Je, binti wa Kim Jong Un anaweza kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini?

Chanzo cha picha, KCNA VIA KNS via AFP
Wakati kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, anaitishia Seoul na kuapa kuendelea kupanua mpango wake wa silaha za nyuklia zilizowekewa vikwazo, swali ambalo wengi wanajiuliza ni iwapo binti yake mwenye umri wa miaka 13 atatangazwa rasmi kuwa mrithi wake.
Hakujakua na ishara ya hilo kufanyika wiki iliyopita.
Ila mjadala umeibuliwa kuhusu uwezekano wa Kim Ju Ae, kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini, taifa lenye watu millioni 25, na ambayo imeongozwa na wanafamilia wa Kim pekee.
Katika mkutano wa wafanyikazi wa Party Congress, ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano, ujumbe wa Kim katika mkutano huu hufuatiliwa kwa karibu na Seoul na Washington.
Lakini wakati huu mtazamo umebadilika. Wiki iliyopita, shirika la ujasusi la Seoul liliwapa wabunge taarifa kwamba linaamini Kim amemchagua binti yake kuwa mrithi wake, na kwamba alionekana kutoa maoni yake kuhusu masuala ya sera.
Ingawa siku za hivi karibuni ameonekana zaidi kando ya baba yake katika vyombo vya habari, mengi kumhusu bado ni fumbo. Korea Kaskazini haijawahi kuchapisha jina au umri wake.
Uwepo wake ulitangazwa kwa mara ya kwanza hadharani wakati nyota wa mpira wa kikapu Dennis Rodman alipoambia gazeti la The Guardian jina lake baada ya ziara yake mjini Pyongyang mwaka 2013. Inadhaniwa kuwa ana miaka 13, kutokana na makadirio ya ripoti za uchunguzi.
"Ilikuwa makosa ya kijasusi" alisema Cheong Seong-chang, mfuatiliaji wa Korea Kaskazini na makamu wa rais wa Taasisi ya Sejong, ambaye alikuwa mtetezi wa mapema wa nadharia kwamba Ju Ae atakuwa mrithi wa Kim.
Cheong na wachambuzi wengine wanaamini kuwa Ju Ae, ndiye binti mkubwa wa Kim na ana dadayake mwenye umri wa miaka tisa.
Ju Ae, alionekana mara ya kwanza katika televisheni ya kitaifa mwaka wa 2022, akiwa amemshikilia babake mkono akikagua makombora ya Korea Kaskazini.

Chanzo cha picha, KCNA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Cheong anasema kwamba kuonekana kwake kwenye televisheni na vyombo vya habari vya serikali kumtaja kama "mtoto anayeheshimiwa" ni ishara ya kutosha kwamba amekuwa mrithi rasmi.
"Vyombo vya habari vya serikali vinatumia maneno yanayotumika kwa kiongozi mkuu," anasema.
Ukaribu wake na jeshi la nchi hiyo ni ishara nyingine, Cheong anaongeza.
Alikagua vikosi vya jeshi na silaha akiwa pamoja na baba yake. Mara kadhaa, majenerali wakuu walionekana wakiinama na kumsemeza sikioni wakati akiwa amekaa pamoja na baba yake akitazama sherehe ya kijeshi.
Cheong anaeleza kwamba nguvu za Kim Jong Un zinategemea udhibiti wake wa jeshi. Ikiwa Ju Ae atafuata nyayo zake, anahitajika kuonekana kama kamanda wa kijeshi anayeaminika.
Wakati akikagua gwaride la jeshi akiwa na baba yake, yeye huvaa koti ndefu nyeusi na miwani ya jua kama anavyovaa babake.
Wakati Kim Jong Un alipochukua madaraka, ilitokea ghafla sana. Alionekana hadharani kwa mara ya kwanza mwaka mmoja tu kabla ya kifo cha baba yake.
Cheong anaamini kwamba Kim anajaribu kuepuka mabadiliko ya ghafla kama hayo kwa kumtambulisha Ju Ae mapema kwenye utawala wa Korea Kaskazini na hadharani.
Hakuna ushahidi kwamba Kim Jong Un ana matatizo ya kiafya, isipokuwa marejeleo kuhusu uzito wake, tabia ya kuvuta sigara na kunywa pombe.
Lakini Kim anaweza kuwa anajaribu kumteua mrithi wake mapema ili kuepuka mgogoro wa urithi, kulingana na Cheong.
Hata hivyo, afisa wa zamani wa Korea Kaskazini, Ryu Hyun-woo, anasema kuna uwezekano mdogo wa mwanamke kuitawala nchi hiyo.
Ryu, ambaye alihudumu kama balozi kabla ya kutoroka nchi hiyo mwaka 2019, anasema kwamba kanuni ya kisheria ya Korea Kaskazini, iliyoundwa na familia ya Kim, inahitaji nchi hiyo iendeshwe na mtu wa kizazi cha damu cha Paektu, mrithi wa moja kwa moja wa mwanzilishi wa nchi Kim Il Sung.
Ingawa Ju Ae ni wa kizazi cha Kim, mfumo kidume wa uongozi wa Korea Kaskazini, huenda usimuwezeshe kuitawala nchi hiyo ingawa anatokea kizazi cha Kim.

Chanzo cha picha, KCNA VIA KNS via AFP
Wanawake nchini Korea Kaskazini wanapitia changamoto ya ukosefu wa usawa. Kumpata Afisa wa kike katika ngazi ya juu ni nadra, na hata ni nadra zaidi kumpata kamanda wa kijeshi ambaye ni mwanamke.
Mjini Pyongyang, madereva wengi wa teksi hukataa kuwabeba wanawake ikiwa wao ndio wateja wao kwanza wa siku hiyo, kutokana na imani potofu kwamba italeta bahati mbaya, anasema Ryu.
"Iwapo watakubali , wanakamilisha safari kisha kwenda nyuma ya gari lao na kutema mate mara tatu ili kuondoa bahati mbaya," anasema.
Sababu hizi zinamfanya Ryu kufikiria kuwa itakuwa vigumu kwa Ju Ae kuiongoza Korea Kaskazini.
Kwa maoni ya Ryu, Kim anamuonyesha binti yake kwenye vyombo vya habari ili kuondoa taswira kuwa yeye ni mkali, na kuanzisha wazo la urithi mwingine wa kifamilia.
Lakini ujasusi wa Korea Kusini, unaamini vinginevyo.
Kwanza, hadhi ya wanawake nchini Korea Kaskazini imepiga hatua kubwa tangu kile kinachojulikana kama kipindi kigumu 'Arduous March' njaa kali iliyosababisha mfumuko wa bei za bidhaa miaka ya 1990 na kuporomoka kwa uchumi wa Korea Kaskazini.
Wakati wanaume walikuwa wakianya kazi za serikali, huku mshahara na ruzuku zao zikipunguzwaa, wanawake ndiyo waliokuwa wakitafuta njia za kulisha familia zao. Walianza biashara, kuuza bidhaa sokoni kwa siri, na wengine kufanya ulanguzi wa kuingiza bidhaa nchini humo kinyume cha sheria.
Song Hyun-jin, ambaye aliwahoji wakimbizi zaidi ya 120 wa Korea Kaskazini kuhusu uongozi wa wanawake katika mfumo wa utawala wa taifa hilo, anasema si nadra tena kuona wanawake wakisimamia viwanda na kushikilia viti vya chama nchini Korea Kaskazini.
Katika miaka ya hivi karibuni, vipindi vya televisheni vya Korea Kaskazini vimeonyesha wanaume wakiwa wanafanya kazi za nyumbani ishara ya mabadiliko nchini humo.

Chanzo cha picha, KCTV
Song anasema kwamba jinsia ya Ju Ae haitakuwa kikwazo ikiwa baba yake ataamua kwamba atachukua nafasi yake. Familia yake na malezi yake ya kifalme katika nchi ambayo kwa ujumla ni maskini vinatosha kumfanya raia wa kawaida wa Korea Kaskazini kumkubali kama kiongozi.
"Hatuwezi kuifikiria Korea Kaskazini kwa mantiki yetu. Tunapaswa kuwawazia kama enzi ya Joseon," anasema Song, akirejelea ufalme wa Korea wa zama za kati. "Nani angeweza kuthubutu kumpinga mtu wa damu ya kifalme anayechukua kiti cha enzi?"
Wiki hii, Kim Yo Jong, dada mkubwa wa Kim Jong Un, alipandishwa cheo kuwa waziri . Cheong anaamini hii ni ishara kwamba Kim Jong Un anamfanya dada yake kuwa mlezi wa binti yake.
Wakati Kim Jong Un alipochukua madaraka akiwa na umri wa miaka 27, na kumfanya kuwa kiongozi mdogo zaidi duniani wakati huo, wengi walitumaini kwamba angeifungua Korea Kaskazini kwa ulimwengu wa nje.
Ndoto hiyo ilitoweka haraka mwaka 2013, alipomuua mjomba wake aliyekuwa akionekana kutaka mageuzi.
Katika miaka iliyofuata, mpango wake wa silaha za nyuklia umeendelea kukua, na ameimarisha udhibiti mkali wa utawala wa taifa hilo.
Cheong anasema hakuna sababu ya kuamini kwamba Ju Ae hataendelea katika mkondo huo huo. Anapuuza wazo kwamba huenda akawa wazi zaidi au mpole zaidi, akisema inatokana na dhana potofu kuhusu wanawake.
Ryu, anasema mjadala kuhusu mrithi wa Kim huenda wenyewe ni lengo la Kim kuzungumziwa.














