Vita vya Israel-Iran vyamfukuzisha kazi Mkuu wa Idara ya Ujasusi Marekani

Luteni Jenerali Jeffery Kruse, ametimuliwa ikiwa ni wiki chache tu baada ya Ikulu ya White House kukosoa ripoti kuhusu athari za mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran ya Juni 22, 2025.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Eze ajiunga Arsenal, atangazwa punde

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Arsenal imemaliza usajili wa mshambuliaji wa England, Eberechi Eze, kutoka Crystal Palace.

    Gunners walikubaliana na mkataba wa pauni milioni 60, ikiwa ni pamoja na pauni milioni 8 za ziada, kumfanya mshambuliaji huyo wa miaka 27 kuwa usajili wao wa saba wa majira ya joto.

    Eze alikuwa mojawapo ya walchezaji wanaosakwa na Tottenham msimu huu, na Spurs walikuwa wamekubaliana na Palace na Eze kuhusu masharti ya mkataba.

    Hata hivyo, mahasimu wa Spurs wa Kaskazini mwa London walifanya harakati za kumsajili Eze siku ya Jumatano, na shabiki huyo wa Arsenal tangu utotoni aliamua kujiunga na Gunners, baada ya kuanza taaluma yake ya vijana na klabu hiyo.

    Mkurugenzi wa Michezo, Andrea Berta, alielezea Eze kama “kipaji cha ubunifu chenye ubora mkubwa wa kiufundi”.

    Kocha Mikel Arteta alisema: “Ni mchezaji mwenye nguvu na wa kusisimua ambaye atatupa kitu kipya katika mchezo wetu kwenye kushambulia. Kinachoibuka sawa na kipaji chake na akili yake kama mchezaji ni jinsi ambavyo amejitahidi kwa bidii katika taaluma yake hadi kufikia hapa alipo sasa.

    “Safari yake, mtazamo wake, na tamaa yake ndizo tunazotaka kwenye kikosi chetu, na tunapenda jinsi ambavyo kumefanya yeye na familia yake kujiunga na klabu yetu.”

  2. Vita vya Iran vyamfukuzisha kazi Mkuu wa Idara ya Ujasusi Marekani

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, amemfukuza kazi mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Ulinzi (DIA), Luterni Jenerali Jeffery Kruse, wiki chache tu baada ya Ikulu ya White House kukosoa ripoti kuhusu athari za mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.

    Inaripotiwa pia kuwa makamanda wengine wawili wa ngazi za juu katika jeshi wametimuliwa na Pentagon, ingawa wizara ya ulinzi haijatoa maelezo ya haraka kuhusu hatua hiyo.

    Mwezi Juni, Rais Donald Trump alipinga vikali ripoti iliyovuja kutoka DIA iliyodai kuwa mashambulizi ya Marekani yalichelewesha mpango wa nyuklia wa Iran kwa miezi michache pekee. White House ilitaja tathmini hiyo kuwa “si sahihi kabisa.” Trump alidai maeneo ya nyuklia ya Iran “yameharibiwa kabisa,” na akaushutumu vyombo vya habari kwa “kujaribu kudhalilisha moja ya mashambulizi ya kijeshi yenye mafanikio zaidi katika historia.”

    Akiwa katika mkutano wa kilele wa NATO wakati huo, Hegseth alisema ripoti hiyo ilitokana na “uelewa wa kijasusi wa kiwango cha chini” na akathibitisha kuwa FBI ilikuwa inachunguza uvujaji huo wa taarifa. Kuondolewa kwa Kruse kuliwekwa wazi kwa mara ya kwanza na gazeti la Washington Post. BBC imewasiliana na Pentagon kwa maoni zaidi.

    Idara ya Ujasusi ya Ulinzi (DIA), ambayo ipo chini ya Pentagon, hushughulikia ujasusi wa kijeshi unaosaidia operesheni, ikikusanya taarifa nyingi za kiteknolojia, tofauti na CIA ambayo inahusiana zaidi na ujasusi wa kisiasa na kidiplomasia.

    Chanzo kimoja kiliiambia Reuters kuwa Hegseth pia ameagiza kuondolewa kwa mkuu wa hifadhi ya wanamaji wa Marekani na kamanda wa Jeshi Maalum la Wanamaji (Naval Special Warfare Command).

    Katika taarifa yake, Seneta Mark Warner wa Marekani alionya kuwa kufukuzwa kwa Kruse ni dalili kuwa Trump ana “tabia hatari ya kuchukulia ujasusi kama kipimo cha uaminifu badala ya kinga ya usalama wa taifa letu.”

    Hii si mara ya kwanza Trump kuwaondoa maafisa ambao tathmini zao zimeonekana kutokubaliana na mitazamo yake. Mwezi Julai, aliagiza kufukuzwa kwa Kamishna wa Takwimu za kazi, Erika McEntarfer, baada ya ripoti kuonyesha ukuaji wa ajira umepungua.

    Aprili, Trump alimfukuza Jenerali Timothy Haugh kutoka nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Usalama wa Taifa (NSA), pamoja na wafanyakazi zaidi ya kumi na wawili wa Baraza la Usalama la Taifa katika Ikulu.

    Aidha, Hegseth ameendelea kuwaondoa maafisa kadhaa wa kijeshi Pentagon; Februari alimuondoa Jenerali C. Q. Brown wa Jeshi la Anga pamoja na majenerali na makamanda wengine sita.

  3. Man City yaduwazwa na Spurs nyumbani, yachapwa 2-0 EPL

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tottenham Hotspur wameendeleza mwanzo mzuri chini ya kocha mpya Thomas Frank baada ya kushinda kwa mara ya pili mfululizo katika Ligi Kuu ya England, wakiishtua Manchester City kwa mara nyingine katika dimba la Etihad Stadium.

    Spurs walikuwa wameishushia City kipigo cha mabao 4-0 Novemba iliyopita, na safari hii wakarudi tena na kuzoa alama zote tatu baada ya kucheza kwa nidhamu kubwa ya kiulinzi na kushinda 0-2.

    Manchester City walianza kwa kasi kupitia mshambuliaji wao Omar Marmoush, ambaye mara mbili alikaribia kuipatia timu yake bao la mapema, akilazimisha kipa wa Spurs, Guglielmo Vicario, kufanya maajabu langoni.

    Hata hivyo, pamoja na mashambulizi hayo, City walijikuta nyuma baada ya Spurs kutumia nafasi yao ya kwanza muhimu. Richarlison alipiga krosi ya chini iliyounganishwa kwa usahihi na Brennan Johnson. Bao hilo mwanzoni lilikataliwa kwa kuotea, lakini VAR lilibadilisha uamuzi na kukubaliwa.

    Dakika za nyongeza saba zilizopewa kutokana na majeraha ya beki wa City Rayan Aït-Nouri zilitosha kwa Spurs kuongeza bao la pili. Kipa James Trafford alitoa pasi mbovu ndani ya eneo lake, ikanaswa na Joao Palhinha ambaye aliuweka mpira wavuni. Ilikuwa dakika ngumu kwa Trafford ambaye pia aliepuka kadi nyekundu kufuatia kugongana na Mohammed Kudus.

    Erling Haaland alipoteza nafasi ya wazi ya kufunga kabla ya mapumziko baada ya kupiga kichwa nje akiwa karibu na lango. Kipindi cha pili City walijaribu kila njia, lakini ukuta wa Tottenham uliimarika na kuzuia mashambulizi yote. Matokeo haya yamewapa Spurs mechi ya pili mfululizo msimu huu bila kuruhusu bao, na kuiacha City ikiwa na maswali mazito ya kujibu, kuhusu kiwango chake.

  4. CHAN 2024: Uganda kulinda heshima ya Afrika Mashariki?

    C

    Chanzo cha picha, CAF

    Baada ya Kenya na Tanzania kutolewa jana katika robo fainali ya CHAN 2024, matumaini ya Afrika Mashariki sasa yapo mikononi mwa Uganda pekee. Cranes jioni hii wanakabiliana na mabingwa watetezi Senegal katika uwanja wa Mandela National Stadium jijini Kampala, mechi ambayo inaweza kuandika historia mpya.

    Uganda imepiga hatua kubwa kwa mara ya kwanza kufuzu hatua ya mtoano baada ya kuongoza Kundi C kwa alama saba. Mafanikio haya yamewasha moto wa matumaini kwa mashabiki, huku kocha Morley Byekwaso akisisitiza kwamba nyumbani kwao hakuna lisilowezekana. “Ni mchezo maalum kwa sababu tunacheza mbele ya mashabiki wetu. Tunahitaji nidhamu na ujasiri ili kuibuka washindi,” alisema.

    Kwa kuondolewa kwa jirani zao, Cranes sasa wanabeba bendera ya ukanda mzima. Waganda wanajua ushindi dhidi ya Senegal si tu kwa ajili yao bali pia kwa heshima ya Afrika Mashariki. Mashabiki wa Kenya na Tanzania bila shaka wataelekeza macho yao kwa Cranes katika pambano hili la moto.

    Kurejea kwa kiungo Joel Sserunjogi baada ya kutumikia adhabu ya kadi ni nguvu ya nyongeza kwa kikosi cha Uganda. Nyota huyo wa KCCA FC anasema “Kesho kwetu ni fainali. Nitajitahidi kutoa kila kitu kwa timu na mashabiki wetu.”

    Kwa mashabiki wa Cranes, kumbukumbu ya sare ya 3-3 dhidi ya Afrika Kusini bado ipo motomoto, wakiamini ari ile ile inaweza kuwa silaha kubwa. Ikiwa Uganda wataiondoa Senegal, basi kweli watakuwa wametetea heshima ya Afrika Mashariki.

  5. 'Chawa' wa rais wa zamani ahukumiwa miaka 67 jela kwa ukatili

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mtu mmoja mwenye asili ya Gambia, aliyekuwa sehemu ya kikundi cha silaha kilichosimamiwa na dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Yahya Jammeh, na ambaye alihukumiwa kwa ukatili na jopo la majaji Marekani mnamo Aprili, amehukumiwa zaidi ya miaka 67 jela, kulingana na Tume ya Sheria ya Marekani Ijumaa.

    Michael Sang Correa, raia wa Gambia, alihukumiwa na jopo la majaji watatu huko Colorado kwa kushiriki kwake katika ukatili dhidi ya watu wengi nchini Gambia mwaka 2006, waliopigwa na kuchomwa moto, kutokana na washukiwa wa kuhusika katika njama ya mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo, ilisema Tume ya Sheria ya Marekani.

    Correa alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wanamtetea na kumpigia debe rais wa wakati huo Jammeh, kwa kiwango kinachotajwa cha kupitiliza ambacho kwa Tanzania watu hawa wanafahamika kama 'chawa'.

    Correa, mwenye umri wa miaka 46, alipewa hukumu ya miezi 810 jela na Jaji Mkuu Christine Arguello wa Wilaya ya Colorado baada ya kutolewa hukumu kwa kosa moja la njama ya kufanya ukatili na makosa matano ya ukatili, kulingana na taarifa ya tume hiyo.

    Kesi hii ilibainisha kesi ya kwanza ya jinai dhidi ya mtu aliyehusika na kikundi kilichokuwa kinahofiwa kinachojulikana kama "The Junglers", kilichofanya kazi katika taifa lenye sera kali ya kijeshiwakati wa utawala wa Jammeh. Rais huyo wa zamani alishika madaraka mwaka 1994 na kuzuia jaribio kadhaa la kumng’oa madarakani kabla ya kupoteza uchaguzi wa mwaka 2016.

    Correa alikamatwa mwaka 2020 chini ya sheria inayotambua uhalifu kwa mtu yeyote nchini Marekani hata kama katenda ukatili katika nchi nyingine. Jammeh alipinga madai ya ukatili wakati wa utawala wake.

    The Junglers walikuwa tawi la siri la jeshi la Gambia lililofuata amri za Jammeh. Vikundi vya haki za binadamu na majeruhi wa zamani wanasema walikuwa wakitekeleza ukatili mkali zaidi baada ya jaribio lililoshindikana la mapinduzi mwaka 2006.

    Washukiwa wa njama za mapinduzi na wapinzani wengine waliosikika kupinga utawala wa Jammeh walipelekwa kwenye Shirika la Taifa la Ujasusi, karibu na mojawapo ya fukwe za mchanga mweupe za mji mkuu Banjul, kulingana na majeruhi.

    Baadhi walikuta wakiwa ndani ya chumba cha ukatili ambapo waliteswa kwa kutumia umeme, kupigwa, na kuchomwa kwa kutumia kemikali, walisema.

  6. Uingereza kulipa Wakenya fidia ya $4 milioni kwa moto wa Laikipia 2021

    a

    Chanzo cha picha, Reuters

    Uingereza imekubali kulipa fidia ya pauni milioni 2.9 ($4 milioni) kwa wakazi wanaoishi karibu na hifadhi ya wanyamapori nchini Kenya, kufuatia moto uliosababishwa na mazoezi ya kijeshi ya Jeshi la Uingereza mwaka 2021, wakili wa walalamikaji alisema Ijumaa.

    Jeshi la Uingereza hufanya mazoezi ya pamoja na Kenya katika eneo la Laikipia kaskazini, ambapo lina kambi katika mji wa Nanyuki.

    Moto huo ulizuka karibu na eneo la Lolldaiga mnamo Machi 2021. Serikali ya Uingereza siku ya Ijumaa ilieleza masikitiko yake kuhusu tukio hilo.

    “Moto wa Lolldaiga ulikuwa wa kusikitisha sana, na Uingereza inatambua muda mrefu uliotumika kutatua suala hili na msongo wa mawazo uliosababishwa katika jamii zilizoathirika,” msemaji wa Ubalozi wa Uingereza jijini Nairobi alisema katika taarifa.

  7. Korea Kusini yakiri kuwashambulia wanajeshi wa Korea Kaskazini mpakani

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Korea Kusini imethibitisha kuwa ilifyatua risasi za onyo mapema wiki hii dhidi ya wanajeshi wa Korea Kaskazini waliovuka kwa muda mfupi mpaka ulioimarishwa vikali unaozitenganisha nchi hizo mbili.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini vilizitaja risasi hizo kama “uchokozi wa makusudi” na Pyongyang imeituhumu Seoul kwa kuhatarisha “mvutano usioweza kudhibitiwa.”

    Tukio hili limewekwa hadharani wakati Rais mpya wa Korea Kusini, Lee Jae Myung, akiondoka Seoul Jumamosi kuelekea Tokyo na Washington kwa ziara rasmi.

    Pyongyang imeongeza msimamo wake mkali katika wiki za hivi karibuni, huku dada wa kiongozi Kim Jong Un akipinga jitihada za maridhiano zilizofanywa na serikali ya Lee.

    Tukio hilo lilitokea katikati ya juhudi za Korea Kaskazini, zilizoanza mwaka jana, za kufunga kabisa mpaka wake na Korea Kusini.

    Kuna eneo ambalo hapaswi kuonekana mtu, linaloitwa Demilitarised Zone (DMZ), linalotenganisha korea Kaskazini na Korea Kusini, na mara kwa mara uvamizi hutokea na kuongeza mvutano. Mpaka wa DMZ hauna uzio na alama zake zimezibwa na uoto mnene wa miti na vichaka.

    Wakuu wa Majeshi ya Pamoja ya Korea Kusini (JCS) walisema katika taarifa kwamba baadhi ya wanajeshi wa Korea Kaskazini waliokuwa wakifanya kazi kwenye eneo la mpaka walivuka mstari wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili majira ya saa 9 alasiri kwa muda wa Seoul siku ya Jumanne.

    Wanajeshi hao baadaye walirudi upande wa kaskazini, JCS waliongeza.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini, Luteni Jenerali Ko Jong Chol alisema “Hii ni hatua ya mwanzo yenye uzito mkubwa ambayo bila shaka itasukuma hali katika eneo la mpaka wa kusini, ambako majeshi makubwa yako tayari, kufikia hatua isiyoweza kudhibitiwa,” vyombo vya habari vya serikali vilimnukuu akisema.

  8. 'Hakuna kinachoitwa orodha ya Epstein" - Maxwell

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ghislaine Maxwell, mshirika na swahiba wa mfanyabiashara wa ngono aliyetiwa hatiani Jeffrey Epstein, aliwaambia maafisa wa Marekani kwamba “orodha ya wateja” inayozungumziwa sana haipo, kulingana na nakala ya mahojiano yake iliyowekwa wazi.

    Katika mahojiano hayo ya Julai na Naibu Mwanasheria Mkuu Todd Blanche, Maxwell alisema kuwa hakujua chochote kuhusu vitisho vya kutumika kama “Msaliti” na hakushuhudia mwenendo wowote usiofaa kutoka kwa Rais Donald Trump au Rais wa zamani Bill Clinton.

    Alizungumzia pia uhusiano wake na Epstein pamoja na Prince Andrew, na akaita madai kwamba alijihusisha na ngono na msichana mdogo nyumbani kwake kama jambo “lisilowezekana kabisa kufikirika.”

    Maxwell anatafuta msamaha kutoka kwa Trump na ameshtumiwa kwa kudanganya maafisa.

    Mahojiano hayo yalifanyika wakati serikali ya Trump ilikuwa chini ya shinikizo la kuendelea kufichua taarifa zaidi kuhusu Epstein ambaye Trump alikuwa na urafiki naye kabla ya urafiki wao kufa mwaka 2004, kwa mujibu wa rais huyo.

    Muda mfupi baada ya mahojiano na Blanche ambaye hapo awali alikuwa wakili binafsi wa Trump Maxwell alihamishwa kutoka gereza la Florida hadi gereza jingine lenye ulinzi mdogo huko Texas. Haijajulikana ni kwa nini uhamisho huo ulifanyika.

    Ikulu ya White House imesisitiza kwamba “hakuna upendeleo unaotolewa au kuzungumziwa” katika kesi ya Maxwell.

    Kwa sasa, Maxwell anatumikia kifungo cha miaka 20 kwa makosa ya ulanguzi wa ngono, na ameomba Mahakama Kuu ya Marekani kufuta hukumu yake. Wakili wake amesema wangepokea kwa mikono miwili msamaha kutoka kwa rais.

    Shinikizo pia limekuwa likiongezeka kutoka ndani ya chama cha Republican cha Trump kwa ajili ya uwazi zaidi kuhusu uchunguzi wa Epstein. Lakini rais amewashutumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kutumia kesi hiyo kuondoa umakini kutoka kwenye kile anachokiita mafanikio ya serikali yake.

    Katika nakala za mahojiano zenye kurasa 300, baadhi zikiwa zimefichwa sehemu, Maxwell alisema kwamba ingawa anaamini Trump na Epstein walikuwa marafiki “katika mikusanyiko ya kijamii”, haoni kama walikuwa karibu sana.

    Pia alisema hakumbuki Trump kutuma ujumbe wa heri za siku ya kuzaliwa kwa Epstein mnamo 2003, uliokuwa gumzo baada ya kuripotiwa na jarida la Wall Street Journal hivi karibuni.

    Katika mahojiano hayo, Blanche pia alimuuliza Maxwell kuhusu “orodha ya wateja” yenye majina makubwa ambayo imekuwa kiini cha nadharia za njama kwa miaka ya hivi karibuni.

    Maxwell aliulizwa kuhusu watu mashuhuri wengine, akiwemo Bill Gates, Elon Musk, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Ehud Barak, Waziri wa Afya na Huduma za Binadamu Robert F. Kennedy Jr, mwigizaji Kevin Spacey, mwanamitindo Naomi Campbell na Prince Andrew ambapo alikanusha kuwa ndiye aliyemtambulisha Andrew kwa Epstein.

    Orodha ya marafiki wake mashuhuri imekuwa kitovu cha nadharia za njama, zikidaiwa kufichwa na “deep state” ili kulinda wahusika wakuu katika uhalifu wa Epstein.

    Viongozi kadhaa wa serikali ya Trump akiwemo Mkurugenzi wa FBI Kash Patel na naibu mkurugenzi Dan Bongino waliwahi kurudia madai hayo zamani, ingawa sasa wameyakanusha.

    “Hakuna orodha,” Maxwell alisema.

  9. Hujambo! Karibu katika habari zetu za moja kwa moja Jumamosi ya leo