aliyedekezwa na kwamba hawezi kuwasiliana kwa lugha asilia ya nyumbani kwasababu alizaliwa Congo-Brazzaville, kulelewa nchini Ufaransa.

Kufuatia kifo cha Baba yake aliyekuwa madarakani kwa miaka 41, alichaguliwa kuendelea na uongozi wa taifa hilo mwezi Agosti mwaka 2009.

Siku chache baada ya uchaguzi uliyofanyika Agosti 30 mwaka 2009 alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata 42% ya kura.

Matokeo ya uchaguzi huo yaliidhinishwa mara moja na mahakama ya kikatiba.

Upinzani ulipinga matokeo hayo rasmi ya uchaguzi ukidai kuwa ulikumbwa na udanganyifu.

Hatua ambayo ilisababisha maandamano makubwa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Gabon.

Nyota wa Argentina na Barcelona Lionel Messi alizuru Gabon mwaka 2015

Chanzo cha picha, Steve Jordan/AFP/Getty Images

Maelezo ya picha, Nyota wa Argentina na Barcelona Lionel Messi alizuru Gabon mwaka 2015

Ili kujibu madai hayo mahakama ya katiba iliamuru kuwa kura za uchaguzi wa uraisi zihesabiwe upya.

Ali Bongo aliibuka tena mshindi baada ya kupata 41.79% ya kura zote zilizopigwa wakati wa uchaguzi uliyofanyika oktoba 12 mwaka 2009.

Aliapishwa kuwa raisi wa Gabon oktoba 16 katika hafla iliyohudhuriwa na marais kadhaa wa mataifa ya Afrika.

Rais Ali Bongo ana mke na watoto wanne.