Finland na Sweden kujiunga na Nato ni tishio au kutaimarisha usalama wa bara la Ulaya?

Fin

Chanzo cha picha, Getty Images

Finland na Sweden, nchi mbili za Nordic zisizoegemea upande wowote, zimetiwa hofu na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kwamba nchi zote mbili sasa zinafikiria kwa dhati kujiunga na Nato, mapema msimu huu wa kiangazi.

Urusi imewaonya wasifanye hivyo. Imetishia "kuzishambulia kijeshi" ikiwa watafanya hivyo.

Kwa hivyo, Ulaya ni mahali salama au hatari zaidi ikiwa aidha au zote mbili za nchi hizi zitakuwa sehemu ya Nato?

Nato - Shirika la Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini - ni muungano wa kujihami wa mataifa 30 ulioanzishwa muda mfupi baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia. Ina makao yake makuu huko Brussels Ubelgiji lakini inaongozwa na nguvu kubwa ya kijeshi na nyuklia ya Marekani.

Finland na Sweden ni nchi za kisasa, za kidemokrasia ambazo zina vigezo vyote vinavyotakiwa na kuwa mwanachama wa Nato.

Luteni mstaafu wa Jenerali wa Jeshi la Marekani Ben Hodges, ambaye aliviongoza vikosi vyote vya nchi kavu vya Marekani barani Ulaya, hana shaka ya manufaa ya hili kwa nchi za Magharibi:

"Sweden na Finland kujiunga na Nato ni hatua kubwa - maendeleo mazuri sana. Ni nchi mbili za kidemokrasia zenye nguvu sana, na majeshi ya nchi zote mbili yana nguvu sana, yenye uwezo na ya kisasa, na mifumo mizuri."

Tatizo ni nini ikiwa mojawapo au nchi zote mbili zitataka kujiunga Nato?

Urusi, na haswa Rais Vladimir Putin, haioni Nato kama muungano wa kujihami. Anatazama kinyume kabisa. Anaiona kama tishio kwa usalama wa Urusi. Ameangalia kwa masikitiko jinsi Nato inavyozidi kupanuka kuelekea mashariki - karibu na Moscow - baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991.

Putin alipokuwa afisa mdogo wa ujasusi katika vyombo vya usalama vya serikali ya Sovieti, KGB, Moscow ilidhibiti nchi zote za Ulaya ya mashariki, na wanajeshi wa Urusi walikuwa wamekaa katika nchi nyingi. Leo, karibu nchi hizo zote zimechagua kuangalia upande wa magharibi na kujiunga na Nato. Hata mataifa ya Baltic - Estonia, Latvia na Lithuania - nchi ambazo hapo awali, bila kupenda, zilikuwa sehemu ya Umoja wa Kisovyeti, zimejiunga na muungano huo.

Nato
Maelezo ya picha, Mchoro kuonyesha namna Nato ilivyotanuka tangu mwaka 1997

Ni 6% tu ya mipaka mikubwa ya Urusi iliyo na nchi za Nato, bado Kremlin inahisi imezingirwa na kutishiwa. Muda mfupi kabla ya Rais Putin kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine tarehe 24 Februari, alidai kuchorwa upya kwa ramani ya usalama ya Ulaya. Wanajeshi wa Nato, alisisitiza, wanapaswa kujiondoa kutoka kwa nchi hizi zote za mashariki mwa Ulaya, na hakuna nchi mpya ziruhusiwe kujiunga.

Neema iwapo nchi hizi zitajiunga Nato

Kwa mtazamo wa kijeshi tu, kuongezwa kwa wanajeshi wengi wa Finland na Sweden kungekuwa msukumo mkubwa kwa nguvu ya ulinzi ya Nato kaskazini mwa Ulaya, ambako inazidiwa kwa wingi na vikosi vya Urusi.

Ben Hodges anasema Finland inaleta ndege za kivita za F35, Sweden inaleta betri za makombora za Patriot na imekilinda tena kisiwa chake kikubwa cha Baltic cha Gotland, ambako Urusi imekuwa ikifanya uchunguzi hivi karibuni. Vikosi vya kijeshi vya nchi hizi mbili ni wataalam wa vita vya Aktiki, wakijifunza kwa bidii kupigana na kuishi katika misitu iliyoganda ya Skandinavia. Wakati Urusi ilivamia Finland katika Vita vya pili vya dunia, Wafini walipigana vikali dhidi ya wavamizi, na kusababisha hasara kubwa.

Kijiografia, kuongezwa kwa Finland kunaongeza nguvu kubwa katika ulinzi wa Nato, na kuongeza mara mbili ya mpaka wake na Urusi. Usalama na utulivu katika Bahari ya Baltic, anasema Hodges, sasa umeboreshwa sana.

Kisiasa, ingeongeza mshikamano wa ulinzi wa pande zote wa nchi za magharibi, ikituma ishara kwa Putin kwamba karibu Ulaya yote imeungana dhidi ya uvamizi wake wa nchi huru, Ukraine.

Hatari iwapo zitajiunga na Nato

Kwa ufupi, hatari hapa ni kwamba upanuzi mkubwa kama huu wa Nato, kwenye mlango wa Urusi, ni ishara ya kuikasirisha Kremlin kiasi kwamba inajibu kwa kupiga kelele kwa namna fulani. Wakati Putin alitishia kuchukua "hatua za kiufundi za kijeshi" katika kujibu hili, inazingatiwa kuwa mambo mawili - kuimarisha mipaka yake mwenyewe kwa kusogeza askari na makombora karibu na Magharibi, na ikiwezekana kuzidisha kwa mashambulio ya kimtandao kwenye eneo la Skandinavia.

Kutoegemea upande wowote kumeinufaisha Sweden kwa miaka mingi. Kuacha kutoegemea upande wowote hakupaswi kuchukuliwa kirahisi. Pia kutakuwa na gharama ya kiuchumi kwa sekta ya silaha za ndani ya Sweden ikiwa nchi italazimika kununua silaha za Nato badala ya zake.

Msemaji wa Kremlin Dmitri Peskov alisisitiza akionya kwamba Finland na Sweden kujiunga na Nato "hakutaleta usalama zaidi kwa Ulaya".

Putin na washauri wake tayari wanailaumu Nato, pamoja na uhalali fulani, kwa kukwamisha mipango yao ya kuichukua Ukraine. Ikiwa wataamua, bila sababu, kwamba upanuzi huu wa ghafla kwenye ubavu wao wa kaskazini unatoa tishio linalowezekana kwa usalama wa Urusi basi hakuna kujua ni nini hasa Moscow inaweza kufanya katika kujibu mapigo.