Matokeo ya Urais Kenya 2022: Kauli tano kuu kutoka kwa rais mteule William Ruto

Chanzo cha picha, WilliamRuto/TWITTER
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
Rais mteule wa Kenya William Ruto amepongeza Tume ya uchaguzi kwa kuendesha uchaguzi huru na wa haki.
Bw. Ruto alisema nini baada ya kutawazwa mshindi wa uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali katika historia ya Kenya?
Tunaangazia kauli tano katika hutuba yake.
Kuhusu uchaguzi
Alisema: "IEBC ambayo ni tume ya uchaguzi ilitushangaza sote…ninataka kupongeza IEBC kwa kuongeza uaminifu wa viwango vingine.
Pia amepongeza mchakato wa uchaguzi, licha ya kwamba hapo awali kundi la makamishena walisema hawakuweza kushiriki katika utoaji wa matokeo.
"Wananchi wa Kenya walipiga kura, makamishena hawafai kupiga kura. Makamishena hao wanne hawana tishio lolote kwa uhalali wa matokeo. Msimamizi wa uchaguzi ndiye atangaza matokeo, na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alifanya hivyo kwa mujibu wa sheria,"Ruto alisema.
"Wafula Chebukati ambaye ni mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ndiye shujaa wetu."
"Watu wa Kenya wameonyesha kutuamini, sio kwa sera za makabila yetu, bali kwa kile tulichokuwa tunakizungumzia."
Ruto aahidi 'serikali yenye uwazi'
Akizungumza na waandishi wa habari Bw. Ruto alisema anafahamu kuwa anakabiliwa na wapinzani wengi baada ya kupata zaidi kidogo tu ya asilimia 50 ya kura.
"Nitaendesha serikali ya uwazi, na ya kidemokrasia," amesema.
"Ninataka kuwaahidi watu wote wa Kenya, kwa njia yoyote waliyopiga kura kwamba hii itakuwa serikali yao.
"Hatuna haja ya kuangalia nyuma. Hatuna haja ya kunyoosheana vidole. Hatuna tamaa wala haja ya kutupiana lawama. Ni lazima tushirikiane kwa ajili ya Kenya inayofanya kazi, ya kidemokrasia na yenye ustawi."
''Ninataka kuwaahidi watu wote wa Kenya, bila kujali jinsi walivyopiga kura kuwa hii itakuwa serikali yao. Najua wengi wanashangaa, haswa wale ambao wametenda mambo mengi dhidi yetu, nataka kuwaambia kwamba hawana chochote cha kuogopa," Ruto alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuhusu Upinzani
"Nilimpigia simu Raila na tukafanya mazungumzo naye na tukakubaliana kuwa vyovyote itakavyokuwa, tutafanya mazungumzo."
Hata hivyo, alipuuzilia mbali kupeana mkono na Raila au washindani wake akisema yeyote anayepinga matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anafaa kwenda mahakamani.
"Uchaguzi huu ulikuwa wa uwazi zaidi kuwahi kufanyika nchini Kenya. Labda watu waliokatishwa tamaa walikuwa watu walioamini serikali ya kina," alisema.
Bw Ruto pia aliahidi atashirikiana upinzani kwa kiwango ambacho watatoa usimamizi kuhus utawala wake.
"Nataka kuwaambia wapinzani kwamba hawana chochote cha kuogopa, hakuna nafasi ya kulipiza kisasi. Ninafahamu kabisa kwamba nchi yetu ipo katika hatua ambayo tunahitaji juhudi za pamoja ili kusonga mbele.''
Kuhusu utawala wa sheria
Akiangazia jinsi Tume ya Uchaguzi ilivyochukuwa muda kutoa matokeo ya uchaguzi wa urais na jinsi alivyosubiri kukamilika kwa mchakato huo alisema: "Mimi ni mwanademokrasia. Ninaamini katika utawala wa sheria. Ninaheshimu taasisi. Tutaheshimu uamuzi wa kila taasisi nyingine."
"Nina uhakika kutakuwa na mazungumzo. Mimi ndiye Rais mteule na kutakuwa na mpito na nina uhakika kutakuwa na majadiliano kati ya Rais wa sasa na mimi," Ruto alisema.
Kuhusu mkondo wa siasa za nchi
"Kama kungekuwa na mtu wa kuamua mkondo wa siasa za nchi ningejua, nadhani dhana hizo zimetokomezwa," alisema.
"Uchaguzi huu ulikuwa wa uwazi zaidi kuwahi kufanyika nchini Kenya. Labda watu waliokatishwa tamaa ni wale walioamini kuna watu watakaosaidia kuamua mkondo wa siasa za nchi," alisema.

Pia unaweza kusoma:














