Kwa nini 'upande mchafu' wa kimbunga unaweza kuwa na nguvu 50% zaidi kuliko 'upande msafi'

Chanzo cha picha, Nasa Earth Observatory/ Wanmei Liang
Katika dhoruba za kitropiki, eneo ni muhimu linapokuja suala la utarajie nini katika uharibifu - haswa katika upande "mchafu" wa kimbunga, ambapo upepo unaweza kuwa na nguvu hadi 50%."
Vimbunga vinaweza kuwa vigumu kutabiri.
Kasi na njia ya kimbunga hutegemea mwingiliano usio wa kawaida kati ya dhoruba na mizunguko yake ya ndani, na angahewa ya Dunia.
Mifumo ya shinikizo la juu na chini inaweza kubadilisha kasi na njia ya kimbunga, wakati hewa ambayo iko kwenye kimbunga na ndiyo yenye kuitumia kusafiri inasonga na kubadilika kila wakati.
Kwa kawaida husogea kwa kasi ya 15 hadi 20mph (24 hadi 32km/h), lakini vingine hukawia - na kusababisha mvua kubwa na mafuriko.
Vinaweza kuongeza kasi - kufikia 60mph (97km/h) na kusafiri kwa mstari ulionyooka, au vinaweza kuyumba yumba.
Msimu wa vimbunga wa 2024
Wakati kimbunga Francine kilipopiga kusini mwa Marekani kwa upepo mkali na mvua kubwa, jamii za Louisiana zilikumbwa na mafuriko, huku maelfu ya watu wakiachwa bila umeme katika maeneo ya Alabama na Mississippi.
Vimbunga vinazidi kuwa visivyotabirika - na hatari, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Shirika la Usimamizi wa Dharura Marekani limewataka umma kujiandaa, na kuonya kwamba utabiri wa kimbunga wa Utawala wa Kitaifa wa Bahari na Anga kwa 2024 ndio "utabiri mkali zaidi katika rekodi".
Vimbunga pia vina upande wa kulia na wa kushoto – upande wa Kizio cha Kaskazini, unajulikana kama upande "mchafu" na "msafi" mtawalia. Lakini ikiwa uko katika upande wa Kizio cha Kusini, pande za ‘uchafu’ na ‘usafi’ hubadilika - upande wa kushoto unakuwa mchafu, kwa sababu upepo wa kimbunga huzunguka katikati kwa mwendo wa saa, tofauti na upande wa Kizio cha Kaskazini ambako huzunguka kinyume na saa.
Robert Rogers, mtaalamu wa hali ya hewa katika Maabara ya Bahari ya Atlantiki huko Miami, Florida, anaelezea kwa nini vimbunga vina upande chafu.
Kwa nini vimbunga vina upande mmoja hatari zaidi kuliko mwingine?
Kawaida, upande mmoja wa kimbunga una upepo mkali zaidi kuliko upande mwingine - tunaita aina hii ‘asymmetry’. Kuna sababu kadhaa za hili, lakini sababu ya msingi ni kwamba mwendo wa dhoruba huongezeka kwenye mzunguko wa nyuma wa kimbunga.
Katika Kizio cha Kaskazini, hiyo ina maana kwamba upepo huwa na nguvu zaidi upande wa kulia wa mwelekeo wa mwendo wa dhoruba. Vile vile, upepo huwa dhaifu zaidi upande wa kushoto wa mwelekeo wa mwendo wa dhoruba.
Upande mchafu ni ule upande wenye upepo mkali zaidi, upande wa kulia wa mwendo wa dhoruba. Upande msafi ni upande wa kushoto wa mwendo wa dhoruba – ikiwa tena ni katika Kizio cha Kaskazini.
Kwa nini upande wa uchafu ni hatari zaidi, na kwa kiasi gani?

Chanzo cha picha, EPA
Ni hatari zaidi kwa sababu hapo ndipo upepo una nguvu zaidi. Wakati mwingine upepo unaweza kuwa na nguvu hadi 50% upande wa uchafu kuliko upande msafi, haswa ikiwa dhoruba inasonga kwa kasi, kwa mfano, 15 hadi 20mph (24 hadi 32km/h).
Sababu nyingine inaweza kuwa hatari kwa upande mchafu ni kuwa, wakati wa kutua, huo ndio ni upande ambapo maji yanasukumwa mbele zaidi, na kusababisha kuongezeka kwa dhoruba.
Je, tofauti hiyo ni kubwa zaidi katika vimbunga fulani kuliko vingine?
Tofauti hiyo ni kubwa zaidi kwa vimbunga vinavyosonga kwa kasi mno.
Tunaweza kutabiri kwa usahihi kiasi gani upande mchafu utakuwa hatari zaidi?
Modeli za kompyuta kwa kiasi kikubwa ina uwezo wa kutabiri kwa usahihi katika muundo, kama vile mabadiliko ya upepo kwenye kimbunga. Kwa hivyo inaweza kutabiriwa vizuri.
Je, kuna jambo lolote ambalo watu wanahitaji kufanya ili kujiandaa kwa athari zitakazotokana na hatari za upande mchafu?
Iwapo unatarajiwa kuwa katika upande mchafu wa kimbunga, unapaswa kujiandaa kwa hali mbaya zaidi, kama vile upepo, [dhoruba] kuongezeka, ikiwezekana mvua na hali ya hewa kali, kuliko ikiwa uko upande msafi.
Kwa kuwa upepo kwa kawaida huenea eneo kubwa zaidi kwenye upande mchafu, unapaswa pia kutarajia hali kuwa mbaya mapema kuliko ikiwa uko kwenye upande msafi.
Je, upande huu umeathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa - je, umekuwa hatari zaidi, au ni vigumu kuhitimisha hilo?
Kwa kuwa upande mchafu dhidi ya msafi kiasi kikubwa huamuliwa na mwendo wa kimbunga, haijulikani ikiwa mabadiliko ya hali ya hewa yanafanya upande mchafu kuwa mbaya zaidi.
Kwa kiwango ambacho mabadiliko ya hali ya hewa hubadilisha kasi ya mwendo wa kimbunga, hiyo inaweza kuathiri upande mchafu. Aidha, utafiti fulani umependekeza kwamba kasi ya mwendo wa kimbunga inapungua kutegemea na mabadiliko ya hali ya hewa. Ingawa, uhusiano huu bado unajadiliwa.
Imetafsiriwa na Asha Juma












