Patriot: Kwanini makombora haya yanamnyima usingizi Putin?

a

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakati mapigano kati ya Ukraine na Urusi yakiingia mwaka wa tatu, mjadala mkubwa unaendelea kuhusu aina ya msaada wa kijeshi unaotakiwa kuikabili Urusi.

Katika mjadala huo, silaha moja imeibuka kama kipenzi cha wengi na tishio la moja kwa moja kwa Kremlin, Urusi na rais wake Vladimir Putin: mfumo wa makombora ya ulinzi wa anga wa Marekani ujulikanao kama Patriot.

Rais wa Marekani Donald Trump, alieleza Ukraine itahitaji makombora ya Patriot kwa ajili ya ulinzi wake, baada ya kuzungumza na Rais Volodymyr Zelensky siku ya Ijumaa, na kueleza kukatishwa tamaa na Rais wa Urusi, Putin kushindwa kusitisha mapigano.

Wiki hii ndege zisizo na rubani karibu ikiwa ni rekodi tangu kuanza kwa vita ya Ukraine zilishambulia mji mkuu wa nchi hiyo, jambo linalotishia uhai wake. Rais Trump sasa ametangaza tena kuunga mkono upatikanaji wa mfumo huo kwa Ukraine, akisisitiza kuwa ni silaha muhimu kwa uhai wa taifa hilo.

Lakini ni nini hasa kinachomfanya Putin awe na hofu kubwa dhidi ya mfumo huu?

Kwa nini Patriot ni silaha ya kipekee duniani?

s

Chanzo cha picha, Reuters

Mfumo wa Patriot, ambao jina lake kamili ni Phased Array Tracking Radar for Intercept on Target, umetengenezwa mahsusi kwa ajili ya ulinzi wa anga dhidi ya mashambulizi ya kisasa. Umeundwa kwa rada zenye uwezo mkubwa wa kugundua vitisho kutoka mbali, na makombora yanayozinduliwa haraka na kwa usahihi wa hali ya juu. Mfumo huu unaweza kugundua tishio kutoka zaidi ya kilomita 150, kulenga kombora adui au ndege, na kuifuatilia hadi kuharibiwa hewani kabla haijafika ardhini.

Tofauti na mifumo mingine ya ulinzi, Patriot hutumia teknolojia ya "track-via-missile", ambapo rada inaendelea kuongoza kombora hadi kulenga shabaha yake kwa usahihi wa hali ya juu. Inaweza kushughulikia mashambulizi ya wakati mmoja kutoka pande tofautitofauti, ikiwa ni pamoja na makombora ya balistiki, cruise, na ndege zisizo na rubani. Hii inaipa nafasi ya kipekee kwenye maeneo ya vita ambako mashambulizi huja kwa wingi na kwa kasi.

Zaidi ya uwezo wa kiufundi, Patriot pia imejaribiwa kwenye mazingira halisi ya kivita kwa zaidi ya miongo mitatu. Kutoka vita ya Ghuba mwaka 1991 hadi mashambulizi dhidi ya Israel, mfumo huu umejijengea hadhi ya kuaminika duniani kote. Ni silaha ambayo haizungumziwi kwa nadharia tu, bali ina historia ya ushindi dhidi ya makombora halisi.

Ukraine inahitaji Patriot si kwa dharura tu bali uhai

s

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ukraine kwa sasa inakabiliwa na moja ya mashambulizi makubwa zaidi ya anga katika historia yake. Mashambulizi ya kila siku ya ndege zisizo na rubani na makombora kutoka Urusi yamekuwa yakilenga miji mikuu, vituo vya nishati, hospitali na maeneo ya raia. Katika hali hiyo, uwezo wa Ukraine wa kuzuia mashambulizi hayo unategemea sana msaada wa nje, hasa mifumo ya hali ya juu kama Patriot.

Rais Volodymyr Zelenskiy amekuwa mstari wa mbele kuomba Marekani na washirika wake kuipatia Ukraine mifumo zaidi ya Patriot. Katika hotuba zake za kila wiki, amekuwa akisisitiza kuwa bila ulinzi wa anga, Ukraine itabaki kuwa hatarini dhidi ya mashambulizi ya kiholela.

Tayari baadhi ya vifaa vya Patriot vimeonesha mafanikio makubwa, zikiweza kuangusha makombora ya Urusi yaliyoelekezwa kwenye majengo ya makazi.

Hofu ya sasa ya Kyiv ni kwamba mashambulizi haya yanaongezeka kwa kiwango ambacho hifadhi ya makombora ya ulinzi inakaribia kuisha.

Marekani imekuwa na mashaka ya kuendelea kutoa msaada bila masharti, lakini kauli ya hivi karibuni ya Trump ya kuunga mkono upatikanaji wa mifumo zaidi ya Patriot imeleta tumaini jipya. Ukraine sasa inaona fursa ya kujenga safu thabiti ya ulinzi wa anga ambayo itabadilisha kabisa mkondo wa vita.

Kwa nini Patriot ni tishio kwa mkakati wa anga wa Urusi?

x

Chanzo cha picha, Reuters

Kwa miaka miwili ya vita, Urusi imekuwa ikitegemea mashambulizi ya anga kama njia kuu ya kuishambulia Ukraine. Makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani (drones) zenye mabomu zimekuwa zikitumika kusambaratisha miji mikuu na kuleta hofu miongoni mwa raia. Hata hivyo, kuwasili kwa mfumo wa Patriot kunamaanisha kuwa mashambulizi haya hayawezi tena kufanikiwa kwa urahisi.

Urusi inaelewa kuwa Patriot inaweza kuangusha makombora yake kabla hayajafanya uharibifu wowote. Hii inamaanisha hasara kubwa ya vifaa, kushuka kwa morali ya wanajeshi, na kupoteza nguvu ya kijeshi.

Kwa mfano, mashambulizi kadhaa yaliyofanywa dhidi ya Kyiv yamekwama kwa sababu mfumo wa Patriot uliangusha makombora yote yaliyorushwa, hali iliyowasha taharuki ndani ya Moscow. Ukraine inayo baadhi ya Patriot, lakini sasa inayahitaji zaidi kutoka kwa Marekani.

Zaidi ya hayo, Urusi inaogopa ujumbe wa kisiasa unaotumwa na mfumo huu. Kwa kuweka Patriot katika ardhi ya Ukraine, Marekani inaonesha kuwa iko tayari kuweka teknolojia ya hali ya juu kwenye mpaka wa ushawishi wa Urusi.

Hili linaifanya Kremlin kuhisi kuwa heshima yake ya kijeshi imevunjwa, na linaongeza wasiwasi kuhusu mustakabali wa ushawishi wake katika kanda ya Ulaya ya Mashariki. Lakini zaidi uhusiano wake na Marekani

  • Imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali ikiwemo wionews