Cameroon: Rais Paul Biya anapania kurefusha utawala wake wa miaka 36 madarakani.

Rais Paul Biya awania tena urais
Maelezo ya picha, Rais Paul Biya awania tena urais
Muda wa kusoma: Dakika 3

Shughuli za kuhesabu kura zinaendelea nchini Cameroon baada ya raia wa nchi hiyo kushiriki uchaguzi mkuu jana Jumapili .

Rais Paul Biya anapania kurefusha utawala wake wa miaka 36 madarakani.

Waangalizi wanasema shughuli ya kuhesabu kura huenda ikachukua hadi wiki mbili kukamilika.

Mchakato mzima wa kupiga kura ulikuwa wa amani katika taifa hilo lililo na watu wengi wanaozungumza kifaransa.

Watu watatu wameripotiwa kuuawa na maafisa wa usalama katika eneo la Bamende ambalo linakaliwa na watu wanaozungumza kiingereza

Maafisa wanadai waathiriwa walikuwa ni wafuasi wa kundi linalotaka kujitenga ambao wamekua wakifyetua risasi kila pembe ya eneo hilo

Inasemekana kuwa maelfu ya watu katika eneo la Bamende hawakuweza kupiga kura kwa kuhofia usalama wao.

Paul Biya akipiga kura

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Paul Biya akipiga kura

Taifa hilo lililowahi kuwa koloni la Wajerumani,Wafaransa na Waingereza linashuhudia kiongozi wa pili Afrika kwa kukaa muda mrefu madarakani yaani Paul Biya akiwania tena muhula wa saba,ameiongoza Cameroon kwa miaka 36.

Mabango makubwa ya rais Paul Biya yapo kila mahala mitaani katika mji wa Bafoussam Magharibi mwa taifa hilo.

Mwandishi wa BBC Ngala Killian Chimtom anayefuatilia uchaguzi huo,anasema kwamba wafuasi wa rais Paul Biya,wanajigamba kwamba mgombea wao huyo amekuwa na uzoefu wa uongozi kwa hiyo anastahili kupatiwa kipindi kingine.

Wafuasi wa chama tawala cha Paul Biya wanamuita mgombea wao kama shujaa,lakini kwa vijana wengi wanahoji kwamba kumekuwa na ahadi nyingi ambazo hazitekelezeki,wao wanahitaji mabadiliko

Pamoja na hali ya vurugu na matumizi ya nguvu kutoka vyombo vya dola,upinzani wanaomuunga mkono mgombea wa CRM Maurice wanasema zama za raias Biya zimekwisha na kwamba ni wakati wao sasa.

raia wa Cameroon

Mgombea wa upinzani wa kiti cha urais kwa mara ya kwanza Joshua Osih, wa chama cha SDF ametamba kwambva ana uwezo wa kutatua matatizo ya Cameroon ndani ya siku 100.

Kuna jumla ya wagombea tisa wa nafasi ya urais katika uchaguzi huo mkuu wa Cameroon,huku taifa hilo likionekana kuwa na mgawanyiko mkubwa kwa misingi ya lugha.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Masuala ibuka katika uchaguzi huu ni yapi?

  • Umri wa rais Biya - Baadhi ya watu wanahoji kuwa rais anastahili kuwapatia viongozi wengine nafasi ya uongozi ikizingatiwa changamoto kadhaa zinazokabili taifa hilo
  • Kuibuka kwa makundi ya wanamgambo wanaopigania kujitenga kwa maeneo mawili makuu ya watu wanaozungumza kiingereza.
  • Uhasama unaoshuhudiwa kati ya serikali na maeneo ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi mwa Cameroon unatishia umoja wa kitaifa
  • Ukosefu wa usalama- kwa mujibu wa shirika la kukabiliana na majanga ya kibinadamu ghasia zimesababisha zaidi ya watu 300,000 kutoroka makwao
Mipaka barani Africa ilimeguliwa na wakoloni

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha, Mipaka barani Africa ilimeguliwa na wakoloni

Cameroon mikononi mwa wakoloni tofauti

Cameroon kwanza ilitawaliwa na wajerumani mwaka 1884

Vikosi vya Uingereza na Ufarasa vilifurusha majeshi ya Ujerumani kutika nchini humo mwaka 1916.

Cameroon iligawanyika miaka mitatu baadae - 80% ikachukuliwa na Ufaransa huku 20% ikisalia mikononi mwa Uingereza.

Ufaransa ilitawala Cameroon hadi ilipojinyakulia utawala wake mwaka 1960.

Kufuatia kura ya maamuzi eneo la kusini lililotawaliwa na Uingereza liliunganishwa na Cameroon, huku eneo la Kaskazini likaunganishwa na Nigeria