Umoja wa Mataifa waitaka Tanzania kuchunguza mauaji ya siku ya uchaguzi

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za binadamu ameitaka Tanzania kuchunguza madai haya mazito ya ukiukaji wa haki za binadamu, kikamilifu na kwa uwazi, na kuwawajibisha wale waliohusika.

Muhtasari

Moja kwa moja

Asha Juma & Rashid Abdallah

  1. Meya wa Instambul anakabiliwa na makosa anayoweza kuhukumiwa zaidi ya miaka 2,000 jela

    gf

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Ekrem Imamoglu amekuwa kizuizini kabla ya kesi katika jela nje kidogo ya Istanbul tangu Machi.

    Mwendesha mashtaka katika jiji kubwa la Uturuki anamshutumu meya maarufu Ekrem Imamoglu kwa makosa 142 ya ufisadi ambayo yanaamuru vifungo vya jela kati ya miaka 828 hadi 2,352.

    Imamoglu, anayechukuliwa kuwa mpinzani mkuu wa kisiasa wa Rais Recep Tayyip Erdogan, amewekwa mahabusu kabla ya kesi yake tangu Machi kwa tuhuma za rushwa.

    Meya wa Istanbul na chama chake cha upinzani cha Republican People's Party (CHP) wanakanusha makosa yoyote na kumshutumu rais na washirika wake kwa kufungua masako makubwa ili kukabiliana na kupungua kwa umaarufu wa Erdogan.

    Hata hivyo, mwendesha mashtaka mkuu wa jiji hilo amesema sio Imamoglu pekee bali na watu wengine 401, kwa madai ya kuendesha mtandao wa ufisadi huku meya akiwa "mwanzilishi na kiongozi".

    Baada ya uchunguzi wa miezi minane, mwendesha mashtaka Akin Gürlek amesema washukiwa hao, ambao 105 walikuwa kizuizini, wameunda shirika kubwa la uhalifu ambalo lilikuwa likijihusisha na kuchukua na kupokea hongo pamoja na utapeli wa pesa.

    Imamoglu, mgombea wa chama cha CHP katika uchaguzi wa urais mwaka 2028, ametajwa katika makosa 12 ya hongo, saba ya utakatishaji fedha kutokana na mapato na makosa mengine saba ya ulaghai dhidi ya taasisi na mashirika ya umma.

    Shirika la habari la Anadolu lilikadiria mashtaka hayo yanabeba kifungo cha miaka 2,430 jela.

    Kuzuiliwa kwa meya mwezi Machi kulisababisha maandamano makubwa, mamia ya watu kukamatwa na msako mkali wa polisi. Tangu wakati huo, amekuwa akishikiliwa katika gereza la Marmara nje kidogo ya Istanbul.

    Mbali na kesi hiyo ya rushwa, waendesha mashitaka wamemtuhumu kwa msururu wa makosa mengine yakiwemo ya ujasusi na kughushi stashahada yake ya chuo kikuu, stashahada ambayo imefutwa na bila diploma ya chuo kikuu hawezi kugombea urais 2028.

    Mamlaka ya Uturuki inakanusha madai ya meya kwamba mahakama inatumika kama chombo cha kisiasa,

    Imamoglu, 54, alichaguliwa kuwa meya kwa mara ya kwanza mwaka 2019 na alichaguliwa tena Aprili 2024, akimshinda mgombeaji mkuu wa Chama cha AK kwa karibu kura milioni.

    Tayari amekata rufaa dhidi ya kifungo cha Julai cha mwaka mmoja na miezi minane kwa kumtusi na kumtishia mwendesha mashtaka wa Istanbul. Pia anakata rufaa dhidi ya hukumu ya awali ya kifungo jela kwa kuwakosoa maafisa wa uchaguzi.

  2. Muswada unaopendekeza hukumu ya kifo wasomwa katika Bunge la Israel

    b

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Waziri wa Usalama wa Israel mwenye siasa kali za mrengo wa kulia Itamar Ben-Gvir alitoa peremende baada ya mswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza

    Bunge la Israel limesikiliza usomwaji wa kwanza wa mswada unaopendekeza hukumu ya kifo kwa wanaopatikana na hatia ya ugaidi – muswada ambao una maana kwamba kuna uwezekano wa kutumika hukumu ya kifo dhidi ya Wapalestina wanaopatikana na hatia ya mashambulizi dhidi ya Waisraeli.

    Waziri wa Usalama kutoka chama cha mrengo mkali wa kulia Itamar Ben-Gvir - ambaye chama chake cha Jewish Power kimeleta mswada huo - alisherehekea Jumatatu kwa kutoa peremende baada ya mswada huo kusomwa katika bunge la viti 120, na kupitishwa kwa hatua ya awali kwa kura 39 dhidi ya 16.

    "Baada ya sheria kupitishwa - magaidi wataachiliwa tu kuzimu," alisema.

    Muswada huo lazima upigiwe kura mara mbili zaidi kabla ya kuwa sheria.

    Katika kikao hicho, Knesset pia iliidhinisha kusomwa kwa mara ya kwanza kwa mswada mwingine wenye utata unaoruhusu serikali ya Israel kufunga chombo cha habari cha kigeni bila idhini ya mahakama. Kura hizo zilikuwa 50 za ndio na 41 zilipinga.

    Sheria hiyo inalenga kubadilisha amri ya kuifunga kwa muda kwa Al Jazeera inayomilikiwa na Qatar tangu Mei 2024, na kuwa sheria ya kuifungia kwa kudumu. Lakini sheria hiyo imepingwa na washauri wa kisheria wa serikali.

    Ingawa hukumu ya kifo ipo kwa idadi ndogo ya makosa lakini imetumika mara mbili tu tangu 1948 wakati serikali ilipoundwa. Mara ya mwisho ilikuwa wakati mhalifu wa vita vya Nazi, Adolf Eichmann, alinyongwa 1962.

    Muswada huo unapendekeza: ‘Gaidi atakayepatikana na hatia ya mauaji yaliyochochewa na ubaguzi wa rangi au chuki dhidi ya umma, na chini ya hali ambapo kitendo hicho kilifanywa kwa nia ya kudhuru Taifa la Israel na uwepo wa taifa la Kiyahudi atahukumiwa adhabu ya kifo - ya lazima."

    Kifungu kuhusu kuidhuru Israel kinaweka uwezekano kwamba Wapalestina wanaopatikana na hatia ya mashambulizi, watahukumiwa kifo lakini sio Wayahudi wa Israeli.

    Wizara ya mambo ya nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina - ambayo inasimamia baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu - iliita sheria inayopendekezwa kuwa "aina mpya ya itikadi kali za Israel na uhalifu dhidi ya watu wa Palestina".

    Ben-Gvir ametaka kwa muda mrefu muswada wa hukumu ya kifo uletwe kupigiwa kura na Knesset, lakini hatua kama hiyo ilipingwa awali na viongozi wa kisiasa na usalama wa Israel ambao walidai inaweza kutatiza juhudi za kuwakomboa mateka wa Israel waliokuwa wanashikiliwa na Hamas huko Gaza.

    Huo sio wasiwasi tena tangu kurejea kwao baada ya kuanza kwa usitishaji mapigano Gaza mwezi uliopita.

  3. Umoja wa Mataifa waitaka Tanzania kuchunguza mauaji ya siku ya uchaguzi

    fv

    Chanzo cha picha, AFP

    Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametaka uchunguzi juu ya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29 nchini Tanzania, huku ripoti zikiibuka kwamba miili inachukuliwa na vikosi vya usalama na kupelekwa katika maeneo ambayo hayajajulikana.

    Taarifa zilizopatikana na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kutoka vyanzo tofauti nchini Tanzania zinaonyesha mamia ya waandamanaji na watu wengine waliuawa na idadi isiyojulikana kujeruhiwa au kushikiliwa. Ofisi imeshindwa kuthibitisha kwa uhuru takwimu za majeruhi kutokana na hali tete ya usalama na kuzimwa kwa intaneti wakati wa kupiga kura.

    "Taarifa za familia zinazosaka wapendwa wao kila mahali kwa kutembelea kituo kimoja cha polisi baada ya kingine na hospitali moja baada ya nyingine ni za kutisha. Naomba sana serikali ya Tanzania itoe taarifa kuhusu hatma na mahali walipo wote waliopotea, na kukabidhi miili ya waliouawa kwa wapendwa wao ili wazikwe kwa heshima," amesema Türk.

    "Pia kuna ripoti kwamba vikosi vya usalama vimeonekana vikiondoa miili kutoka mitaani na hospitalini na kuipeleka kwenye maeneo ambayo hayajajulikana katika jaribio la kuficha ushahidi."

    Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za binadamu ameitaka Tanzania kuchunguza madai haya mazito ya ukiukaji wa haki za binadamu, kikamilifu na kwa uwazi, na kuwawajibisha wale waliohusika.

    Ametoa wito kwa mara nyingine kuachiwa huru bila masharti vigogo wote wa upinzani waliokamatwa kabla ya uchaguzi mkuu akiwemo kiongozi wa chama cha upinzani cha Chadema Tundu Lissu na watu wengine wote waliowekwa kizuizini tangu siku ya uchaguzi.

    Inaarifiwa kuwa zaidi ya watu 150 wametiwa mbaroni tangu siku ya kupiga kura - wakiwemo watoto walioshtakiwa kwa uhaini.

    "Ni muhimu wale wote waliokamatwa au kuzuiliwa kwa makosa ya jinai wawasilishwe mara moja mbele ya a mahakama. Na wale wote wanaozuiliwa lazima wapewe haki kamili chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu," amesema Türk.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Lamine Yamal ameondolewa kwenye kikosi cha Uhispania

    p;

    Chanzo cha picha, getty

    Maelezo ya picha, Lamine Yamal alikuwa sehemu ya timu ya Uhispania iliyoshinda Euro 2024

    Nyota wa Barcelona Lamine Yamal ameondolewa kwenye kikosi cha Uhispania kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Georgia na Uturuki chini ya kocha Luis de la Fuente.

    Yamal alipaswa kuucheza mechi hizo mbili baada ya kuichezea Barcelona katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Celta Vigo Jumapili lakini sasa ameondolewa kwenye nafasi hiyo.

    Meneja wa Barcelona Hansi Flick aliikosoa Uhispania kwa kumchezesha Lamine Yamal katika mechi ya kufuzu dhidi ya Bulgaria na Uturuki mwezi Septemba.

    Alikosa mechi nne za Barcelona kutokana na jeraha la paja baada ya mapumziko hayo ya kimataifa na hakuwepo kwenye mechi za Uhispania dhidi ya Georgia na Bulgaria mnamo Oktoba.

    Bado Barcelona wameweka wazi kwamba Yamal anatakiwa kupona kile kinachojulikana kuwa jeraha gumu, na sasa atapumzika vizuri wakati wa mapumziko ya kimataifa.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Vitu vya kale vya Ufalme wa Asante wa Ghana vyarudishwa kutoka Uingereza na Afrika Kusini

    rf

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Baadhi ya vitu vilivyoporwa kutoka ufalme wa Asante vilirejeshwa kwa mfalme mwaka jana

    Mfalme wa Asante wa Ghana amekaribisha kurejeshwa kwa vitu 130 vya dhahabu na shaba kutoka Uingereza na Afrika Kusini ambavyo baadhi viliporwa wakati wa ukoloni na vingine kununuliwa kwenye soko la wazi.

    Vitu hivyo vinajumuisha mavazi ya kifalme, ngoma na mapambo ya sherehe, kutoka miaka ya 1870.

    Vipande 25 kati ya hivyo vilitolewa na mwanahistoria wa sanaa wa Uingereza Hermione Waterfield na vingine na kampuni ya uchimbaji madini ya Afrika Kusini AngloGold Ashanti.

    Wakikabidhi vipande hivyo katika hafla iliyofanyika katika Kasri ya Manhyia, katika mji wa Kumasi, maofisa kutoka kampuni ya AngloGold Ashanti ya Afirka Kusini wamesema kitendo hicho kimefanywa kama heshima na maridhiano ya kitamaduni.

    Kumekuwa na mvutano katika eneo la kati la Ashanti huko Ghana kati ya AngloGold Ashanti na wakaazi, ambao wameshutumu kampuni hiyo kwa kunyonya rasilimali za madini bila kufanya mengi kuendeleza eneo hilo au kuunda kazi.

    Mfalme wa Asante Otumfuo Osei Tutu wa Pili aliishukuru AngloGold Ashanti kwa kurudisha kwa hiari vitu vya kale vilivyonunuliwa katika masoko ya wazi.

    Wanajeshi wa Uingereza walihusika katika mfululizo wa migogoro mwishoni mwa Karne ya 19 katika kile kilichoitwa vita vya Anglo-Asante. Ikulu ya mfalme, au Asantehene, iliporwa mara mbili.

    Wito wa nchi za Kiafrika wa kurejeshwa kwa vitu vilivyoporwa umepokewa kwa mafanikio katika miaka ya hivi karibuni.

    Mnamo 2022, Ujerumani ilikuwa nchi ya kwanza kurudisha shaba za Benin kwa Nigeria katika juhudi za kukabiliana na "historia yake ya ukoloni" .

  6. Serikali ya Uingereza kukomesha majaribio ya kisayansi kupitia wanyama

    e

    Chanzo cha picha, get

    Maelezo ya picha, Uchunguzi wa dawa kupitia sungura unaweza kumalizika mwishoni mwa mwaka huu

    Serikali ya Uingereza imeelezea kwa mara ya kwanza jinsi inavyolenga kutimiza ahadi yake ya kuondoa tafiti na majaribio kupitia wanyama.

    Mipango hiyo ni kupunguza matumizi ya mbwa na sokwe katika vipimo vya dawa za binadamu kwa angalau 35% ifikapo 2030.

    Chama cha Labour kilisema katika manifesto yake kwamba "kitashirikiana na wanasayansi, viwanda, na mashirika ya kiraia kukomesha tafiti kupitia wanyama.''

    Waziri wa Sayansi Lord Vallance aliambia BBC, ipo siku matumizi ya wanyama katika sayansi yatakomeshwa kabisa lakini anakubali kwamba itachukua muda.

    Majaribio kupitia wanyama nchini Uingereza yalifikia milioni 4.14 mwaka 2015 kutokana na ongezeko kubwa la tafiti za urekebishaji jeni – hasa kwenye panya na samaki.

    Kufikia 2020, idadi hiyo ilishuka kwa kasi hadi milioni 2.88 huku mbinu mbadala zikibuniwa.

    Lord Vallance aliiambia BBC anataka kubadilisha majaribio ya wanyama ili kuwepo majaribio kupitia tishu za wanyama, AI, na kompyuta.

    Kulingana na mipango ya serikali, ifikapo mwisho mwa 2025, wanasayansi wataacha kutumia wanyama kwa majaribio makubwa na kubadili njia mpya katika maabara zinazotumia seli za binadamu.

  7. Rais wa zamani wa Ufaransa Sarkozy aachiliwa kutoka gerezani baada ya wiki tatu

    j

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Nicolas Sarkozy aliwasili nyumbani kwake magharibi mwa Paris saa moja baada ya mahakama kuruhusu kuachiliwa kwake.

    Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameachiliwa kutoka jela, wiki tatu baada ya kifungo cha miaka mitano jela kwa kushiriki katika njama ya uhalifu.

    Atakuwa chini ya uangalizi mkali wa mahakama na kuzuiwa kuondoka Ufaransa kabla ya kesi yake ya rufaa itakayosikilizwa mwaka ujao.

    Tarehe 21 Oktoba, rais huyo wa zamani wa siasa za mrengo wa kulia mwenye umri wa miaka 70, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kula njama ya kufadhili kampeni yake ya uchaguzi wa 2007 kwa pesa kutoka rais wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi.

    Timu yake ya wanasheria iliwasilisha ombi la kutaka rufaa ili aachiliwe.

    Akiandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuachiliwa, Sarkozy alisema "nguvu zake ni katika lengo moja la kuthibitisha kutokuwa na hatia. Ukweli utashinda... Mwisho wa hadithi bado haujaandikwa."

    Gari la Sarkozy lilionekana likitoka kwenye gereza la La Santé mjini Paris, chini ya saa moja na nusu baada ya mahakama kukubali kuachiliwa kwake. Muda mfupi baadaye, alionekana akiwasili nyumbani kwake magharibi mwa Paris.

    Christophe Ingrain, mmoja wa mawakili wa Sarkozy, alipongeza kuachiliwa kwa mteja wake kama "hatua muhimu" na kusema sasa watakuwa wakijiandaa kwa kesi ya rufaa inayotarajiwa Machi.

    Sharti moja la kuachiliwa kwa Sarkozy ni kwamba asiwasiliane na mashahidi katika kile kinachojulikana kama "kesi ya Libya" au wafanyakazi wowote wa wizara ya haki.

    Wakati wa kifungo chake, alitembelewa na Waziri wa Sheria Gérald Darmanin. Ziara hiyo iliwafanya mawakili 30 wa Ufaransa kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya Darmanin, wakiangazia kile walichosema ni mgongano wa kimaslahi kwani Darmanin alikuwa mfanyakazi mwenza wa zamani na rafiki wa Sarkozy.

    Akizungumza na mahakama mjini Paris kupitia video Jumatatu asubuhi, Sarkozy alielezea hajawahi kuwa na "wazo" la kumwomba Gaddafi pesa na akasema "hatakubali kamwe kitu ambacho sijafanya."

    Sarkozy pia alitoa pongezi kwa wafanyakazi wa magereza kwa kuonyesha ubinadamu.

    Mke wa Sarkozy, mwimbaji na mwanamitindo Carla Bruni-Sarkozy, na wana wawili wa rais huyo wa zamani walikuwepo katika chumba cha mahakama kumuunga mkono.

    Sarkozy ndiye kiongozi wa kwanza wa zamani wa Ufaransa kuwekwa rumande tangu kiongozi wa wanazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Philippe Pétain kufungwa kwa uhaini mwaka 1945.

    Tangu aingie gerezani, Sarkozy amekuwa akishikiliwa katika chumba cha peke yake, chenye choo, bafu, dawati, jiko dogo la umeme na TV ndogo - ambayo alilipa ada ya kila mwezi ya €14 (£ 12) - na friji ndogo.

    Pia alikuwa na haki ya kupokea taarifa kutoka nje na kutembelewa na familia, pamoja na mawasiliano ya maandishi na simu - lakini alikuwa katika kifungo cha upweke. Aliruhusiwa kutoka nje ya chumba saa moja tu kwa siku kwa ajili ya mazoezi, ambayo alifanya peke yake.

    Walinzi wawili waliwekwa karibu na chumba chake, jambo ambalo waziri wa mambo ya ndani Laurent Nuñez alisema lilitokana na hadhi ya Sarkozy.

    Sarkozy alikuwa rais kutoka 2007 hadi 2012. Tangu aondoke madarakani, amekuwa akikabiliwa kesi za uhalifu na kwa miezi kadhaa ilimbidi kuvaa kifaa cha kielektroniki kwenye kifundo cha mguu baada ya kutiwa hatiani Desemba mwaka jana kwa kujaribu kumuhonga hakimu ili apate taarifa za siri kuhusu kesi tofauti.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Sita wafariki baada ya kimbunga cha pili ndani ya wiki moja kuikumba Ufilipino

    efd

    Chanzo cha picha, BBC/Lulu Luo

    Maelezo ya picha, Zaidi ya watu milioni 1.4 walihamishwa kabla ya kimbunga Fung-wong kuwasili Ufilipino.

    Takriban watu sita wamefariki dunia baada ya kimbunga kikali kuikumba Ufilipino, siku chache tu baada ya kimbunga kilichosababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

    Kimbunga kikubwa cha Fung-wong kilileta mafuriko na maporomoko ya ardhi, ambayo yamesababisha vifo.

    Zaidi ya watu milioni 1.4 walihamishwa kabla ya kimbunga hicho. Sasa kinaelekea Taiwan, ambako zaidi ya watu 3,000 wamehamishwa.

    Fung-wong kilikuwa kimbunga cha 21 kukumba taifa hilo la Kusini Mashariki mwa Asia mwaka huu, wakati ambapo wakazi wengi bado wanatatizika kujikwamua kutokana na majanga ya asili yanayotokea mara kwa mara.

    Kimbubga hicho kilipiga katika jimbo la Aurora siku ya Jumapili kwa upepo mkali wa karibu kilomita 185 kwa saa (115mph).

    Fung-wong kilimwaga mvua nyingi nchini humo, na kuacha nyumba zipatazo 4,100 zikiwa zimeharibiwa.

    Kinakuja siku chache baada ya kimbunga cha Kalmaegi kukumba eneo hilo hilo, na kuwaacha maelfu ya watu wakihangaika. Na mwezi Septemba, tetemeko la ardhi la kipimo cha 6.9 lilipiga mkoa wa Cebu.

    Wakati Ufilipino inakabiliwa na majanga ya asili, mfululizo huu wa majanga "sio wa kawaida," Shirika la Kimataifa la Mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu lilisema katika taarifa yake siku ya Jumapili.

    "Ni ukumbusho wa hali mbaya mbaya ya hewa inayoongezeka," ilisema.

  9. Watu 12 wameuawa katika mlipuko wa kujitoa muhanga nje ya mahakama Pakistan

    fv

    Chanzo cha picha, Zulqarnain

    Takriban watu 12 wamefariki katika mlipuko uliotokea nje ya mahakama katika mji mkuu wa Pakistan Islamabad.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan Mohsin Naqvi ameviambia vyombo vya habari kuwa watu 12 wamefariki na watu 27 wamejeruhiwa katika tukio hili.

    Mohsin Naqvi amesema, "Shambulio la kujitoa mhanga lilitokea mahakamani saa za jioni. Shambulio hili limesababisha uharibifu mkubwa, na watu 12 wameuawa na karibu 27 kujeruhiwa."

    Shirika la habari la Reuters lkimnukuu msemaji wa polisi akisema kuwa hali za baadhi ya waliojeruhiwa ni mbaya.

    Mlipuko huo ulitokea karibu na lango la Mahakama ya Wilaya ya Islamabad, ambayo kwa kawaida huwa na watu wengi wanaokuja mahakamani.

    Baada ya tukio hili, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan Khawaja Asif amechapisha kwenye Instagram akisema kuwa Pakistan iko katika hali ya vita.

    Aliandika kwenye X, "Ikiwa mtu yeyote anafikiri kwamba Jeshi la Pakistan linapigana vita katika eneo la mpaka wa Afghanistan na Pakistani na maeneo ya mbali ya Balochistan, basi shambulio la leo la kujitoa mhanga katika Mahakama ya Wilaya ya Islamabad ni wito kwamba hivi ni vita kwa Pakistan yote."

    Pia unaweza kusoma:

  10. Wahamiaji wa Warohingya waliofariki baada ya boti kupinduka wafikia 21

    g

    Chanzo cha picha, Walinzi wa Pwani ya Malaysia

    Maelezo ya picha, Shughuli za utafutaji na uokoaji zimeingia siku ya tatu kwa mamia ya wahamiaji waliopotea baharini

    Takriban watu 21 wamefariki baada ya mashua iliyokuwa imebeba wahamiaji wasio na vibali kuzama karibu na kisiwa cha mapumziko cha Malaysia cha Langkawi, karibu na mpaka na Thailand.

    Shughuli za utafutaji na uokoaji zimeingia siku ya tatu. Watu kumi na watatu wameokolewa lakini makumi ya wengine bado hawajapatikana. Jeshi la Majini la Malaysia wanakadiria takriban watu 70 walikuwa kwenye boti hiyo.

    Wale waliokuwa kwenye boti hiyo wanaaminika wengi wao ni Warohingya - ambao waliondoka katika jimbo maskini la Rakhine nchini Myanmar wiki mbili zilizopita, imesema serikali ya Malaysia.

    Boti nyingine iliyobeba abiria 230 bado haijapatikana.

    Mamlaka ya usafiri wa baharini ya Malaysia inatarajia operesheni hiyo, inayohusisha utafutaji juu ya bahari, kudumu kwa siku saba.

    Mwili mmoja uliopatikana ulikuwa wa mtoto, taarifa imesema.

    Kati ya 13 waliookolewa, 11 ni Warohingya na wawili ni WaBangladeshi.

    Warohingya, ambao ni Waislamu, ni miongoni mwa makabila madogo nchini Myanmar na wananyimwa uraia na serikali ya Myanmar.

    Tangu Agosti 2017, ukandamizaji mbaya wa jeshi la Myanmar ulipelekea maelfu ya Warohingya kukimbilia Bangladesh.

    Migogoro na hali duni ya maisha nchini Bangladesh hata hivyo pia imewafanya baadhi ya Warohingya kufanya safari za hatari kwenye meli zilizojaa watu hadi Malaysia, nchi yenye Waislamu wengi ambayo baadhi wanaiona kuwa ni kimbilio salama katika eneo hilo.

    Zaidi ya Warohingya 150,000 wamekimbilia katika kambi za wakimbizi za Bangladesh tangu mwishoni mwa 2023, huku maelfu wakiwa wameyakimbia makazi yao kimataifa, kwa mujibu wa makadirio ya Amnesty International.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Watu wanane wauawa baada ya gari kulipuka India

    fed

    Chanzo cha picha, RAJAT GUPTA/EPA/Shutterstock

    Watu wanane wameuawa siku ya Jumatatu jioni baada ya gari kulipuka katika mji mkuu wa India, Delhi.

    Kamishna wa polisi wa Delhi anasema mlipuko huo ulitokea wakati gari lililokuwa likitembea polepole kusimama kwenye taa nyekundu kabla ya kulipuka.

    Bado hakuna uthibitisho rasmi juu ya nini kilisababisha mlipuko huo.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa India Amit Shah na maafisa wengine wamesema "wanachunguza uwezekano wote " juu ya kile ambacho kumesababisha mlipuko huo.

    Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema waliohusika na mlipuko huo 'hawatasalimika.'

  12. Zungu Spika Mpya wa Bunge la Tanzania

    S

    Chanzo cha picha, EA

    Mussa Azzan Zungu amechaguliwa kuwa Spika mpya wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

    Zungu alipata kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa na wabunge katika mkutano wa kwanza na kikao cha kwanza cha bunge la 13 la Tanzania.

    Kwa ushindi huo, Mussa Azzan Zungu anakuwa Spika wa nane wa Bunge hilo tangu kuanzishwa kwake, baada ya kuwashinda wagombea wa vyama vingine waliopata jumla ya kura mbili pekee.

    Zungu aliteuliwa na chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwania nafasi hiyo, huku Spika, Dk. Tulia Ackson akijitoa katika kinyang’anyiro hicho kwa sababu ambazo hazikuelezwa wazi. Zungu, atasaidiwa na Daniel Sillo ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Spika.

    Miongoni mwa waliowahi kushika wadhifa huo wa Spika katika historia ya Tanzania ni Adam Sapi Mkwawa, Erasto Andrew Mbwana Mang’enya, Pius Msekwa, Samuel John Sitta, Anna Makinda, Job Ndugai, na Dk. Tulia Ackson.

  13. Makumi ya wafungwa wapatikana wamenyongwa katika gereza la Ecuador

    .

    Chanzo cha picha, LUIS SUAREZ/AFP kupitia Getty Images

    Takriban wafungwa 31 wamepatikana wameuawa katika gereza moja kusini mwa Ecuador, wakiwemo 27 waliokuwa wamenyongwa, maafisa wanasema.

    Wafungwa wanne waliuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa katika makabiliano kati ya magenge hasimu katika gereza la El Oro katika mji wa Machala alfajiri ya Jumapili.

    Saa chache baadaye, walinzi waliokuwa wametahadharishwa kuhusu kuzuka upya kwa ghasia za magenge waliwapata wengine waliokuwa wamenyongwa kwenye ghorofa ya tatu ya jengo hilo, idara ya magereza ya Ecuador ilisema.

    Magereza yenye msongamano wa watu nchini humo yamekuwa eneo la ghasia mbaya na mapigano ya magenge ambapo mamia ya wafungwa wameuawa katika miaka ya hivi karibuni.

    Soma zaidi:

  14. ‘Tulizuia njama ya Ukraine na Uingereza kuiba ndege ya MiG-31’ - Urusi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Idara ya Ujasusi ya Urusi (FSB) imesema kuwa ilizuia njama ya majasusi wa Ukraine na Uingereza kuwajaribu marubani wa Urusi kuiba ndege ya MiG-31 iliyokuwa na kombora la hypersonic la Kinzhal kwa $ 3 milioni, vyombo vya habari vya serikali viliripoti Jumanne.

    Shirika la habari la RIA lilinukuu FSB likisema kwamba ndege hiyo iliyotekwa nyara ingesafirishwa kuelekea kituo cha jeshi la anga la NATO katika mji wa Constanta nchini Romania, ambapo ingedunguliwa na walinzi wa anga, shirika hilo liliripoti.

    FSB, mrithi wa KGB ya enzi ya Usovieti, ilisema Ukraine na Uingereza zilipanga "uchokozi" mkubwa kwa kutumia ndege iliyotekwa nyara, na kwamba ujasusi wa kijeshi wa Ukraine ulijaribu kulaghai marubani wa Urusi kwa dola milioni 3 ili kuiba ndege hiyo.

    "Hatua zilizochukuliwa zimezuia mipango ya huduma za kijasusi za Ukraine na Uingereza kutekeleza uchochezi mkubwa zaidi," RIA ilinukuu FSB ikisema.

    Hata hivyo, shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha madai hayo kwa kujitegemea.

    Kwa muda mrefu Urusi imeiweka Uingereza kama adui yake mkuu na kuishutumu kwa kuchochea vita vya Ukraine na ujasusi wa Uingereza kuisaidia Ukraine kuanzisha mfululizo wa operesheni ndani ya Urusi.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Nyuki mpya apewa jina 'Shetani' kwa muonekano wa pembe zake

    .

    Chanzo cha picha, Dk Kit Prendergast

    Wanasayansi wa Australia wamegundua aina mpya ya nyuki wa asili mwenye pembe ndogo - na kumpa jina la shetani.

    Watafiti walimgundua nyuki ‘Megachile Lucifer’ walipokuwa wakitazama ua adimu la mwituni ambalo hukua katika eneo la Goldfields la Australia Magharibi peke yake, 470km (292mi) mashariki mwa Perth.

    "Pembe za nyuki huyo wa aina yake" ziko kwenye nyuki jike pekee na zinaweza kutumika kama njia ya kujilinda, kukusanya chavua au nekta, au kukusanya nyenzo kama vile resini kwa viota.

    Mwanasayansi mkuu wa utafiti huo alisema alivutiwa na jina la ‘Shetani’ alipokuwa akitazama kipindi cha Netflix kilichokuwa na jina kama hilo wakati huo.

    Aliongeza kuwa kuna aina mpya kabisa ya nyuki katika kipindi cha miaka 20.

    Soma zaidi:

  16. Seneti Marekani yapitisha mswada wa ufadhili kumaliza mkwamo wa shughuli za serikali

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Bunge la Seneti la Marekani limepitisha mswada muhimu wa ufadhili ambao unaweza kumaliza mkwamo wa shughuli za serikali ambao umeshuhudiwa kwa muda mrefu zaidi katika historia yan chi hiyo.

    Mswada huo ulipitishwa kwa kura 60-40 mwishoni mwa Jumatatu, na karibu Warepublican wote wakiungana na Wanademokrasia wanane ambao walijitenga na chama ili kuiidhinisha.

    Mpango huo unafadhili serikali hadi mwisho wa Januari.

    Pia unajumuisha ufadhili wa mwaka mzima kwa Idara ya Kilimo, pamoja na ufadhili wa ujenzi wa kijeshi na mashirika ya kutunga sheria.

    Baraza la Wawakilishi sasa litalazimika kupitisha mswada huo kabla ya Rais Donald Trump kuutia saini ili kuanza kutumika. Trump aliashiria kuwa tayari kufanya hivyo mapema Jumatatu.

    Makubaliano hayo yalitimia mwishoni mwa juma, baada ya baadhi ya Wanademokrasia kujiunga na Republican na kujadili makubaliano ya kuwarejesha wafanyakazi wa serikali kazini na huduma muhimu kuanza tena.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Mwandishi habari wa Uingereza kuachiliwa kutoka kizuizini Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

    Mwanahabari wa Uingereza Sami Hamdi anatazamiwa kuachiliwa kutoka kizuizini nchini Marekani wiki mbili baada ya kuzuiliwa na Idara ya uhamiaji, familia yake ilisema Jumatatu.

    Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha ya Marekani (ICE) ilimkamata Hamdi, mchambuzi wa vyombo vya habari na mkosoaji mkubwa wa Israel, mwezi uliopita alipokuwa katika ziara nchini Marekani.

    Wizara ya Mambo ya Nje na Idara ya Usalama wa Ndani (DHS) ilidai wakati huo Hamdi anaunga mkono ugaidi na ni tishio kwa usalama wa taifa, huku mawakili wake wakidai kwamba alilengwa kwa kukosoa Israeli na vita vilivyokuwa vikiendelea huko Gaza.

    Hamdi ataachiliwa kutoka kizuizini siku chache zijazo na kurejea Uingereza, wawakilishi wake wanasema.

    Hamdi alikuwa akizuru Marekani kwa ajili ya kuhutubia hafla za Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR), kikundi cha kutetea Waislamu, wakati maafisa wa ICE walipomkamata kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa San Francisco tarehe 26 Oktoba.

    Kuzuiliwa kwake kulikuja baada ya serikali ya Marekani kubatilisha visa ya Hamdi na ukosoaji kutoka kwa mwanaharakati wa siasa kali za mrengo wa kulia na mshirika wa Trump Laura Loomer, ambaye alimshutumu kwa kuunga mkono magaidi.

    Soma zaidi:

  18. Mtoto wa mwisho wa Gaddafi aliachiliwa baada ya miaka 10 kizuizini

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Hannibal Gaddafi, mtoto wa mwisho wa aliyekuwa rais wa Libya aliyeondolewa madarakani Muammar Gaddafi, ameachiliwa huru na Lebanon baada ya kuzuiliwa kwa takriban miaka 10 bila kufunguliwa kesi.

    Mamlaka ya Lebanon ilimkamata mtoto wa Gaddafi, ambaye sasa ana umri wa miaka 49, mwaka 2015, wakimtuhumu kwa kuficha habari kuhusu hatima ya mhubiri wa Kishia wa Lebanon ambaye alitoweka nchini Libya mwaka 1978.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani shutuma hizo.

    Wakili wake aliliambia shirika la habari la AFP dhamana yake ya $900,000 (£682,938) imelipwa.

    Laurent Bayon alisema: "Ni mwisho wa madhila kwake ambayo yamedumu kwa miaka 10."

    Mnamo mwezi Oktoba, jaji alitoa dhamana ya $11m dhidi ya kuachiliwa kwa Gaddafi lakini hii ilipunguzwa wiki iliyopita baada ya timu yake ya utetezi kuwasilisha rufaa, kulingana na AFP.

    Bw Bayon alisema mteja wake ataondoka Lebanon kuelekea mahali pa "siri".

    "Ikiwa mtoto wa Gaddafi alizuiliwa kiholela nchini Lebanon kwa miaka 10, ni kwa sababu mfumo wa haki haukuwa huru," Bayon alisema, kulingana na AFP.

    Mnamo 2015, Hannibal Gaddafi alitekwa nyara na kundi lenye silaha nchini Lebanon kabla ya kuachiliwa. Baadaye aliwekwa kizuizini na mamlaka ya Lebanon.

    Baada ya babake kupinduliwa na waasi na kuuawa mwaka 2011, alikimbilia Syria na alikuwa ameishi chini ya kifungo cha nyumbani huko Oman na mkewe Aline Skaf.

    Kutoweka kwa kasisi wa Shia Musa al-Sadr nchini Libya mwaka 1978 kumekuwa chanzo cha mvutano kati ya Libya na Lebanon kwa miongo kadhaa.

    Hannibal Gaddafi alikuwa na umri wa miaka miwili pekee wakati huo na hakuwa na wadhifa wowote nchini Libya akiwa mtu mzima.

    Pia unaweza kusoma:

  19. Syria kujiunga na muungano unaoongozwa na Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Syria itajiunga na muungano wa kimataifa kupambana na kundi la Islamic State, na hivyo kuashiria mabadiliko katika sera ya kigeni ya Marekani katika Mashariki ya Kati, afisa mkuu wa utawala wa Trump amethibitisha.

    Tangazo hilo lilitolewa wakati Rais Donald Trump alipokutana na Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa katika Ikulu ya Marekani - ziara ya kwanza kama hiyo kutoka kwa kiongozi wa Syria katika historia ya nchi hiyo.

    Katika mahojiano na Fox News, al-Sharaa alisema ziara hiyo ni sehemu ya "zama mpya" ambapo nchi hiyo itashirikiana na Marekani.

    Trump ameeleza uungaji mkono wake kwa al-Sharaa, ambaye hadi hivi majuzi alikuwa ametambuliwa kama gaidi na serikali ya Marekani.

    Soma zaidi:

  20. Trump atishia kuishtaki BBC

    .

    Chanzo cha picha, Reuters / AFP via Getty Images

    Donald Trump ametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya BBC, kufuatia ukosoaji kuhusu jinsi hotuba yake ilivyohaririwa na kutumika katika makala ya Panorama.

    Timu yake ya wanasheria imeipa BBC makataa ya tarehe 14 Novemba "kuondoa kabisa" makala hiyo "kwa ajili ya uwepo wa haki" - au shirika hilo likabiliwe na mashtaka ya kulitaka ilipe $1bn (£760m).

    Taarifa ya ndani ya BBC iliyovuja ilisema kipindi hicho kilipotosha watazamaji kwa kuunganisha sehemu mbili za hotuba ya Trump ya tarehe 6 Januari 2021, na kuifanya ionekane kana kwamba alikuwa akiwahimiza watu kushambulia Ikulu ya Marekani baada ya kushindwa katika uchaguzi.

    Mkurugenzi Mtendaji wa BBC anayeondoka Deborah Turness alisisitiza kuwa shirika hilo "halikuwa na upendeleo wa kitaasisi", baada ya kujiuzulu pamoja na mkurugenzi mkuu Tim Davie.

    Kujiuzulu kwao Jumapili baada ya shinikizo kuongezeka kufuatia kuchapishwa wiki iliyopita katika mtandao wa Telegraph taarifa iliyoandikwa na Michael Prescott, mshauri huru wa zamani wa nje wa kamati ya viwango vya uhariri wa shirika hilo la utangazaji.

    Taarifa hiyo inaishutumu BBC kwa utangazaji wake wa masuala ya Gaza, chuki dhidi ya Trump na Israel na kuripoti kwa upande mmoja kwa waliobadili jinsia - miongoni mwa "mambo yenye utata". Pia inaangazia hariri ya makala ya Panorama.

    Soma zaidi: