Uharamia Somalia: BBC yazungumza na majambazi wa bahari kuu

Chanzo cha picha, Hassan Lali/BBC
Wavuvi wawili wa Kisomali waliovalia mitandio mikubwa juu ya vichwa vyao ili kuficha nyuso zao walitazama huku na huko huku wakiingia chumba cha mkutano wa siri ili kunieleza ni kwa nini hivi karibuni wameamua kuwa maharamia wanaotumia bunduki - wakitafuta fidia ya dola milioni.
"Uko huru kurekodi - tunakubali," mmoja ananiambia huku wakiketi chini kwa woga kwa mahojiano ambayo yamechukua miezi kadhaa hadi kufanyika katika mji mdogo wa pwani wa Eyl.
Tabia hii ni tofauti na maharamia ambao walikuwa wakizunguka karibu na bandari hii ya zamani ya kupendeza iliyo katikati ya milima kame kwenye pwani ya Bahari ya Hindi nchini Somalia.
Daima imekuwa ikifahamika kama ya kimkakati, sio tu kwa sababu ya eneo lake lakini pia kwa sababu ina chanzo cha maji safi - na kipindi uharamia unaongezeka mapema hadi katikati ya miaka ya 2000 maharamia waliifanya kuwa kambi yao.
Ilijulikana kama "Harunta Burcadda" - Mji Mkuu wa Uharamia. Kuanzia hapa, walilenga meli za kontena zinazosafirisha bidhaa kote ulimwenguni na hata meli za mafuta, na kulazimisha kampuni za meli kubadilisha njia zao.
Mamlaka za jimbo hazikuwa na nguvu - na jeshi la polisi la eneo hilo liliogopa sana kuingia mjini.
Maharamia walitumia meli zilizotekwa nyara kutia nanga ufukweni na biashara katika mji na jimbo hilo zilinufaika kutokana na malipo ya fidia. Kati ya 2005 na 2012 Benki ya Dunia inakadiria vikundi vya maharamia vilipata kati ya $339m (£267m) na $413m.
Lakini mambo yalibadilika kwa maharamia hao wakati majeshi ya majini ya kimataifa yalipoanza kushika doria kwenye bahari karibu na Somalia na siku hizi Jeshi la Polisi la Wanamaji la Puntland lina kambi huko Eyl.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Watu wengi katika mji huo walifurahia jambo hili kwani maharamia hao walileta mfumuko mkubwa wa bei, dawa za kulevya, pombe na mwenendo mmbaya ambao wazee wa Kiislamu wa eneo hilo hawakuridhishwa nao.
Lakini chuki ya muda mrefu iliyohisiwa kuelekea meli za kigeni, hasa meli za uvuvi, haijawahi kutoweka katika mji uliojaa wavuvi ambao unategemea bahari kuendesha maisha yake.Hadi leo wanashutumu boti hizi za uvuvi kwa kuwadhulumu maisha yao – mara zote kwa kutumia nguvu.
Meli zilikuja na kuchukua vifaa na mali zetu zote," Farah, mmoja wa wavuvi waliogeuka kuwa maharamia ananiambi ahuku akijiziba kwa kutumia skafu yake ya bluu.
Jina lake na la rafiki yake Diiriye, ambaye amevikwa hijabu nyeupe, yamebadilishwa -kama moja ya masharti ya mkutano wetu.
Yeye na wengine wachache walikuwa wamewekeza takriban $10,000 katika mradi wa uvuvi kwa kutumia boti, injini ya nje na nyavu.
Lakini Farah anasema mwaka jana wafanyakazi wa meli moja ya kigeni walikuja na kuiba nyavu, pamoja na samaki wake, na kisha kufyatulia risasi injini - na kuiharibu.
Wawili hao wanatoa mfano mwingine: baadhi ya jamaa zao walikuwa wametoka nje kwenda kuangalia nyavu zao asubuhi moja na hawakurudi tena - kwa kawaida mvuvi hutoka alfajiri na kurudi kabla ya jua la mchana kuwa kali.
Siku tatu baadaye walipatikana, wakielea kuelekea ufukweni.
"Kulikuwa na majeraha ya risasi katika miili yao," Diiriye anasema.
"Hawakuwa na bunduki; walikuwa wamekwenda baharini na nyavu zao ili kujipatia riziki."

Chanzo cha picha, Hassan Lali/BBC
Farah anaendelea: "Tunafanya kazi na kuishi kando ya bahari. Bahari ni shughuli kwetu.
"Wakati mtu anakutisha na kukuibia, ni lazima kujitetea. Walisababisha mapigano. Kama hawangechukua mali yetu, tusingeenda kwenye uharamia."
Wanaume hawa - wenye umri wa miaka 30 – hawakuwa peke yao katika kufanya uamuzi mwaka uliopita wa kugeukia uharamia.
Kwa mujibu wa kikosi cha wanamaji cha Umoja wa Ulaya Operesheni Atalanta, ambayo inashika doria karibu, kulikuwa na mashambulizi 26 ya maharamia kati ya 2013 na 2019 - na kisha hakuna hata moja kutoka 2020 hadi 2022.
Lakini yalianza tena 2023, na mashambulizi sita na yaliyoongezeka hadi 22 mwaka huu, takwimu za hadi tarehe 5 Desemba zinaonyesha.
Mapigano mengi,hayaishii katika utekaji wenye mafanikio - lakini inapotokea,huwa na faida.
Maharamia wanasema walipokea fidia ya $5m ili kuachilia meli yenye bendera ya Bangladesh MV Abdullah, iliyotekwa Machi 2024.
Mmiliki wa meli hiyo hajathibitisha hili, lakini alisema iliachiliwa baada ya mazungumzo.
Vyanzo vya habari katika jimbo la Puntland, ambako Eyl yuko, viliiambia BBC kwamba wanakadiria takriban magenge 10, kila moja likiwa na takriban wanachama 12, yanaendesha shughuli zake katika eneo hilo.
Wanaenda baharini kwa siku 15 hadi 30 kwa wakati mmoja, wakipakia boti zao ndogo za mwendo kasi na AK-47, mabomu ya kurushwa kwa roketi (RPGs), vyakula na mafuta.
Farah na Diiriye wanasema lengo lao ni kuteka nyara meli ya ukubwa wa kati ndani ya Bahari ya Hindi na kisha kuirejesha kwenye meli yao mama, kwa kutumia mfumo wake wa ufuatiliaji wa GPS hutafuta meli kubwa zaidi kutimiza azma hiyo.
"Unaweza kushambulia meli kwa kutumia boti ndogo za mwendo kasi," anasema Farah.
Kirusha roketi chao cha Bazooka pia ni sehemu muhimu ya mkakati wao.
"Tunatumia RPG kusimamisha meli. Meli isiposimama, tunapiga risasi juu yake. Hatuui. Lengo ni kupata kitu, si kuua. [Lengo ni] kuwatisha," Anasema Diiriye.
Silaha zote hizi hazina bei nafuu - kwa hivyo magenge yanatafuta ufadhili kutoka kwa wawekezaji wanaopenda. Wavuvi wasioridhishwa hufanya harambee mara nyingi ikihusisha wafanyabiashara tofauti kutoka miji ya Garowe na Bosaso.
Mtu anaweza kufadhili boti, mwingine silaha na aina ya tatu kama mafuta. Wafanyabiashara hawa wakati mwingine huwekeza katika vikundi kadhaa kwa matumaini kwamba mmoja wao atapata bahati wakati chombo kinapokamatwa ili waweze kupata malipo yao ya fidia.
Na ni rahisi kupata bunduki nchini Somalia - hata huko Eyl unaweza kuchukua AK-47 kwa takriban dola 1,200, urithi wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miongo miwili na miaka kadhaa ya kushuhudia uvunjaji sheria.
Farah na Diiriye wanasema hawakuhusika katika ukuaji wa uharamia na hawajachukua ushauri wowote kutoka kwa maharamia waliostaafu, ambao baadhi yao pia walianza kama wavuvi wasioridhika.
Wengi wa maharamia hawa wazee wameondoka eneo hilo - mara nyingi wamekwenda nje ya nchi au wameungama na kuacha.
Katika kisa kimoja maarufu cha maharamia wa zamani - Abdirahman Bakeyle - alitoa mali yake. Mnamo 2020, alitoa nyumba na hoteli alizonunua huko Garowe kwa mashirika ya kutoa misaada ya Kiislamu na sasa ni muhubiri anayesafiri kutoka mji hadi mji huko Puntland akiwahimiza watu kuishi maisha ya uadilifu.
Adado, mji ulioko katikati mwa Somalia ambako maharamia waliwahi kuwekeza, ulipata jina la utani "Mji wa Bluu" kwa sababu majumba yao mapya yaliyojengwa mara nyingi yalikuwa na paa za chuma zilizopakwa rangi ya buluu.
Sehemu nzuri ya nyumba hizi sasa hazina kitu - au zinapatikana kwa kukodisha kwa chini ya $100 kwa mwezi.
Huko Eyl, wazee wa mji huo wanasema urithi mkuu wa uharamia ni kuenea kwa pombe, ambayo mara nyingi huingizwa kutoka Ethiopia, na dawa za kulevya kama vile opioids - kwa wasiwasi kwamba baadhi ya vijana tayari wanatafuna majani yanayojulikana kama leaf khat, na kuchangia vijana wengi kuwa waraibu.
Wanaume wanaokusanyika nje kwa wauza chai mchana kucheza bao na kujadili masuala mbalimbali wanasema hawaungi mkono uharamia - ingawa wanaelewa uadui dhidi ya meli za kigeni.
Tukio la hivi karibuni la wavuvi watatu waliouawa kwa kupigwa risasi linaonekana kugusa wengi.
Ali Mursal Muse, ambaye amekuwa akivua kamba na papa karibu na Eyl kwa takriban miaka 40 ili kusaidia mke wake na watoto 12, anaamini kuwa wanaweza kuwa wamekosea maharamia - kama alivyokuwa akifanya miaka kadhaa iliyopita.
"Tuliondoka hapa na mashua nyingine ya wavuvi na kwenda baharini. Wakati huo huo maharamia walijaribu kuteka meli. Ndege ilikuja. Boti yangu ilifika ufukweni; mashua nyingine ya wavuvi ilishambuliwa," anakumbuka.

Chanzo cha picha, Hassan Lali/BBC
Mjane mwenye umri wa miaka 40 Hawa Mohamed Zubery anaamini kwamba mumewe alipatwa na hali kama hiyo miaka 14 iliyopita alipotoweka.
Hii ilikuwa wakati uharamia ulikuwa tatizo kuu na alikuwa ametoka tu kujifungua mtoto wa kiume, ambaye walitaka kumtahiri.
"Mume wangu alikuwa akifikiria kwamba ikiwa angekamata papa basi tungeweza kulipa ili mtoto atahiriwe," anaambia BBC, akionyesha wazi kuwa bado ana huzuni kuhusu kifo chake. Anasema anatatizika kulipa karo ya shule kwa ajili ya watoto wake kutokana na maisha yake ya kuuza sambusa.
Bw Muse anasema suala kuu kwake siku hizi ni tabia isiyofaa ya meli za wavuvi kutoka nchi kama Iran na Yemen ambazo mara nyingi huiba vifaa vyake.
Anaamini kuwa wamepewa leseni bandia za uvuvi na wafadhili wenye nguvu Somalia ambao pia huwapa watu wenye silaha kuwalinda. Aliwashutumu kwa kupora samaki wao na kukusanyika kwenye maeneo yao ya uvuvi.
"Wana eneo wanalofanyia kazi na hata wanakuja ufukweni. Tunapoenda kuomba vifaa vyetu virudi wanatupiga risasi.Hivi karibuni waliumiza baadhi ya watu. Walimpiga risasi kijana mmoja na kumjeruhi mkono na mguu."
Mvuvi huyo anasema amelalamika kwa mamlaka za mitaa mara kadhaa, lakini hakuna kinachofanyika.
Waziri wa Habari wa Puntland Caydid Dirir anakiri kuwepo kwa baadhi ya meli haramu na anasema baadhi ya meli za kigeni zinaweza kupewa leseni na "kuzitumia vibaya".
"Uvuvi haramu upo katika bahari zote, na uharamia unaweza kutokea popote pale. Maendeleo yanafanywa hatua kwa hatua," anaiambia BBC.
Uvuvi haramu umekuwa suala tata nchini Somalia kwa miaka mingi.
Meli nyingi za uvuvi zinafanya kazi bila leseni au kwa leseni zinazotolewa na mashirika yasiyo na mamlaka ya kufanya hivyo, kulingana na Mpango wa Kimataifa wa Kupambana na Uhalifu wa Kimataifa.
Inanukuu ushahidi, ikijumuisha data ya ufuatiliaji wa satelaiti, kuonyesha kwamba meli nyingi zinatoka China, Iran, Yemen na kusini-mashariki mwa Asia. Ripoti kutoka kwa ubalozi wa Marekani mjini Mogadishu inasema Somalia inapoteza $300m kila mwaka kutokana na uharamia.
Aliyekuwa kiongozi wa Operesheni Atalanta Manuel Alvargonzález Méndez anasema vikosi vyake vinalenga tu meli za maharamia na sasa pia wanapaswa kulinda meli kutoka kwa waasi wa Houthi wa Yemen.
Lakini anasisitiza kuwa eneo hilo ni salama zaidi na Wasomali sasa wanaweza "kutupa nyavu zao za uvuvi bila woga" - kama vile Jeshi la Wanamaji la Puntland, ambalo linafanya kazi kwa karibu na ujumbe wa wanamaji wa Umoja wa ulaya EU.

Chanzo cha picha, Hassan Lali/BBC
Kamanda wake Farhan Awil Hashi ana imani kwamba haitarejea katika "siku mbaya za zamani" za uharamia.
Anaamini suluhu la kudumu ni "kutengeneza ajira".
"Vijana lazima wapate kazi, kila mara. Ikiwa mtu huyo ana shughuli nyingi za kufanya jambo fulani, hatafikiria kuhusu kuelekea baharini na kuteka meli," anaiambia BBC.
Farah na Diiriye wanajenga hoja sawa - wanasema kwa sababu uvuvi haulipi tena, kuteka meli kwa ajili ya fidia ndiyo njia pekee wanayoweza kusaidia watoto wao.
Wanajua uharamia si sahihi - na Diiriye anakubali kuwa anaogopa sana kumwambia mama yake mwenyewe.
"Kama angejua, angekatishwa tamaa sana. Kwa hakika, angearifu mamlaka."
Imetafsiriwa na Martha Saranga












