Uturuki inasema Jamal Khashoggi 'aliuawa' alipoingia ubalozi wa Saudi Arabia nchini Uturuki

Chanzo cha picha, EPA
Hofu inazidi kuongezeka kufuatia kutoweka kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi baada ya maafisa wa Uturuki kusema wanaamini ameuawa.
Bw Khashoggi, raia wa Saudi Arabia alitoweka baada ya kuingia ubalozi wa Saudi Arabia mjini Insabul siku ya Jumanne.
Afisa mmoja wa Uturuki aliiambia BBC kuwa uchanguzi wa awali ulionyesha kuwa aliuawa huko.
Saudi Arabia imekana madai hayo na kusema kuwa imeanza kumtafuta.
Mwandishi wa BBC mjini Istabul Mark Lowen, alisema hii itachangia uhusiano kati ya Saudi Arabia na Uturuki kuwa mbaya zaidi.

Chanzo cha picha, AFP
Maafisa wa Uturuki wameanzisha uchunguzi na wamekuwa wakizungumza na vyombo vya habari.
Hata hivyo hawajatoa ushahidi kwa madai yao, wala kueleza ni jinsi gani aliuawa.
Alionekana mara ya mwisho lini?
Jamal Khashoggi ni mkosoaji mkubwa wa mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman. Ana zaidi ya wafuasi milioni 1.6 katika mtandao wa Twiter na amelifanyia kazi gazeti la the Washington Post .
Siku ya Jumanne alikuwa kwenye ubalozi kupata stakabadhi za kumtaliki mke wake wa zamani ili apate kufunga ndoa na mchumba wake raia wa Uturuki Hatice Cengiz.
Ms Cengiz alisema alisubiri nje kwa saa 11 lakini hakutoka ndani ya ubalozi huo.
Alisema Bw Khashoggi alihitajika kusalimisha simu yake ambayo ni sheria kwenye balozi nyingi. Alimuambia ampigie simu mshauri wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ikiwa hangerudi kutoka ubalozi huo.

Chanzo cha picha, EPA












