'Hatujali': China inavyokaidi ushuru wa Trump na kulenga masoko zaidi nje ya Marekani

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 7

Na Laura Bicker

Mwandishi wa China

Laura Bicker anaelezea jinsi ushuru unavyoathiri biashara za Marekani na bidhaa za vichezeo vya China. "Hatujali kuhusu mauzo kwa Marekani," anasema Hu Tianqiang huku moja ya ndege zake za kivita za kuchezea zikiruka kupitia juu ya vichwa vyetu.

Ni vigumu kumsikiliza huku ndege za kuchezea zikitoa sauti za kuvuma na ndege zisizo na rubani ndogo, kutokana na mandhari ya karibu ya vinyago vinavyomzunguka, vyote vikipiga kelele kuwavutia wanunuzi.

Duka la Hu, Zhongxiang Toys, liko ndani ya soko kubwa zaidi la jumla ulimwenguni lililopo katika jiji dogo la China la Yiwu.

Ni chumba kikubwa cha maonyesho cha maduka zaidi ya 75,000 ambapo wanunuzi huja kutafuta karibu kila kitu, kuanzia taa za Krismasi zinazometameta na vyombo vya jikoni hadi miavuli na vifaa vya kusinga (massage). Inaweza kuchukua muda mwingi wa siku kuzunguka idara moja ikizingatiwa kila idala moja ina ukubwa wa uwanja wa ndege kwa ajili ya maonyesho ya bidhaa hizo.

Yiwu iko katika mkoa wa Zhejiang, kando ya pwani ya mashariki ya China. Kitovu cha utengenezaji na usafirishaji, ni kitovu cha bandari zaidi ya 30, na lilichangia 17% ya mauzo yote ya bidhaa za Wachina zinazokwenda Marekani mwaka jana.

Hiyo inaiweka Yiwu, na eneo hili, kuwa mstari wa mbele wa vita vya kibiashara kati ya Marekani na China.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bwana Hu, pia, yuko mstari wa mbele. Anakaa kati ya safu za ndege za kuchezea, mbwa wanaopiga kelele, wanyama waliojaa laini, wanasesere wa barbies na buibui wanaoendesha pikipiki – ikiwa ni sehemu ya vitu vya kuchezea vyenye thamani ya $34bn (£25bn) ambavyo China ilisafirisha mwaka wa 2024.

Takriban $10bn kati yake ilikwenda Marekani. Lakini sasa, mauzo haya ya nje ya China kwenda Marekani yanakabiliwa na ushuru wa hadi 245%. Na Rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi kuwa anailaumu Beijing hasa kwa kuingiza soko kubwa la ulimwengu.

Lakini mambo yamebadilika hapa tangu vita vya kwanza vya kibiashara vya Trump dhidi ya China, ambavyo vilianza mnamo 2018. Ilimpa funzo Yiwu, lililofupishwa na Bw Hu: "Nchi zingine zina pesa pia!"

Ukaidi huo umekuwa mada inayojulikana katika taifa hilo lenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, ambalo linajiandaa kwa urais mwingine wa Trump wenye misukosuko.

Beijing, ambayo imekuwa ikiuambia ulimwengu mara kwa mara kwamba Marekani imekuwa ikidhulumu nchi katika mazungumzo ya kibiashara, bado haijarudi nyuma kutokana na vita vya kibiashara.

Propaganda zimeongezeka, zikipongeza uvumbuzi wa China na diplomasia tofauti na kutokuwa na uhakika kwa ahadi zilizotolewa na Trump. Kwenye mitandao ya kijamii inayodhibitiwa sana nchini humo, kuna machapisho mengi yanayorejelea ahadi ya uongozi kwamba China itaendelea kupambana.

Na katika viwanda na masoko, wafanyabiashara na wauzaji nje sasa wanasema wana njia zingine, zaidi ya Marekani ya Trump. Bw Hu, kwa mfano, anasema karibu 20% -30% ya biashara yake ilitoka kwa wanunuzi wa marekani . Lakini hali sio ilivyo tena.

g

Chanzo cha picha, BBC/ Xiqing Wang

Maelezo ya picha, China ilisafirisha bidhaa za kuchezea zenye thamani ya $34bn pekee mwaka wa 2024
h

Chanzo cha picha, BBC/ Xiqing Wang

Maelezo ya picha, Na baadhi ya $10bn kati ya vifaa hivyo zilikwenda Marekani

"Hatujali kuhusu hiyo 20-30%," Bw Hu anasema. "Sasa tunauza zaidi Amerika Kusini na Mashariki ya Kati. Hatukosi pesa, sisi ni matajiri."

Tunapouliza kuhusu Trump, mwenzake Chen Lang anaingia ndani, akikodoa macho yake: "Anafanya mzaha . Kuongeza ushuru kwake ni kama kufanya mzaha."

Karibu, mmoja wa maelfu ya wanunuzi wanaomiminika kwenye soko hili kila siku anajadili bei ya kununua zaidi ya roboti 100 ambazo hubadilika kuwa magari katika mfululizo wa milio . Baada ya kugonga nambari mbalimbali kwenye calculator, bei ya mwisho imeandikwa kwa chaki kwenye sakafu.

Tunaambiwa, mnunuzi anatoka Dubai. BBC ilikutana na wengine wengi kutoka kote Afrika na Amerika Kusini.

Lin Xiupeng anasema ameona mabadiliko kutoka kwa wanunuzi wa Marekani katika miaka yake 10 iliyopita katika biashara ya vinyago.

"Siku chache zilizopita, duka lililo karibu nasi lilikuwa na agizo kutoka kwa mteja wa Marekani. Lina thamani ya zaidi ya yuan milioni moja. Lakini kwasababu ya ushuru, mmiliki wa duka aliamua kughairi," anasema, akitupatia vikombe vya chai.

"Lazima wahitaji China," anasema, akiongeza kuwa nchi hiyo inasambaza vitu vingi vya kuchezea vya Marekani.

"Nadhani kuna biashara nyingi nchini Marekani zinazoandamana siku hizi."

g

Chanzo cha picha, BBC/ Xiqing Wang

Maelezo ya picha, Watu katika biashara ya vichezeo ambao BBC ilizungumza nao walisema walikuwa na maslahi mengi kutoka sehemu zingine za ulimwengu kando na Marekani

Bwana Lin yuko sahihi. Baadhi ya wamiliki wa maduka ya vinyago nchini Marekani wameiandikia Ikulu ya White House wakielezea ushuru huo kama "mbaya" kwa biashara zao.

Aliwekeza $500 yake ya mwisho katika kampuni yake, Loyal Subjects, mwaka wa 2009, ambayo alikimbia kutoka kwa bungalow yake ya vyumba viwili vya kulala huko West Hollywood. Anasema sasa ni biashara ya mamilioni ya dola, lakini ushuru unaweza kuharibu mipango yake.

"Sekta nzima ya vifaa vya kuchezea inaweza kwenda chini. Itakuwa mbaya sana," anaonya.

Anasema kubadilishana wasambazaji ni kazi kubwa: "Unahitaji rasilimali nyingi ardhini ili kutengeneza toy na wengi wa wafanyabiashara hawa wa China wametumia miaka 40 kukamilisha ufundi wao."

Hakika sio nzuri kwa China. Ushuru wa Trump sio changamoto kubwa inayoikabili nchi, ambayo pia inakabiliana na maumivu ya kiuchumi ya ndani, kutoka kwa matumizi ya chini hadi shida ya makazi ambayo imepunguza akiba ya watu na imani katika siku zijazo.

Wakati mbaya kando, ushuru unauma biashara za Wachina.

Goldman Sachs ametabiri kuwa uchumi wa China utakua kwa 4.5% mwaka huu, pungufu ya lengo la serikali kwa : 5%.

China imekuwa sehemu kubwa ya siku 100 za kwanza za Donald Trump ofisini, huku utawala wake ukipambana na Beijing.

"Anaonekana kuzindua vita dhidi ya ulimwengu wote," anasema Kanali Mwandamizi wa zamani Zhou Bo, ambaye alihudumu katika Jeshi la Ukombozi wa Watu. "Lakini bila shaka anajaribu kuipiga China kwa bidii zaidi."

Trump aliishutumu China kwa kuendesha Mfereji wa Panama, ambao unaendeshwa na kampuni ya Hong Kong, na kuapa kuurudisha. Amekuwa akiwinda njia za kuchimba madini adimu ya ardhini, ambayo China ina ukiritimba, na kuifanya hii kuwa sehemu muhimu ya makubaliano yoyote na Ukraine. Vitisho vyake vya kuchukua Greenland pia vinaweza kulenga kuzuia matarajio ya China katika Arctic.

Na, kwa kweli, alianzisha vita vingine vya kibiashara, ambavyo vinalenga sana majirani wa China, kama vile Vietnam na Kambodia, ambazo zimekuwa muhimu kwa ugavi wake unaoendelea.

h

Chanzo cha picha, BBC/ Xiqing Wang

Maelezo ya picha, Zhou Bo anaiambia BBC kwamba Trump anaonekana kuzindua "vita vya msalaba dhidi ya ulimwengu wote"

Katika wiki iliyopita, alipendekeza kuwa ushuru kwa bidhaa za China unaweza kupunguzwa kwa nusu na akazungumza juu ya "makubaliano ya haki na China" ambayo utawala wake ulikuwa ukijadiliana "kikamilifu".

Lakini Wizara ya Biashara ya China ilikataa hili kama "isiyo na msingi wowote". Vichwa vya habari katika vyombo vya habari vya serikali pia havijamuepusha: "Trump labda ndiye rais mbaya zaidi katika historia ya Amerika," ilisoma moja ya taarifa kwenye Runinga ya serikali.

Inaonekana rais wa Merika anasubiri mwenzake wa China Xi Jinping kuchukua simu.

g

Chanzo cha picha, BBC/ Xiqing Wang

Maelezo ya picha, Wafanyabiashara kutoka kila mahali huja Yiwu kununua bidhaa, wakitoa masoko mapya kwa wauzaji nje wa China

Wakati BBC ilipiga simu kwa wasambazaji ili kuona ikiwa usafirishaji kwenda Marekani umeanza tena, kilichoibuka ni picha ya fujo. Mtoa huduma mmoja alisema alikuwa na nguo nusu milioni zinazosubiri kusafirishwa hadi Walmart, na wengine wachache waliunga mkono kutokuwa na uhakika wake. Lakini wauzaji nje wawili tuliozungumza nao walisema baadhi ya usafirishaji kutoka kwa wauzaji wa reja reja wa Marekani ulikuwa umeanza upya.

Kwa biashara zozote, bila shaka mtumiaji wa Marekani atahisi kutokuwepo, au uwezekano wa bei ya juu, ya bidhaa za Kichina.

Fursa zaidi ya Marekani

Marekani bado inategemea sana utengenezaji wa Wachina ili kukidhi mahitaji yake ya ndani - fikiria simu, kompyuta, semiconductors, fanicha, nguo na, bila shaka, vinyago. Elektroniki na mashine pekee huchangia zaidi ya 50% ya uagizaji wa Amerika.

Walmart na Target waliripotiwa kumwambia Bw Trump katika mkutano wiki iliyopita kwamba wanunuzi wana uwezekano wa kuona rafu tupu na bei ya juu kutoka mwezi ujao. Pia walionya kuwa mshtuko wa usambazaji unaweza kuendelea hadi Krismasi.

Baadhi ya 90% ya mapambo yote ya Krismasi yaliyotundikwa karibu na nyumba za Marekani yanatoka Yiwu nchini Uchina, ambapo wauzaji, wakiwa wamezungukwa na ishara za zinzotakikana ulimwengu "Feliz Navidad" walituambia sasa wanajaribu kuzingatia mauzo kwa Amerika Kusini.

Na juhudi hizo zinaonekana wazi katika Yiwu.

Wauzaji huko Yiwu wanajifunza kuzungumza na wanunuzi kutoka nchi tofauti

g

Chanzo cha picha, BBC/ Xiqing Wang

Maelezo ya picha, Wauzaji katika Yiwu wanajifunza kuzungumza na wanunuzi kutoka nchi mbalimbali

Haya ni masomo ya bure yanayotolewa na chama cha serikali za mitaa. Wanafunzi wengi ni wanawake, wamevaa mavazi yao bora ili kuwavutia wateja wao.

"Wanawake hawa ndio uti wa mgongo wa biashara kote China," anasema mmiliki mmoja wa duka, ambaye asili yake ni Iran na anatoa masomo ya kibinafsi kwa mwanafunzi mwenye hamu.

Wafanyabiashara wengi tayari wanaweza kuzungumza maneno machache ya Kiingereza. Sasa wanasema wanahitaji kusalimiana na wanunuzi wao wapya kwa Kihispania na Kiarabu - ishara ndogo lakini muhimu ya mabadiliko ya uhusiano wa kibiashara wa China.

Oscar, Mkolombia ambaye alituambia jina lake la kwanza tu, alikuwa akizunguka kwenye kumbi za soko na mifuko iliyojaa sungura na dubu.

Anasema vita vya kibiashara vya Amerika na China vinatoa "fursa nyingi" kwa wafanyabiashara kutoka sehemu zingine za ulimwengu.

"Kufanya biashara na China ni muhimu sana," anasisitiza. "[Kufanya biashara na] Marekani siku hizi, kidogo."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi