Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wakwama huku Israel ikifunga vivuko vya kimataifa

Chanzo cha picha, Reuters
Israel imefunga kivuko pekee kati ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel na nchi jirani ya Jordan, na kuwazuia zaidi ya Wapalestina milioni mbili kuingia.
Mamlaka ya viwanja vya ndege vya Israel, ambayo inasimamia kivuko cha Allenby Bridge, ilisema kuwa itafungwa kwa muda usiojulikana kuanzia Jumatano asubuhi "kwa maelekezo ya uongozi wa kisiasa". Haikutoa sababu.
Kufungwa huko kumekwamisha Wapalestina wengi katika Ukingo wa Magharibi, ambao hawawezi kwenda kwa safari zilizopangwa nje ya nchi.
Wale ambao wako nje ya nchi wameshindwa kusafiri nyumbani.
Hatua hii inakuja siku chache baada ya wanajeshi wawili wa Israel kuuawa kwa kupigwa risasi karibu na kivuko na mtu aliyekuwa na bunduki kutoka Jordan, ambaye aliuawa katika eneo la tukio.
Kivuko hicho, pia kinajulikana kama Daraja la King Hussein, kiko karibu nusu kati ya Amman na Jerusalem na ndio kivuko pekee rasmi kati ya Ukingo wa Magharibi na Jordan.
Pia ni sehemu ya pekee ya kuingia Ukingo wa Magharibi ambayo haipiti Israeli. Wapalestina wengi katika Ukingo wa Magharibi hawaruhusiwi kusafiri kupitia viwanja vya ndege vya Israel au vivuko vingine vya mpaka wa Israel, kumaanisha daraja hilo ni muunganisho muhimu kwa ulimwengu wa nje.
Mwanasiasa mashuhuri wa Palestina Mustafa Barghouti aliiambia BBC kuwa ni "hatua hatari" ambayo ilimaanisha "kuwafunga" watu katika Ukingo wa Magharibi na "kuwanyima njia pekee ya kutoka". "Unazungumza hapa kuhusu kuvuruga uhusiano kati ya mamia ya maelfu ya familia ambazo kwa kawaida huunganishwa kupitia Jordan," alisema.
Unaweza kusoma;











