Khamenei: Tatizo letu na Marekani haliwezi kutatuliwa

f

Chanzo cha picha, Leader.ir

Muda wa kusoma: Dakika 4

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, akizungumza katika hafla ya maombolezo ya Imamu wa nane wa Kishia amesema kuwa, Marekani inataka "kutoa amri kwa taifa la Iran," na hiyo ndiyo sababu ya mivutano, pamoja na uungaji mkono wa Marekani kwa Israel katika vita vya siku 12.

Matamshi hayo ya Ayatollah Khamenei yanakuja huku muda wa mwisho wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa Iran kufikia makubaliano mapya ya nyuklia ukikaribia kuisha.

Nchi hizi tatu za Ulaya ziliipa Iran hadi mwishoni mwa mwezi wa Agosti kuingia katika makubaliano mapya ya nyuklia, na kutishia kuchukua hatua kutokana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kufungua njia ya kurejeshwa kwa maazimio ya Baraza la Usalama na vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikiwa mmoja wa pande zinazohusika na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyofikiwa mwaka 2015 hataridhishwa na hatua za Iran katika makubaliano hayo, anaweza kuanzisha upya vikwazo vya Baraza la Usalama, kupitia mchakato unaojulikana kwa jina la "trigger mechanism.”

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amewakemea Wairani waliounga mkono misimamo ya serikali ya Marekani na Israel katika vita vya hivi karibuni na kusema:

"Tarehe 13 Juni Iran ilishambuliwa. Siku moja baadaye, Juni 14, kundi la mawakala wa Marekani liliketi katika mji mkuu wa Ulaya na kuanza kujadili serikali mbadala kwa Jamhuri ya Kiislamu."

Mbali na hilo, Ayatullah Khamenei amekosoa vikali Israel katika vita vya Gaza, akisema "njia za kuipa Israel misaada" ya kijeshi zinapaswa kufungwa "kutoka pande zote."

Amesema Jamhuri ya Kiislamu "imejiandaa kikamilifu" kufanya "kila linalowezekana" katika suala hili. Kwa mara nyingine tena aliita Israeli "kansa" na kueleza matumaini kwamba "mizizi yake itang'olewa."

Pia unaweza kusoma

Utetezi kwa rais

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika hotuba yake, Ali Khamenei ametoa wito wa kuungwa mkono Massoud Pezzekian, akisema: "Muungeni mkono rais. Rais ni mchapakazi, mwenye bidii na mvumilivu."

Alitoa wito wa kuwepo kwa "umoja kati ya serikali na taifa" na kusema ushauri wake ni kwamba "umoja kati ya taifa na serikali, kati ya viongozi mbalimbali, kati ya jeshi na wananchi, kati ya wananchi, hili ni jambo ambalo lazima lihifadhiwe kwa gharama yoyote."

Masoud Pezhakian hivi karibuni aliwahutubia wapinzani wa mazungumzo ya nyuklia katika mkutano na vyombo vya habari: "Mazungumzo haimaanishi kujisalimisha. Ikiwa hatuna mazungumzo, unataka kupigana? Hatupaswi kuweka hisia mbele.”

Kufuatia matamshi ya Pezzekian, duru mpya ya ukosoaji dhidi ya maneno na matendo yake ilianza. Wakosoaji wa Bw. Pezzekian katika bunge walitoa wito wa kuthibitishwa kuwa "hana uwezo wa kisiasa" na kumlinganisha na Abolhassan Banisadr, rais wa kwanza wa Iran ambaye uzembe wake wa kisiasa ulipigiwa kura na bunge na kufukuzwa kazi na Ayatollah Khomeini.

Katika wiki kadhaa baada ya vita vya Israel na Iran, wanaharakati wengi na makundi ya kisiasa na kijamii yametoa mapendekezo ya kubadili mtazamo na wakati mwingine muundo wa serikali ya Iran.

Baadhi wametaka kura ya maoni ifanyike akiwemo Mir Hossein Mousavi ambaye yuko chini ya kifungo cha nyumbani na kutaka kura ya maoni ifanyike kuhusu mabadiliko ya katiba na kuunda Bunge la Katiba katika taarifa yake.

Kutakuwa na mbadiliko?

Baada ya kumalizika vita hivyo vilivyodumu kwa siku 12, wengi walikuwa na matumaini viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu wangekubali mabadiliko. Kadiri siku zinavyopita, serikali inaonyesha dalili chache za kubadilisha tabia yake.

Katika sera ya mambo ya nje ya Iran, hakuna vita wala amani. Katika sera ya ndani, hakuna mabadiliko wala utulivu. Mashaka haya yamemaliza uvumilivu wa wengi.

Muda wa mwisho uliowekwa unakaribia kumalizika ndani ya wiki moja, kiongozi wa serikali ya Iran anasema, tatizo la Iran na Marekani haliwezi kutatulika na kuwakumbusha wakosoaji wa ndani kwamba hata kama mabadiliko yatawezekana, mabadiliko hayo hayatakuwa makubwa.