Israel inatarajia mateka kuachiliwa Jumatatu asubuhi;Trump akijiandaa kwa ziara ya Mashariki ya Kati
Msemaji wa serikali ya Israeli Shosh Bedrosian ameviambia vyombo vya habari kwamba tumebakisha saa kadhaa kabla ya kuachiliwa kwa "mateka wetu wote".
Muhtasari
- Miili ya wahamiaji zaidi ya 60 yapatikana pwani ya magharibi ya Libya
- Israel iko tayari kupokea mateka mapema Jumatatu asubuhi, serikali inasema
- Msafara wa malori ya misaada yaingia ndani ya Khan Younis, Gaza
- Hamas yashinikiza kubadilishwa kwa orodha ya wafungwa wa Palestina dakika za mwisho, BBC imefahamishwa
- Taliban inasema wanajeshi 58 wa Pakistan waliuawa katika mashambulizi ya 'kisasi' mpakani
- Ofisi ya rais wa Madagascar inasema jaribio la kunyakua mamlaka linaendelea
- Watu 237 wakamatwa katika mkutano wa maandamano nchini Ivory Coast
- Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel amshukuru Trump kwa juhudi zake za kuleta amani
- Mwimbaji Ian Watkins aliyefungwa kwa kudhulumu watoto afariki gerezani
- Raia wa Cameroon wanapiga kura kumchagua rais
- Rais wa Madagascar akanusha taarifa kuwa ametoroka nchi
- Hamas yawaita wapiganaji wake Gaza huku hofu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ikiongezeka
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Miili ya wahamiaji zaidi ya 60 yapatikana pwani ya magharibi ya Libya

Chanzo cha picha, AFP
Mamlaka nchini Libya inasema takriban miili 61 ya wahamiaji imepatikana katika wiki mbili zilizopita kando na pwani ya magharibi ya Libya, magharibi mwa mji mkuu wa Tripoli.
Kituo cha Huduma za Dharura, shirika la serikali chini ya Wizara ya Afya, ilisema mabaki hayo yalipatikana katika maeneo yaliyoanzia Zuwara hadi Ras Ijdir, karibu na mpaka wa Tunisia.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, kituo hicho kilisema "mabaki ya miili mitatu yalipatikana huko Mellitah na 12 huko Zuwara, wote ni wahamiaji wasiojulikana."
Chombo cha habari cha Reuters kinaripoti kwamba miili mingine 34 iligunduliwa huko Zuwara, Abu Kammash na Mellitah, pia walinukuu kituo hicho.
Miili kumi na mbili imeripotiwa kuzikwa, wakati mingine ikipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kutambuliwa.
Picha zilizowekwa kwenye ukurasa wa Facebook zilizothibitishwa zilionyesha timu za matibabu zikikusanya miili hiyo kutoka kwenye fukwe na kuifunga kwenye mifuko meupe ya plastiki.
Ugunduzi huu wa kutisha unajulikana wiki kadhaa baada ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) kuripoti kwamba watu wasiopungua 50 walikuwa wamekufa katikati ya mwezi Septemba wakati chombo kilichobeba wakimbizi 75 wa Sudan kilishika moto pwani ya Libya.
Libya inasalia kuwa njia kuu ya usafirishaji kwa wahamiaji kutoka Afrika na Mashariki ya Kati wakitaka kufikia Ulaya kupitia bahari.
IOM inakadiria kuwa karibu wahamiaji 900,000 kutoka nchi 45 kwa sasa wanaishi Libya, wengi wakiwa katika hali mbaya.
Israel iko tayari kupokea mateka mapema Jumatatu asubuhi, serikali inasema

Chanzo cha picha, GPO
Msemaji wa serikali ya Israeli Shosh Bedrosian katika mkutano wa waandishi wa habari huko Tel Aviv amesema kuwa nchi hiyo iko tayari kupokea wafungwaJumatatu asubuhi.
Bedrosian ameviambia vyombo vya habari kwamba tumebakisha saa kadhaa kabla ya kuachiliwa kwa "mateka wetu wote".
Israel imekuwa tayari "tangu Jumamosi usiku kupokea mateka wetu", amesema.
Bedrosian ameongeza kuwa Hamas wangewaachilia mateka miaka miwili iliyopita.
Amesema kuwa Israel inatarajia mateka wote 20 walio hai watakabidhiwa shirika la Msalaba Mwekundu mapema Jumatatu asubuhi. Kisha watahamishwa kuvuka mpaka hadi Israeli na kupelekwa kwenye kituo cha kijeshi cha Re'im.
Miili ya mateka waliofariki itawekwa kwenye majeneza yaliyofunikwa bendera za Israel na kuletwa katika taasisi ya uchunguzi wa kitaalamu kwa ajili ya utambuzi.
Msafara wa malori ya misaada yaingia ndani ya Khan Younis, Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
Malori yaliobeba misaada yameshuhudiwa yakiingia Gaza. Chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano, "msaada kamili" inatakiwa kuingia katika eneo hilo mara moja.
Katika taarifa yake ya hivi punde siku ya Alhamisi, Cogat - chombo cha kijeshi cha Israel kinachosimamia uingiaji wa misaada Gaza - kilisema malori 500 yaliingia katika eneo hilo ambayo karibu 300 ni ya UN na mashirika mengine.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takriban malori 600 ya misaada yanahitajika kila siku ili kuanza kushughulikia mzozo wa kibinadamu wa Gaza.
Soma zaidi:
Hamas yashinikiza kubadilishwa kwa orodha ya wafungwa wa Palestina dakika za mwisho, BBC imefahamishwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Afisa wa Palestina anayefahamu mazungumzo hayo aliiambia BBC kwamba duru mpya ya mazungumzo ilianza saa 10:30 saa za eneo (08:30 BST), yenye lengo la kutatua masuala ambayo bado hayajakamilika kuhusiana na orodha ya wafungwa.
Afisa huyo alisema Hamas bado inashinikiza kuachiliwa kwa wafungwa saba wenye hadhi ya juu, akiwemo Marwan Barghouti na Ahmad Saadat.
Kulingana na vyanzo, mpangilio wa makubaliano ya kubadilishana inaelekeza kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina wenye vifungo vya juu zaidi - na majina saba ya hadhi ya juu yanakidhi vigezo hivi.
Lakini tangu mwanzo wa mazungumzo Israeli imekataa kuwaachilia.
Hamas bado inasemekana kushinikiza zaidi - na kundi hilo liliwafahamisha wapatanishi kwamba ikiwa Israel itakubali kuwaachilia hata wawili kati yao, itawaachilia mateka hao leo, mapema kuliko ilivyopangwa sasa Jumatatu.
Haijabainika nini kitatokea iwapo matakwa ya Hamas hayatatekelezwa.
Mazungumzo ya leo pia yanalenga kukubaliana na muda na usafirishaji wa watakaoachiliwa huru mateka wote 20 wa Israeli, pamoja na kurejeshwa kwa miili ya mateka ambayo Hamas ina uwezo wa kuipata.
Soma zaidi:
Taliban inasema wanajeshi 58 wa Pakistan waliuawa katika mashambulizi ya 'kisasi' mpakani

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Taliban inasema wanajeshi 58 wa Pakistan waliuawa katika mashambulizi ya 'kisasi' mpakani
Serikali ya Taliban imethibitisha kuwa iliwashambulia wanajeshi wa Pakistan katika maeneo mengi ya milima kwenye mpaka wa kaskazini.
Msemaji wa Taliban alisema wanajeshi 58 wa Pakistan wameuawa katika kile walichokiita "kitendo cha kulipiza kisasi". Ilidai kuwa Pakistan ilikiuka anga ya Afghanistan na kulipua soko ndani ya mpaka wake siku ya Alhamisi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan Mohsin Naqvi alisema mashambulizi ya Afghanistan "hayakuchochewa" na raia walifyatuliwa risasi, akionya kwamba vikosi vya nchi yake vitajibu "jicho kwa jicho".
Islamabad imeishutumu Kabul kwa kuwahifadhi magaidi wanaolenga Pakistan katika ardhi yake, madai ambayo serikali ya Taliban imekanusha.
Soma zaidi:
Ofisi ya rais wa Madagascar inasema jaribio la kunyakua mamlaka linaendelea

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ofisi ya Rais wa Madagascar Andry Rajoelina imesema jaribio la kunyakua mamlaka kinyume cha sheria na kinyume cha katiba linaendelea nchini humo.
Saa kadhaa baadaye, kitengo cha jeshi kinachojulikana kama CAPSAT kilidai kwamba kilikuwa kimechukua uongozi wa kamandi ya kijeshi, na sasa kilikuwa kinadhibiti vikosi vyote vya jeshi - ardhini, angani na majini.
Hiki ndicho kitengo kile kile ambacho kilikuwa na jukumu muhimu katika mgogoro wa kisiasa wa 2009 wa Madagascar, kilichomsaidia Rajoelina kuingia madarakani.
Madagascar ilikumbwa na maandamano kwa mara ya kwanza tarehe 25 mwezi Septemba dhidi ya ukosefu wa maji na kukatwa kwa umeme, lakini yameongezeka na kuakisi kutoridhika zaidi na serikali ya Rajoelina juu ya ukosefu mkubwa wa ajira, ufisadi, na mzozo wa gharama ya maisha.
Watu 237 wakamatwa katika mkutano wa maandamano nchini Ivory Coast

Chanzo cha picha, Reuters
Watu 237 wamekamatwa na polisi wakati wa maandamano ya upinzani katika mji mkuu wa Ivory Coast Abidjan.
Polisi walirusha gesi ya kutoa machozi kutawanya maandamano yaliyoandaliwa na "Front Commun", muungano wa upinzani unaoongozwa na Chama cha African People's -Côte d'Ivoire (PPACI) na Chama cha Democratic Côte d'Ivoire - African Democratic Rally (PDCI-RDA).
Vyama vyote viwili vinapingana vikali hatua ya Ouattara kutafuta kuchaguliwa tena.
Maandamano ya Abidjan yalikuwa yamepigwa marufuku siku iliyotangulia.
Mvutano huu unafanyika wiki mbili kabla ya uchaguzi wa urais nchini Ivory Coast.
Mpinzani mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa shirika la Mikopo ya Suisse, Tidjane Thiam na Rais wa zamani Laurent Gbagbo waliondolewa kwenye orodha ya wagombea.
Wakati huohuo Rais wa miaka 83 wa Alassane Ouattara alifanya kampeni katika uwanja wa mkoa wa Daloa, mji mkubwa magharibi Jumamosi.
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel amshukuru Trump kwa juhudi zake za kuleta amani

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, María Corina Machado ameiambia BBC kuwa anashukuru kwa kile Rais wa Marekani Donald Trump anafanya "ulimwenguni kote kwa ajili ya amani".
Machado, kiongozi wa upinzani wa Venezuela, alitunukiwa tuzo ya Amani ya Nobel baada ya kufanya kampeni kwa muda mrefu dhidi ya Rais wa nchi hiyo Nicolás Maduro Moros, ambaye utawala wake wa miaka 12 unatazamwa na watu wengi kuwa usio halali.
Aliiambia BBC Mundo kwamba wakati wa simu ya pongezi na Trump alimwambia "jinsi watu wa Venezuela wanavyoshukuru kwa kile anachofanya, sio tu Marekani, lakini ulimwenguni kote kwa ajili ya amani, uhuru, kwa demokrasia".
Trump hakufanya siri kuhusu kutaka kushinda tuzo hiyo mwenyewe, kwani mara kwa mara alizungumzia vita saba anavyodai alifanikiwa kuvimaliza.
Machado alisema "alifurahi sana" kuzungumza na rais wa Marekani na "niliweza kumpa shukrani zetu".
Machado alizuiwa kugombea katika uchaguzi wa rais wa mwaka jana, ambapo Maduro alishinda muhula wa tatu wa uongozi wa miaka sita.
Uchaguzi huo ulipuuzwa kwa kiasi kikubwa katika jukwaa la kimataifa kwa madai kuwa haukuwa huru na wa haki, na ulizua maandamano kote nchini.
Soma zaidi:
Mwimbaji Ian Watkins aliyefungwa kwa kudhulumu watoto afariki gerezani

Chanzo cha picha, South Wales Police
Mwimbaji wa kundi la Lostprophets Ian Watkins amefariki dunia baada ya kushambuliwa akiwa jela, vyanzo vya habari vimethibitisha.
Mwanamuziki huyo wa muziki wa rock alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 29 huko HMP Wakefield kwa makosa ya ngono dhidi ya watoto.
Polisi wa West Yorkshire walisema waliitwa gerezani Jumamosi asubuhi kwa sababu ya mfungwa aliyeshambuliwa, ambaye alitangazwa kuwa amekufa katika eneo la tukio.
Watkins, 48, alifungwa jela Disemba 2013 kwa msururu wa makosa ya ngono dhidi ya watoto, likiwemo jaribio la kumbaka mtoto mchanga.
Msemaji wa Polisi wa Magereza alisema wanafahamu tukio lililotokea katika gereza hilo.
"Hatuwezi kutoa maoni zaidi wakati polisi wanaendelea na uchunguzi."
Alishambuliwa kwa kisu na mfungwa mwingine, PA iliripoti, ikinukuu vyanzo.
Polisi walisema wapelelezi wanaendelea na uchunguzi katika eneo la tukio.
Alishambuliwa gerezani mnamo Agosti 2023, lakini majeraha yake hayakuwa ya kutishia maisha.
Watkins alihukumiwa kifungo cha miaka 29 jela na miaka sita zaidi ya leseni, na washtakiwa wenzake wawili, waliofungwa jela miaka 14 na 17.
Shambulizi katika Gereza la Wakefield linajulikana chini ya wiki mbili baada ya ripoti katika kituo hicho kuchapishwa iliyogundua kuwa ghasia katika gereza hilo "zimeongezeka sana".
Mshindi wa Nobel ameambia BBC kuwa wanamshukuru Trump kwa anachofanya kwa ajili ya amani
Raia wa Cameroon wanapiga kura kumchagua rais

Raia wa Cameroon wanapiga kura leo Jumapili kumchagua rais mpya, wakati kampeni za uchaguzi zimefungwa usiku wa manane.
Kwa wiki mbili, wagombea katika uchaguzi wa rais walisafiri kote nchini humo wakiwarai wapiga kura kuwachagua.
Wagombea kumi wako kwenye kinyang’anyiro hicho huku Rais Paul Biya akitafuta kuchaguliwa tena kwa muhula wa nane mfululizo.
Wakati wagombea wengine tisa walikuwa wakifanya kazi kampeni mchana na usiku, Biya alionekana mara moja tu katika mkoa wa mbali wa kaskazini.
Hii ilifuatia ukosoaji wa kutokuwepo kwake kwenye mikutano ya kisiasa na uzindua wa kampeni yake na video iliyotengenezwa na AI.
Uchaguzi wa rais unakuja huku kukiwa na mfumko wa bei, ukosefu wa ajira kwa vijana, changamoto za usalama, ufisadi, na huduma duni za kijamii.
Miongoni mwa wapinzani wa Biya katika kinyang’anyiro hicho ni washirika wake wa zamani wa Kaskazini, Issa Tchiroma Bakary na Bello Bouba Maigari ambao wamekosoa mtindo wa utawala wa rais na kuahidi kuleta mabadiliko.
Zaidi ya watu milioni nane wamesajiliwa kupiga kura, na Baraza la Katiba linatarajiwa kutangaza matokeo ndani ya siku 15 baada ya raia kupiga kura.
Kiongozi mkuu wa upinzaji Maurice Kamto aliondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho, akiibua wasiwasi juu ya uaminifu wa mchakato wa uchaguzi.
Soma zaidi:
Rais wa Madagascar akanusha taarifa kuwa ametoroka nchi

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina, amewahakikishia wananchi kwamba yeye na Waziri Mkuu wanadhibiti hali nchini humo.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa ofisi yake, Rajoelina pia alikanusha uvumi kwamba ametoroka nchi.
Katika video tofauti iliyowekwa kwenye akaunti ya Facebook, Waziri Mkuu Jenerali Rufin Zafisambo alitaka utulivu na kusihi pande zote kuweka kipaumbele kwenye mazungumzo.
"Haiwezekani kwamba vikosi vyenye silaha vinafyatuliana risasi," alisema.
Hapo awali, kulikuwa na ripoti za kurushiana risasi kati ya vitengo vya usalama vya CAPSAT na Gendarmerie kwenye kambi.
Aliongeza kuwa yuko yatari kutatua mgawanyiko ndani ya jeshi kupitia majadiliano, haswa na masuala ya kitengo cha CAPSAT.
Waziri Mkuu alitangaza kuwa mashauriano ya kitaifa yatafanyika hivi karibuni chini ya uangalizi wa Baraza la Makanisa ya Kikristo ya Madagascar (FFKM), na ushiriki wa jamii ya kiraia na wadau wengine wa kitaifa, kwa lengo la kutafuta suluhisho la amani.
"Nchi haiwezi kuhimili mgogoro mwingine", alihitimisha.
Soma zaidi:
Hamas yawaita wapiganaji wake Gaza huku hofu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ikiongezeka

Chanzo cha picha, Reuters
Kundi la Hamas limewaita wanachama wapatao 7,000 wa vikosi vyake vya usalama kudhibiti tena maeneo ya Gaza ambayo yameachwa hivi karibuni na wanajeshi wa Israel, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani.
Kundi hilo pia liliteua magavana wapya watano wote wenye asili ya kijeshi, ambao hapo awali waliongoza brigedi.
Amri hiyo imeripotiwa kutolewa kupitia simu na ujumbe mfupi ambao ulisema lengo lilikuwa "kusafisha Gaza dhidi ya wahalifu na washirika na Israeli" na kuwataka wapiganaji kuripoti ndani ya masaa 24.
Ripoti kutoka Gaza zinaonyesha kuwa vikosi vya Hamas vyenye silaha tayari vimesambazwa katika wilaya kadhaa, baadhi wakiwa wamevalia nguo za kiraia na wengine katika sare za bluu za polisi wa Gaza.
Mvutano uliongezeka sana na haraka baada ya wanachama wawili wa vikosi vya wasomi wa Hamas kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wenye silaha kutoka ukoo wenye nguvu wa Dughmush katika kitongoji cha Sabra katika mji wa Gaza.
Mmoja wao alikuwa mtoto wa kamanda mkuu katika mrengo wa kijeshi wa Hamas, Imad Aqel, ambaye sasa anaongoza ujasusi wa kijeshi wa kundi hilo.
Miili yao iliachwa barabarani, na kusababisha hasira na kuongeza matarajio ya Hamas kujibu.
Wanachama wa Hamas baadaye walizingira eneo kubwa ambapo zaidi ya wapiganaji 300 wa kundi la Dughmush waliaminika kuwa wamejificha huku wakiwa na bunduki na vilipuzi.
Jumamosi asubuhi, Hamas ilimuua mtu mmoja wa ukoo wa Dughmush, na inasemekana kuwateka nyara wengine 30.
Soma zaidi:
Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 12/10/2025. Mimi ni Asha Juma
