Hofu yatanda dunia ikikumbwa na joto kali zaidi kuwahi kutokea

Chanzo cha picha, Reuters
Wimbi kali la joto sasa linaenea kote Amerika Kaskazini na Ulaya. Kuanzia Marekani hadi China na Japan, joto kali limetatiza maisha katika nchi nyingi za Ukanda wa Kaskazini. Wataalamu wanaita wimbi hili la joto kuwa 'halikuwahi kutokea'.
Mwezi Juni mwaka huu ulikuwa wa joto zaidi kuwahi kurekodiwa tangu rekodi za joto duniani kuanza.
Moja ya eneo lilikumbwa na hali mbaya zaidi ya joto kali ni eneo la kusini mwa Mediterania la Ulaya. Halijoto katika bara la Ulaya sasa iko karibu na viwango vya juu zaidi.
Tahadhari zimetolewa kote Italia. Takriban watu 500 wamehamishwa baada ya moto mkali kuzuka katika kisiwa cha La Palma nchini Hispania. Nyumba na magari viliteketea katika moto huko Croatia
Halijoto nchini Ugiriki ilikuwa juu zaidi kuwahi kutokea katika miaka ya 40 au zaidi siku ya Ijumaa. Acropolis, mojawapo ya vivutio maarufu vya watalii vya Athens, kimefungwa wakati wa msimu wa kilele wa watalii kutokana na joto kali.
Watalii kadhaa nchini Italia na Ugiriki walikumbwa na athari za joto na kuzimia kutokana na joto hilo. Mtu mmoja alikufa kaskazini mwa Italia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu wanashauriwa kunywa angalau lita mbili za maji kwa siku na kujiepusha na unywaji wa pombe na kahawa - kwani vinywaji hivi hupunguza maji mwilini.
Shirika la anga za juu la Ulaya linasema wimbi jingine kubwa la joto litapiga wiki ijayo na hali inaweza kuwa mbaya zaidi nchini Italia, Hispania, Ufaransa, Ujerumani na Poland.
Onyo kali la joto pia limetolewa katika nchi ya Afrika Kaskazini ya Morocco.
Baadhi ya maeneo ya China na Japan pia yalikumbwa na joto lisilo la kawaida.
Wimbi la joto kali nchini Marekani
Wimbi kali la joto linaenea kote Marekani. Kutoka jimbo la Washington kaskazini-magharibi hadi Florida, Texas, California - kila mahali kumekuwa na joto kali.
Halijoto inatabiriwa kuwa nyuzi joto 46 wakati wa mchana na wimbi la joto linasemekana kuendelea hadi wiki ijayo.
Katika majimbo ya kusini-magharibi, joto limekuwa mbaya zaidi.
Halijoto huko Phoenix imepanda hadi nyuzi joto 43 au zaidi kwa wiki mbili zilizopita. Mnamo Ijumaa Julai 14, joto lilikuwa nyuzi 46 huko Phoenix, nyuzijoto 45 huko Las Vegas, na nyuzi joto 51 huko Death Valley.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kutokana na joto kali, matumizi ya viyoyozi katika jimbo la Texas yamevuka rekodi ya awali. Matumizi ya siku ya Alhamisi yalikuwa MW 81,406 - rekodi mpya.
Viwanja, makumbusho au biashara zimefungwa au zimepunguzwa saa za kufunguliwa katika maeneo mbalimbali.
Kuna angalau moto wa nyika 900 nchini Canada - huku mioto takriban 560 ukiteketeza maeneo bila kudhibitiwa. Kijana wa zimamoto mwenye umri wa miaka 19 amefariki dunia alipokuwa akizima moto magharibi mwa British Columbia.
Kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wastani wa halijoto duniani wiki iliyopita ulikuwa nyuzi joto 17.23 - rekodi mpya ya juu ya wakati wote.
Wanasayansi wanasema sababu ya ongezeko hili la joto ni mabadiliko ya hali ya hewa na mzunguko wa asili wa hali ya hewa unaoitwa 'El Niño'. El Nino hii hutokea mara moja kila baada ya miaka mitatu hadi saba - wakati joto linapoongezeka.
Wanasayansi wanasema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha hali ya hewa isiyo ya kawaida kote ulimwenguni na joto au baridi isiyo ya kawaida, mvua, mafuriko, dhoruba, mafuriko, vimbunga, moto wa nyika - n.k. huenda ikawa matukio ya mara kwa mara.
Joto la dunia limeongezeka kwa takriban nyuzijoto 1.1 na litaendelea kuongezekampaka pale Serikali zitakapofanya juhudi za kuounguza uzalishaji wa kaboni.












