Dairo Antonio Úsuga David alias Otoniel: Mfahamu mlanguzi mkuu wa dawa za kulevya aliyekamatwa

Otoniel aliongoza kundi kubwa la walanguzi wa mihadarati nchini Colombia

Chanzo cha picha, COLOMBIAN POLICE/HANDOUT VIA REUTERS

Maelezo ya picha, Otoniel aliongoza kundi kubwa la walanguzi wa mihadarati nchini Colombia

Kichwa chake Dairo Antonio Úsuga David alias Otoniel kilikuwa kimewekewa zawadi: Marekani ilikuwa imetanganza zawadi ya dola milioni 5 kwa habari ambazo zingechangia kukamatwa kwake huku serikali ya Colombia nayo ilikuwa imetangaza zawadi ya dola 800,000.

Licha ya haya, oparesheni za kumkamata mlanguzi mkubwa zaidi wa madawa ya kulevya nchini Colombia, mkuu wa kundi kubwa zaidi la walanguzi wa madawa ya kulevya la Gulf Clan, ilifikia kikomo Jumamosi ya tarehe 23 mwezi huu baada ya karibu miaka kumi ya kutafutwa kwake.

Otoniel mwenye umri wa miaka 50 alikamatwa katika manispaa ya Necocli, kaskazini mashariki mwa Colombia kwenye operesheni ya pamoja ambapo zaidi ya wanajeshi 300 kutoka jeshi la nchini kavu, jeshi la wanahewa na polisi walishirikiana wakitumia zaidi ya helikopta 20.

"Ni pigo kubwa zaidi ambalo limewapata walanguzi wa dawa za kulevya katika karne hii nchini mwetu. Pigo hilo linaweza kulinganishwa na kuanguka kwake Pablo Escopar miaka ya 1990." alisema Rais wa Colmbia Iván Duque, wakati akisherehekea habari hizo.

Mwaka 2015 mamlaka za Colombia zilianzisha oparesheni ya kumkamata Otoniel ambapo wanajeshi 1200 kutoka kikosi bora zaidi nchini humo walishirikia, zaidi ya mara mbili ya wanajeshi 500 waliomsaka Escobar.

Kuna zaidi ya mashtaka 100 yatakayofunguliwa dhidi ya Otoniel

Chanzo cha picha, Reuters

"Otoniel alikuwa mlanguzi wa dawa za kulevya aliyegopewa sana duniani, muuaji wa polisi, wanajeshi, viongozi wa jamii, muajiri wa watoto," alisema Rais Duque.

Kuhusu genge la Gulf Clan, waziri wa ulinzi nchini Colombia Diego Molano alisema Jumatano, kuwa genge hilo limekuwa tisho miaka ya hivi karibuni kutokana na kiwango cha madawa za kulevya yanayosafirishwa kwenda Marekani na Ulaya, katika shughuli zinazosimamiwa na genge hilo.

Historia ya ghasia

Lakini Je Otoniel ni mtu wa aina gani?

Otoniel alizaliwa huko Antioquia mwanzoni mwa miaka ya 1970 na akiwa na umri wa miaka 16 alijiunga la vuguvugu lililosambaratika la Popular Liberation Army (EPL) pamoja na ndugu yake.

Baadaye pamoja na ndugu yake Juan de Dios Úsuga David, alias "Giovanni", alijiunga na kundi la FARC na baadaye katika kile kilichoonekana kama kubadili maamuzi kwa njia kubwa wakajiunga na United Self-Defense Forces of Colombia.

Mwaka 2005 kundi hilo liliweka silaha nchini lakini ndugu hao wakajiunga na mlanguzi wa madawa ya kulevya Daniel Rendón Herrera, alias "Don Mario."

Wakati alikamatwa mwaka 2009, Otoniel na Giovani waliachwa kuongoza kundi hilo.

Otoniel akawa kiongozi mkuu wakati ndugu yake aliuawa Januari mosi mwaka 2012.

Kutoka kwa familia hadi kundi la kimataifa

Likitajwa kuwa kubwa, genge la Clan del Golfo lilikuwa awali linafahamika kama Urabeños, jina lilitokana na eneo la Urabá linaloendesha oparesheni zake, licha ya genge hilo kuwa na mizizi kote nchini na hata zaidi. ( wanachama wa kundi hilo wamekamatwa Brazil, Argentina, Peru, Uhispania na Honduras.

Kukamatwa kwa Otoniel kulihitaji ushirikiano wa karibu wa vikosi vya usalama nchini humo

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kukamatwa kwa Otoniel kulihitaji ushirikiano wa karibu wa vikosi vya usalama nchini humo

Katika kitovu chake limekuwa genge la familia la the Úsuga ambalo Otoniel na Giovanii walikuwa na pia binamu zao kadhaa na watu wengine wa karibu.

Kwa mfano Francisco José Morelo Peñata, alias "El Negro Sarley" aliyeuawa na polisi Aprili mwaka 2013 alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa dada zake Otoniel, kwa mujibu wa polisi na alikuwa wa pili kwenye genge baada ya kuuawa kwa Giovanni.

Mtu aliyesimamia fedha za kundi alikuwa rafiki yake Otoniel, Blanca Senobia Madrid Benjumea, alias "La Flaca", ambaye alikamatwa mwaka 2015.

Na aliyetajwa na polisi kama mtu aliye na mahusiano na magenge ya Mexico ni yule anayesimamia usafirishaji wa dawa za kulevya kwenda Amerika ya kati alikuwa mpwa wa Otoniel na mtoto wa kambo wa El Negro Sarley, Harlison Úsuga, alias "Pedro Arias", ambaye pia alikamatwa mwaka 2015.

Serikali ya taifa hilo ililinganisha kukamtwa kwa Otoniel na kule kwa Pablo Escobar

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Serikali ya taifa hilo ililinganisha kukamtwa kwa Otoniel na kule kwa Pablo Escobar

Agosti iliyopita, serikali ya Colombia iliamuru kusafirishwa Marekani kwa Alexander Montoya Úsuga alias 'El Flaco', binamu yake Otoniel ambaye alikamatwa mwaka 2012 nchini Hunduras.

Idara ya sheria nchini Marekai ilkuwa imetaja genge la Gulf Clan kuwa moja ya makundi makubwa zaidi la kimataifa yanayotishia nchi hiyo.

Kukwepa kukamatwa

Uhusiano wa ndani wa kifamilia, na pia kuishi eneo nchini Colimbia ambalo wanalielewa vizuri ni baadhi ya sababu zilizofanya iwe vigumu mamlaka kumkamata Otoniel.

Baada ya kifo cha Giovanni, kundi hilo lilifanya mgomo ambao uliacha shughuli zikiwa zimekwama kwa siku kadhaa.

Lakini Otoniel pia alikuwa na mbinu kadhaa za kuwakwepa waliokuwa wanamwinda.

Kwa mfano alitumia mbwa waliokuwa wamepewa mafunzo kumjulisha wakati mtu mgeni alikuwa anakaribia ili apate muda wa kutosha kukimbia.

Katika moja ya harakati zake za kutoroka aliacha nyumba moja ya wanyama hao.

Polisi walimchukua na kumpa jina Oto na kumfunza na kumtumia katika operesheni ya mwaka 2015 kuwasadia kumtafuta aliyekuwa mkuu wake.

Kulingana na vyombo vya habari nchini Colombia, Otoniel hakutumia vifaa vya kisasa vya mawasiliano kama simu ili kuzuia kufuatiliwa. Kwa hivyo aliwasiliana na wanachama wa kundi lake kwa kutumia ujumbe uliosambazwa kupitia vifaa kama rekoda na kutumia binadamu kusambaza vifaa hivyo.

Hofu ya kukamatwa pia ilisababisha mara kwa mara abadilishe maeneo alikuwa analala usiku msituni mara kwa mara akilala kwenye vibanda.

Vibanda hivyo vilikuwa na televisheni kubwa, vinywaji ghali na manukato ambayo mamlaka zilipata wakati wakimsaka.

Kitu kingine walichogundua ni uwepo wa mito maalum na ghali, iliyosadia kuondoa maumivu ya viungo.

Sasa wakati huu ameshakamatwa, haijulikani ikiwa atashawishi mamlaka zimruhusu alalie mito kama hiyo akiwa gerezani.