BBC yamwomba Trump msamaha lakini yakataa kulipa fidia

Mawakili wa Trump wametishia kuishtaki BBC kwa fidia ya $1bn (£759m).

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja, nakutakia wikendi njema. Kwaheri

  2. Rais Samia Suluhu awaonya wanaotaka 'kuiharibu Tanzania'

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa nchi hiyo itaendelea kulinda maslahi yake kwa misingi ya utu, heshima na urithi wa misingi ya taifa kutoka kwa waasisi wake.

    “Katika kulinda maslahi ya nchi hakuna mbadala; ni lazima tulinde utu na heshima yetu. Tutaendelea kuongozwa na sera ile iliyofungamanishwa na wazee wetu wa zamani,” alisema Samia wakati wa ufunguzi rasmi wa Bunge la 13,

    Rais Samia aliongeza kuwa Tanzania itaendelea kuchangia katika kulinda utulivu wa kikanda na ndani ya nchi, akisema: “Taifa la Tanzania litaendelea kushiriki katika amani, katika kikanda na humu nchini.”

    Rais Samia pia amesisitiza umuhimu wa heshima katika mahusiano ya kikanda na kimataifa:

    “Tungependa tuheshimiwe kama vile tunavyoyaheshimu mataifa mengine.”

    Aidha, ametoa tahadhari juu ya juhudi zinazofanywa na baadhi ya watu kutaka kuharibu mwenendo wa taifa:

    “Ni lazima tudhibiti wachache wanaotaka kuturejesha nyuma.”

    Akitoa msimamo wa Tanzania, amesema:

    “Msimamo wetu ni haki badala ya visasi. Taifa la Tanzania limefanya hivyo kwa misingi ya siasa. Nguvu zinazotumika kutaka kuchafua Tanzania hatutakubaliana nazo.”

    Soma pia:

  3. Rais Samia aomboleza waliofariki katika maandamano

    g

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Rais wa Jamhuri ya Muungano ametoa risala za rambirambi kwa familia ambazo wapendwa wao waliangamia katika maandamano ya tangu uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 hadi tarehe 31 mwezi huo.

    Akiongea wakati wa ufunguzi rasmi wa Bunge la 13, Rais Samia Suluhu pia ameweka wazi kuwa kamati maalum imeundwa ili kuchunguza kujua kiini cha maandamano ya vurugu.

    Akigusia suala la vijana waliokamatwa kwa tuhuma za uhaini ameielekeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupitia upya mashitaka yanayowakabili wale waliokamatwa kuhusiana na vurugu hizo. Amesisitiza kwamba waendesha mashtaka wazingatie kupunguza au kufuta mashitaka kwa wale ambao huenda walijikuta katika machafuko bila kuelewa kikamilifu walichokuwa wakishiriki.

    “Ninatambua kuwa vijana wengi wamekamatwa na kushitakiwa kwa uhaini. Hawakuelewa kikamilifu kile walichokuwa wanajihusisha nacho,” alisema. “Kama mama na mlezi wa taifa hili, naielekeza mifumo ya sheria, hususan ofisi ya DPP, ionyeshe huruma.”

    Akiwasihi vijana nchini humo amewarai kutokubali kutumiwa vibaya kuiharibu nchi.

    ''Vijana wangu tuongozwe na dhamira ya maelewano, ushirikiano na tusikubali kutumiwa kuchoma taifa letu'' asema rais Samia.

    Akiongezea, ''Vijana wangu, msimkubali kukata tawi kwa mti mlioukaliwa msikubali kushinikizwa kuharibu nchi yenu’.

    Akinukuu Biblia, alikumbusha maneno ya Yesu katika Luka 23:34: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.”

    Haya yanajiri baada ya Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu pamoja na uongozi wa Chama cha Chadema kudai ni watu zaidi ya 700 wameuawa katika maandamano ya vurugu nchini humo.

    Serikali ya Tanzania mpaka sasa haijatoa idadi kamili ya waliofariki wakati wa maandamano hayo yaliyokumbwa na vurugu.

    Kauli zake zinakuja siku chache baada ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, kuzihimiza mamlaka za Tanzania kufanya uchunguzi kamili na wa wazi kuhusu taarifa za mauaji na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wakati na baada ya uchaguzi wa tarehe 29 Oktoba.

    Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi kwa asilimia 98 ya kura, matokeo ambayo upinzani umeelezea kama “dhihaka kwa demokrasia.”

    Pia unaweza kusoma:

  4. 'Ndani ya siku mia moja tutafanya mageuzi ya katiba' - Rais Samia Suluhu

    Rais wa Tanzania akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa bunge la 13

    Chanzo cha picha, Screengrab

    Maelezo ya picha, Rais wa Tanzania akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa bunge la 13

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu amewaeleza wabunge kuwa serikali yake ina mpango wa kuanza mchakato wa kufanyia mageuzi katiba ya nchi hiyo katika muhula wa pili kwa awamu ya sita kwa kuanza na Tume ya Usuluhishi na Maelewano

    ''Katika siku mia moja tutaanza mchakato wa kuwa na katiba mpya na tuko tayari kujirekebisha katika safari ya demokrasia'' asema Rais Samia Suluhu.

    Haya yanajiri miezi michache baada ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini Tanzania kupendekeza kwa Rais wa taifa hilo Samia Suluhu Hassan, mchakato wa katiba mpya uanze baada ya uchaguzi wa 2025.

    Sababu ya kwanza aliyoitaja Profesa Kisabya ya kurekebisha katiba ya Tanzania ni uwepo wa haja ya kuainisha dira mpya ya maendeleo ya 2063 itakayotoa muelekeo wa katiba mpya na suala la kukosena kwa muda wa kutosha kuanza kutumia katiba mpya ndani ya kalenda ya uchaguzi wa 2025.

    Masuala mengine waliyoibua kikosi hicho ni haja ya kutoa fursa kwa marekebisho ya sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa pamoja na haja ya kutoa fursa ya kutosha kufanyia kazi masuala ya muda wa kati ikiwa ni pamoja na kuaninisha dira mpya ya maendeleo.

    Wito wa kufanyia mageuzi ya katiba umekuwa ukitolewa kabla ya uchaguzi mkuu na kupelekea kiongozi wa chama cha Chadema Tundu Lissu kuwataka wafuasi wake kutoshiriki uchaguzi mkuu hadi pale vipengele vya sheria ya uchaguzi vibadilishwe.

    Akiongea katika hafla ya ufunguzi wa bunge la 13, Rais Samia amesema yuko tayari kufanya mazungumzo ya maridhiano.

    ''Nawaomba vyama vya kisiasa nchini tufanye mazungumzo ya arudhiano, tujue ni wapi tulikosea na namna ya kurekekebisha ili kusonga mbele, asema Rais Samia.

    Hata hivyo amesema mchakato huo sio kwa misingi ya shinikizo bali ni kwa hiari ya serikali yake.

    Haya yanajiri baada ya bunge la Ulaya kutaka serikali ya Tanzania kufanya mazungumzo ya maridhiano na kuchunguza ukiukwaji wa haki za kibinadamu.

    Soma pia:

  5. Vita vya Sudan: UN yatathmini uchunguzi maalum wa ukiukaji wa haki za binadamu Sudan

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liliandaa kikao maalum mjini al-Fashir, Sudan, Ijumaa ya Novemba 4, 2025 kujadili ombi la kutuma misheni ya uchunguzi juu ya mauaji ya kimbari baada ya jiji kushikiliwa na nguvu za kijasusi.

    Ujumbe wa kutafuta ukweli, uliojumuishwa katika rasimu ya azimio, pia ungetafuta kutambua wahusika wa ukiukaji unaodaiwa kufanywa na Vikosi vya RSF na washirika wao huko al-Fashir.

    Katika hotuba ya ufunguzi kwa wajumbe, mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa aliitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua.

    "Kumekuwa na kujifanya na kujitia hamnazo, na hatua ndogo sana zinafanywa. Ni lazima isimame dhidi ya ukatili huu - onyesho la ukatili wa wazi linalotumika kutiisha na kudhibiti idadi ya watu wote," Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu Volker Turk alisema.

    Hata hivyo, RSF imekanusha kushambulia raia au kuzuia misaada, ikisema vitendo hivyo vinasababishwa na wahalifu binafsi.

    Turk pia aliitaka hatua zichukuliwe dhidi ya watu binafsi na kampuni zinazofaidika na vita, akitoa onyo kuhusu ongezeko la vurugu katika mkoa wa Kordofan, ikiwemo mabomu, kuzuiliwa kwa njia na watu kulazimishwa kuondoka makazi yao.

    Soma pia:

  6. Wapalestina waruhusiwa kuingia Afrika Kusini

    Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka ya Afrika Kusini (BMA) imethibitisha kuwa Wapalestina 153 waliwasili nchini tarehe 13 Novemba, huku kukiwa na mzozo wa awali wa kukataliwa kuingia, kwa kuwa hawakuwa na mihuri ya kuwaruhusu kuondoka nchini mwao katika pasipoti zao.

    Haijabainika ni nani aliyekodisha ndege iliyowabeba Wapalestina kutoka Kenya hadi Afrika Kusini, lakini 130 kati yao sasa wameruhusiwa kuingia.

    Mamlaka ya Afrika Kusini ilisema kwamba abiria hao awali walikataliwa kuingia kwa sababu pasipoti zao hazikuwa na stempu za kuondoka na hawakuwa wameomba hifadhi.

    Baada ya kukaa siku nzima kwenye lami ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Johannesburg, waliruhusiwa kuingia Alhamisi jioni.

    Watasalia chini ya uangalizi wa shirika lisilo la kiserikali la kibinadamu la Afrika Kusini, Gift of the Givers, ambalo limesema litawapatia malazi.

    Abiria 23 waliosalia watasafiri kwenda maeneo mengine watakayochagua.

    Wiki mbili zilizopita, ndege nyingine iliyokuwa na Wapalestina 176 ilitua Johannesburg, huku baadhi ya abiria wakielekea nchi nyingine.

    Wapalestina wanaruhusiwa kuzuru Afrika Kusini kwa siku 90 bila visa.

    Serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikiunga mkono kwa kiasi kikubwa suala la Palestina, na mwaka 2023 iliwasilisha kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

  7. Hamas inarudisha udhibiti kimya kimya huko Gaza huku mazungumzo ya amani yakiendelea

    g

    Chanzo cha picha, AFP

    Hamas inaongeza udhibiti wake Gaza, kutoka kudhibiti bei ya kuku hadi kutoza ushuru kwenye sigara na mafuta, huku mipango ya Marekani kuhusu mustakabali wa eneo hilo ikitafakari polepole.

    Baada ya usitihaji mapigano kuanza, Hamas iliimarisha haraka udhibiti katika maeneo yaliyokuwa yameondolewa na Israel, ikidai kuwaua Wapalestina walioshirikiana na adui, wizi au uhalifu mwingine.

    Wakazi wanasema wanahisi udhibiti huu pia kwa kudhibiti bidhaa zinazoingizwa na kuangalia bei.

    Serikali ya Hamas inakanusha kutoza ushuru mpya, ikisema inalenga kudhibiti bei na kuhakikisha mpito wa utawala mpya unafanyika kwa utulivu.

    Ismail Al-Thawabta, mkuu wa ofisi ya habari ya serikali ya Hamas, alisema taarifa kuhusu kutozwa ushuru wa sigara na mafuta hazikuwa sahihi, akikanusha kuwa serikali inaongeza ushuru wowote. Mamlaka yalikuwa yakitekeleza tu kazi za kibinadamu na kiutawala za dharura huku yakifanya “majaribio makali” kudhibiti bei, alisema Thawabta wakati anazungumza na Shirika la Reuters.

    Pia alisisitiza utayari wa Hamas kuhamisha madaraka kwa utawala mpya wa wataalamu, akisema lengo ni kuepuka machafuko Gaza:

    “Lengo letu ni kuhakikisha mpito unafanyika kwa utulivu.”

    Bei za bidhaa bado ziko juu kutokana na upungufu wa bidhaa Gaza, hali inayosababisha maisha kuwa magumu.

    Hatem Abu Dalal, mmiliki wa jengo la maduka Gaza, alisema bei ziko juu kwa sababu bidhaa chache zinakuja Gaza. Wawakilishi wa serikali walikuwa wakijaribu kuleta utaratibu katika uchumi - wakienda sehemu mbali mbali, wakikagua bidhaa na kuweka bei, alisema.

    Sasa, Wapalestina kumi na wawili wanasema wanahisi udhibiti wa Hamas kwa njia nyingine pia.

    Mohammed Khalifa, akifanya manunuzi katika eneo la Nuseirat katikati ya Gaza, alisema bei zinabadilika kila wakati licha ya jitihada za kuzidhibiti. “Ni kama soko la hisa,” alisema. “Bei ni kubwa. Hakuna kipato, hali ni ngumu, maisha ni magumu, na msimu wa baridi unakuja,” alisema.

    Mpango wa Marekani ulihakikisha usitishaji wa mapigano na kuachiliwa kwa mateka wote wa mashambulizi ya Hamas Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel.

    Mpango huo unatoa wito wa kuanzishwa kwa mamlaka ya mpito, kutumwa kwa kikosi cha kimataifa cha usalama, upokonyaji silaha wa Hamas, na kuanza kwa ujenzi upya.

    Soma pia:

  8. Video za mauaji yaliotokea wiki ya uchaguzi Tanzania zilizothibitishwa na BBC

    Maelezo ya video, Video za mauaji yaliotokea wiki ya uchaguzi Tanzania zilizothibitishwa na BBC

    ONYO: Maudhui ya kutisha

    BBC yathibitisha video za mauaji yalitokea wiki ya uchaguzi nchini Tanzania.

    Tumethibitisha baadhi ya video hizo kwa kutumia picha za setalaiti na kulinganisha maeneo.

    Aidha video hizo zilizosambaa zinaonesha miili ya watu waliopigwa risasi, majeraha katika sehemu mbalimbali za miili, na vikosi vya usalama vikilenga raia wiki ya uchaguzi mkuu nchini humo.

    Juhudi za BBC kupata mamlaka kujibu tuhuma zilizomo kwenye ripoti hii hazikufua dafu.

  9. China yamwita balozi wake wa Japan juu ya matamshi ya Waziri Mkuu mpya

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wizara ya Mambo ya Nje ya China imemwita balozi wake wa Japan nyumbani kwa sababu ya matamshi yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Japan Takaichi Sanae kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mzozo juu ya Taiwan.

    Takaichi alikiambia kikao cha Bunge la Chini wiki iliyopita kwamba uvamizi wa China huko Taiwan kunaweza kuchukuliwa kama "hali ya kutishia maisha", na kusababisha Japani kuchukua hatua ya kijeshi.

    Makamu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China Sun Weidong alisema Takaichi anapaswa kubatilisha matamshi yake "vinginevyo chochote kitakachotokea Japan itawajibika," kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje huko Beijing.

    Hata hivyo, Waziri Mkuu Takaichi, baadaye alisema matamshi hayo yalitolewa kwa dhana ya hali mbaya zaidi inayoweza kutokea na haibadilishi msimamo uliopo wa serikali.

    Wizara ya China ilisema Sun iliita matamshi ya Takaichi kuwa "ya nia mbaya" na kunukuliwa kuwa kile alichosema Takaichi kinadhoofisha msingi wa kisiasa wa uhusiano wa China na Japan.

    Soma zaidi:

  10. Urusi yafanya mashambulizi makubwa Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Urusi imefanya mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na maeneo mengine ya nchi.

    Mapema siku ya Ijumaa, ilithibitishwa kwa mtu mmoja ameuawa huko Kyiv na moto mkubwa umetokea ambao umeharibu jengo la makazi katika wilaya nyingi za mji mkuu, Meya Vitali Klitschko alisema.

    Takriban watu 26 walijeruhiwa huku wafanyakazi wa dharura wakijibu mashambulizi mengi, kulingana na maafisa.

    Klitschko alisema huenda watu wengine wawili waliuawa katika shambulio hilo, lakini bado haijathibitishwa kwani waokoaji hawakuweza kutoa miili kutoka kwenye vifusi.

    Wakati huo huo, shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa vikosi vya ulinzi wa anga vya Urusi vimedungua au kunasa ndege za Ukraine usiku kucha, Wizara ya Ulinzi ilisema siku ya Ijumaa.

    Wizara hiyo ilisema imeangusha ndege zisizo na rubani katika eneo la kusini mwa Urusi la Krasnodar, ambapo maafisa walisema awali bohari ya mafuta na bandari ilikuwa ikilengwa.

    Gavana wa mkoa wa Saratov nchini Urusi alisema kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yameharibu miundo mbinu ya raia, huku mkuu wa mkoa wa Volgograd akisema kuwa ulinzi wa anga umezuia shambulio la usiku kucha la ndege zisizo na rubani kwenye miundombinu ya nishati.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Saa ya dhahabu iliopatikana katika meli ya Titanic kupigwa mnada

    .

    Chanzo cha picha, BNPS

    Saa ya mfukoni ya dhahabuiliyopatikana kwenye mwili wa mmoja wa abiria tajiri zaidi katika meli ya Titanic iliyozama inatarajiwa kuuzwa mnadani kwa karibu dola milioni 1.3.

    Isidor Strauss na mkewe Ida walikuwa miongoni mwa zaidi ya watu 1,500 waliokufa wakati meli ya Titanic ilipozama baada ya kugonga jiwe la barafu mnamo Aprili 14, 1912.

    Bw. Strauss alikuwa mfanyabiashara na mwanasiasa wa Marekani aliyezaliwa Bavaria na mmiliki mwenza wa duka kuu la Macy huko New York.

    Mwili wake uligunduliwa katika Bahari ya Atlantiki siku chache baada ya meli ya Titanic kuzama, na miongoni mwa mali zake ni saa ya mfukoni ya dhahabu ya karati 18, ambayo itapigwa mnada Novemba 22.

    Andrew Aldridge, mkurugenzi wa kampuni ya mnada huko Wiltshire, Uingereza, aliiambia BBC: "Kupitia saa hii, tunasimulia hadithi ya Isidor. Ni kumbukumbu nzuri sana... Walikuwa wanandoa mashuhuri sana wa New York. Kila mtu anawajua kuanzia kwa filamu ya Titanic iliyoandikwa na kuelekezwa na James Cameron, katika tukio ambapo wanandoa wazee wanakumbatiana wakati meli inazama. Walikuwa ni Isidor na Ida."

    Usiku wa kuzama kwa meli ya Titanic, inaaminika kuwa mke wake aliyejitolea alikataa kuingia kwenye mashua ya kuokoa maisha kwa sababu hakutaka kumwacha mumewe, akisema afadhali afe karibu naye. Mwili wa Ida haukupatikana.

    Saa hii ya mfukoni ilisimama saa 02:20, wakati meli ya Titanic ilipotea chini ya mawimbi.

    Soma zaidi:

  12. Wanajeshi wa Libya wasambaza mafuta kwa kikosi cha RSF nchini Sudan - The Sentry

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kikundi cha uratibu chenye makao yake Marekani kinasema kwamba wanajeshi wanaomuunga mkono kamanda wa Libya, Khalifa Haftar, wamekuwa wakisambaza mafuta kwa Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan kwa niaba ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

    Kundi hilo, lijulikanalo kama The Sentry, linasema Haftar amekuwa msambazaji muhimu wa mafuta na silaha kwa RSF wakati wote wa vita.

    Kamanda huyo wa Libya ameshtumiwa mara si moja kwa kusambaza silaha na mafuta kwa kikosi cha RSF kwa niaba ya falme za kiarabu, madai ambayo amekanusha.

    Falme za kiarabu pia imekanusha kuhusika na vita vinavyoendelea Sudan.

    Ripoti ya The Sentry inasema kuwa, hatua ya Haftar kuwapa mafuta kikosi cha RSF, kumewasaidia kudhibiti eneo la Darfur ambayo sasa ni ngome yao kuu.

    Eneo zima la Darfur magharibi mwa Sudan, linapakana na Libya pamoja na Chad, na liko chini ya udhibiti wa RSF ambao waliuteka mji wa mwisho wa El-Fasher ambao ulikuwa unadhibitiwa na jeshi la Sudan.

    Ripoti ya Umoja wa mataifa, imeishtumu falme za kiarabu kwa kuipa RSF silaha na ndege za kivita zisizo na rubani.

    Jeshi la Sudan, pia limeshtumu Falme za Kiarabu kwa kuwatuma mamluki kutoka Colombia kupitia mataifa jirani kupigana vita vinavyoendelea nchini humo.

    Mshauri wa Rais wa Falme za Kiarabu (UAE), Anwar Gargash, alilaani ukatili unaoendelea mjini El-Fasher na kupinga vikali kile alichokiita “habari za uongo” kuhusu Falme za Kiarabu kuhusika na vita vinavyoendelea Sudan.

    Libya imegawanyika kati ya serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli, inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah, na utawala wa Haftar ulioko mashariki mwa nchi hiyo.

    Taifa hilo la kaskazini mwa Afrika, limegawanyika tangu mapinduzi yaliyotokea mwaka wa 2011, yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo Muammar Gaddafi.

    Soma zaidi:

  13. Kiongozi wa zamani Bangladesh ameiambia BBC kuwa hana hatia ya uhalifu dhidi ya binadamu

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri mkuu wa zamani wa Bangladesh Sheikh Hasina amekanusha kutenda uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa msako mkali dhidi ya maasi ya mwaka jana yaliyomuondoa madarakani, siku chache kabla ya mahakama maalum inayomkabili kutoa uamuzi.

    Hasina anatuhumiwa kuwa nyuma ya mamia ya mauaji wakati wa maandamano makubwa ya kupinga utawala wake wa kiimla - madai ambayo anayakanusha.

    Katika mahojiano yake ya kwanza na BBC tangu atoroke nchini tarehe 5 Agosti 2024, alisema kesi yake bila kuwepo mahakamani ilikuwa "ujinga" uliopangwa na "mahakama isiyo na haki" inayodhibitiwa na wapinzani wa kisiasa.

    Waendesha mashtaka wanapendekeza hukumu ya kifo dhidi ya Hasina iwapo atapatikana na hatia siku ya Jumatatu.

    Hasina alidai kesi hiyo ilikusudiwa kutoa "hukumu iliyopangwa mapema".

    Usalama umeimarishwa ndani na karibu na mahakama hiyo katika mji mkuu Dhaka kabla ya uamuzi wa Jumatatu.

    Uamuzi wa kesi hiyo itaadhimisha wakati muhimu kwa nchi na pia kwa jamaa za waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga serikali yaliyoongozwa na wanafunzi ambayo yalimuondoa madarakani Hasina.

    Wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema takriban watu 1,400 waliuawa wakati Hasina na serikali yake walipotumia ghasia za kimfumo na mbaya dhidi ya waandamanaji katika azma iliyoshindwa ya kusalia madaraka.

    Waziri mkuu huyo wa zamani amekataa kurejea kutoka nyumbani kutoka India kuhudhuria kesi hiyo.

    Soma zaidi:

  14. Israel yapokea maiti huku Hamas ikisema ni ya mateka

    .

    Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

    Israel imethibitisha kuwa imepokea jeneza ambalo Hamas inasema lina mwili wa mateka mwingine.

    Magari ya Shirika la Msalaba Mwekundu yalichukua mwili huo saa chache baada ya Hamas kutoa taarifa ya pamoja na Palestina Islamic Jihad ikisema imeipata katika eneo la Khan Younis kusini mwa Gaza.

    Ofisi ya waziri mkuu wa Israel ilisema mwili huo utahamishiwa Israel, ambapo utapokelewa katika sherehe za kijeshi kabla ya kufanyiwa mchakato wa utambulisho.

    Kuthibitishwa kuwa ni maiti ya mateka kutamaanisha kuwa mateka 25 kati ya 28 waliofariki wamekabidhiwa kwa Israel chini ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya sasa ya kusitisha mapigano ambayo ni sehemu ya mpango wa Marekani wa kumaliza vita vya Gaza.

    Pia unaweza kusoma:

  15. BBC yamwomba Trump msamaha lakini imekataa kulipa fidia

    .

    Chanzo cha picha, Reuters / AFP via Getty Images

    BBC imemuomba msamaha Rais wa Marekani Donald Trump kwa kipindi cha Panorama ambacho kiliunganisha sehemu za hotuba yake ya tarehe 6 Januari 2021, lakini ikakataa madai yake ya kulipwa fidia.

    Shirika hilo lilisema hariri hiyo imetoa "hisia potofu kwamba Rais Trump alikuwa ametoa mwito wa moja kwa moja wa vitendo vya vurugu" na kusema kwamba haitaonyesha mpango wa kipindi hicho wa mwaka 2024 tena.

    Mawakili wa Trump wametishia kuishtaki BBC kwa fidia ya $1bn (£759m) isipokuwa shirika hilo liondoe makala hiyo, liombe msamaha na kumfidia.

    Kutokea kwa kashfa hiyo kulisababisha mkurugenzi mkuu wa BBC Tim Davie na mkuu wa habari Deborah Turness kujiuzulu siku ya Jumapili.

    "Tunakubali kwamba hariri yetu bila kukusudia ilisababisha hisia kwamba tulikuwa tukionyesha sehemu moja ya hotuba inayoendelea, badala ya nukuu kutoka kwa vidokezo tofauti kwenye hotuba, na kwamba hii ilitoa maoni potofu kwamba Rais Trump alikuwa ametoa mwito wa moja kwa moja wa vitendo vya vurugu," ilisema.

    Mawakili wa BBC wameandikia timu ya wanasheria wa Rais Trump kujibu barua iliyopokelewa siku ya Jumapili, msemaji wa BBC alisema.

    Soma zaidi:

  16. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 14/11/2025