Kenya yapokea ushahidi 'wa kuhuzunisha' dhidi ya wanajeshi wa Uingereza

- Author, Gladys Kigo
- Nafasi, BBC News Nanyuki
Jopo la uchunguzi wa kihistoria kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu uliyofanywa na wanajeshi wa Uingereza nchini Kenya limekuwa likipokea ushahidi "wa kuhuzunisha" kutoka kwa wale wanaosema walidhulumiwa.
Makumi ya watu wiki hii wametoa ushahidi mbele ya kamati ya bunge kuhusu madai ya utovu wa nidhamu wa wanajeshi kutoka Kitengo cha Mafunzo ya Jeshi la Uingereza Kenya (Batuk).
Miongoni mwao ni familia ya msichana anayedaiwa kulemaa baada ya kugongwa na na lori la Jeshi la Uingereza, mama ambaye anasema alitelekezwa akiwa mjamzito na mwanamume aliyevamiwa na simba kufuatia moto unaodaiwa kuwashwa wakati wa zoezi la mafunzo ya kijeshi.
Kituo cha Batuk kilichopo Nanyuki, takriban kilomita 200 kaskazini mwa mji mkuu, Nairobi, na kilianzishwa mwaka wa 1964 muda mfupi baada ya taifa hilo la Afrika Mashariki kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.
Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale amesema kuwa Kenya itashinikiza mashtaka dhidi ya mwanajeshi yeyote wa Uingereza anayedaiwa kuvunja sheria wakati wanajeshi hao walipokuwa nchini humo miongo kadhaa iliyopita.
Ubalozi wa Uingereza nchini Kenya uliiambia BBC kuwa unafahamu shauri hilo na kwamba unanuia kutoa ushirikiano kwa wachunguzi.
Mamia ya watu wiki hii wamemiminika katika mikutano minne ya hadhara iliyofanyika karibu na kambi ya Batuk ili kusikiliza simulizi zenye hisia kuhusiana na madai ya utovu wa nidhamu wa wanajeshi wa Uingereza.
Memusi Lochede alielezea jinsi maafisa wa Uingereza waliahidi kumtunza bintiye Chaula Memusi mwenye umri wa miaka 22, ambaye yuko kwenye kiti cha magurudumu baada ya kudaiwa kugongwa na lori la jeshi la Uingereza na kujeruhiwa mnamo Januari 2019.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Walituma mwakilishi kuniambia kwamba hawataki kesi mahakamani na kwamba watamtunza binti yangu," mama huyo mwenye umri wa miaka 45 alitoa ushahidi mbele ya moja wapo wa vikao vilivyokuwa vikifanyika nje chini ya ukumbi wa Archers Post, ambapo jeshi la Uingereza hufanya mazoezi.
Chini ya makubaliano na serikali ya Kenya, hadi vikosi sita vya askari wa miguu kwa mwaka hufanya mazoezi ya wiki nane nchini Kenya.
Bi Lochede alisema walilipia bili za hospitali ya bintiye kwa miaka miwili, lakini walishindwa kulipa fidia kama walivyoahidi.
Lino Lemaramba aliambia BBC kuwa alishuhudia ajali hiyo na alishtuka kuona lori la jeshi la Uingereza likiondoka baada ya kugongana. Alisimama kumsaidia Bi Memusi.
"Lilikuwa lori aina ya Batuk, nilijaribu kulisimamisha lakini likaendelea kusonga," alidai.
"Lilikuwa tukio la kusikitisha, damu imetapakaa, mifupa yake ilipondwa ... watu waliogopa kumgusa," alisema, akielezea jinsi ilivyokuwa vigumu kumuinua kwenye gari lake na kumpeleka hospitali.

Ushuhuda mwingine wa kusikitisha katika kesi hiyo ulitoka kwa Generica Namoru mwenye umri wa miaka 28, ambaye alikuwa ameandamana na binti yake wa miaka mitano.
Aliwaambia wajumbe wa uchunguzi huo, ulioanzishwa na kamati ya ulinzi ya bunge la Kenya, kwamba alipata ujauzito alipokuwa katika uhusiano na mwanajeshi wa Uingereza Batuk.huko
Alipomjulisha kuwa ni mjamzito, alikatisha uhusiano na kuondoka Kenya, akamwacha alee mtoto peke yake. Waliendelea kuwasiliana kwa muda na akamwambia kuhusu kuzaliwa kwa binti yao, lakini mawasiliano hayakuendelea tena.
"Ninachotaka tu ada ya matunzo ili mtoto wangu aweze kwenda shule na kuwa na maisha bora ya baadaye," alisema.
Vikao hivyo pia vilisikia ushahidi kutoka kwa msururu wa watu ambao walisema walikuwa na matatizo makubwa ya kiafya kufuatia moto unaodaiwa kuwashwa na wanajeshi wa Uingereza wakati wa mazoezi yaliyokuwa yakiandaliwa katika hifadhi ya wanyamapori mwaka 2021.

Moto huo unaosemekana kudumu kwa siku nne, uliharibu zaidi ya ekari 12,000 za ardhi na kusababisha mtu mmoja kupoteza maisha.
Lipaso Legei aliyekuwa amevalia vazi la kitamaduni la kimasai katika kikao hicho, alieleza kuwa aliponea kifo baada ya kuvamiwa na simba aliyekuwa akitoroka moto katika makazi yake ya asili.
“Nilivamiwa na simba karibu nifariki. Chini ya shuka hizi nina makovu ya majeraha mgongoni mwangu"
Aliongeza kuwa ukulima pia haujawezekana: "Hatuwezi kupanda mahindi, wanyama wanaendelea kuvamia, mbwa wetu wamevamiwa na fisi na chui."
Watu kadhaa walisema walikuwa na matatizo makubwa ya kupumua na kuumwa na macho. Simon Kaburu aliwasilisha rekodi zake za matibabu kwa wabunge na kueleza kwamba alilazimika kuwa na dawa za kukabiliana na "matatizo ya kifua baada ya kuvuta moshi".
Zaidi ya watu 7,000 wa eneo hilo wanaaminika kuanza hatua za kisheria dhidi ya jeshi la Uingereza kufuatia moto huo.
Uchunguzi huo kwa kiasi kikubwa umechochewa na kesi ya kushangaza ya Agnes Wanjiru.
Mwili wake ulipatikana kwenye tanki la maji taka mwaka 2012 baada ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 21 kuonekana akiwa na kundi la wanajeshi wa Uingereza baada ya usiku wa kujivinjari .
Uchunguzi wa 2019 ulihitimisha kwamba aliuawa na askari mmoja au wawili wa Uingereza.

Uchunguzi wa umma wiki hii ulisikia madai zaidi kwamba Batuk na mamlaka ya Kenya walihusika katika kuficha kifo chake.
Mpwa wa Bi Wanjiru, Esther Njoki aliambia mojawapo ya vikao hivyo, katika Ukumbi wa Kijamii wa Nanyuki siku ya Jumanne vile familia yake ilivyofadhaika kutokana na kucheleweshwa kwa mashtaka yoyote.
"Tunataka kufungwa, tunadai haki," alisema.
Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya imefungua uchunguzi kuhusu kifo hicho, lakini haijafunguliwa mashtaka yoyote na Kenya haijaomba kurejeshwa kwa washukiwa hao.
Uingereza imedokeza kuwa haitapinga ombi lolote la kutaka mshukiwa arejeshwe.

Mbunge Nelson Koech, mwenyekiti wa kamati ya ulinzi ya bunge la Kenya, aliambia BBC baadhi ya madai yaliyowasilishwa kwenye vikao hivyo ni "mpya na ya kuhuzunisha".
"Imenigusa kwamba mambo yamekuwa yakifanyika hapa, tutabaini kama ni kweli au la," alisema.
Waziri wa ulinzi alisema katika mahojiano ya televisheni wiki hii kwamba Kenya imefaidika na ushirikiano wa kihistoria wa ulinzi na Uingereza na kusema zaidi ya watu 1,500 wa eneo hilo waliajiriwa huko Batuk.
Lakini Bw Duale alisema uchunguzi wa sasa unaweza kusababisha serikali kutafuta ushirikiano wa karibu na Uingereza kutokana na masuala yaliyoibuliwa, na kuongeza: “Vitendo vyote vya uhalifu vinavyofanywa katika ardhi yetu vitashughulikiwa katika nchi mwenyeji, hiyo ni Kenya.”
Msemaji wa Ubalozi wa Uingereza nchini Kenya alisema: "Tunafahamu kwamba Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Ulinzi, Ujasusi na Uhusiano wa Kigeni ya Kenya inaendesha uchunguzi wa bunge kuhusu shughuli za Batuk nchini Kenya. Ubalozi wa Uingereza mjini Nairobi na Batuk unakusudia kutoa ushirikiano.
"Ushirikiano wa ulinzi wa Uingereza na Kenya ni mojawapo ya nguvu kuu za uhusiano wetu na mafunzo na operesheni zetu za pamoja na Jeshi la Ulinzi la Kenya zinanaimarisha usalama wa Wakenya na Waingereza."
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












