'Wanajeshi wa Israel waliiteka nyumba yangu, wakaitumia kama hoteli, kisha wakaiteketeza'

Akiwa ameshikilia pete ya maua ya silikoni na taa ya Ramadhani iliyoungua, Nasser Fartawi anapekua mabaki ya duka lake maarufu kwa vifaa vya karamu huko Tulkarm, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Kuta za orofa tatu za juu, vyumba vya kifahari vya familia yake, vimefunikwa kwa graffiti; kuna hata michoro ya kukera ya sehemu za siri za kiume sebuleni na chumba cha bintiye.
Samani za bei ghali ndani ya nyumba zimevunjwa au kutupwa nje ya dirisha, mapambo ya kifahari yameng'olewa ukutani, kurasa zote za Quran zimechanika, na harufu kali ya chakula kilichooza imeenea hewani.
Nasser ananiambia, "Walikuja na kuharibu kila kitu nilicho nacho. Kwao, kila kitu hakina thamani na kinaweza kuharibiwa, kwa sababu ninaishi katika mji huu; kwa sababu mimi ni Mpalestina."
Mnamo Machi 3, jeshi la Israeli lilikwenda nyumbani kwa Fartawi, na kuipa familia hiyo saa moja na nusu kuondoka. Jeshi la Israel lililiteka jengo hilo wakati huo huo katika operesheni kubwa karibu na kambi ya wakimbizi ya Tulkarm.
Nasser anasema kwa kutoamini: "Waligeuza nyumba hiyo kuwa kituo cha kijeshi, wakakaa humo kama hoteli kwa muda wa miezi mitatu na nusu, kisha wakaiteketeza."

Anasema Juni 11, alishuhudia kwa mbali ghala na duka lake ambalo watu walileta magari yao kupamba kwa ajili ya harusi vimeteketea kwa moto.
"Ilikuwa vigumu sana kwangu kuona biashara yangu ikiteketea," asema Nasser. "Kila kitu nilichokifanya kwa bidii kwa zaidi ya miaka 30 kilitoweka." Jirani yake ilikuwa hadi hivi majuzi eneo la kijeshi lililozuiliwa, na aliruhusiwa tu kurejea mwanzoni mwa mwezi huu.
Walipoulizwa kuhusu hali ya nyumba hiyo, jeshi la Israel liliambia BBC kwamba "halikuwa na habari kuhusu uchomaji wowote uliofanywa vikosi vyake" na kwamba malalamiko "yamesajiliwa na yanachunguzwa".
Taarifa ya jeshi la Israel iliendelea kusema: "Uharibifu wa mali ya raia unaofanywa na askari ni kinyume na maadili ya jeshi la Israel, na kesi yoyote ambayo iko nje ya amri na kanuni za jeshi hili itachunguzwa na kufuatwa na makamanda." Taarifa hiyo haikutoa maoni yoyote kuhusu graffiti hiyo ya kukera.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Eneo hilo limevutia umakini wa kimataifa tangu mashambulizi mabaya ya Hamas dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7, 2023, ambayo yalichochea vita vya umwagaji damu vya Gaza.
Lakini wakati huo huo, hali ya wasiwasi katika Ukingo wa Magharibi pia imeongezeka kwa kasi, na mashambulizi ya walowezi wa Israel na operesheni za kijeshi ambazo Israel inasema zinawalenga wanamgambo wa Kipalestina.
Umoja wa Mataifa unasema katika kipindi hiki, zaidi ya Wapalestina 900 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na jeshi la Israel na walowezi, wakati huo huo Waisraeli zaidi ya 60 wamepoteza maisha katika mashambulizi yanayohusishwa na Wapalestina au katika mapigano ya silaha katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ndani ya Israel.
Wakati wa operesheni kubwa za Israel, nyumba za Wapalestina mara nyingi hubadilishwa kuwa kambi za muda za kijeshi na vituo vya mahojiano, huku jeshi la Israel likihalalisha hatua hizi kama hitaji la usalama.
Jeshi la Israel lilitangaza: "Ili kutambua na kuharibu miundombinu ya kigaidi katika mizizi yao, wakati mwingine inalazimika kutumia nyumba katika eneo sawa na vituo vya kupeleka na operesheni kwa muda fulani, kulingana na hali ya uendeshaji na mahitaji."

Kutoka kwenye roshani ya ghorofa ya juu, nyumba ya Nasser inaangalia kambi ya wakimbizi ya Tulkarm, ambayo sasa inafanana na jiji lisilo na watu, na baadhi ya wakazi 10,600 bado wameyahama makazi yao.
Matingatinga ya Israel yamechimba barabara mpya katika kambi hiyo, na kuigawanya katika sehemu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limeripoti kuwa zaidi ya amri 1,400 za kubomoa zimetolewa katika eneo lote la Ukingo wa Magharibi tangu operesheni ya Israel ya "Iron Wall" ilipoanza kuanzia Januari hadi Julai.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) sasa linawasaidia wakimbizi ambao wameishi katika nyumba za kibinafsi ndani na karibu na Tulkarm, na limeanzisha kituo cha afya cha muda na shule kadhaa kwa ajili yao, na limeanza elimu ya mtandaoni kwa wanafunzi.
Waziri wa Ulinzi wa Israel ametangaza kuwa jeshi litasalia katika kambi hizi tatu za wakimbizi hadi angalau mwisho wa mwaka.

Ingawa Nasser Fartawi amerejea nyumbani kwake, hajui ni jinsi gani ataweza kuijenga upya. Anakadiria jumla ya uharibifu wake karibu $700,000. Anaweza kushtaki mamlaka ya Israeli, lakini ushahidi uliopita unaonyesha kwamba kupokea fidia yoyote kuna uwezekano mkubwa.
Mamlaka ya Palestina, ambayo inasimamia sehemu ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kutegemea misaada kutoka nje, hapo awali ililipa sehemu ya gharama ya kurekebisha uharibifu uliosababishwa na uvamizi wa jeshi la Israel; lakini sasa inakabiliwa na ufinyu wa bajeti kiasi kwamba inashindwa hata kulipa mishahara kamili ya wafanyakazi wa serikali.
Nasser, ambaye alipoteza duka lake na bidhaa zake kuharibiwa, sasa hana chanzo cha mapato na anahofia kuwa hataweza tena kumsaidia mtoto wake wa kiume na wa kike, wanaosomea udaktari nchini Misri. Ametoa wito kwa mashirika ya kimataifa kwa usaidizi.
"Mimi ni mtu wa kawaida na mfanyabiashara," anasema. "Ninapenda amani. Sijawahi kuwa na bunduki nyumbani kwangu na sijawahi kuwa na matatizo na jeshi la Israel. Nataka tu kuishi kwa amani, lakini hawataki amani."
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












