Meya wa Instambul anakabiliwa na makosa anayoweza kuhukumiwa zaidi ya miaka 2,000 jela

Chanzo cha picha, Reuters
Mwendesha mashtaka katika jiji kubwa la Uturuki anamshutumu meya maarufu Ekrem Imamoglu kwa makosa 142 ya ufisadi ambayo yanaamuru vifungo vya jela kati ya miaka 828 hadi 2,352.
Imamoglu, anayechukuliwa kuwa mpinzani mkuu wa kisiasa wa Rais Recep Tayyip Erdogan, amewekwa mahabusu kabla ya kesi yake tangu Machi kwa tuhuma za rushwa.
Meya wa Istanbul na chama chake cha upinzani cha Republican People's Party (CHP) wanakanusha makosa yoyote na kumshutumu rais na washirika wake kwa kufungua masako makubwa ili kukabiliana na kupungua kwa umaarufu wa Erdogan.
Hata hivyo, mwendesha mashtaka mkuu wa jiji hilo amesema sio Imamoglu pekee bali na watu wengine 401, kwa madai ya kuendesha mtandao wa ufisadi huku meya akiwa "mwanzilishi na kiongozi".
Baada ya uchunguzi wa miezi minane, mwendesha mashtaka Akin Gürlek amesema washukiwa hao, ambao 105 walikuwa kizuizini, wameunda shirika kubwa la uhalifu ambalo lilikuwa likijihusisha na kuchukua na kupokea hongo pamoja na utapeli wa pesa.
Imamoglu, mgombea wa chama cha CHP katika uchaguzi wa urais mwaka 2028, ametajwa katika makosa 12 ya hongo, saba ya utakatishaji fedha kutokana na mapato na makosa mengine saba ya ulaghai dhidi ya taasisi na mashirika ya umma.
Shirika la habari la Anadolu lilikadiria mashtaka hayo yanabeba kifungo cha miaka 2,430 jela.
Kuzuiliwa kwa meya mwezi Machi kulisababisha maandamano makubwa, mamia ya watu kukamatwa na msako mkali wa polisi. Tangu wakati huo, amekuwa akishikiliwa katika gereza la Marmara nje kidogo ya Istanbul.
Mbali na kesi hiyo ya rushwa, waendesha mashitaka wamemtuhumu kwa msururu wa makosa mengine yakiwemo ya ujasusi na kughushi stashahada yake ya chuo kikuu, stashahada ambayo imefutwa na bila diploma ya chuo kikuu hawezi kugombea urais 2028.
Mamlaka ya Uturuki inakanusha madai ya meya kwamba mahakama inatumika kama chombo cha kisiasa,
Imamoglu, 54, alichaguliwa kuwa meya kwa mara ya kwanza mwaka 2019 na alichaguliwa tena Aprili 2024, akimshinda mgombeaji mkuu wa Chama cha AK kwa karibu kura milioni.
Tayari amekata rufaa dhidi ya kifungo cha Julai cha mwaka mmoja na miezi minane kwa kumtusi na kumtishia mwendesha mashtaka wa Istanbul. Pia anakata rufaa dhidi ya hukumu ya awali ya kifungo jela kwa kuwakosoa maafisa wa uchaguzi.



















