Saa za mwisho za Sheikh Hasina kama dikteta aliyechukiwa

w

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wapinzani wa Sheikh Hasina wakishangilia mbele ya picha yake iliyoharibiwa mjini Dhaka
Muda wa kusoma: Dakika 6

Sheikh Hasina alipoitisha kikao cha usalama na mgogoro ili kumaliza machafuko yanayoendelea nchini Bangladesh siku ya Jumapili, alionekana kutokukubali kuwa muda wake umeisha kama waziri mkuu.

Ndani ya saa chache, alifurushwa kwa nguvu za umma- kwa kweli, ni wachache wangeweza kutabiri kasi ya kuondoka kwake.

Alishauriwa na familia yake kutoroka na sio maafisa wakuu wa usalama, BBC iliambiwa na mwanawe.

Bi Hasina alichukua uamuzi wakati muafaka, kisha umati wa watu uliingia katika makazi yake ndani ya saa chache baada ya kutoroka.

Maelezo ya video, Tazama: Waandamanaji wa Bangladesh wakivamia kasri la Waziri mkuu
Unaweza pia kusoma:

Kikao cha Kamati ya Usalama ya Kitaifa - kilichoitishwa Jumapili asubuhi - kiliwakutanisha Waziri Mkuu pamoja na wakuu watatu wa kijeshi wa nchi hiyo, maafisa wakuu wa usalama na polisi.

Shinikizo dhidi ya Waziri Mkuu lilikuwa likiongezeka kwa wiki kadhaa huku maandamano ya kuipinga serikali yakiendelea kote nchini.

Mamia wameuawa katika ghasia mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Bangladesh tangu vita vyake vya kupata uhuru mwaka 1971.

Siku ya Jumapili pekee, takribani watu 90 walipoteza maisha, wengi wao wakiwa waandamanaji waliopigwa risasi na vikosi vya usalama - lakini pia kuna idadi kubwa ya polisi waliouawa na umati wa watu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

BBC Bangla imeelezwa na maafisa kwamba Sheikh Hasina alitaka kuwepo mambo mawili. Maandalizi ya kuondoka nchini na kusalia madarakani kwa nguvu hadi dakika ya mwisho.

Viongozi wa kijeshi hawakukubali. Siku ya Jumapili, waandamanaji walichangamana na askari waliokuwa mitaani na maafisa wengine wa jeshi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Baada ya kuona hali hiyo, maafisa wakuu wa jeshi waligundua kuwa mambo yako nje ya udhibiti wao.

Wakuu wa jeshi mmoja baada ya mwingine katika mkutano huo walimwambia Waziri Wkuu kwamba wanajeshi hawawezi kuwafyatulia risasi raia - lakini wanaweza kutoa msaada wa kiusalama kwa polisi, duru ziliiambia BBC.

Pia ilibainika baadaye kuwa wakuu wa polisi, walilalamika kuwa walikuwa wakiishiwa na risasi.

Hata hivyo Sheikh Hasina, hakutaka kusikiliza na hakuna mtu aliyekuwa tayari kupingana naye ana kwa ana.

Baada ya mkutano, mwandishi wake wa habari aliwasilisha ujumbe wake wa dharau. Aliwaita waandamanaji hao "magaidi" na kuwataka watu kuwapinga wale aliowataja kuwa "wachomaji moto."

Vikosi vya usalama vilihofia kuwa baada ya muda mfupi vinaweza kukabiliwa na hali inayokaribia kuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Ghasia ziliongezeka siku ya Jumapili. Hapa muandamanaji anakimbia karibu na kituo cha polisi kilicho chomwa moto na waandamanaji mjini Dhaka

Picha za ghasia za Jumapili zilikuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku idadi ya waliofariki ikiongezeka mara kwa mara.

Picha za vijana waliokuwa na majeraha ya risasi, waliopigwa risasi na polisi na wanachama wa tawi la vijana la chama tawala cha Awami League, zilikuwa zikizua hasira zaidi.

Wakati mapigano hayo yalipodhihirika kuwa ni makali, viongozi wa wanafunzi waliwasilisha wito wa maandamano makubwa ya siku moja huko Dhaka, na kuishangaza serikali.

Taarifa za kijasusi zilionyesha kuwa madai ya wanafunzi yalikuwa yakiungwa mkono zaidi na zaidi na maelfu ya watu walikuwa wakipanga kuingia kwenye mji mkuu siku iliyofuata.

Taarifa hizo ziliashiria kuwa iwapo vikosi vya usalama vitajaribu kuwazuia waandamanaji, kungekuwa na umwagaji mwingine wa damu. Kwa hiyo mkuu wa jeshi Waker-Uz-Zaman aliamua kuzungumza na waziri mkuu tena.

Vyanzo vya kuaminika vilisema wakuu watatu wa jeshi walikutana naye Jumapili jioni na wakamweleza kwa upole kwamba hali ilikuwa inaendelea kuwa tete zaidi na zaidi, na maelfu ya watu wanatarajiwa kuingia Dhaka Jumatatu asubuhi na wasingeweza kumhakikishia usalama wa makazi yake.

Sheikh Hasina hakukubali ushauri wao, lakini waandishi wa habari huko Dhaka walisema walikuwa wakihisi kuwa serikali inabadilika. Kufikia Jumapili usiku, polisi hawakuwepo katika maeneo mengi na vizuizi vingi vya usalama havikuwa na mtu.

g

Siku ya Jumatatu asubuhi, umati mkubwa wa watu ulikuwa umeanza safari ya kuelekea Dhaka. Jenerali Zaman alikuwa kwenye makazi ya Bi Hasina kwa mara nyingine tena akimwelezea uzito wa hali hiyo. Watu walikuwa wakivunja amri ya kutotoka nje na vurugu zilikuwa tayari zimeanza.

Polisi walikuwa wakiondolewa sehemu nyingi za Dhaka na Jenerali Zaman alimwambia kuwa hawawezi kuzuia umati wa watu kufika Gono Bhaban, makao rasmi ya Waziri Mkuu katika mji mkuu, kwa muda mrefu zaidi.

Katika hatua hii, wakuu wa kijeshi waliamua kuwaita wanafamilia kuingilia kati.

Polisi na wakuu wa kijeshi walifanya mazungumzo na dada yake Sheikh Hasina, Rehana Siddiq, kuona kama angeweza kumshawishi dada yake mkubwa kuondoka.

"Viongozi hao walifanya mazungumzo na Sheikh Rehana kwenye chumba kingine, wakamtaka amweleze Sheikh Hasina. Kisha Sheikh Rehana akazungumza na dada yake mkubwa, lakini Sheikh Hasina alidhamiria kushikilia madaraka," Gazeti la kila siku Prothom Alo la lugha ya Kibengali lilisema.

Kisha mwana wa kiume wa Bi Hasina, Sajeeb na binti yake Saima, ambao wote wanaishi nje ya nchi, walizungumza naye kwa simu na kumsisitiza kwamba aondoke. Wakati wa mazungumzo haya ya kifamilia, mkuu wa jeshi, ambaye ni jamaa na Bi Hasina kwa ndoa, alikuwepo muda wote.

"Mama yangu hakutaka kuondoka nchini hata kidogo. Ilibidi tumshawishi," Sajeeb Wazed Joy aliambia BBC siku ya Jumanne, na kuongeza kuwa mama yake alianza kufikiria kujiuzulu Jumamosi jioni.

“Sisi wanafamilia tulimsihi, tukamsihi, hili ni kundi la watu, wako nje kwa vurugu na watakuuwa na tunahitaji kukupeleka kwenye usalama. Muda wa waandamanaji kufika katika kasri lake ndio uliokuwa umebaki tu. Hatimaye, waliondoka tu bila maandalizi yoyote.

"Nilimpigia simu jana huko Delhi. Yuko imara lakini amevunjika moyo sana. Amekatishwa tamaa sana na watu wa Bangladesh."

w

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Watu wakitembea karibu na magari yaliyoharibiwa katika kituo cha polisi huko Dhaka siku ya Jumanne

Jumatatu asubuhi, vyanzo vya habari vilisema, Sheikh Hasina aliwasiliana na maafisa wa serikali mjini Delhi, India kuomba hifadhi.

Ushauri kutoka India, nchi mshirika mkubwa katika maisha yake yote ya kisiasa, ulikuwa ni kwamba aondoke.

Siku moja kabla, inaelezwa kuwa Marekani iliwaambia maafisa wa Wizara ya mambo ya nje ya India kwamba wakati wa Bi Hasina umekwisha. Hana chaguo.

Lakini mara tu alipokubali kwa kusita kusaini hati za kuachia wadhifa wake, bado kulikuwa na swali la jinsi ya kumtoa nje ya nchi kwa usalama.

Afisa mmoja mkuu wa jeshi ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia BBC Bangla kwamba ni Kikosi Maalumu cha Usalama, Kikosi cha Walinzi wa Rais na baadhi ya maafisa wakuu wa jeshi katika makao makuu ya jeshi waliojua muda ambao Sheikh Hasina alitia saini barua ya kujiuzulu na kupanda helikopta ya kijeshi ambayo ingeweza mpeleke nje ya makazi yake.

Kila kitu kilifanyika kwa usiri mkubwa.

Mnamo saa nne unusu kwa saa za eneo hilo (05:00GMT), mamlaka ilizima intaneti ili kuzuia habari kuhusu mienendo ya Sheikh Hasina kuenea kwenye mitandao ya kijamii.

Ilifunguliwa tu baada ya yeye kutoroka.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya juu vya jeshi, mipango iliwekwa ili kumfikisha Sheikh Hasina uwanja wa ndege akiwa salama.

Kulikuwa na wasiwasi kwamba msafara wake unaweza kushambuliwa, kwa hivyo njia nzima iliwekwa ulinzi na mahali pa kuondokea pakalindwa.

Lakini ikaonekana kuwa haikuwa salama kumpitisha barabarani, kwa hiyo helikopta ilitumiwa kumuondoa kwenye makazi yake.

Hadi wakati wa kuondoka, Sheikh Hasina alisitasita kuingia, mtoto wake alisema.

"Alitaka shangazi yangu ndio aondoke," mwanawe alisema. "Mama yangu hakutaka kupanda helikopta. Nilikuwa kwenye simu, nikimshawishi mama yangu, nikimwambia shangazi, lazima waondoke wote wawili.

Mara baada ya kupanda, walisafirishwa kutoka Gono Bhaban hadi kwenye ndege ya Bangladeshi Air Force C-130 Hercules ambayo ilikuwa imetayarishwa.

Sajeeb Wazed Joy anasema anaamini walikwenda Agartala, mji mkuu wa jimbo la mashariki mwa India la Tripura na walisafirishwa kwa ndege kutoka huko hadi Delhi.

India tayari ilikuwa imefahamishwa na kukubali kumpokea, maafisa walisema.

Duru nyingine zinasema alichukuliwa kwa helikopta hadi uwanja wa ndege huko Dhaka, kisha akasafirishwa kwa ndege hadi Delhi.

Karibu saa sabu na nusu mchana kwa saa za huko, Bi Hasina, dada yake na mbunge mkuu wa chama cha Awami, Salman Fazlur Rahman, walihamishwa kutoka kwenye helikopta na kuwekwa kwenye ndege iliyowapeleka Delhi, maafisa walisema.

Video kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha masanduku manne au matano yakisubiri kupakiwa. Mali nyingine alizoziacha zilikuwa zikisukumwa na umati wa watu waliovamia makazi yake, akiwa angani.

Saa kadhaa baadaye, ndege hiyo ilitua Delhi. Huko Dhaka, mtandao ulikuwa umerejea na kote Bangladesh, sherehe zilikuwa zikianza kuashiria mwisho wa utawala wa miaka 15 wa Sheikh Hasina.

Mwanamke ambaye aliyetazamwa kama mwanademokrasia lakini baadaye akalaaniwa na watu wengi kama dhalimu, alikimbia kama mkimbizi huku mitandao ikiwa imezimwa.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Rashid Abdallah