Sababu na uwezo wa China kwenda jino kwa jino na Marekani katika ushuru wa bidhaa

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Sammy Awami
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kuweka ushuru kwa bidhaa zinazotoka nchi mbalimbali ulimwenguni imezua taharuki kubwa ya kibiashara na uchumi nchini Marekani na kwingineko ulimwenguni
Wakati viongozi waandamizi wa serikali ya Trump, na hasa washauri wake wa kiuchumi walishikilia msimamo wao kwamba kuweka ushuru ni uamuzi sahihi, masoko ya hisa yaliitikia uamuzi huo kwa mshtuko na kuporomoka kwa kiasi kikubwa
Nchi za Ulaya na kwingineko duniani, viongozi walihaha, wachache – kama Canada - wakiukosoa uamuzi wa Trump wazi wazi na kuapa kulipiza kisasi kwa kupandisha ushuru kwa bidhaa za Marekani zinazoingia nchini mwao.
Kwa mujibu kwa Trump mwenyewe, makumi ya viongozi walikuwa wakimpigia simu wakitaka kujadiliana nae juu ya kupunguza ushuru huo.
Zimbabwe, kwa mfano, Rais Emmerson Mnangagwa yeye alitangaza kuondoa ushuru wote kwa bidhaa zinazotoka Marekani kama hatua ya kujenga uhusiano mzuri na serikali ya Trump, iliyoiwekea Zimbabwe 18% ya ushuru kwa bidhaa zake.
"Hatua hii imelenga kuwezesha upanuzi wa uagizaji wa bidhaa kutoka Marekani ndani ya soko la Zimbabwe, huku ikihamasisha pia ukuaji wa mauzo ya nje ya bidhaa za Zimbabwe zinazoelekezwa Marekani" aliandika Rais Emmerson Mnangagwa katika ukurasa wake wa X
Lakini China, pamoja na kuchalazwa na kiwango kikubwa cha ushuru cha 145%, si tu kwamba iliirudishia Marekani kwa kuziwekea bidhaa zake ushuru wa 125%, lakini pia ikaapa kupambana na hasimu wake huyo hadi dakika ya mwisho.
"Tishio la Marekani kuongeza ushuru zaidi kwa bidhaa za China ni kosa juu ya kosa. China haitakubali. Na ikiwa Marekani itang'ang'ania msimamo wake huo, China itapambana hadi dakika ya mwisho," ilisema taarifa kutoka Wizara ya Biashara ya China
Hii imewafanya wengi kujiuliza kwanini China imekuwa na ujasiri wa kuisimikia Marekani kiasi hicho?
Si biashara tu, ni itikadi na ubabe wa Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa China, hatua ya Marekani kupandisha ushuru kwa kiwango kile halikuwa swala la biashara tu. Wao wamelitafsiri kama muendelezo wa ubabe wa Marekani lakini pia vita ya kiitikadi. Hii imeifanya China kuapa kuendelea kupimana nguvu na Marekani hadi dakika ya mwisho
"China ni nchi inayowajibika. Majibu yetu dhidi ya ubabe wa Marekani si tu yanalinda maslahi na haki halali za China, lakini pia zinalenga kulinda kanuni za kimataifa za biashara, na maslahi ya nchi zingine zote duniani" alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi
Wang aliongeza kwamba nchi inapokabiliwa na ubabe wa Marekani, suluhisho haliwezikuwa kusalimu amri.
Soko mbadala

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Marekani ni soko muhimu sana kwa bidhaa za China. Mwaka jana tu, China ilipeleka bidhaa zenye thamani zaidi ya $400 bilioni. Hata hivyo, kwa miaka mingi China imekuwa ikitafuta na kupanua zaidi masoko katika mabara na nchi nyingi zaidi zikiwemo za Ulaya, Asia na Afrika pia.
Kufuatia ushuru wa Marekani uliozikumba hata nchi za Ulaya, wiki iliyopita (10 Aprili) China na Kamisheni ya Ulaya zimefanya mazungumzo kuangalia namna pande hizo mbili zitaimarisha ushirkiano wao wa kibiashara.
Kwa kuanza, Ulaya tayari iko mbioni kuondoa ushuru kwa bidhaa za magari ya umeme za China na badala yake iweke tu bei ya chini kwa bidhaa hizo. Ni ushirika wa dharura unaoibuka baada ya wawili hao kukumbwa na ushuru wa Marekani.
Ijumaa iliyopita, Rais Xi Jinping wa China alimwambia mwenzake wa Uhispania aliyemtembelea kwamba "China iungane na Umoja wa Ulaya kupinga vitendo vya kibabe vya Marekani"
Wiki hii, Rais Xi anatarajiwa kutembelea Malaysia, Vietnam and Cambodia, nchi ambazo ni miongoni mwa zilizokumbwa na ushuru mkali wa Marekani.
Fursa za China kuiumiza Marekani
China inafahamu pia kwamba Marekani inaihitaji sana China – hasa kwa bidhaa za kilimo kama mtama, kuku, mayai na maharage – ambayo kwa kiasi kikubwa vinatoka majimbo ambayo watu wake wengi ndio walimpigia kura Trump kwa wingi kupitia chama cha Republican. Hii inaweza kuwa na madhara kisiasa kwa Trump hata akapoteza uungwaji mkono.
Lakini Marekani inaihitaji sana China katika utengenezaji na uuzwaji wa bidhaa za kielekroniki kama simu na magari, hasa kupitia makampuni kama Apple na Tesla. Tayari kuna taarifa kwamba China inapanga kuongeza masharti katika uendeshwaji wa makampuni na uzalishaji wa bidhaa za makampuni haya nchini humo.
Si ajabu ndio sababu wawekezaji wa Kimarekani nchini China kama Elon Musk, ambaye pia ni mshauri na mwandani wa Trump wamekuwa wakipinga hadharani hatua ya serikali ya Trump kuongeza kiwango cha ushuru mkubwa kwa China.
Siasa za China na uwezo wa kustahimili

Chanzo cha picha, Getty Images
Pasi na shaka, ushuru huu wa Marekani utaiumiza China. Marekani ni soko kubwa na muhimu sana kwa China, hasa kwa bidhaa kama samani, nguo, vitu na vifaa vya matumizi ya nyumbani na midori ya kuchezea Watoto. Hata hivyo, China inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kustahimili maumivu na kwa muda mrefu.
'China imekuwepo kwa miaka takribani 5000. Na kwa kiasi kikubwa katika muda wote huu Marekani haikuwepo, na tulistahimili vizuri tu" amenukuliwa Victor Gao, mchambuzi wa masuala ya China alipozungumza na kituo cha habari cha Uingereza cha Channel 4
Mfumo wa China wa kisiasa pia unafanya serikali iwe na uwezo si tu wa kuzisaidia biashara kwa njia ya ruzuku na zinginezo, lakini pia kudhibiti malalamiko na ukaidi wa namna yoyote ambao ni rahisi kuibuka na kuoneakana nchini Marekani













