Siku ya Wanawake 2026: Safari ya usawa inayoendelea

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maelfu ya wanawake na wasichana waliandamana 7 Machi 2026 huko London London, Uingereza kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kila mwaka tarehe 8 Machi, dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake, tukio linalokumbusha safari ndefu ya wanawake kuelekea usawa wa kijinsia na haki za kisheria.

Siku hii ni fursa ya kusherehekea mafanikio ya wanawake kote duniani, lakini pia inatambua changamoto zinazobaki, ikiwemo ubaguzi wa kijinsia, ukosefu wa elimu sawa, upungufu wa fursa za kiuchumi na unyanyasaji wa kijinsia.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Haki, usawa na matendo kwa wanawake na wasichana wote", ikisisitiza kwamba haki na usawa si ndoto tu bali ni malengo yanayohitaji matendo halisi (hatua halisi) na uangalizi wa kimkakati. Kwa wengi wanaopiganinia haki za kundi hili wanasema 'hakuna haki bila hatua" na ndio hasa msisitizo wa kauli mbiu hii. Sio maneno haki ni hatua.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyo na usawa kamili wa kijinsia, na itachukua karne moja au zaidi kufanikisha usawa wa kweli.

Hali ya haki za wanawake duniani 2026

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Siku ya Kimataifa ya Wanawake 2026 inakuja katika wakati mgumu kwa mifumo ya sheria na haki za binadamu. Migogoro, ukandamizaji na mvutano wa kisiasa umedhoofisha utawala wa sheria, na matokeo yake ni kwamba wanawake na wasichana wana haki sawa na wanaume kwa asilimia 64 tu.

Wanawake wengi wanakumbana na vikwazo wanapojaribu kupata msaada wa kisheria, wanapotezwa heshima, au wanakabiliwa na unyanyasaji zaidi. Takriban nchi 70 duniani hazina sheria zinazohakikisha mshahara sawa kwa kazi yenye thamani sawa, na 44% ya nchi hazina ufafanuzi wa dhana ya ubakaji.

Vilevile, nchi nyingi bado zinaruhusu ndoa za utotoni, jambo linalokatisha ndoto za elimu, fursa za kiuchumi na maisha bora ya wasichana. Kwa wanawake milioni 676 wanaoishi karibu na maeneo yenye migogoro, mifumo ya kisheria mara mingi haipo, na wahalifu wanaendelea kuendesha matendo bila kuadhibiwa.

Kuhakikisha haki halisi kunahitaji hatua thabiti na mshikamano wa kimataifa. Sheria zinazolinda wanawake na wasichana dhidi ya ukatili, ubaguzi na unyonyaji lazima zitekelezwe kikamilifu, huku mahakama zikihakikisha kuwa kila mwanamke ana imani na ulinzi.

Msaada wa kisheria lazima uwe rahisi kupatikana na gharama nafuu, huku wanawake wakipewa msaada wa kisaikolojia na kijamii pale haki zao zinapokiukwa.

Siku ya kimataifa ya wanawake ilikujaje?

Clara Zetkin

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Clara Zetkin

Asili ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani inarudi karne moja nyuma, pale harakati za wanawake wafanyakazi zilipoibuka. Mnamo mwaka 1908, wanawake wapatao 15,000 waliandamana mjini New York wakidai muda mfupi wa kazi, malipo bora na haki ya kupiga kura.

Mwaka 1910, mwanaharakati Clara Zetkin alipendekeza siku hii kuadhimishwa kimataifa kwenye mkutano wa kimataifa wa wanawake wafanyakazi huko Copenhagen, ambapo wazo lake likakubalika kwa kauli moja na wanawake kutoka nchi 17.

Siku ya kwanza ya kimataifa ya wanawake iliadhimishwa mwaka 1911, ikifanyika kwa pamoja Austria, Denmark, Ujerumani na Uswisi. Umoja wa Mataifa ulianza kuadhimisha siku hii rasmi mwaka 1975, na tangu wakati huo imekuwa tukio la kimataifa lenye umuhimu mkubwa wa kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Kwa nini huadhimishwa tarehe 8 Machi?

Tarehe 8 Machi ilichaguliwa kufuatia mgomo wa wanawake wa Urusi mnamo 1917 waliodai "mkate na amani" wakati wa vita, hatua iliyosababisha mfalme wa nchi hiyo kujiuzulu na serikali ya muda kuwapa wanawake haki ya kupiga kura.

Katika kalenda ya Gregori, mgomo huu ulianza mnamo 8 Machi, na hivyo tarehe hiyo ikawa alama ya kihistoria ya mapambano ya wanawake. Siku hii sasa inaadhimishwa kwa njia mbalimbali duniani kote: maelfu ya matukio, ikiwemo maandamano, mazungumzo ya hadhara, warsha, maonyesho na hafla za kitaifa.

Katika nchi kadhaa, kama China, wanawake hupata mapumziko ya nusu siku, huku Marekani ikitambua Machi kama Mwezi wa Historia ya Wanawake, ukizingatia mafanikio ya wanawake katika siasa, jamii na taaluma mbalimbali.

Kwa nini ni muhimu?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanawake wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali kuchangia kipato cha familia

Siku ya kimataifa ya wanawake ni muhimu kwani inatoa fursa ya kusherehekea mafanikio ya wanawake na kuangazia changamoto zinazobaki. Hii inajumuisha ubaguzi wa kisheria, ukosefu wa fursa za kiuchumi, unyanyasaji wa kijinsia, na upungufu wa elimu kwa wasichana.

Katika mwaka huu, Umoja wa Mataifa unasema wanawake kote duniani bado hawashiriki kwa usawa na wanaume katika masuala ya kisheria, kiuchumi na kijamii.

Kauli mbiu ya mwaka huu, "Haki, usawa na matendo kwa wanawake na wasichana wote", inaleta mwito wa kimataifa wa kuchukua hatua dhahiri: kutetea haki za wanawake, kuondoa vikwazo vya kijinsia na kisheria, na kutoa fursa za kiuchumi, elimu na usalama.

Kampeni ya kimataifa ya siku hii, "Give To Gain", inasisitiza kwamba uwekezaji na msaada kwa wanawake huzaa faida kwa jamii nzima.

Je, kuna siku ya kimataifa ya wanaume?

Ndiyo, Siku ya Kimataifa ya Wanaume hufanyika tarehe 19 Novemba kila mwaka.

Tukio hili halitambuliwi rasmi na Umoja wa Mataifa, lakini limekuwa likishuhudiwa katika zaidi ya nchi 80 duniani.

Lengo lake ni kuangazia mchango chanya wa wanaume kwa jamii, familia na ulimwengu kwa ujumla, kuongeza ufahamu wa ustawi wa wanaume, na kuboresha mahusiano ya kijinsia.

Hata hivyo, Siku ya kimataifa ya wanawake ina umuhimu wa kipekee kwani inasisitiza historia, changamoto, na juhudi za kimataifa za kuhakikisha usawa wa kijinsia unaotekelezeka kila mwaka.

Imeandaliwa na Yusuph Mazimu kupitia vyanzo mbalimbali