Urusi na Ukraine: Mashambulizi yaongezeka licha ya mazungumzo ya kusitisha mapigano kuanza

Chanzo cha picha, Reuters
Mapigano yameendelea katika siku ya tano ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, licha ya mazungumzo yanayolenga kupata makubaliano ya kusitisha mapigano kuendelea.
Mashambulizi ya makombora yaliwaua raia kadhaa katika mji wa pili nchini humo, Kharkiv, huku mashambulizi ya anga yakisikika tena katika mji mkuu, Kyiv.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameyaita mashambulizi hayo ya Urusi ya Kharkiv kuwa "uhalifu wa kivita".
Kulikuwa na ripoti za mashambulizi makali ya makombora katika mji wa kaskazini wa Chernihiv.
Urusi inaishambulia Ukraine kutoka kila upande, lakini kasi ya mashambulizi hayo yamepunguzwa na upinzani wa Ukraine.
Mpaka sasa Miji hii mitatu bado iko chini ya udhibiti wa Ukraine.
Mbali na uwanja wa vita, hatua za kiuchumi na kidiplomasia zimeendelea.
Rais Vladimir Putin amepiga marufuku Warusi kuhamisha fedha nje ya nchi wakati akijaribu kuzuia kushuka kwa thamani ya fedha hizo kufuatia kuwekwa kwa vikwazo.
Na kikao cha dharura kisicho cha kawaida cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kimesikia ombi kutoka kwa katibu mkuu la umoja wa mataifa la kusitisha mara moja uhasama.
Katika mpaka wa kaskazini na Belarus, maafisa wa Ukraine na Urusi walimaliza duru yao ya kwanza ya mazungumzo.
Kulikuwa na matarajio kidogo kwamba kikao hicho kitaleta mafanikio, lakini afisa wa Ukraine alisema pande zote mbili sasa zitarudi kwenye miji yao kwa mashauriano zaidi kabla ya duru ya pili ya mazungumzo.
Urusi imesema pande zote mbili zimekubaliana kuendelea kuzungumza na zitakutana tena katika siku chache zijazo.
Katika hatua nyingine:
- Canada yapiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Urusi
- Zaidi ya watu nusu milioni wamekimbia makazi yao ili kuepuka vita nchini Ukraine, Umoja wa Mataifa unasema.
- Rais Putin aliyaweka majeshi ya nyuklia ya Urusi katika hali ya tahadhari baada ya matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Liz Truss na wengine, Kremlin imesema.
- Putin na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamekuwa na mazungumzo ya simu ambapo kiongozi huyo wa Urusi alitoa wito wa maslahi halali ya usalama ya Moscow kushughulikiwa.
- Shirikisho la soka duniani, FIFA na shirikisho la soka barani Ulaya, Uefa, zimesitisha vilabu vya Urusi na timu za taifa kushiriki katika mashindano yoyote.

Chanzo cha picha, Reuters
Katika hotuba yake ya usiku wa manane, Bwana Zelensky alisema kulikuwa na ushahidi kuwa raia walilengwa kwa makusudi wakati wa shambulio la Kharkiv.
Alitoa wito kwa mataifa ya magharibi kufikiria kuhusu zuio la kuruka kwa ndege kwenye anga ya Ukraine - jambo ambalo Marekani hadi sasa imeliweka kando kwa hofu kwamba inaweza kuiingiza katika mgogoro wa moja kwa moja na Urusi.

Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi
- MOJA KWA MOJA:Ukraine na Urusi: Wanajeshi 70 wauawa huku msafara wa magari ya kijeshi ya Urusi ukikaribia Kyiv
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine

Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha maroketi yakitua Kharkiv, katika kile ambacho baadhi ya wachambuzi wa masuala ya ulinzi wamekielezea kama mfano wa shambulio la bomu katika eneo la mjini.
Awali Urusi ilikanusha kulenga maeneo ya makazi.
Picha mpya za satelaiti zilionyesha msafara wa kijeshi wa Urusi ukiwa takriban maili 40 (kilomita 64) kaskazini mwa Kyiv.
Lakini ripoti za mapigano mapya katika viunga vya mji mkuu ziliwalazimisha wakaazi kurejea katika maeneo yao ya kujificha Jumatatu jioni.
Video nyingine iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha moshi mkubwa katika maeneo ya maduka yaliyokuwa yanaungua moto huko Chernihiv, mji mwingine ambao umekuwa chini ya shinikizo kubwa la mashambulizi ya Urusi.
Mwalimu mmoja huko Chernihiv, Oksana Buryak, ameiambia BBC kuwa hali ni mbaya ni kama 'filamu ya kutisha'.
"Tumeumizwa mioyo, hatuelewi chochote," alisema.

Kwa upande wa kusini, vikosi vya Urusi vinajaribu kuchukua udhibiti wa bandari muhimu ya kimkakati ya Mariupol, karibu na Crimea iliyoharibiwa na Urusi. Ukraine imekanusha taarifa kwamba Zaporizhzhia, kilipo kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya, kimeangukia mikononi mwa Urusi.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Denys Monastyrskyy, akizungumza na BBC, alisema hali nchini humo ni mbaya, lakini imara.
"Kila siku adui anatuma vikosi zaidi na zaidi. Lakini majeshi yetu tukufu yamekuwa yanaharibu kila kitu kinachoingia Kyiv," aliongeza.
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema mamilioni ya raia wanalazimika kujilinda na mabomu kwa kujificha katika maeneo kama vile vituo vya reli ya chini ya ardhi ili kuepuka milipuko.












