Tamko la Umoja wa Mataifa dhidi ya madai ya mauaji ya Tanzania lina maana gani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Siku chache baada ya kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kueleza wasiwasi wake juu ya mauwaji yaliyotokea nchini Tanzania katika wiki ya uchaguzi mkuu, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk naye ametoa tamko akiitaka mamlaka nchini humo kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za uwajibikaji kuhusiana na mauwaji hayo.
Kwa ujumla, siku za hivi karibuni, matamko kutoka Umoja wa Mataifa yamekuwa yakipuuzwa au kutokuchukuliwa kwa uzito unaostahili.
Chukua mfano wa kile ambacho kimekuwa kikiendelea katika ukanda wa Gaza ambapo pamoja na makemeo na tahadhari za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikitolewa na Umoja wa Mataifa, si Israel pekee lakini hata nchi za Ulaya na Marrekani ambazo zingeweza kusaidia kupunguza mateso ya Wapaelstina zimekuwa zikiangalia pembeni, zisichukue hatua zozote za muhimu kulingana na taarifa na ripoti za Umoja wa Mataifa.
Hii haimaanishi kwamba kauli kutoka Umoja wa Mataifa, hasa kwa viongozi waandamizi kama Katibu Mkuu na wengine hazina mashiko, la hasha. Na hasa kwa kile kilichotokea Tanzania, kauli za wawili hao kutoka Umoja wa Mataifa zina maana kubwa katika muktadha wa mfumo wa haki katika jumuiya ya kimataifa.
Kwanza katika kuweka unyeti juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu na hasa mauwaji ambayo hadi hivi sasa hakuna taarifa kwa umma juu ya kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya washukiwa wakuu wa vitendo vile.
Kwa kutoa matamko yale, Katibu Mkuu na Kamishna wa Haki za Binadamu wanathibitisha kwamba kilichotokea hakikuwa kidogo cha kuachwa kubaki ndani ya mipaka ya Tanzania bali kimeshitua macho na masikio ya jumuiya ya kimataifa.

Lakini kwa kuzungumzia mauwaji yale na kutaka uwajibikaji wa waliohusika, Umoja wa Mataifa unapiga muhuri maumivu na vilio vya waathirika na watu wengine walioguswa moja kwa moja na ghasia zilizotokea kana kwamba kusema malalamiko na vilio vyao ni halali.
Hatua hii ya Umoja wa Mataifa pia inaweka kumbukumbu na rejea ya muhimu ambavyo vinaweza kutumika katika kuchukua hatua zozote ambazo nchi moja moja au jumuiya ya kimataifa itataka kuchukua. Hii imeonekana kwa nchi kama Rwanda au Israel ambapo nchi fulani zilipotaka kuchukua hatua kama za vikwazo vile, walitumia kauli na tafiti za Umoja wa Mataifa kama rejea za uamuzi wao
Kama ambavyo Katibu Mkuu wa pili wa Umoja wa Mataifa Dag Hammarskjöld alivyowahi kusema kwamba Umoja wa Mataifa haukuundwa kuwapeleka binadamu peponi, bali kuwaokoa kutoka kuzimu.
Wakati Hammarskjöld alikuwa akizungumzia zaidi uzoefu wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na namna ambavyo Umoja wa Mataifa umesaidia katika kudhibiti umiliki na matumizi ya silaha za nyuklia takribani miongo sita iliyopita, mtazamo wake hauko mbali sana na matukio ambayo yameendelea kutokea hivi karibuni si tu nchini Tanzania bali katika nchi zingine barani Afrika na duniani kwa ujumla ambao mamlaka zimeonekana kuvuka mipaka ya utu na haki zinapohusiana na watu wake.
Serikali ya Tanzania haijatoa majibu au msimamo wake dhidi ya kauli hizo kutoka Umoja wa Mataifa.












