Mgogoro wa Ethiopia wa Tigray: Jinsi TPLF ilivyolizidi maarifa jeshi la Ethiopia

Chanzo cha picha, AFP
Wakati mmoja jeshi la Ethiopia lilikuwa na nguvu na uwezo wa kipekee uliolifanya kuheshimiwa na Marekani, lakini sasa limepata hasara kubwa kwenye mstari wa mbele kwamba serikali imechukua hatua ya ajabu ya kutoa wito kwa raia wa kawaida kujiunga na vita dhidi ya waasi wa Tigrayan.
Ni ishara ya mabadiliko makubwa katika katika mafanikio ya jeshi hilo
Mwaka mmoja uliopita ilikiondoa chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) kama chama tawala katika eneo la kaskazini la Tigray - sasa wapiganaji wa kundi hilo wanachukua miji katika njia ya kuelekea mji mkuu, Addis Ababa.
"Wapiganaji wa TPLF walilimwaga damu ya jeshi kwanza kupitia vita vya msituni Tigray kwa kufanya mashambulizi ya kuvizia ," mchambuzi wa Pembe ya Afrika mwenye makazi yake Marekani Faisal Roble anaelezea.
"Kisha wakaingia kwenye vita ili kulimaliza."
Hata hivyo, Achamyaleh Tamiru - mwanauchumi na mchambuzi wa kisiasa wa Ethiopia - anaamini kuwa hatua za TPLF ni "za muda mfupi tu".
"Waethiopia kutoka matabaka yote wanajitokeza kutetea na kuikomboa Ethiopia," alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbinu za wapiganaji wa TPLF zinamkumbusha mhariri wa zamani wa BBC Tigrinya Samuel Ghebhrehiwet maisha yake kama mpiganaji wa msituni wa Eritrea ambaye, pamoja na Watigraya, walipigana na utawala wa Mengistu Haile Mariam wa Ethiopia hadi ulipopinduliwa mwaka 1991.
Walikuwa "na silaha nyepesi, wepesi sana, wakiishi kwa chakula cha kujikimu, na wakionyesha uthabiti wa kina na azimio".
Eritrea iliweza kujinyakulia uhuru wake, huku TPLF ikichukua mamlaka nchini Ethiopia - ingawa utawala wake wa kisiasa ulifikia kikomo mwaka 2018 kufuatia maandamano makubwa.
Viongozi wake walirudi Tigray ambapo kundi hilo lilifyatua risasi katika mzozo wa sasa mapema Novemba 2020 kwa kuanzisha mashambulizi kwenye kambi ya kijeshi ya serikali kuu kwa msaada wa wafuasi watiifu katika jeshi - ikiwa ni pamoja na makamanda na askari - ambao walijitenga na safu yake.
Sio tu kwamba hifadhi kubwa ya silaha ilikamatwa, lakini maafisa wa ngazi za juu na askari waliokataa kusalimu amri waliuawa au kukamatwa kwa maelfu yao.
"Shambulio la usiku kwenye kambi hiyo limezua pengo ambalo linaifanya Ethiopia kutokuwa na jeshi la serikali," Bw Achamyeleh alisema.
Hata hivyo, wanajeshi - kwa msaada muhimu kutoka kwa jeshi la Eritrea, na vikosi na wanamgambo kutoka eneo la Amhara nchini Ethiopia - walishinda changamoto hiyo, na kuanzisha mashambulizi ya angani na mashambulizi ya ardhini ambayo yalipelekea TPLF kuondolewa mamlakani huko Tigray chini ya mwezi mmoja.
Lakini, Bw Samuel alisema, walipofanya ukatili mkubwa dhidi ya raia - ikiwa ni pamoja na kubaka, kuua na kuchoma mimea - Watigraya kutoka "tabaka zote za jamii kisha wakajiunga na TPLF kulinda hadhi zao".
"Wazazi waliwaambia watoto wao: 'Badala ya kufa nyumbani nenda upigane.' Ikawa vita kati ya watu wa Tigray na jeshi - sio tu vita kati ya TPLF na jeshi."

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na Bw Roble, majenerali wa zamani ambao walikuwa wamestaafu au waliohama walienda kwenye milima na mapango ya Tigray kuunda Kikosi cha Ulinzi cha Tigray (TDF) kama tawi la kijeshi la TPLF ili kuhakikisha kwamba makumi ya maelfu ya wanajeshi wapya wamejipanga vyema.
"Majenerali hawa waliona ni jukumu lao kuwalinda raia wa Tigray. Kwa ujuzi wao wa ndani wa jeshi walipanga kulishinda jeshi la Ethiopia ," Bw Roble alisema.
Huku wapiganaji wa Tigraya sasa wakiwa chini ya kilomita 300 (maili 185) kutoka mji mkuu, ni wazi kwa sasa wana uwezo mkubwa juu ya jeshi ambalo lilikuwa moja ya majeshi yenye nguvu zaidi barani Afrika, anasema.
"Ethiopia ilikuwa mshirika nambari moja wa Marekani katika kile kinachoitwa vita dhidi ya ugaidi katika Pembe ya Afrika, hasa nchini Somalia, ambako ilipindua Muungano wa Mahakama za Kiislamu [mtangulizi wa al-Shabab]. Marekani ilifadhili jeshi hilo, ikaipatia silaha, na hata kuwapa wanajeshi wake vyakula vilivyo tayari kuliwa," Bw Roble alisema.
"Na Umoja wa Afrika uliitegemea kwa misheni za kulinda amani, lakini Ethiopia yenyewe sasa haina utulivu na jeshi lake sasa gogo tu la uthabiti wake wa zamani ."
Chanzo cha mzozo na mabadiliko
Matatizo kwa TPLF yalianza wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipoingia madarakani mwezi Aprili 2018, kufuatia idadi kubwa ya watu kutoka makabila mawili makubwa ya Ethiopia - Oromos na Amharas - kufanya maandamano dhidi ya miaka 27 ya uongozi wa kundi hilo serikalini.
Bw. Abiy alipendekeza mageuzi makubwa, na kusababisha mpasuko mkubwa ama kutoelewa na TPLF.

"Watigrinya ni takriban 6% tu ya watu nchini humo na wakati TPLF ilikuwa mamlakani, iliunda mfumo wa shirikisho ambao uliyapa makabila kuwa na majimbo yao ya kikanda," Bw Roble alisema.
"TPLF ilihisi kuwa Bw. Abiy [kutoka kabila la Oromo] alitaka kuweka mamlaka kuu. Hilo likasababisha mzozo mkubwa kati yao na hatimaye kusababisha vita," Bw Roble alisema.
Alex de Waal, mkurugenzi mtendaji wa Wakfu wa Amani ya Dunia yenye makao yake nchini Marekani, alisema kuwa Bw Abiy pia alidhamiria kulifanyia marekebisho jeshi la nchi hiyo ili kuhakikisha linakuwa jeshi tiifu kwake, na kushughulikia wasiwasi kuhusu utawala wa Tigrinya.
"Watigrinya waliunda takriban 18% ya jeshi lote. Idadi yao ilikuwa kubwa ikilinganishwa na idadi ya watu. Bw Abiy alianza mageuzi ya kuwaondoa Watigrinya, na kuunda jeshi aminifu kwake," Prof De Waal alisema.
"Mabadiliko hayo yalivuruga jeshi, na kuondoa mshikamano. Bw Abiy hakuwa na muda wa kuliunda upya kabla ya vita kuanza."
Alisema kati ya vitengo 20 vya jeshi hilo, Vitengo 10 - vinavyoundwa na askari wapatao 5,000 kila kitengo- vimesambaratishwa, na askari wasiopungua 10,000 waliuawa na idadi sawa na hiyo kukamatwa.
BBC ilijaribu kupata kauli ya msemaji wa Ulinzi wa Taifa wa Ethiopia, lakini haikujibiwa.
Mashambulizi na ushirikishwaji wa raia
Baada ya kutwaa tena sehemu kubwa ya jimbo la Tigray mwezi Juni, TPLF ilianzisha mashambulizi katika maeneo jirani ya Amhara na Afar, huku Bw Abiy akitoa wito kwa Waethiopia wote wenye uwezo kujiunga na jeshi kusaidia kukabiliana na waasi.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Ili kuzuia harakati za TPLF, jeshi lilipanga [huko Amhara] mashambulizi kwa kuwatumia wakulima, wanafunzi na vijana wa mijini. Walikuwa na shauku ya kulinda ardhi yao lakini walikuwa na mafunzo ya kimsingi ya wiki chache tu, kama sehemu ya Kikosi cha Ulinzi cha Tigray (TDF) . " Prof De Waal alisema.
"Hawakuweza kukaa nyumbani bila kufanya kazi wakati wanamgambo wa TPLF walipokuwa wakipita nyumba kwa nyumba kuwasaka watu wa amhara, kuwaua akina mama na kuwabaka binti zao."
"Inaleta hali ngumu ya haki za binadamu kwa sababu inafifisha tofauti kati ya mpiganaji na raia. Pia inaongeza chuki na inafanya kuwa vigumu zaidi kufikia amani na upatanisho."
Majadiliano sio ukamataji
TPLF pia inahusika katika mashambulizi yanayoendelea yenye lengo la kuizingira Addis Ababa - ambayo ina wakazi zaidi ya milioni tano.

Chanzo cha picha, Getty Images
"TPLF wanaipa shinikizo serikali ya Abey kufanya mazungumzo. Sidhani kama wataingia Addis Ababa. Hawakubaliki sana huko," anasema Bw Samuel.
Prof De Waal anasema serikali inakabiliwa na "kushindwa kijeshi, lakini TPLF haiwezi kudai imeshinda kwa sababu kushinda siasa.
"Wanahitaji uungwaji mkono na ushirikiano wa idadi ya kutosha ya watendaji wa kisiasa, ambao hawana.
"Kwa hiyo itabidi kuwe na mazungumzo, na lengo la TPLF litakuwa katika kupata mustakabali wa Tigray."














