Heche na viongozi wengine wa CHADEMA waachiwa kwa dhamana Tanzania

Makamu Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche alikamatwa zaidi ya wiki tatu zilizopita bila kufikishwa mahakamani, na hata familia yake haikujua alipo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Kwaheri

  2. Heche na viongozi wengine wa CHADEMA waachiwa kwa dhamana

    Heche

    Chanzo cha picha, John Heche/Facebook

    Makamu Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, pamoja na viongozi wengine wa chama hicho wameachiwa kwa dhamana, hatua ambayo imethibitishwa rasmi na CHADEMA.

    Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na chama hicho, Heche alikuwa akikabiliwa na matatizo ya kiafya alipokuwa chini ya ulinzi wa polisi, na leo polisi walimpeleka hospitalini kwa matibabu kabla ya kumuachia.

    Heche alikamatwa zaidi ya wiki tatu zilizopita bila kufikishwa mahakamani, na hata familia yake haikujua alipo.

    Baadaye, alipelekwa kituo cha polisi na kusomewa mashtaka ya ugaidi

    Miongoni mwa viongozi wengine wa CHADEMA walioachiwa kwa dhamana ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.

    Viongozi hao walikamatwa kwa tuhuma za kuchochea maandamano yaliyodaiwa kulenga kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

    Wakati hayo yakijiri, Mahakama leo imeahirisha kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu kwa kile kilichotajwa kuwa ni sababu za kiusalama.

    Kesi hiyo imepangwa kuendelea tena tarehe 12 mwezi Novemba.

    Maelezo zaidi:

  3. Sarkozy aachiliwa kutoka gerezani baada ya wiki tatu

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameachiliwa wiki tatu baada ya kuanza kuhudumia kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kula njama ya uhalifu.

    Sarkozy atakuwa chini ya uangalizi mkali wa mahakama na kuzuiwa kuondoka Ufaransa.

    Tarehe 21 Oktoba rais huyo wa zamani wa mrengo wa kulia mwenye umri wa miaka 70, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kula njama ya kufadhili kampeni yake ya uchaguzi wa 2007 kwa pesa kutoka kwa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi.

    Mawakili wake waliwasilisha ombi la kutaka aachiliwe, wakisubiri kesi ya rufaa itakayosikiliza mwezi Machi mwakani.

    Akiongea na mahakama mjini Paris kwa njia ya video, Sarkozy alielezea muda wake katika kifungo cha upweke kama "uchungu" na "ndoto mbaya".

    Mwendesha mashtaka wa umma Damien Brunet alipendekeza kwamba ombi la Sarkozy la kuachiliwa likubaliwe, lakini rais huyo wa zamani apigwe marufuku kuwasiliana na mashahidi,

    Sarkozy, ambaye amekuwa akikana kufanya kosa lolote, aliiambia mahakama kupitia njia ya video kwamba hajawahi kuwa na "wazo la kichaa" la kumuomba h marehemu Gaddafi pesa na kusema "sitakubali kitu ambacho sikufanya".

    Maelezo zaidi:

  4. Mshawishi wa TikTok auawa nchini Mali

    Mariam Cissé

    Chanzo cha picha, Mariam Cissé / Tiktok

    Mshawishi wa kike wa mtandao wa TikTok anayetuhumiwa kusaidia jeshi la Mali amekamatwa na kuuawa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wenye itikadi kali za kidini.

    Mariam Cissé, 20, aliyekua na wafuasi zaidi ya 100,000 TikTok, alichapisha video kuhusu maisha katika mji aliozaliwa wa Tonka katika eneo la kaskazini la Timbuktu na mara nyingi alionyesha kuunga mkono jeshi la nchi hiyo.

    Kifo chake kimeshtua taifa, ambalo limekuwa likipambana na wanamgambo wa kijihadi tangu 2012.

    Televisheni ya serikali ilisema mshawishi huyo alitaka kukuza jamii yake na kuunga mkono jeshi kupitia machapisho yake ya TikTok.

    Mali inakabiliwa na uhaba wa mafuta kufuatia kizuizi kilichowekwa na makundi ya wanamgambo ambayo yametatiza maisha ya kila siku, huku Umoja wa Afrika ukielezea "wasiwasi wake" kuhusu hali nchini humo.

    Bi Cissé alikamatwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo alipokuwa akitiririsha moja kwa moja kutoka sokoni katika mji jirani, kitui cha redio cha Ufaransa RFI kiliripoti.

    "Dada yangu alikamatwa siku ya Alhamisi na wanajihadi," kaka yake aliliambia shirika la habari la AFP, akisema kuwa walimshtumu kwa "kuliarifu jeshi la Mali kuhusu mienendo yao".

    Pia unaweza kusoma:

  5. Binti wa Jacob Zuma akanusha mashtaka ya ugaidi dhidi yake

    Duduzile Zuma-Sambudla amesema kesi ya serikali dhidi yake ni dhaifu

    Chanzo cha picha, Gallo Images via Getty Images

    Maelezo ya picha, Duduzile Zuma-Sambudla amesema kesi ya serikali dhidi yake ni dhaifu

    Binti ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amekanusha mashtaka yanayohusiana na ugaidi yaliowasilishwa mahakamani dhidi yale mjini Durban.

    Duduzile Zuma-Sambudla ameshtakiwa kufutia matamshi aliyoyatoa kwenye mitandao ya kijamii miaka minne iliyopita wakati wa maandamano mabaya nchini Afrika Kusini kufuatia kukamatwa kwa babake.

    Machafuko yaliyokumba maeneo kadhaa ya nchi mnamo Julai 2021, yalisababisha vifo vya takriban watu 300 na uharibifu wa mali ya thamani ya takriban dola bilioni 2.8 za Kimarekani.

    Zuma-Sambudla, 43, analituhumiwa kuchochea machafuko hayo na anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea ugaidi na ghasia za umma.

    Maandamano yalifanyika katika majimbo ya Gauteng na KwaZulu-Natal baada ya rais huyo wa zamani kukamatwa kwa kwa kutotii amri ya mahakama iliyomtaka kutoa ushahidi wake katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi alipokuwa madarakani.

    Bi Zuma-Sambudla amekuwa akikana mashtaka dhidi yake, huku wakili wake akiitaja kesi ya serikali kuwa dhaifu.

    Maelezo zaidi:

  6. Bunge la Seneti Marekani lafikia mkataba kurejesha ufadhili kwa serikali

    John Thune

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa Wengi katika Seneti nchini Marekani John Thune alisaidia kujadili makubaliano ya wikendi

    Makubaliano ya kumaliza mzozo wa ufadhili wa bajeti uliosababisha ufungwaji wa shughuli za serikali ya Marekani yamefikiwa na Baraza la Seneti.

    Haya yanajiri baada ya mazungumzo yaliyofanyika wekendi jijini Washington, wabunge wa chama cha Democratic waliungana na wenzao wa Republican kupiga kura ya kuunga mkono makubaliano hayo.

    Kura hiyo ni hatua ya kwanza kuelekea maelewano ya kufadhili shughuli za serikali ambayo iliishiwa na pesa tarehe 1 Oktoba.

    Itahitaji kuondoa vikwazo vingine kadhaa - ikiwa ni pamoja na kura kutoka kwa Baraza la Wawakilishi - kabla ya wafanyikazi wa umma na huduma za kwaida kurejea.

    Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya hasara kubwa sana, hasa kwenye sekta ya usafirishaji, ambapo zaidi ya safari 7,000za ndege zilicheleweshwa siku ya Jumapili (Novemba 9), huku zaidi ya 1,000 zikifutwa siku ya Ijumaa, na zaidi ya 1,500 siku ya Jumamosi.

  7. Rais wa Israel anazuru Zambia, DR Congo

    Rais wa Israel Isaac Herzog anazuru mataifa ya Zambia na DR Congo leo na kesho katika juhudi za kufufua uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na Afrika, vyombo vya habari vya Israel na tovuti inayomilikiwa na watu binafsi ya Mwebantu vimeripoti.

    Ziara ya Herzog nchini Zambia itakuwa ya kwanza kuwahi kufanywa na rais wa Israel ingawa rais Hakainde Hichilema alikuwa Israel mwezi Juni 2023. Herzog na Hichilema wanatarajiwa kujadiliana kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa, yakiwemo masuala ya amani na usalama.

    Viongozi hao pia watajadili ushirikiano katika sekta ya kilimo, afya, elimu, teknolojia, biashara na uwekezaji.

    Mnamo mwezi Agosti, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Sa'ar alifungua ubalozi wa Israel mjini Lusaka, zaidi ya miongo mitatu baada ya nchi hizo mbili kurejesha uhusiano wa kidiplomasia.

    Herzog ataelekea DR Congo kesho kwa mazungumzo na rais Felix Tshisekedi.

    Zambia na DR Congo ni wanachama wa Jumuiya ya Sadc inayoongozwa na Afrika Kusini, ambayo imewasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki juu ya tuhuma za mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.

    Mataifa yote ya Afrika yametambua rasmi taifa la Palestina sipokuwa Eritrea na Cameroon.

    Soma pia:

  8. Mkutano wa hali ya hewa wa COP30 unaanza huku ukiwa hauna malengo mahususi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mkutano wa COP30 unafunguliwa leo Jumatatu huku zaidi ya nchi 190 zikishiriki, lakini haijafahamika wazi ni nini hasa wangejadili wakati wa mkutano wa kilele wa wiki mbili wa Umoja wa Mataifa katika mji wa Amazon wa Belem nchini Brazili.

    Pia haijulikani ni jinsi gani watashughulikia masuala ambayo yamekuwa kama majaribu, kama vile ahadi ya 2023 ya kuondoa vyanzo vya nishati vinavyochafua mazingira na mahitaji ya ufadhili kuwezesha hilo kufanyika.

    Nchi kama vile Brazili wamependekeza kuwa nchi zilenge juhudi ndogo ambazo hazihitaji makubaliano, baada ya miaka mingi ya mikutano ya COP ambayo imesherehekea kuwa na ahadi chungu nzima lakini nyingi zikiishia bila kutekelezwa.

    "Ninachopendelea sio kuwa uamuzi wa COP," Rais wa COP30 Andre Correa do Lago alisema katika mahojiano na Reuters na vyombo vingine vya habari. "Ikiwa nchi zina hamu kubwa ya uamuzi wa COP, bila shaka tutalifikiria suala hilo na kulishughulikia."

    Do Lago alibainisha kuongezeka kwa umuhimu wa China katika mazungumzo hayo, huku Marekani ikiahidi kujiondoa kwenye Mkataba wa Paris mwezi Januari na Umoja wa Ulaya nao ukijitahidi kudumisha azma yake huku kukiwa na wasiwasi juu ya usalama wa nishati.

    Soma zaidi:

  9. Mamia wajitokeza kwa maandamano ya kupinga uchafuzi wa mazingira India

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamia ya watu mjini Delhi waliingia mitaani siku ya Jumapili kupinga uchafuzi wa mazingira huku ubora wa hewa ukiendelea kuzorota katika mji mkuu wa India na maeneo jirani.

    Watu wa rika zote wakiwemo watoto walishika mabango na kupiga kelele wakiitaka serikali kuchukua hatua kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.

    Takriban watu 80 walizuiliwa kwa muda mfupi na polisi, ambao walisema waandamanaji hawakuwa na kibali cha kukusanyika katika eneo husika ambalo ni kitovu cha jiji hilo.

    Ingawa uchafuzi wa hewa ni tatizo la mara kwa mara kaskazini mwa India, hasa katika majira ya baridi, haya yalikuwa maandamano makubwa ya kwanza kuhusu suala hilo kwa muda mrefu.

    "Mapafu yetu yanaharibika. Serikali inapaswa kutangaza kuwa ni dharura ya kiafya hadi watakapopata suluhu," mwandamanaji mmoja aliambia shirika la habari la PTI.

    Ubora wa hewa mjini Delhi na vitongoji vyake ni duni kwa kiasi cha mwaka mzima kutokana na utoaji wa moshi wa magari, vumbi na vichafuzi vya viwandani.

    Lakini tatizo huwa mbaya zaidi wakati wa majira ya baridi kali kwa sababu ya wakulima kuchoma makapi ya mazao katika majimbo jirani, pamoja na kasi ya chini ya upepo kunasa vichafuzi karibu na ardhi.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Kesi ya Lissu yaahirishwa sababu za kiusalama - Mwanasheria

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, (CHADEMA), Tundu Lissu, ambayo ilitarajiwa kuendelea leo Jumatatu, Novemba 10, 2025, imeahirishwa hadi Jumatano ya Novemba 12, ambapo itatajwa tena mahakamani.

    Awali, upande wa Jamhuri ulipanga kuwasilisha shahidi wa nne katika kesi hiyo, lakini hilo halikuwezekana kutokana na hali ya sintofahamu iliyoibuka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kufuatia maandamano ya siku tatu yaliyoanza Oktoba 29, 2025. Mashahidi wanaotoka mikoa ya Ruvuma na Mbeya wameshindwa kusafiri kufika jijini kutokana na changamoto hizo za kiusalama.

    Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka, hali hiyo imeathiri mchakato wa mashahidi kufika, na hivyo kufanya kesi ishindwe kuendelea kama ilivyopangwa. Wakili wa Serikali Mkuu, Thawabu Issa, aliieleza Mahakama kuwa ombi la kuahirisha linatolewa chini ya kifungu cha 302(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 (Toleo la 2023), akibainisha kuwa mashahidi wameshindwa kufika kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.

    Kwa upande wa Jamhuri uliomba kesi iahirishwe kwa siku 14, Jaji Danstan Ndunguru aliamua ihahirishwe kwa siku mbili na kwamba shauri hilo litaendelea Jumatano ijayo badala ya muda huo mrefu uliotakiwa.

    Wakili wa Lissu, Rugemeleza Nshalla, aliyeeleza kuhusu kuhairishwa kwa sababu ya usalama amesema wao wameweza kufika Mahakamani maana yake hali inaruhusu wengine kufika Mahakamani.

    "Na tunafahamu kuwa mashahidi wengine ni wale wa kufichwa hata sijui usalama wao unahatarishwa vipi”, alihoji Nshalla na kuongeza, “Bahati mbaya mwenyekiti anajiwakilisha mwenyewe, hivyo hakuweza kuzungumza, tunatumaini kwamba umma ungependa kujua nini kinaendelea”.

    Hata hivyo mwishoni mwa wiki, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, akizungumza kwenye mkutano wa nchi wanachama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwamba hali ya nchi iko shwari.

    "Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za kurejesha utengemano katika nchi yetu ambao sasa nchi yetu (hali) ni shwari, na kila mtu anafuata utawala wa sheria", alisema Dk Nchimbi.

  11. Indonesia yamtaja dikteta wa zamani Suharto 'shujaa wa taifa'

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Indonesia imemtaja rais wa zamani Suharto kuwa shujaa wa taifa, hata ingawa utawala wa udikteta umezusha maandamano makali kupinga hatua hiyo.

    Wakati wa utawala wa Suharto katika miaka ya 1960 hadi 1990, Indonesia ilishuhudia enzi ya ukuaji wa haraka wa uchumi lakini pia ukandamizaji mkali wa kisiasa.

    Mamia ya maelfu ya wapinzani wa kisiasa walisemekana kuuawa katika kipindi hicho.

    Tuzo la shujaa wa kitaifa ni jambo la kila mwaka, linalokusudiwa kuwaheshimu watu binafsi kwa michango yao kwa nchi.

    Siku ya Jumatatu, marehemu Suharto alikuwa miongoni mwa majina 10 mapya yaliyoongezwa kwenye orodha hiyo, katika hafla iliyoongozwa na rais wa sasa wa Indonesia Prabowo Subianto, mkwe wa zamani wa Suharto.

  12. Muingereza afariki baada ya kupigwa risasi wakati wa tukio la wizi nchini Ghana

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamume mmoja raia wa Uingereza amefariki baada ya kupigwa risasi wakati wa wizi nchini Ghana siku ya Ijumaa, polisi wanasema.

    Ashraf Qarmar Parvez, 68, alipigwa risasi baada ya kujaribu kuzuia jaribio la kuiba simu yake katika eneo la kunywa pombe huko Tema, mji ulio mashariki mwa mji mkuu wa Ghana, Accra. Baadaye alifariki hospitalini, polisi walisema.

    Mamlaka nchini Ghana inamsaka mshambuliaji - mmoja wa kundi la washukiwa sita ambao wanasema walikuwa katika eneo la tukio na walitoroka kwa pikipiki.

    Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema ilikuwa ikisaidia familia ya mtu aliyefariki.

  13. Israel yapokea maiti ya mwanajeshi aliyeuawa Gaza mwaka 2014

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mwanajeshi wa IDF Hadar Goldin aliuawa huko Gaza mnamo mwaka 2014

    Israel imepokea mwili wa Lt Hadar Goldin, mwanajeshi aliyeuawa na Hamas mwaka 2014 na ambaye mwili wake umeshikiliwa huko Gaza tangu wakati huo.

    Jeshi la Israel lilisema Lt Goldin, ambaye alikuwa na umri wa miaka 23 alipofariki, alitambuliwa rasmi na sasa atazikwa. Aliacha wazazi, dada, kaka wawili, na mchumba.

    Mrengo wa kijeshi wa Hamas ulisema Jumapili kwamba utakabidhi mwili wa Lt Goldin kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Hamas sasa imewarudisha mateka wote 20 walio hai, na mateka 24 kati ya 28 waliofariki chini ya awamu ya kwanza ya mpango huo.

    Pia unaweza kusoma:

  14. RSF inaondoa miili kuficha madai ya ukatili dhidi ya raia - Jumuiya ya madaktari wa Sudan

    ,

    Chanzo cha picha, AP

    Jumuiya ya madaktari wa Sudan imeshutumu vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) kwa kuondoa mamia ya miili kutoka mitaa ya El Fasher huko Darfur kuficha madai ya ukatili dhidi ya raia.

    Mtandao wa Madaktari wa Sudan ulisema katika taarifa Jumapili, kuwa maiti kadhaa zilizikwa kwenye makaburi ya halaiki.

    Mtandao huo ulisema mazishi hayo ni "mauaji ya halaiki" na "ukiukaji wa kanuni zote za kimataifa na za kidini ambazo zinahakikishia wafu haki ya mazishi yenye heshima," taarifa ilisema.

    Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa hali katika eneo la Al Fasher ni " zaidi ya janga la kibinadamu" yenye kulenga maisha ya mwanadamu huku kukiwa na "ukimya wa kutisha wa kimataifa".

    Mnamo Oktoba 26, RSF ilichukua udhibiti wa eneo la Al Fasher, mji mkuu wa Darfur ya Kaskazini, na kufanya mauaji, kulingana na mashirika ya ndani na ya kimataifa.

    Tangu Aprili 15, 2023, Jeshi la Sudan na RSF wmekuwa katika vita ambavyo upatanishi wa kikanda na kimataifa umeshindwa kuvimaliza.

    Mzozo huo umewauwa maelfu ya watu na kuhamishwa kwa mamilioni ya wengine.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Kimbunga kinaondoka Ufilipino baada ya kuua watu wawili

    .

    Kimbunga kilichodhoofika cha Fung-wong sasa kinapita kwenye Bahari ya Kusini ya China na kinatarajiwa kuelekea Taiwan, baada ya kusababisha vifo vya watu wawili nchini Ufilipino.

    Takriban watu milioni 1.4 nchini Ufilipino walikuwa wamehamishwa kabla ya kimbunga Fung-wong kutua Jumapili kikibeba upepo wa kasi ya 185km/h (115mph) na dhoruba za 230km/h (143mph).

    Kimekumba eneo la Aurora huko Luzon - kisiwa chenye watu wengi zaidi nchini - saa 21:10 saa za eneo (13:10 GMT) na kudhoofika saa chache baadaye.

    Kimbunga Fung-wong kinajiri siku chache baada ya kimbunga cha Kalmaegi kilichosababisha vifo vya takriban watu 200.

    Mamlaka ya Ufilipino inaripoti uharibifu mdogo kuliko ilivyotarajiwa - ingawa jamii kadhaa bado zimetatizika kutokana na mafuriko.

    Kulipopambazuka, upepo wa Kimbunga Fung-wong zilizokuwa zimevuma usiku kucha zilikuwa zimeisha, na watu wakatoka kuona uharibifu.

    Kulikuwa na uharibifu mkubwa wa majengo, lakini maandalizi mazuri yanaonekana kuzuia kurudiwa kwa athari zilizoonekana baada ya kimbunga Kalmaegi kukumba eneo la kati la Ufilipino wiki iliyopita.

    Soma zaidi:

  16. Mkurugenzi Mkuu wa BBC ajiuzulu

    .

    Chanzo cha picha, PA Media

    Mkurugenzi mkuu wa BBC Tim Davie na mkuu wa habari Deborah Turness wamejiuzulu baada ya kukosolewa kwamba makala ya Panorama ilipotosha watazamaji kwa kuhariri hotuba ya Donald Trump.

    Davie, alikabiliwa na shinikizo linaloongezeka juu ya utata na shutuma za upendeleo ambazo zimetawala shirika hilo la utangazaji la umma.

    .

    Chanzo cha picha, PA/BBC

    Telegraph ilichapisha maelezo ya taarifa ya ndani ya BBC iliyovuja Jumatatu ambayo ilipendekeza kipindi cha Panorama kilihariri sehemu mbili za hotuba ya rais wa Marekani ili aonekane kuhimiza ghasia za Capitol Hill za Januari 2021.

    Viongozi wa kisiasa wa Uingereza walielezea matumaini kuwa kujiuzulu kwao kutaleta mabadiliko, huku Trump akikaribisha uamuzi huo.

  17. Hujambo msomaji wetu. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 10/11/2025.