Rais Trump atia saini hati ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza katika mkutano wa kilele wa amani Misri

Mpango wa amani wa Trump wenye vipengele 20 unasema Gaza itasimamiwa na kamati ya muda ya mpito ya wanateknolojia wa Palestina - inayosimamiwa na "Bodi ya Amani" inayoongozwa na Trump.

Muhtasari

Moja kwa moja

Asha Juma na Mariam Mjahid

  1. Shukran mpenzi msomaji kwa kufuatilia habari za moja kwa moja kuanzia asubuhi hadi sasa nakutakia usiku mwanana.

  2. Trump atia saini hati ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza katika mkutano wa kilele wa amani

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump baada ya kufungua mkutano wa kilele wa amani nchini Misri pamoja na Rais Abdul Fattah al-Sisi, Trump amekuwa akisalimiana na viongozi wa dunia waliohudhuria kikao hicho huko Misri.

    Trump ametia saini, na kusema: "Hii ilichukua miaka 3,000 kufikia hatua hii, unaweza kuamini? Na itasimama pia". Bahasha hilo pia likapokezwa Rais Sisi wa Misri, ambaye pia ameitia saini.

    Lengo la mkutano huu wa kilele wa Sharm el-Sheikh kuweka shinikizo la mwisho juu ya makubaliano ya kina ya kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza.

    Wakati macho yote yakielekezwa kwa Sharm el-Sheikh, ambayo kwa mara nyingine inabadilika na kuwa uwanja wa kidiplomasia wa kimataifa, awamu inayofuata ya mpango wa amani itazinduliwa, ikiwa ni pamoja na kufikia makubaliano ya mwisho ya kusitisha mapigano na kuanzisha mipango ya baada ya vita kwa Ukanda wa Gaza, hasa kuhusu utawala, usalama na ujenzi mpya.

  3. Baraza la mateka wa Israel lashutumu Hamas kwa kukiuka makubaliano

    Miili ya mateka wanne kukabidhiwa kwa shirika la Msalaba mwekundu

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Miili ya mateka wanne kukabidhiwa kwa shirika la Msalaba mwekundu

    Baraza la familia za mateka na waliopotea limeitaka serikali kusitisha mara moja utekelezaji wa makubaliano yoyote yaliyopo, hadi miili ya mateka wote waliopoteza maisha irejeshwe kutoka Gaza.

    Mapema leo, baraza hilo lilieleza kuwa liliarifiwa kwamba ni miili ya mateka wanne tu ndiyo ingerejeshwa.

    Baadaye, Hamas ilithibitisha majina ya mateka hao wanne, na kusema kuwa miili yao itarudishwa leo.

    Kupitia taarifa yake, baraza hilo limesisitiza, “Uvunjaji wa makubaliano unaofanywa na Hamas unapaswa kujibiwa kwa hatua madhubuti kutoka kwa serikali na wapatanishi. Makubaliano lazima yaheshimiwe na pande zote mbili. Ikiwa Hamas haitatekeleza wajibu wake, basi Israel pia isitekeleze wake. Tunadai kurejeshwa kwa mateka wote 28. Hatutakubali kumwacha yeyote nyuma hadi kila mmoja arejeshwe.”

    Katika taarifa tofauti, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema kuwa hatua ya Hamas kurejesha miili ya mateka wanne pekee leo ni “kutotekeleza makubaliano” na ni ushahidi wa kutofikia ahadi.

    Muktadha: Kwa mujibu wa nakala ya makubaliano ya kusitisha mapigano iliyochapishwa na vyombo vya habari vya Israel, mabaki ya mateka wote waliopoteza maisha yanapaswa kuwa yamekabidhiwa ifikapo saa 6:00 mchana (kwa saa za huko, sawa na saa 4:00 asubuhi BST) siku ya Jumatatu.

    Hata hivyo, makubaliano hayo pia yanatambua uwezekano kwamba Hamas na makundi mengine ya Kipalestina huenda yasifanikiwe kuipata miili yote ndani ya muda huo uliowekwa.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Urusi: Tutaipatia Iran zana za kijeshi inazohitaji

    Sergei Lavrov amesema kuwa kukidhi mahitaji ya kiufundi na kijeshi ya Iran "kutatekelezwa kwa kufuata kikamilifu sheria za kimataifa."

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Maelezo ya picha, Sergei Lavrov amesema kuwa kukidhi mahitaji ya kiufundi na kijeshi ya Iran "kutatekelezwa kwa kufuata kikamilifu sheria za kimataifa."

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema ushirikiano wa kijeshi na Iran utaendelea "kwa mujibu wa sheria za kimataifa," hata kama vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa vilivyoondolewa baada ya JCPOA kurejeshwa Oktoba 25.

    Urusi haitambui vikwazo hivyo.

    "Hakuna vikwazo kwa ushirikiano wetu wa kijeshi na kiufundi na Iran baada ya kuondolewa vikwazo vya Umoja wa Mataifa, kwa hivyo tunatoa vifaa ambavyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavihitaji kwa kufuata kikamilifu sheria za kimataifa.

    ''Nasisitiza tena kwamba hilo linafanyika kwa kufuata kikamilifu sheria za kimataifa," Bw Lavrov aliambia Reuters.

    Marufuku ya silaha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ilimalizika Oktoba 2020.

    Chini yake, Iran haikuwa na vikwazo vya kisheria vya kununua na kuuza silaha, lakini Baraza la Usalama lilipiga kura ya kurejesha maazimio haya na vikwazo vinavyohusiana.

    Marekani iliunga mkono, huku China na Urusi zikipinga kurejeshwa kwa vikwazo hivyo.

    Nchi tatu za Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kwa kuzingatia mamlaka ya Azimio 2231, zilifungua njia ya kurejeshwa kwa vikwazo hivi, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya silaha.

    Serikali ya Iran imezitaka nchi duniani kote kutotekeleza tena maazimio ya Baraza la Usalama na vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

    Katika barua, wameutaka Umoja wa Mataifa kukomesha vizuizi vyote vinavyohusiana na azimio nambari 2231 katika tarehe ya mwisho ya Oktoba 18.

    Hata hivyo, kwa uanzishaji wa utaratibu wa 'trigger mechanism' na kurudi kwa vikwazo, tarehe hii imepitwa na wakati, lakini Iran inatambua.

    Baada ya kufufua maazimio hayo, Umoja wa Mataifa umeziarifu nchi wanachama juu ya utekelezaji wake upya katika taarifa rasmi.

    Soma pia:

  5. Sintofahamu yaongezeka kuhusu aliko Rais wa Madagascar

    Gen Z wa Madagascar wakionyesha hamaki mitaani

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Gen Z wa Madagascar wakionyesha hamaki mitaani

    Hatima ya Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina, bado haijafahamika, huku shinikizo la kumtaka ajiuzulu likizidi kuongezeka kufuatia kuibuka kwa maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana mwishoni mwa mwezi Septemba.

    Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kuwa Rais Rajoelina alisafirishwa kutoka nchini kwa ndege ya kijeshi ya Ufaransa siku ya Jumapili.

    Hata hivyo, taarifa rasmi kutoka serikali ya Madagascar haijathibitisha madai hayo, na hali ya sintofahamu kuhusu mahali alipo inaendelea kutanda.

    Ofisi ya Rais imetangaza kuwa Rajoelina atalihutubia taifa jioni ya Jumatatu, taarifa ambayo imezua matarajio miongoni mwa raia wanaotaka kujua mustakabali wa uongozi wa nchi hiyo.

    Wakati huo huo, jeshi la Madagascar limechukua hatua za kutuliza hali ya taharuki kufuatia makabiliano ya risasi kati ya wanajeshi na vikosi vya gendarmerie mwishoni mwa wiki, ambapo watu kadhaa walipoteza maisha.

    Katika juhudi za kurejesha utulivu, Mkuu mpya wa majeshi, Jenerali Demosthene Pikulas, amesema kuwa jeshi na gendarmerie wanafanya kazi kwa ushirikiano kuhakikisha hali ya amani inarejea nchini.

    Akizungumza pamoja na Kamanda mpya wa Gendarmerie, Jenerali Pikulas alisisitiza kuwa lengo lao ni kudumisha utulivu, si kuchukua madaraka ya kisiasa.

    Soma pia:

  6. Usalama wa Israel hautishiwi tena baada ya kupokonywa silaha kwa Hamas - Trump

    Trump akitoa hotuba akiwa katika bunge la Israel

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump akitoa hotuba akiwa katika bunge la Israel

    Baada ya kutua Tel Aviv na kufika katika bunge la Israel Rais wa Marekani ameanza hotuba yake kwa kutoa shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye anamwita "mtu mwenye ujasiri wa kipekee".

    Akizungumza akiwa Knesset Trump ametaja kuwa vita vya Gaza vilikuwa vikubwa kuwahi kutokea duniani na hatimaye vimefikia mwisho wake.

    Tumeipatia Israeli silaha "isiyo na kifani" ili kufikia usawa wa nguvu na amani.

    Pia ameeleza mbinu iliyotumika kuafikia yaliyoshuhudiwa leo.

    ''Hatutapigana vita "kwa busara" na tutafikia amani kwa nguvu'' anasema Trump.

    Kama ilivyozoeleka Trump amejipiga kifua kwa kuwa kiongozi ambaye amesuluhisha vita vingi ambavyo watangulizi wake walishindwa.

    ''Nilimaliza vita nane katika miezi minane, na nitaongeza vita hivi vya Israel na Hamas kwenye orodha nitakapotia saini rasmi mjini Misri'', Trump aliongezea.

    Baadhi katika umati wamesikika wakisema "Bibi" - lakabu ya waziri mkuu wa Israel.

    Trump pia anashukuru mataifa ya Kiarabu ambayo yalisaidia katika mazungumzo.

    Ni "ushindi wa ajabu" walifanya kazi pamoja, anasema. Sasa "itakuwa enzi ya dhahabu ya Israeli", Trump anaongeza, pamoja na "zama za dhahabu" kwa eneo zima.

    Hotuba ya Trump ilikatishwa tu wakati MK (mbunge wa bunge la Israel) aliinua karatasi iliyosema "Itambue Palestina kama taifa huru".

    Spika Amir Ohana alipaza sauti ya kutaka utaratibu huku kukiwa na pingamizi kubwa dhidi ya MK aliyekuwa akiandamana ambaye alitolewa nje haraka.

    Ohana alisikika akiita jina la Ofer Cassif, mwanasiasa wa mrengo wa kushoto, lakini haijatambuliwa ni nani aliyetolewa nje.

    Trump alianza tena hotuba yake akisema hiyo "ilikuwa nzuri sana".

    Pia unaweza kusoma:

  7. 'Tumesubiri kwa hamu muda kama huu' - Netanyahu

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Tukirejea katika bunge la Israel ambapo Rais wa Marekani anatarajiwa kuhutubia baada ya ubadilishanaji wa mateka waliohai wa Israel na Palestina kukamilika, Waziri mkuu Benjamin Netanyahu amemshukuru Trump.

    "Tunatambua jukumu muhimu ambalo Rais Trump amefanya katika kuwarudisha waliotekwa nyara," Netanyahu aliwaambia wanachama wa Knesset, na kuongeza, "Tumewarudisha wote waliotekwa nyara walio hai, na pia tumejitolea kurudisha miili ya waliofariki."

    Netanyahu alipongeza msimamo wa Trump wa kuunga mkono Israel akisema, "Tunamshukuru Rais Trump kwa kutambua haki zetu za kihistoria katika Ukingo wa Magharibi na kwa kusimama dhidi ya uongo dhidi ya Israel kwenye Umoja wa Mataifa."

    Alisisitiza kuwa "hakuna Rais wa Marekani aliyeifanyia Israel mambo mengi kama Rais wa Marekani wa sasa Donald Trump."

    Netanyahu alielezea pendekezo la amani la Trump kama hatua "muhimu" kuelekea amani, na kuongeza, "Nimejitolea kwa amani hii, mmejitolea kwa amani hii, na tutafikia amani hii pamoja."

    Soma pia:

  8. Picha za kwanza zinaonyesha wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa wakilakiwa na familia zao

    Mateka aliyeachiwa na Israeli

    Chanzo cha picha, Reuters

    Hizi hapa picha za kwanza za baadhi ya wafungwa wa Kipalestina walioachiwa huru wakiwasili Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel.

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Akina mama na baba walilia huku wakiwakumbatia wapendwa wao, huku wengine wakiwanyanyua kwenye mabega yao kusherehekea kuachiliwa kwao.

    Wengi wa walioachiliwa leo walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha baada ya kutiwa hatiani na mahakama za Israel kwa makosa ya uhalifu yakiwemo mauaji.

    Wengi wao walionekana dhaifu na wengine walikuwa na majeraha yanayoonekana.

    Wengine walijitahidi kutembea.

    Ni wazi kwamba familia nyingi hapa zina wasiwasi kuhusu hali ambazo jamaa zao wako ndani.

    Soma pia:

  9. Tundu Lissu akubaliwa kutumia maelezo ya shahidi wa Jamhuri

    Tundu Lissu akiwa mahakamani jijini Dar es Salaam
    Maelezo ya picha, Tundu Lissu akiwa mahakamani jijini Dar es Salaam

    Katika uamuzi mdogo Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na upande wa Jamhuri dhidi ya maombi ya mshitakiwa mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu ya kutaka maelezo ya maandishi ya shahidi wa pili kupokelewa mahakamani, hivyo mahakama imeridhia ombi hilo.

    Mahakama imesema mshtakiwa amefuata taratibu zote zinazohitajika kisheria katika kuomba kielelezo hicho kupokelewa Mahakamani.

    Dhamira ya Lissu kutaka kutumia maandishi hayo ni kutaka kuonyesha kukinzana kwa kile shahidi wa pili alichokisema akiwa chini ya kiapo nakile alichoandika katika ushahidi wa maandishi.

    Lissu ameendelea kumhoji Mkaguzi wa polisi John Kaaya ambaye amejitetea kuwa hangeweza kuandika maelezo hayo yote aliyoyasema kwa mdomo kizimbani.

    Ni jibu ambalo halijamridhisha kiongozi huyo wa upinzani akidokeza kuwa iwapo atashurutishwa kufafanua ili kusawazisha maswali na waendesha mashtaka hatakubali kamwe.

    Haya yanajiri katika kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi huyo wa upinzani inayosikilizwa na majaji watatu.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Mabasi yaliyobeba wafungwa wa Kipalestina yawasili mjini Ramallah

    Wafungwa wa Kipalestina wakilakiwa kwa bashasha na familia zao

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mabasi yaliyokuwa yamewabeba wafungwa wa Kipalestina sasa yamewasili Ramallah, mji mkuu wa Palestina wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

    Kama ilivyotajwa, takriban wafungwa 1,700 kutoka Gaza na wafungwa 250 wa Kipalestina wanaachiliwa leo kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

    g

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Makumi ya watu kote Gaza wamejitokeza barabarani kusherehekea kabla ya kuwasili kwa mamia ya wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru chini ya makubaliano ya hivi karibuni ya kubadilishana mateka na Israel.

    Huko Khan Younis, mamia wamekusanyika katika mraba uliopambwa kwa bendera na mabango ya Palestina huku vipaza sauti vikicheza nyimbo za kizalendo.

    Familia za wafungwa zikibeba picha za wapendwa wao, huku wengine wakicheza na kuimba katika matukio ya furaha adimu baada ya miaka miwili ya vita na kufurushwa.

    Kwa Wapalestina wengi, siku hii ina umuhimu maradufu kurejea kwa wafungwa wao na kukabidhiwa na Hamas kwa mateka wa Israel, hatua ambayo inaweza kufungua njia kwa awamu ya pili muhimu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

    "Watu wanachotaka sasa ni vita viishe, mara moja na kwa wote," anasema Abu Omar Saleh. "Tumetosheka na mauaji, uharibifu, na kuishi katika mahema."

    Baada ya miaka miwili ya mzozo ambao uliiacha Gaza ikiwa imeharibiwa, wengi hapa wanaamini kuwa kuwaachilia mateka wa Israel kunaondoa mojawapo ya sababu kuu za Israel za kuendelea na operesheni za kijeshi.

    Kuna matumaini makubwa kwamba hatua hii inaweza kusaidia kupata mwisho wa kudumu wa mapigano.

    Soma pia:

  11. Vikosi vya usalama vya Hamas vimewaua wanachama 32 wa 'genge' la Gaza

    Vikosi vya Hamas vimewaua wanachama 32 wa "genge" katika mji wa Gaza katika kampeni ya usalama iliyozinduliwa baada ya kusitishwa kwa mapigano kuanza kutekelezwa siku ya Ijumaa, wakati wafanyakazi wake sita pia waliuawa katika ghasia hizo, chanzo cha usalama cha Palestina kilisema Jumatatu.

    Afisa huyo alisema operesheni ya usalama katika mji wa Gaza ililenga wanachama wa "genge hatari lenye mafungamano na familia moja katika mji wa Gaza".

    Operesheni hiyo ilisababisha kukamatwa kwa watu 24 na wengine 30 kujeruhiwa, afisa huyo alisema.

    Tangu kusitishwa kwa vita vilivyodumu kwa miaka miwili na Israel, Wizara ya Mambo ya Ndani inayosimamiwa na Hamas huko Gaza imetuma vikosi vya usalama katika kile ilichoeleza kuwa ni juhudi za kuzuia kadhia ya uhalifu.

    Wakati Rais wa Marekani Donald Trump ameitaka Hamas kupokonywa silaha chini ya mpango wa kumaliza vita vya Gaza, alionyesha kuwa wamewaruhusu kufanya operesheni za usalama wa ndani, akisema wanataka "kukomesha matatizo" na "tuliwapa idhini kwa muda".

    Haya ni kwa mujibu wa shirika la Reuters.

    Soma pia:

  12. Tunachojua kuhusu awamu ya pili baada ya ubadilishanaji wa mateka

    g

    Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

    Iwapo mateka na wafungwa wa pande zote mbili watabadilishana kwa mafanikio, inaaminiwa kuwa mazungumzo yatafuata kuhusu awamu za mwisho za mpango wa vipengele 20 uliowasilishwa na Trump.

    Mpango huo wa kusitisha mapigano Gaza unabainisha kuwa iwapo utakubaliwa na pande zote mbili, vita vitasitishwa mara moja.

    Aidha mpango huo pia unapendekeza kuwa Ukanda wa Gaza uvuliwe silaha, na miundombinu yote ya kijeshi, ya kigaidi na ile ya mashambulizi iharibiwa kabisa.

    Katika awamu ya mpito, Gaza itatawaliwa na kamati ya muda ya wataalamu wa Kipalestina (technocrats), chini ya usimamizi wa “Bodi ya Amani” itakayoongozwa na Donald Trump, kwa ushirikiano na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair.

    Hatimaye, mamlaka ya kuongoza Gaza yatakabidhiwa kwa Mamlaka ya Palestina ambayo kwa sasa inasimamia Ukingo wa Magharibi baada ya kupitia mageuzi ya kimuundo.

    Kulingana na mpango huo, Hamas ambayo imetawala Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2007 haitakuwa na nafasi yoyote katika uongozi wa baada ya vita, iwe kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.

    Wanachama wa Hamas watapewa msamaha endapo watakubali kuishi kwa amani, au watapatiwa njia salama ya kuhamia nchi nyingine.

    Hakuna Mpalesitina atakayelazimishwa kuondoka Gaza, na wale watakaotaka kuondoka watakuwa na haki ya kurejea.

    Mpango wa kiuchumi wa Trump wa kuijenga upya na kuhuisha Gaza utaundwa na jopo maalum la wataalamu wa maendeleo.

    Hata hivyo, Hamas imekuwa ikikataa kuweka silaha chini, ikisisitiza kuwa itafanya hivyo tu baada ya kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina.

    Aidha, katika majibu yake ya awali kwa mpango huu mwishoni mwa wiki iliyopita, Hamas haikutaja chochote kuhusu suala la kusalimisha silaha, jambo lililozua hisia kuwa msimamo wake bado haujabadilika.

    Ingawa Israel imekubali mpango wa Trump kwa ujumla wake, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alionekana kupinga ushiriki wa Mamlaka ya Palestina katika Gaza ya baada ya vita, licha ya kusimama jukwaa moja na Rais wa mamlaka hiyo wiki iliyopita.

    Kwa upande wake, Hamas imesema inatarajia kuwa na nafasi katika mustakabali wa Gaza, ikiwa kama sehemu ya “harakati moja iliyounganisha Wapalestina”.

    Naye Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaya Kallas, alisema kuwa ujumbe wa ufuatiliaji wa kiraia katika kivuko cha mpaka cha Rafah kati ya Ukanda wa Gaza na Misri utaanza tena shughuli zake siku ya Jumatano, akibainisha kuwa ingawa kupatikana kwa amani Gaza bado ni "changamoto sana," ujumbe wa ufuatiliaji unaweza kuchukua "jukumu muhimu" katika kusaidia utulivu wa usitishaji mapigano.

    Swali lingine linalozua mjadala ni kuhusu kiwango cha uondoaji wa majeshi ya Israel.

    Israel imesema kuwa katika hatua ya awali ya kujiondoa, itaendelea kudhibiti takriban asilimia 53% ya Gaza.

    Mpango wa Ikulu ya Marekani unaonesha hatua za ziada za kujiondoa hadi kufikia 40%, na hatimaye 15%.

    Awamu ya mwisho ya uondoaji huo itaweka “eneo la usalama” ambalo litaendelea kudhibitiwa hadi Gaza itakapothibitishwa kuwa salama dhidi ya tishio lolote jipya la ugaidi.

    Hata hivyo, maelezo haya ni ya jumla na hayatoi ratiba maalum ya kuondoka kikamilifu kwa majeshi ya Israel jambo ambalo huenda likawa moja ya mada kuu zitakazoshinikizwa na Hamas katika mazungumzo yajayo.

    Soma pia:

  13. Mateka wote 20 walio hai wakabidhiwa Israel huku Trump akitarajiwa kuhutubia Bunge la Israeli

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mateka wote 20 walio hai wakabidhiwa Israel huku Trump akitarajiwa kuhutubia Bunge la Israeli

    Kilichotokea kufikia sasa:

    Mateka wa Israeli

    • Mateka wote 20 wanaoaminika kuwa hai wameachiliwa
    • Waligawanywa katika kmaundi mawili - saba wameachiliwa huru mapema asubuhi na 13 baadaye
    • Miili ya wale waliokufa bado haijakabidhiwa kwa Israel

    Wafungwa wa Kipalestina

    • Zaidi ya wafungwa 1,700 kutoka Gaza na wafungwa 250 wa Kipalestina pia wamepangiwa kuachiliwa.
    • Kumeonekana magari yanayoaminika kuwabeba katika gereza la Ofer nchini Israel
    • Hospitali za Gaza zinajiandaa kuwapokea

    Donald Trump

    • Rais wa Marekani Donald Trump amewasili katika bunge la Israel, ambapo atahutubia
    • Pia atakutana na familia za mateka
  14. Habari za hivi punde, IDF yathibitisha mateka 13 waliokabidhiwa kwa Msalaba Mwekundu

    Jeshi la Israel limethibitisha hivi punde kwamba kundi la pili la mateka wanaoishi Israel wamekabidhiwa Shirika la Msalaba Mwekundu.

    Mateka hao 13 sasa wako njiani kuelekea Jeshi la Ulinzi la Israel na vikosi vya Shirika la Usalama la Israel katika Ukanda wa Gaza.

    Mapema asubuhi ya leo, Hamas tayari iliwaachilia huru watu saba kama kundi lake la kwanza la kuwaachilia mateka.

  15. IDF yatoa picha za kwanza za mateka walioachiliwa

    .

    Chanzo cha picha, IDF

    Maelezo ya picha, Ndugu pacha Gali na Ziv Berman wakikumbatiana katika Ukanda wa Gaza baada ya kuachiliwa na Hamas

    Jeshi la Israel limetoa picha za kwanza za baadhi ya mateka walioachiliwa kutoka kwa Hamas na kupokelewa na Jeshi la Ulinzi la Israel leo asubuhi.

    Picha hizo zinaonyesha Alon Ohel akikutana na wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza baada ya kuachiliwa, pamoja na ndugu pacha Gali na Ziv Berman wakikumbatiana.

    Gali Berman na Guy Gilboa-Dala pia wanaonekana kukutana na wanajeshi wa Israel huko Gaza asubuhi ya leo.

    .

    Chanzo cha picha, IDF

    Maelezo ya picha, Mateka aliyeachiliwa Alon Ohel akutana na vikosi vya Israel
    .

    Chanzo cha picha, IDF

    .

    Chanzo cha picha, IDF

    Maelezo ya picha, Mateka aliyeachiliwa huru Guy Gilboa-Dala anaonekana akikutana na afisa wa IDF
    .

    Chanzo cha picha, IDF

    Maelezo ya picha, Mateka aliyeachiliwa Eitan Mor akutana na wanajeshi wa IDF baada ya kukaa utumwani kwa zaidi ya siku 735
  16. Israel inatarajiwa kuwaachilia wafungwa wa Kipalestina saa chache zijazo

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Pamoja na kuachiliwa kwa mateka wa Israel, tunatarajia pia kuona kuachiliwa kwa wafungwa 250 wa Kipalestina na wafungwa 1,700 kutoka Gaza, wakiwemo watoto 22, katika saa zijazo.

    Ripoti katika vyombo vya habari vya Israel zinaonyesha wafungwa hao sasa wanatayarishwa kuondoka katika Gereza la Ofer katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

    Majina ya wafungwa watakaoachiliwa yalichapishwa na wizara ya sheria ya Israel siku ya Ijumaa.

    Kwa kadiri tunavyoelewa, orodha hiyo haijumuishi majina saba ya hadhi ya juu ambayo Hamas ilidai kama sehemu ya kubadilishana - ikiwa ni pamoja na Marwan Barghouti na Ahmad Saadat - licha ya mazungumzo ya dakika za mwisho Jumapili.

    Makumi ya familia zimekuwa zikisubiri tangu asubuhi na mapema nje ya gereza kwa ajili ya kuachiliwa kwa jamaa zao.

    Kulingana na mpango huo, wafungwa wapatao 100 wataachiliwa hadi Ukingo wa Magharibi, huku wengine wakipangiwa kupelekwa Gaza au Misri, na idadi ndogo kuachiliwa hadi Jerusalem Mashariki.

  17. Ningependa kutembelea Gaza - Trump

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Sasa tunaweza kukuletea maoni zaidi kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump kabla hajatua Israel.

    Alipoulizwa kama angependa kuzuru Gaza, aliwaambia waandishi wa habari ndani ya Air Force One "itakuwa fahari" kwake.

    "Ninaijua vizuri bila kutembelea," anasema. "Ningependa kwenda, ningependa kuweka miguu yangu juu yake angalau."

    "Lakini nadhani itakuwa muujiza mkubwa katika siku sijazo. Ukienda haraka sana, haitakuwa nzuri.

    Unapaswa kwenda kwa kasi inayofaa, huwezi kwenda haraka sana."

  18. Habari za hivi punde, Magari ya Msalaba Mwekundu yawasili katika awamu ya pili ya makabidhiano ya mateka Gaza

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Msafara wa wanajeshi uliowabeba mateka wakielekea kwenye kituo cha mapokezi

    Magari ya Msalaba Mwekundu yameshawasili katika eneo la makabidhiano ya mateka huko Khan Younis kwa awamu ya pili ya zoezi hilo.

  19. Trump awasili Israel

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Huku kuachiliwa kwa mateka hao wa Israel kukiendelea, Rais wa Marekani Donald Trump amewasili nchini Israel.

    Ndege ya Trump imetua hivi punde katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion viungani mwa Tel Aviv, huku akianza ziara yake ya siku chache nchini humo.

    Watu kadhaa wakuu wamefika kumkaribisha - akiwemo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mkewe Sara, Mjumbe Maalum wa Marekani Steve Witkoff, mshauri Jared Kushner na mkewe - na bintiye Trump - Ivanka Trump.

    Netanyahu anamkaribisha Trump

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameshuhudiwa akipeana mkono na Donald Trump wakati akimkaribisha rais huyo wa Marekani nchini Israel.

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

  20. Mateka ambao bado wako Gaza wazungumza na wapendwa wao

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Nimrod Cohen akizungumza na mama yake kwenye simu
    .

    Chanzo cha picha, BB

    Maelezo ya picha, Ndugu David na Ariel Kunio pia walizungumza na wapendwa wao

    Mateka wengine 13 walio hai wanatarajiwa kuachiliwa leo, pamoja na saba ambao tayari wameachiliwa.

    Bado hatujapata uthibitisho kwamba wameachiliwa, lakini picha zimeshirikiwa zinazoonyesha baadhi ya mateka wakizungumza na wapendwa wao kupitia Video.